JUMATATU WIKI YA 3 YA MAJILIO-C
14/12/2015
Somo: Hes 24:2-7, 15-17a
Zab: 25:4-5ab, 6-7bc, 8-9
Injili: Mt 21:23-27
Nukuu:
“Namwona, lakini si
sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota
itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga
pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia,” Hes 24:17
“Ni kwa
amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii?” Mt 21:23b
“Yesu akajibu
akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia
ni kwa amri gani ninatenda haya,” Mt 21:24
“Ubatizo wa Yohana
ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Mt 21:25
“Wakamjibu Yesu
wakasema, Hatujui. Naye akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri gani
ninatenda haya,” Mt 21:27
TAFAKARI: “Ni kwa amri gani
unatenda mambo haya?”
Wapendwa
wana wa Mungu, Taifa la wana wa Israeli linaingiwa hofu juu ya Mfalme Balaki wa
Moabu. Balaamu akiwa amejawa na roho wa Mungu aliyaandaa maombi kuhusu
sintofahamu ile waliyokutana nayo jangwani. Mungu anampa maono naye
anayatafsiri kama ifuatavyo; “Namwona, lakini si
sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota
itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo
itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia,” Hes
24:17. Je, maono haya ni ashirio la kuja kwake Masiha, hasa Nyota hii kutoka
katika Yakobo?
Hakika nyota hiyo na yote yanayoambatana nayo ni ashirio la
kuja kwa Masiha, ambaye atawaweka huru wana wa Taifa hili teule la Mungu.
Utabiri huu unathibitishwa na Malaika Gabrieli alipompasha habari Bikira Maria na kusema, “Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake
utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu
atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa
hauna mwisho,” Lk 1:31-33. Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo, tunaona Malaika anazungumzia kazi ya yule atakaye
zaliwa na Bikikira Maria na kusema, “Naye atazaa mwana, nawe
utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi
zao,” Mt 1:21. Hivyo tendo hili ni mpango mahususi wa wokovu wa mwanadamu.
Hata
hivyo pamoja na tabiri zote hizi na uthibitisho wa kweli kwa neno kufanyika
Mwili na kukaa kwetu, bado Taifa hili
Teule hawakutaka kuachana na mitazama yao ya kibinadamu, wakabaki kushikilia
sheria za kibinadamu na tafsiri zao zilizokuwa na mwelekeo wa ubinadamu. Kwa maana hiyo, waliingiwa upofu
wa kiroho na kutokuona ishara zilizokuwa zinaufunua Umungu wa Yesu Kristo.
Hivyo Wayahudi, na hasa Wakuu wa Makuhani na wazee wanahoji mamlaka ya Yesu na
kumwambia, “Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri
hii?” Mt 21:23b. Yesu hakuhitaji mamlama
yoyote kutenda aliyoyatenda kwa sababu licha ya kuwa na hali ya ubinadamu, Yeye
ni Mungu pasipo shaka, Yoh 1:1-3.
Hivyo kwa kutambua udhaifu
wao, naye Yesu anawauliza swali, “Ubatizo wa Yohana
ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu?” Mt 21:25. Jibu lao liliwaweka katika mtego mkubwa kwa
sababu wakijibu ubatizo huo ulitoka mbinguni wataonekana hawana imani, hasa
kile alichokitabiri Yohani kuhusu Yesu. Na wakisema ulikoka mwa mwanadamu
waliogopa kwani watu wote waliujua utakatifu wa Yohani Mbatizaji. Kuepukana na
hoja hii ya msingi waliamua kusema hatujui ingawa ukweli waliujua. Naye Yesu
aliwaacha jinsi walivyo kwa sababu ujumbe ulifikia bara’bara. Pasipo shaka
yoyote, Wakuu wa Makuhani na Wazee wanahoji mamlaka ya Yesu kwa sababu
wanahofia nafasi zao na hasa maslahi yao kutokana sheria kandamizi
walizojitungia wenyewe, kutoka amri kumi za Mungu hadi kufikia sheria 613.
Uwepo wa Yesu na nguvu na mamlaka yake katika kufundisha na kutenda kuliwatia
hofu kubwa sana. Kitumbua chao kilianza kuingia mchanga!
Hivyo ndugu zangu, katika
Kristo tunawekwa huru, na yatupasa kutokunaswa katika kongwa la utumwa wa
dhambi. “Katika ungwana huo Kristo
alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la
utumwa,” Gal 5:1. Maisha mapya ndani ya Kristo na katika Kristo hayatulazimu
tena kuhofia au kuwajibika kwa sheria za kibinadamu. Tunawajibika kufanya yote
katika imani itendayo kazi kwa upendo. “Maana katika Kristo
Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa
upendo,” Gal 5:6. Kuyatumikia haya ni kujitia hofu pasipo sababu.
Yesu
Kristo hakuacha kukemea mambo haya yasiyo ya msingi kuhusu imani ya kweli.
Wayahudi nyakati za Yesu walionekana kufuata zaidi tafsiri ya torati kuliko
torati yenyewe. Tafsiri hii, yaani, TALMUD, ulikuwa ukweli wa Mungu
uliopotoshwa kwa maslahi ya kibinadamu. Mambo muhimu ya kuzingatia yalikuwa
kuhusu adili, rehema, na imani ya kweli. Yesu anatoa karipio kwa Waandishi na
Mafarisayo na kuwaambia, “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa
zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani,
adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine
msiyaache,” Mt 23:23. Sheria hizi ambazo kwa
kiasi kikubwa zilikuwa kandamizi zikiendana na utoaji wa sadaka ulionyambuliwa
kwa manufaa yao binafsi. Sheria hizi hazikuwa na mwelekeo wa uzima wa milele.
Ukweli ni kwamba, “kumpenda yeye (Mungu) kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na
kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima
za kuteketezwa na dhahibu zote pia,” Mk 12:33. Mtakatifu Agustino anasema,
‘kupenda kweli utafanya yote.’
Wapendwa katika Kristo, ni vyema tukatambua wajibu wetu na
mapaswa yetu ili tuweze kutumika vyema kadiri ya mpango wa Mungu. Mungu anakila
sababu na wewe ikiwa ni pamoja na maisha yako. Hivyo pigania cheo chako ambacho
ni UTAKATIFU wako. Bila huo huwezi kumwona Mungu.
Tusifu Yesu Kristo!
“Tafuteni kwa bidii
kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona
Bwana asipokuwa nao,” Ebr 12:14
No hay comentarios:
Publicar un comentario