SIKUKUU
YA FAMILIA TAKATIFU MWAKA-C
Yesu,
Maria, na Yosefu
27/12/2015
Somo
I: YbS 3:3-7; 12-17
Zab:
127: 1-5
Somo
II: Kol 3:12-21
Injili:
Lk 2:41-52
Nukuu:
“Amheshimuye baba yake
atafanya upatanisho wa dhambi, naye amtukuzaye mama yake huweka akiba iliyo
azizi,” YbS 3:3-4
“Amheshimuye babaye
atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa,” YbS 3:3:5
“Amtukuzaye baba yake
ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye, na kuwatumikia
wazazi wake kama mabwana. Mwanangu,” YbS 3:6-7
“Mwanangu, umsaidie
baba yako katika uzee wake, wala usipate
kumhuzunisha siku zote za maisha yake,” YbS 3:12
“Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa
upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana,” YbS 3:13
Mwenye kumdharau baba
yake ni mfidhuli, naye mwenye kumlaani mama yake amekwisha kulaaniwa na Bwana,”
YbS 3:16
“Basi, kwa kuwa
mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu
wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana,
na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana
alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi,” Kol 3:12-13
“Zaidi ya hayo yote
jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu,” Kol 3:14
“Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe
na uchungu nao,” Kol 3:18-19
“Ninyi watoto, watiini
wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana,” Kol
3:20
“Ninyi akina baba, msiwachokoze
watoto wenu, wasije wakakata tamaa,” Kol 3:21
“Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi
katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali,” Lk 2:47
“Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu
yake,” Lk 2:47
“Na walipomwona walishangaa, na mama yake
akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa
tukikutafuta kwa huzuni,” Lk 2:48
“Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya
kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na
neno hilo alilowaambia,” Lk 2:49-50
“Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye
alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake,” Lk 2:51
“Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na
kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu,” Lk 2:52
TAFAKARI:
“Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha
ukamilifu,” Kol 3:14
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tukiwa bado katika kipindi cha kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama Kanisa
anaadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kwa namna ya
pekee leo, masomo yote matatu yanamulika swala zima la Familia, muundo wake,
wajibu wake kwa ujumla na kila mmoja katika familia kadiri ya nafasi yake,
Mahangaiko ya familia, na kutengemaa kwa familia yenye kujali na kuwajibika.
Bila shaka msingi wa familia ni ule moyo ya upendo wenye kuzaa hali ya
kuvumiliana na kutabikiana. Hiki ndicho kifungu cha ukamilifu. Kama asemavyo
Mtume Paulo, “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha
ukamilifu,” Kol 3:14. Kuacha hii Familia Takatifu ya Yesu, Marian na Yosefu,
familia zetu si kamili katika maana ya Utakatifu. Familia yetu zina madhaifu
mengi sana. Lakini familia hizi ambazo ni dhaifu husimama imara pale
wanapotazama, jifunza, na kuishi Utakatifu wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria
na Yosefu kama mfano ulio hai wa kuiga.
Ni wazi
kwamba familia iliyosimama katika kweli, haki, upendo, huruma, na kusamehana si
kazi rahisi na si kazi ya siku moja. Leo tunaposheherekea Familia Takatifu ya
Yesu, Maria na Yosefu, haikuwa kazi rahisi kwa Maria na wala Yosefu kumlea
mtoto Yesu. Tuelewa kwamba Yesu ni Mungu na Mwanadamu. Asili hizi mbili
zilileta sintofahamu nyingi kwa Maria na Yosefu katika malezi ya Mtoto Yesu.
Tunaweza kuona jibu la Yesu kwa wazazi wake baada ya kupotea kwa siku tatu na
kumkuta Hekaluni akifundisha. Yesu alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili tu.
Kama ilivyokuwa kawaida kwa wazazi, walipomwona mwanao Yesu, Mama Bikira Maria
alimuuliza, “Mwanangu, mbona umetutenda hivi?
Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni,” Lk 2:48. Yesu bila kupepesa macho aliwajibu wazazi wake, “Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya
kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao
hawakuelewa na neno hilo alilowaambia,” Lk 2:49-50. Kutokuelewa huku kwa wazazi
wake juu ya Yesu kulikuwa pia kwa watu wengine. Tazama kwa umri huu wa miaka
kumi na miwili Yesu alianza kuwashangaza wengi wa hekima na busara aliyokuwa
nayo. “Nao wote waliomsikia walistaajabia
fahamu zake na majibu yake,” Lk 2:47. Hapa
Yesu anawakumbusha wazazi wake na sisi pia asili ya Umungu wake. Mwinjili
anatuamba kwamba “Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia!” Lk 2:50.
Pamoja na kutokufahamu huku wa Bikira Maria, Yosefu mumewe na watu waliomzunguka Yesu, haikuwa nafasi ya kuzuia kukua kwa Yesu kiakili, maadili na imani. “Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu,” Lk 2:52
Pamoja na kutokufahamu huku wa Bikira Maria, Yosefu mumewe na watu waliomzunguka Yesu, haikuwa nafasi ya kuzuia kukua kwa Yesu kiakili, maadili na imani. “Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu,” Lk 2:52
Pamoja na sintofahau hizi, Bikira Maria alikuwa na muda
mwingi wa kutafakari haya asiyoyafahamu. “Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri
moyoni mwake,” Lk 2:19. Kuyaweka moyoni ni kuyapa nafasi ya tafakari kwa yale
tusiyoyajua. Je, wewe kama mzazi mwanao anapofanya ndivyo sivyo, wajiuliza kwa
nini amefanya kama alivyo fanya? Kujua chanzo cha tatizo ni bora kuliko
kukimbilia kulitatua tatizo. Hivyo tafakari ya Bikira Maria ilimsaidia kufahamu
uwezo na kile alicho mwanaye Yesu Kristo. Muujiza wa kwanza ya Yesu kule Kana
unathibitisha ufahamu wa Maria juu ya mtoto wake. Kulipotokea upungufu wa
divai, Bikira Maria alienda moja kwa moja na kumwambia Yesu, Mwanaye, kwamba
hakuna divai. Bikira Maria hakubaki na jibu la mwanaye, ila alienda moja kwa
moja kwa wale wahudumu na kuwaambia, “Lo
lote atakalowaambia, fanyeni,” Yoh 2:5. Kwa tendo hili hakuna shaka kwamba Mama
Bikira Maria anaufahamu uwezo wa mtoto wake. Je, leo wazazi wangu muna muda wa
kutosha kuwafahamu watoto wenu ikiwa ni pamoja na tabia zao? Basi tujifunze kwa
Mama Bikira Maria. Leo tunapoongelea familia na hasa lenye malengo na
mwelekeo, tunaongelea familia ndani ya ndoa Takatifu yenye kujali na
kuwajibika. Hivyo ni vyema kujua fumbo zima la ndoa na chimbuko la famila kama
tunda na matokeo ya ndoa hiyo.
1. Fumbo zima la ndoa na chimbuko la familia
Wapendwa wana wa Mungu, upendo huu wa Mungu kwa watu wake yatupasa kuuona katika mambo yote yenye kutupeleka katika umoja wake, upendo wake, ushirikiano wake na hata katika maagano yetu katika maisha. Ni kwa kupitia umoja huo, upendo huo, na ushirikiano huo wa Mungu na mwanaye mpenzi, Yesu Kristo Mungu hujidhihirisha kwetu kila siku ya maisha yetu hapa duniani. Upendo wa Mungu na mshikamano na mwanaye tunauona katika masakramenti yake, na hasa leo tunavyotafakari kwa ukaribu sakramenti hii ya ndoa. Naye Mtume Paulo anasema, “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili,” Efe 5:22-23. Hapa upendo wa Mungu kupitia Kristo mwenyewe unaonekana kwa utii huu wanaoishi wana ndoa, na hasa kwa mke kumtiii mumewe. Je, ndoa zetu leo ni salama? Akina mama mnaishi ukweli huu katika agano lenu la ndoa? Leo baadhi ya wanawake wamefikia kuwaita waume zao vyuma chakavu. Je, hayo ndiyo makusudio ya Mungu na muungano wenu huo?
Kwa
upande wa wanaume yawapasa kuwapenda wake zao katika kweli na haki. Upendo huu
unafananishwa na upendo wa Kristo na Kanisa lake. “Enyi waume, wapendeni wake
zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili
makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea
Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe
takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27. Wanaume zieshimuni ndoa zetu kwani ndio
utakatifu wenu mnapoziishi katika kweli na haki. Wake zenu hawahitaji mambo ya
pekee sana zaidi ya kuyasadifu yale wayatendayo kila siku katika familia. Tabia
ya kuwaita wake zetu magoli kipa ni chukizo mbele ya Mungu. Muunganiko wenu ni
makusudio ya Mungu, na ndivyo alivyoona inafaa.
Utii wa kweli si utumwa kwenu, bali ni ukamilifu wa makusudio ya Mungu katika maisha ya umilele. Wito wenu wa ndoa ni kuufikia umelele wa maisha yenu mlioandaliwa kupitia sakramenti hiyo. Hivyo, “kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24. Ni kuwa na utii katika Kristo kwa sababu yeye anayo maneno la uzima wa milele. Ni kwa kupitia NENO huyu vyote vilifanyika, na kwa kupitia NENO huyu vyote huwa na uzima wa milele, Yoh 1:3. “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja,” Efe 5:31. Tendo hili la ajabu katika sakramenti hii ya ndoa halimwesabii haki mmoja wa wanandoa kuwa na mambo yake ya pekee na binafsi tena. Hakuna msamiati huu tena wa kusema hiki changu na hiki chako. Kwa kufanya hivyo ni kuujeruhi mwili huu mmoja. Je, jambo hili lina ukweli katika ndoa yako? Je, ni mambo mangapi ya siri unayoyafanya bila kumuhusisha mwenzi wako wa ndoa? Je, hujui kwa kufanya hayo unaijeruhi ndoa yako? Ndugu yangu kama unaishi ukweli huu na kinyume cha sakramenti hiyo ya ndoa, elewa kwamba ndoa hiyo ishakufua katika uhalisia wa mambo na ukweli wa Kimungu. Kilicho baki ni maagizo kuu, na wote mmekuwa wasanii katika sakramenti hii Takatifu.
2. Changamoto kwa watoto na wajibu wao katika familia:
Ni ukweli usiotia shaka
kwamba ni wajibu wetu kuwaheshimu wazazi wetu ikiwa ndiyo amri ya nne ya Mungu.
Tokeo hilo linatupa heri na miaka mingi katika maisha ya umilele. “Amtukuzaye
baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye, na
kuwatumikia wazazi wake kama mabwana. Mwanangu,” YbS 3:6-7. Tendo la kuwapenda
wazazi ni haki na linapendeza machoni mwa Mungu. Ni haki kama asemavyo Mtume
Paulo, "enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo
haki," Efe 6:1. Pia tendo hilo lapendeza machoni mwa Mungu, "ninyi
watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hii lapendeza katka
Bwana," Kol 3:20.
Kwa mantiki hiyo, mtume Paulo anaenda mbali na kutupa angalisho kuhusu kuwatii wazazi wetu, na kusema, "maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi," 2 Tim 3:2. Kwa hiyo ndugu yangu jambo hilo ni wajibu, ni shukrani na ni safi kufanya hivyo. “Mwenye kumdharau baba yake ni mfidhuli, naye mwenye kumlaani mama yake amekwisha kulaaniwa na Bwana,” YbS 3:16. Kwa upende mwingine wazazi ndiyo vielelezo vya Mungu wakiwa kama washiriki wa Mungu katika uumbaji. Kazi hii hata Malaika hakupewa. Ndugu yangu huna Baba zaidi ya Baba uliye naye. Hata kama ni mwendawazimu huyu ndiye Baba yako na unapomweshimu na kutimiza wajibu wako hapo ndipo penye chemchemu ya neema zote. “Amheshimuye baba yake atafanya upatanisho wa dhambi, naye amtukuzaye mama yake huweka akiba iliyo azizi. Amheshimuye babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa,” YbS 3:3-5.
Hivyo ni wajibu wa kila mtoto katika familia kuwaheshimu, kuwajali na kuwatunza wazazi katika uzee wao. Tendo hili linakukumbusha kutoa shukrani kwa majitoleo yao katika maisha yako. “Mwanangu, umsaidie baba yako katika uzee wake, wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana,” YbS 3:12-13. Ndugu yangu, namna unavyomjali na kumweshimu mzazi wako ni kwa namna hiyo hiyo utakavyo heshimiwa na kujaliwa na wanao ufikiapo uzee wako. Ni vyema ukawekeza kuanzia sasa katika jambo hili la muhimu katika maisha.
3.
Changamoto za wazazi kwa watoto wao, na hasa malezi:
Pamoja na hayo niliyokwisha
kuyasema, wazazi yawapasa kuheshi matakwa ya watoto wao ikiwa ni pamoja ya ndoa za watoto wao wakijua wajibu wao wa
kimalezi na kuwaacha watoto wao kuwa huru kuchagua mwenzi wake wa maisha. Pia
wapo wazazi wengi wanaowageuza watoto wao kama miradi yao. Kikomo cha famili na
kugawanyika ni pale watoto ndani ya familia wanapofikia kuwa na familia. Hili
mzazi lazima ulijue na ujiandae vizuri hasa kisaikolojia. Hata kama unampenda
vipi mtoto wako huwezi kuzuia asiumwe, asipate matatizo, na wala asife. Cha
kushangaza, unakuta binti kaolewa na mara kwa mara mama mzazi yupo beneti naye
kwenye shughuli zake, biashara zake, bila taarifa ya Mume wa binti yake. Ndoa
ni ya watu wawili. Muwaache. Wewe mama kila mnada unapenda kwenda na binti yako
kwa nini?
Jambo lingine la wazazi
ni manyanyaso kwa mwali wao. Manyanyaso yakimfumo yasiyokwisha. Mnamfanya mwali
wenu kama remote/kiongozea mbali. Anakuwa kama dekio lenu. Mwajiona ndoa yenu
ni bora kuliko ya mwali huyu. Mbona yenu hatuyasemi. Yawezekana wewe ulimpenda
huyo mume wako kwa kipande tu cha muwa. Usicheke! Kinachowaunganisha wawili na
kuwa familia ni fumbo kubwa sana. Hivyo, “Ninyi
akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa,” Kol 3:21.
Waacheni waishi maisha yao. Ni kweli yawezekana kabla ya mtoto wenu kuoa au
kuolewa vimiminika (tumafuta, tusukari, tunyama, tunguo twa mtimba, na hata
tupesa) vilikuwa vingi nyumbani. Baada ya ndoa, hayo yamepungua au kutoweka
kabisa. Je hamjui ya kwamba, "kwa sababu hayo ndiyo mlioitiwa ili mrithi baraka?"
1Pt 3:9c. Kuyakosa hayo isiwe kero na shiiida kwa ndoa yao.
Ndoa inakuwa na uhai
haya yakizingatiwa kadiri ya mtazamo wa Mtume Petro. "Neno la mwisho ni
hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikivu,
wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye
kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka," 1Pt 3:8-9.
4.
Changamoto za leo kwenye familia, na wajibu wake:
Ndugu yangu, naneno
hayo ni mazito sana kwa wanandoa. Kwa upande wa kina mama, wapo wanaoishi
kwenye ndoa bado hawana utambuzi au tofauti na usichana wao. Mama kwenye ndoa
tambua kwamba kila siku yakupasa "kupungua" kwa ajili ya familia yako
"iongezeke." Familia yaani Baba na watoto wenu waongezeke; upendo, furaha, afya, akili na mambo mengine mengi tu. Je,
utapunguaje? Mtume Petro anatuambia, "kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba
kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe
utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyo haribika; yaani roho ya upole
na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu," 1Pt 3:3-4. Mtume Petro
hapa hapingi mama usiende saloon au kutokuvaa vizuri; bali muelewe kwamba hayo
siyo vipauwa mbele katika familia.
Wengi tumetumia muda
mwigi nje badala ya ndani. Vikao kila siku visivyoisha. Sema za kiroho januari
hadi disemba, mikutano ya injili hadi manane ya usiku, nk. Je, saa ngapi
utaijenga nyumba yako? Huku ni kukosa busara kama tunavyoaswa, "Kama pete
ya dhahabu katika pua ya nguruwe, kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili,"
Mit 11:22. Kwa maana hiyo, "kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba
yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe," Mit 14:1.
Wakati mwingine tunamtafuta mchawi wakati mchawi mwenyewe ndiwe wewe. “Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika
Bwana. Ninyi waume, wapendeni
wake zenu msiwe na uchungu nao,” Kol 3:18-19. Huu ni wajibu msingi katika
maisha ya ndoa na ufahamu wake.
Wanawake wengi ni wawivu kupindukia. Jua
likichomoza tu utakuta mkeka upo nje. Nikujigalagaza kwenye mkeka kama dagaa wa
kigoma. Masikini wa Mungu labda mumewe alivutiwa na umbo lake la kushikika,
baada ya nusu mwaka afadhali ya mkuyu wa handeni. Licha ndoa ni zaidi ya haya
ya nje, ila nayo huleta matamanio ya kutazama kwingine kama tulipo kuna pazia na
kiza. Elewa mumeo kama ameajiriwa au kujiajiri mwenyewe, awapo huko naye
ameolewa na hiyo kazi yake. Awapo nyumbani anaitaji amani na utulivu. Wanawake
wengi hawana muda wa kuyasoma mapigo ya mioyo ya waume zao. Mmewe akifika
nyumbani tu anadakiwa mlangoni na risala ya mahitaji; utasikia, unajua hakuna
sukari, chumvi, unga, nk. Mpe kwanza nafasi ya kupumzika. Muulize habari za
huko alikotoka. Muulize angependa kupata nini kabla ya ulichoandaa. Wakati
mwingine kuandaa meza anafanya mfanyakazi wa ndani. Au akifanya yeye
utashangaa. Ugali kaupika saa sita mchana
wakati mumewe kafika nyumbani saa kumi jioni. Ugali unatoka jasho tu.
Kwa nin usiandae mboga tu na wakati mumeo anapata chai ukawa unasonga ukali?
Angalia! Huko alikotoka
kila mahali kuna ‘bar’ na nyama choma. Na nyumba nyingi pembezoni mwa barabara
kuna kibao kimeandikwa "vyumba bado vipo." Ni kwa namna hii sebule
ujeuka kuwa kwenye Bar. Pale anahudumiwa vizuri na kwa ujuzi. Huuliwa,
"uncle tukusaidie nini? Anajibu, "bia, kilimanjaro." "Ya
baridi "au ya moto? Mhudumu anasisitiza. Kwa vile nyumbani weshagombana na
mkewe, anajibu, "ya baridi." Tazama binti huyu hakai mbali na mteja
wake. Wewe ulipomwandalia chakula ulirudi kwenye mkeka wako. Binti huyu hukaa
nyuzi 45 hivi. Baba huyu akimeza fundo moja la bia ananyanyua macho anakutana
na tabasam. Kama Baba huyu alikuwa na mpango wa kunywa bia moja huongeza zadi
5. Hapa kwishakuwa sebuleni pake. Nani wa kulaumiwa?
Wanawake wengi huwasema
vibaya sana waume zao. Wengine ufikia hata kuwaita waume zao "nyuma chakavu,"
kama nilivyokwisha kusema hapo mwanzo. Onyaneni kindugu tena mkiwa chumbani.
Baadhi ya wanaume nao
ni balaa! Kumtukana hata kumpiga mkewe mbele za watu au marafiki zake na watoto
ni fursa. Ona matusi hayo anavyoyafyatua kama bomu la skadi. "Mwanamke
gani wewe nimekuokota bar? Bado sijaoa!" Unayasema maneno haya mbele ya
watoto wako. Hata kama ni kweli hubakia maumivu makubwa kwa watoto. Mtume Petro anasema, "ninyi waume, kaeni
na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na
kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."
1Pt 3:7. Mke wako haitaji ununulie ndege ili awe na furaha. Ni wewe tu kusadifu
kila kitu kidogo anachokifanya nyumbani. Mmefikia hatua ya kuwaita wake zenu
"magoli kipa." Mkimaanisha wao ni kudaka tu! Jambo hili halipendezi
mbele ya Mungu. Nyote wawili yawapasa kusomana tabia na kupongezana kwa kila
kitu mfanyacho kizuri. Mmeo akikununulia kitu kabla ya kukikosoa mpongeze na
kumwambia siku nyingine ukitaka ninunulia kitu itapendeza tukienda sote wawili.
Kiukweli Wanaume hatuna uhalisi wa kuchambua uzuri kama uzuri, tupo zaidi
katika idadi ya kitu au vitu.
Wapendwa wana wa Mungu,
wazazi wetu wana nafasi yao muhimu sana katika maisha yetu kama viumbe
shirikishi katika uumbaji na Mungu, mahusiano yetu kimaagano yana nafasi yake
katika umilele wetu, na hivyo isiwe sababu ya kudharau au kukengeuka na
kuwakana wazazi wetu. Mwisho yatupasa kujua wajibu wetu kwa wazazi, maisha yetu
ya kimaagano kila mmoja kadiri ya wito wake, na kusudi la kuumbwa wetu na uwepo
wetu hapa duniani. Yote haya ni maandalizi ya maisha ya umilele, kama ilivyo
amri ya nne wa Mungu, “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa
nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kut 20:12
Kijana
Felix aliyemaliza masomo yake ya udaktari alibahatika kumwoa mwanamke mwenye
elimu kama yake. Mwanamke huyu alijipenda sana kupita kiasi kutokana na
mazingira ya makuzi yake. Ni kweli alitoka familia yenye pesa na tajiri sana.
Felix
alitoka familia masikini sana, na soma yake ilikuwa ya shida sana. Felix
alifika hapa alipo kwa kutegemea biashara ndogo ndogo za mama yake mzazi. Baba
yake Felix alifariki muda mrefu, Felix angali darasa la pili.
Akiwa
ameajiriwa na kuwa na mji wake, mama yake mzazi alipenda kumtembelea mtoto
wake. Kwa bahati mbaya au nzuri Mama yake Felix alifika na kumkuta mke wa mtoto
wake. Kwa namna alivyokuwa mama yake Felix, mke wa Felix alikuwa na mashaka
naye kwani alionekana kama ombaomba fulani hivi. Hata kwa kujitambulisha kote
kule mke wa felix hakuweza kumpokea vizuri na kulazimika kumwifadhi moja ya
vyumba vya stoo.
Alipofika
Felix kutoka kazini mkewe alimwambia ujio wa mwanamke mmoja mchafu na waajabu
kutokea, na kusema, “eti mama huyo hapa stoo anasema kuwa wewe ni mwanaye.”
Felix kwa aibu naye hakumpokea vizuri mama yake, na ndipo ugomvi ulipoanzia.
“Kama unasema kuwa wewe ni mama yangu piga mahesabu ya gharama zote
ulizonitunza na kunilea nami nitakulipa,” Felix alimwambia mama yake kwa
hasiri.
“Naombeni
munionyeshe uhani nami nikirudi nitakupa hesabu yangu,” mama yake Felix mjibu
Felix. Baada ya muda kidogo mama yake Felix alirudi akiwa amejipaka kinyesi
chake mwili mzima na kumwambia Felix, “haya naomba uniogeshe na hii ndiyo
gharama yangu kwa siku moja tu katika utoto wako. Kutokana na harufu ile, Felix
hakuweza hata kumsogelea Mama yake. Je, Yesu angemlipa nini Mama yake kwa
mahangaiko aliyoyapata hadi chini ya msalaba alipokata roho? Yesu anamkabidhi
mama yake Kanisa na kusema, “Mama tazama mwanao.” Je, watambua nafasi yako
katika familia?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Mwanangu, wakati wa kufanikiwa
uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapewa kuliko mwenye ukarimu,” YbS 3:17
No hay comentarios:
Publicar un comentario