domingo, 27 de diciembre de 2015

TAFAKARI: JUMATATU, KIPINDI CHA NOELI, SIKUKU YA WATOTO MASHAHIDI

JUMATATU KIPINDI CHA NOELI
Sikukuu ya Watoto Mashahidi
28/12/2015
Somo: 1Yoh 1:5:2:2
Zab: 124:1-5, 7b-8
Injili: Mt 2: 13-18
Nukuu:
Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli,” 1Yoh 1:6

bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote,” 1Yoh 1:7

Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu,” 1Yoh 1.8

Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote,” 1Yoh 1:9

Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote,” 1Yoh 2:1b-2 

Na hao walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize,” Mt 2:13

Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi,” Mt 2:16

TAFAKARI: “Tuushinde uovu kwa wema. Kama wafuasi wa Kristo tu mwanga wa Ulimwengu”

Wapendwa wana wa Mungu, Mama Kanisa leo anashereherekea Sikukuu ya Watoto Watakatifu Mashahidi, waliomwaga damu yao pasipo hatia yoyote ile. Huu ni mtikiso wa kwanza pale nguvu na mamlaka za kibidamu zinapoingiwa na hofu. Mtoto Yesu anakuwa tishio kwa utawala na milki ya Mfalme Herodi. Yesu ni mfalme wa AMANI! Neno na mtazamo wa nyakati ule kuhusu MFALME, unamtia hofu Herodi Mfalme. Ukweli huu ni unakuwa hofu kwa wale wote wenye kung’ang’ania madaraka na ukuu. Ni tishio kwa uwepo wa Amani hii anayotupatia Kristo. Kuwa na Amani ndani na katika Kristo Yesu ni kujisalimisha kwake. Aliye kwenye madaraka ni vigumu kujisalimisha kwani kutamwondolea ukuu wake. Hivyo Yesu anatuambia, “Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate,” Lk 9:23. Je, nini nani aliyetayari kuyaacha yale yanayomtukuza na kupokea Amani anayotupatia Kristo Yesu? Wapo wengi wanaouwawa kila dakika ulimwenguni na hasa nchi zetu za kiafrika kwa sababu ya hofu ya madaraka yaliyobebwa na utawala dhalimu.

Hivyo kuhakikisha anamwangamimiza Mtoto Yesu, tangazo linatolewa mara moja baada ya kujua wale Mamajusi wamemdanganya kadiri ya maagizo aliyokwisha wapa, yaani, “Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie,” Mt 2:8. Wakijua nia yake mbaya juu ya mtoto Yesu, Mamajusi walishika njia nyingine baada ya kumsujudu mtoto Yesu na kutoa zawadi zao. Hapa ndipo lilipotolea tangazo la kuwaangamiza watoto wasio na hatia. Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi,” Mt 2:16. Nguvu ya Mungu na mpango wake kwa wale alirithia nao ni tofauti na mipango yetu ambayo kwayo haina uzima ndani yake.

Kama Mungu ndiye mweza wa vyote hakuna chochote kitakachozuia mpango huo, kwani nasi kama tulivyo na mamlaka tuliyonayo humtegemea Mungu huyu huyu.Na hao walipokwisha kwenda zao, (Mamajusi) tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize,” Mt 2:13. Ni nani kama Mungu wetu? Leo tunajionea wenyewe baadhi ya tawala ambazo hazipo tayari kuachia dola kwa AMANI, na hivyo kuleta maafa makubwa ya mauaji ya watu wasio na hatia. Pamoja na ukatili huu, uovu hauwezi kudumu katika umilele. Wale wote wauteteao na kuulinda uovu ujichosha kure. Hivyo, Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure,” Zab 127:1 

Wapendwa wana wa Mungu Kristo kama Mwanga wa limwengu, uwepo wake ni vita dhidi ya giza na uovu wote. Hili ndilo alisemalo Mwinjili Yohane, Yoh 1:9, 8:12. Wakristo, yaani wafuasi wa Kristo, ni washiriki wa mwanga huu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:14. Wakristo ni mwanga unaoangaza duniani, unaojionyesha katika maisha ya Mkristo kupitia Makuu ya Mungu, katika unyenyekevu na kuusifu utukufu wa Mungu Baba aliye mbinguni. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni,” Mt 5:16. Mwanga huu wa utukufu wa Mungu hujidhihirisha katika miale ya UPENDO. Katika miale hii ya upendo kwa Mungu na jirani ndiyo utambulisho wetu kwamba sisi tu wanafunzi wa Kristo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi,” Yoh 13:35. Ni kwa namna hii basi kama tukiwa na umoja sisi kwa sisi tutajenga umoja ndani na katika Kristo, ambao umoja huo ndiyo alama kubwa ya kukabili na kuubadilisha ulimwengu huu kwa kuushinda uovu kwa wema.  Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi,” Yoh 17:23

Wapendwa katika Kristo, umoja huu ndani na katika Kristo, na Kristo ndani ya Baba wa Munguni ndio unaotuwezesha kusafishwa dhambi zetu, kwa nguvu ya utakaso wa damu ya Kristo.  Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote,” 1Yoh 2:1b-2. Kama yeye anatujua hata idadi ya nywele zetu, Mt 10:30, hatuna cha kudanganya na kujihesabia haki kwamba tu wema. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu,” 1Yoh 1.8. Tiba yako na kupona yako kutoka majeruhi ya dhambi ni kuziungama dhambi zako zote bila kuficha. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote,” 1Yoh 1:9. Je! wataka tiba ya Upungufu wa Kinga Rohoni-“UKIRO.”? Basi ijongee sakramenti ya upatanisho pasipo shaka na ukutane na Baba wa HURUMA na MSAMAHA. Huu ni mwaka wa huruma ya Mungu. Twende basi tukajisalimisha kwa Jemedari wetu aliye Upendo, Huruma na Msamaha.

Tumsifu Yesu Kristo!


Ee Bwana, kwa ajili ya jina lako, Unisamehe uovu wangu, maana ni mwingi,” Zab 25:11

No hay comentarios:

Publicar un comentario