JUMANNE, SIKU YA TANO YA OKTAVA YA NOELI
29/12/2015
Somo: 1Yoh 2:3-11
Zab: 95:1-2A, 2b-3, 5a-6
Injili: Lk 2: 22-35
Nukuu:
“Na katika hili twajua
ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake,” 1Yoh 2:3
“Yeye asemaye,
Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake,”
1Yoh 2:4
“Lakini yeye
alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli.
Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake,” 1Yoh 2:5
“Yeye asemaye ya kuwa
anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe,” 1Yoh 2:5
“Yeye asemaye kwamba
yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo gizani,” 1 Yoh 2:9
“Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo
torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama
ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba
ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk
2:22-23
“wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana,
Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24
“Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake
Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na
Roho Mtakatifu alikuwa juu yake,” Lk 2:25
“Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa
utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32
“Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama
yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli,
na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34
“Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe
mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35
TAFAKARI: “Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu
wako Israeli. Huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi.”
Wapendwa wana wa Mungu, kuishi katika Nuru ya kweli ni
kuishi katika KWELI na HAKI. Hii ndiyo mizania au kipimo halisi ndani na katika
Kristo. Mizania hii hutuongoza katika kuzishika amri zake kwa sababu tunajua
kweli juu ya amri hizo na sababu yake kuelekea umilele. Mizania hii hutupeleka
zaidi kwa Kristo, kwani tu huru katika kweli, Yoh 8:32. Na nuru hii ambayo
ndiyo uwepo wa Kristo ndani yetu, ni vita isiyo na kikomo dhidi ya giza.
Mkristo amfuataye Kristo Yesu katika kweli na haki ni mtangaza vita dhidi ya
mwanga na giza, wema na uovu. Mtihani mkubwa ambapo tunaopambana nao katika
hali hii ni pale ninapoishi upendo kati
yangu na Mungu, kati yangu na jirani, na kati yangu na Mazingira
yanayonizunguka. Hivyo huu ndio mwaliko wa kila mmoja wetu kwamba tu chumvi na
nuru katika ulimwengu huu; “Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika
itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na
watu. Ninyi
ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima,” Mt 5:13-14.
Wote wale walio chumvi na nuru katika ulimwengu huu kamwe Mungu hatovunja ahadi
na mategemeo yao.
Hivyo somo letu la kwanza na Injili, yanatutafakarisha juu
ya maisha ya nuru ambayo msingi wake ni kuishi katika kweli na haki. Kweli na
haki hutuongoza kuzishika amri za Mungu kwa uaminifu. “Na katika hili twajua
ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake,” 1Yoh 2:3. Asiyeishi katika
kweli na haki ni vigumu kumwelewa Kristo aliye Haki na kweli. Hakika tutakuwa
waongo wakubwa. Hivyo, “Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala
kweli haimo ndani yake,” 1Yoh 2:4. Kweli
na haki hutuongoza kwenye neno lake ambalo ndilo uzima. Huku ndiko kukamilika
ndani na katika Kristo Yesu. “Lakini yeye
alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli.
Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake,” 1Yoh 2:5.
Kukaa ndani na katika
Kristo ni ukomavu wa kiroho. Hatuendi kwake kwa shuruti wala kulazimishwa mara tunapoutambua ukweli na nafasi ya Kristo
ndani ya maisha yetu. Tunaenda kwake kwa hiari yetu kwa sababu tunajua yeye
ndiye kweli, njia na uzima, Yoh 14:6. Hivyo, “Yeye asemaye ya kuwa
anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe,” 1Yoh 2:5. Ukomavu wa wa Imani
ambao ni nuru chini ya msingi wa kweli na haki utuweka karibu sana na Kristo
Yesu. Hivyo kila tunayekutana naye twamwona Kristo ndani yake. Hivyo hatuwezi
kamwe kuishi katika chuki na yeyote yule kwa sababu twaishi katika nuru ya
kweli. “Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu yake, yumo
gizani,” 1 Yoh 2:9. Kuishi katika chuki yamaanisha kwamba bado hatujakutana na
Kristo na hivyo bado tu gizani.
Matumaini yetu ingawa kama binadamu hatujui ni
lini yatakuwa kweli, Mungu hawezi kuyasahau kwani twaishi kile tunachokiamini
katika kweli na haki. Injili ya leo inatupa mfano ulio hai wa yule aliyeishi
katika nuru ya kweli chini ya msingi wa kweli na haki. Huyu ndiye Simeoni.
Simeoni anakutana na nuru hii ya kweli na haki wakati Yesu anapotolewa hekaluni
kama ilivyo desturi ya Wayahudi kwa kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. “Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao,
kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama
ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba
ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk
2:22-23. Hata hivyo, kumkomboa huyu mzaliwa
wa kwanza kutoka hekaluni iliwapasa wazazi wake kumtolea Bwana sadaka kama
shukrani. “Wakatoe
na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya
njiwa wawili,” Lk 2:24. Sadaka hii inaonyesha umasikini wa Familia hii Takatifu
ya Yesu, Maria na Yosefu.
Ni katika tendo hili pale Hekaluni, Simeoni mtu wa kweli na
haki ahadi yake inatimizwa na Mungu. “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake
Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na
Roho Mtakatifu alikuwa juu yake,” Lk 2:25.
Yesu Kristo hapa ndiye nuru halisi na uhuru wa kweli wa wana wa Taifa la Mungu.
Kristo ndiye ile nuru aliyokuwa
ikisubiriwa, “Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu
wako Israeli,” Lk 2:32. Mungu anaifunua nuru
ya Yesu ndani ya moyo wa Simeoni naye anayaona makuu ndani ya Yesu: “Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama
yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli,
na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34. Kristo ndiye sababu ya kuanguka na
kuinuka wengi, kwa sababu ulimwenguni hapa ni vita dhidi ya mwanga ambaye ndiye
Kristo, na giza ambayo ndiye yule mwovu shetani. Watainuliwa wale
watakaoambatana na mwanga na wataangushwa wale waambatanao na giza, yaani yule
mwovu.
Katika vita hii Mama Bikira Maria hatakuwa salama katika
maana ya kufurahia tu uwepo wa mwanaye. Ni katika uchungu na kushiriki mateso
ya mwanaye nuru ya kweli na haki itafunuliwa ndani yake. Hivyo ni katika
msalaba ambao mwanaye anauendea ndipo utakapokuwepo utukufu wake. “Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako,
ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35. Kwenye Msalaba Mtakatifu na
wenye ushindi wa Bwana Yetu Yesu Kristo ndipo penye utukufu, kufunguliwa kwa
mioyo yetu kutoka utumwa wa dhambi, na kuuelekea uzima wa milele. Hivyo kwa
Mkristo na Mfuasi wa Kristo, hakuna UTUKUFU pasipo MSALABA.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo
hutamka hila. Nuru
ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika,” Mit 12:7, 13:9
No hay comentarios:
Publicar un comentario