MISA
YA MCHANA
25/12/2015
Somo
I: Isa 52:7-10
Zab:
98: 1-6
Somo
II: Ebr 1:1-6
Injili:
Yoh 1:1-18
Nukuu:
“Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa
Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, Ameukomboa
Yerusalemu,” Isa 52:9
“Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa
yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu,” Isa 52.10
“Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa
sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka
kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu,” Ebr 1:1-2
“Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake,
akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi,
aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo
tukufu kuliko lao,” Ebr 1:3-4
“Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na
wamsujudu malaika wote wa Mungu,” Ebr 1:6
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye
Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala
pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1-3
“Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa
Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si
kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13
“Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu
wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh
1:14
TAFAKARI:
“Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa kwa furaha kubwa anaposherehekea siku hii ya kuzaliwa Mwokozi
na Mkombozi wetu Yesu Kristo. Hivyo “Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja,
Enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa Bwana amewafariji watu
wake, Ameukomboa Yerusalemu,” Isa 52:9. Kwa namna ya pekee leo Mama Kanisa ameielekeza
tafakari yake kwenye Umungu wa Yesu Kristo ikiwa ni asili yake ya pili. Jana
usiku kwenye Misa ile ya Kesha la Noeli, Mama Kanisa alifanya tafakari ya kina
kuhusu ubinadamu wa Yesu Kristo. Hivyo asili hizi mbili ndizo alizokuwa nazo
Yesu hapa duniani kwa ajili ya kile alichokijia, yaani, kutukomboa kutoka
katika utumwa wa dhambi, na kuturudishia hadhi yetu tena ya kuwa wana na
warithi wa ufalme wa mbinguni.
Injili ya leo kadiri ya
Mwinjili Yohane, anatutafakarisha kwa undani kabisa asili hii ya Umungu wa
Mwokozi na Mkombozi wetu Yesu Kristo. Ni kwenye sehemu hii ya Injili pia
tunaona nani ni Yesu, na nafasi yake
ilikuwa wapi kabla ya kuumbwa kwa ulimwengu na vyote vinavyoonekana na
visivyoonekana. Siku hii ya leo tukufu ya Mungu, kuzaliwa kwake Yesu Kristo,
imeufunua ukweli ambao haukuwahi kujulikana tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Ukweli
huo ni huu kwamba, “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana
pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18. Huu ndio
msingi na ufupisho wa hayo yote aliyoyasema Mwinjili Yohane.
Ufupisho
huu unagusa subira yote katika historia nzima ya wokovu wetu, kama asemavyo
Nabii Isaya, “Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa
yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu,” Isa 52.10. Kwa hiyo, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa
Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu
wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh
1:1, 14. Ni kwa sababu hiyo katika Mwili ni Mungu kama Baba.
Kwa uwezo
wake wa Kimungu, hakuna chochote kilichokuwa pasipo Yeye, yaani, neno huyu aliyefanyika mwili. “Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa
Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika,” Yoh 1:1-3. Ni kwa maana hii na ukweli huu kwamba, ye yote
amwonaye Kristo, amemwona Baba. Yesu kauthibitisha ukweli huu, anamwondolea
mashaka aliyokuwa nayo Filipo pale alipomtaka amwonyeshe Baba. Naye, “Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi
siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe
wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9. Lakini
“kuona” huku kunawezeshwa tu kwa yule anayelisikia neno, yule ambaye kwa imani
anaona zaidi ya “mwili,” yaani utukufu wa Baba alioupokea. Kwa hiyo kuja kwake
Mwokozi wetu ulimwenguni huku ni “utengano”: kuwatenga watu katika mwanga na
giza, kama mwanga ambao ni wa ulimwengu. “Huyo hakuwa ile nuru, bali
alikuja ili aishuhudie ile nuru. Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika
ulimwengu,” Yoh 1:8-9.
Hivyo
wapendwa katika Kristo, wote watakaoupokea mwanga huo wanaupokea kwa Imani
ikiwa ndiyo zawadi kubwa aliyetuletea Mwokozi na Mkombozi wetu. “Bali wote waliompokea
aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu,
wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh
1:12-13. Mwokozi na Mkombozi wetu leo hii anahitaji nafasi ndani ya Moyo wako.
Bila shaka wengi wetu hii siyo Noeli ya kwanza kusherehekea. Basi nikuombe
ufanye mabadiliko mwaka huu kama tendo la shukrani kwa Mungu. Yakupasa kufanya
mkataba na Mungu kuhusu maisha yako, na iwe tendo lako la kudumu muda wote
uwapo hapa duniani. Fanya hivyo na Mungu atakutumia vizuri kadiri ya mpango na
hitaji lake.
Huna
wakati mwingine tena katika maisha yako wa kufanya jambo hili ninalokuwambia.
Kama Mungu ilifika mahali akasema basi na inatosha, kwa nini wewe usiseme pia
basi inatosha kwa kuanza upya na Mungu? Ni Mungu huyu, “ambaye alisema zamani na
baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi
amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye
aliufanya ulimwengu,” Ebr 1:1-2. Leo tunapewa nafasi ya kuongea naye moja kwa
moja na bila chenga.
Wapendwa
katika Kristo, katika Ukuu na Umungu wake Mwokozi na Mkombozi wetu, “Yeye… ni mng'ao wa utukufu
wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha
kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu; amefanyika bora kupita
malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao,” Ebr 1:3-4.
Hivyo mwisho wa maisha yetu hapa duniani utakuwa na maana na uhakika wa umilele
ndani na katika Kristo Yesu. Jamani Mungu yupo na huyu ndiye tunayemshangilia
na kumsheherekea leo. Hatuna uzima pasipo Yeye.
Mwana
falsafa, mwana mashairi, mwanamziki na mtaalamu wa lugha, aliyejulikana sana, Friedrich Wilhelm
Nietzche (1844-1900), hakuamini kuwa Mungu yupo. Nietzche alikuwa mzaliwa wa
Urusi ya Zamani, ila maisha yake karibia yote aliishi Ujerumani. Falsafa yake
ilijulikana kama “Nihilism and death of God,” kwa maana ya kwamba, “Vyote ni
ubatili na kifo cha Mungu.”
Katika
moja ya maandishi yake yaliyobeba falsafa hii alithubutu kusema “Mungu amekufa
kwa hiyo hakuna Mungu.” Watu wengi wasioamini uwepo wa Mungu walishabikia sana
falsafa yake na hasa eneo la Ulaya. Ila jambo la ajabu, tarehe 25 mwezi wa
Agosti, 1900, Mungu alitangaza kuwa “Mwafalsa mashuhuri Friedrich Wilhelm
Nietzche amefariki,” kwa ugonjwa wa Neumonia katika umri wa miaka 55.
Ndugu yangu
uliyesafiri nami katika tafakari hii, kati ya Nietzche na Mungu, ni nani aliye
mkweli? Tusisahau jambo hili: “Bwana huua, naye
hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye
hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa
yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu,” Isa 52.10
No hay comentarios:
Publicar un comentario