JUMAPILI
YA 3 YA MAJILIO YA MWAKA C
13/12/2015
Somo
I: Sef 3:14-18a
Zab:
12:2-6
Somo
II: Flp 4:4-7
Injili: Lk 3:10-18
Nukuu:
“Imba, Ee binti Sayuni;
piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti
Yerusalemu,” Sef 3:14
“Bwana ameziondoa hukumu
zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati
yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15
“Katika siku ile
Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee,” Sef 3:16
“Bwana, Mungu wako, yu
katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza
katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3;17
“Furahini katika Bwana
sikuzote; tena nasema, Furahini,” Flp 4:4
“Upole wenu na ujulikane na watu wote.
Bwana yu karibu,” Flp 4:5
“Msijisumbue kwa neno lo lote; bali
katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na
zijulikane na Mungu,” Flp 4:6
“Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote,
itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu,” Flp 4:7
“Akawajibu akiwaambia,
Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo
hivyo,” Lk 3:11
“Akawaambia, Msitoze
kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa,” Lk 3:13
“Akawaambia,
Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu,” Lk
3:14b
“Yohana alijibu
akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu
kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye
atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto,” Lk 3:16
“ambaye pepeo lake li
mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani
mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika,” Lk 3:17
TAFAKARI:
“Tufanye nini basi?”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya tatu ya majilio ya mwaka “C”
wa Kanisa. Dominika hii hujulikana kama dominika ya furaha. Masomo yetu yote
hasa somo la kwanza na la pili yanafunua furaha na ujumbe wa Mungu kwetu kuhusu
yule tunayemtarajia kuja, yaani mwokozi wetu. Pamoja na hayo yote, leo Mama
Kanisa anatualika kuwa tayari kila mmoja wetu kujua ni nini cha kufanya ili
ajapo Masiha wetu atukute tupo tayari. Moja ya hatua muhimu za kuchukua ni
kuachana na mazoea yetu. Nabii Isaya anatuwasa tuachane na ibada zisizomfuraisha
Mungu. Yeye, yaani Mungu, ni maminifu tunapokuwa tayari kutembea naye katika
kweli na haki. Kila mmoja wetu yampasa kujitakasa na kuacha kutenda mabaya, Isa
1:16. Mungu aliye upendo na huruma yupo tayari kuanza upya nasi na kusahau yote
yaliyopita, ila kwa sharti ya kuongoka kweli. “Jifunzeni
kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima
haki yake; mteteeni mjane. “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu
zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu
kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:17-18
Bila shaka kila mmoja
wetu anajua yaliyoko ndani ya moyo wake, na wapi anatakiwa kufanya mabadiliko.
Ni vizuri ukatumia muda huu kujitazama kile ulicho ndani ya moyo wako. Kile ambacho
hatupo tayari kukisema au kukisimulia ndicho kile tulicho. Mahubiri ya Yohani
Mbatizaji wanaibua hisia za ndani za wale waliomsikiliza. Wote kwa pamoja
wanamuuliza wafanye nini? Naye anawajibu kwa kusema, “Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye
vyakula na afanye vivyo hivyo,” Lk 3:11. Kumbe wajibu wa kwanza katika safari
hii ya utakaso ni kutambua mahitaji ya wengine. Matendo yetu kama kielelezo cha
wongofu wetu yalenge katika upendo kwa jirani. Mkristo asiyeona uchungu na
mateso ya mkristo mwenzake huyu bado hajamjua Kristo anayemwamini na Mungu
anayemwabudu na kumtumikia. Kati yetu wapo wanaokula na kusaza na kesho yake
kumwaga vyakula hivyo kwenye majalala wakati jirani yake anayesali naye jumuiya
moja hana chakula.
Wapendwa katika Kristo, kila mmoja wetu yampasa kuwajibika
vyema pale alipo. Tumeumbwa ili tuwajibike kila mmoja kadiri ya wito na nafasi
ya kile alicho mbele ya jamii inayomzunguka. Wajibu huu unatuwajibisa kutenda
mema na kuchukia mabaya kama anavyotuasa Nabii Amosi na kusema, “Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi;
hivyo Bwana, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo. Yachukieni mabaya; yapendeni mema;
mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba Bwana, Mungu wa majeshi,
atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu,” Amo 5:14-15. Mfano halisi wa nini cha kufanya tunao katika
Injili ya leo ambapo watoza ushuru wanataka kujua mapaswa yao ili wawe mkono
salama wa Mungu. Naye Yohane Mbatizaji anawajibu kwa kusema, “Msitoze kitu
zaidi kuliko mlivyoamriwa,” Lk 3:13. Hapa tunaonywa kuhusu tamaa ya
kujilimbikizia mali kusiko halali na kutowajali masikini. Leo tunapolitazama
Taifa letu la Tanzania, wapo baadhi yetu wanaishi maisha ya anasa kupindukia,
ilhali wapo wengi ambao maisha yao niyadhiki sana. Ukweli ni kwamba, “ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na
furaha katika Roho Mtakatifu,” Rum 14:17
Wapendwa katika Kristo, si jambo la kushangaza leo
tunapoona wengi wetu waliopewa dhamani na umma wamekuwa mstari wa mbele
kufinyanga haki za wanyonge. Ndugu yangu, nafasi uliyo nayo siyo nafasi ya
kujijenga nafsi yako na kusahau wale waliokupa dhamana. Yakupasa “kutumika”
kwanza na siyo kutumikiwa. Pili, yakupasa “kujitoa” kwa ajili ya wengine.
Yeyote yule anaye wajibika na kujito kwa wengine yupo mikono salama ya Kristo,
na kwake itathibitika “kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika,
na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mt 20:28
Kama ilivyokuwa kwa watoza ushuru ndivyo ilivyokuwa kwa
maaskari. Nao wanamuuliza Yohane Mbatiza nini cha kufanya ili wawe mkono
salama. Yohana Mbatizaji
anawajibu, “Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na
mshahara wenu,” Lk 3:14b. Je, hali lep ipo vipi kwa baadhi ya Maaskari wetu?
Wanatenda haki kweli kwa mujibu wa sheria? Licha ya kwamba hatuwezi
kuwajumuisha wote katika ubaya, ila kwa kiasi kikubwa askari wetu hawatendi
haki kwa raia wao. Wakati mwingine askari wetu wanalazimika kufanya hivyo si
kwa matakwa na utashi wao, bali kwa matakwa ya wakubwa wao. Bado tunaishi
katika siasa za kiimla na kibwana. Baadhi ya wale walio madarakani wanafanya
mahali hapo kama umilele wao. Baadhi ya watawala wetu leo hawapo tayari kuachia
nafasi zao hata pale wanapotakiwa kufanya hivyo wa utaratibu ulio wazi na
wakikatiba. Viongozi hawa wapo tayari kupindisha Katiba kama mwongozo mama, na
kuwatumia askari wetu na vyombo vya usalama kama kukidhi malengo yao. Ila tujue
kwamba mwisho wa siku, “Kadiri ya matendo yao, kwa kadiri iyo hiyo atawalipa, ukali
kwao wampingao, malipo kwa adui zake,” Isa 59:18a
Vyombo hivi badala ya kuwa usalama wa watu na mali zao,
vimekuwa vyombo vya dhuluma na uvunjifu wa haki za raia zao kwa kutimiza
matakwa maovu ya wakubwa wao. Hakika Mungu atasimama katika kweli na haki, na
hata vumilia milele uovu huu. Kwa kila mwenye hofu ya Mungu, wongofu siyo tu
kuacha dhambi kwa kuzitubu, ila kuwa tayari kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu
na kuongozwa naye. “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila
mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea
kipawa cha Roho Mtakatifu,” Mdo 2:38. Tendo hili la kutubu kwa mwono huu
linaturejesha kwenye asili ya kuumbwa kwetu, yaani, kwa sura na mfano wa Mungu,
Mwa 1:27, kuliko fifishwa na dhambi zetu. Tendo hili pia lina tupatia nyakati
za kuburudishwa kwa uwepo wa Kristo tunaye mtumainia. Hivyo wapendwa katika Kristo,
“Tubuni basi, mrejee,
ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake
Bwana,” Mdo 3:19.
Wapendwa wana wa Mungu, Masiha huyu tunayemsubiri siye
Yohane Mbatizaji, ambaye kazi yake ilikuwa kuandaa njia tu. Yohane Mbatizaji
anaweka kweli hii juu ya Masiha wetu na kusema, “mimi nawabatiza kwa maji;
lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza
gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto,” Lk
3:16. Huyu ndiye Masiha tunaye mngoja. “Basi hii furaha yangu
imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua,” Yoh 3:30. Yatupasa
kupungu katika majivuno yetu, dharau zetu, kujigamba kwetu, kujua kwetu,
umaarufu wetu, ili yeye aongezeke. Masiha wetu ndiye kila kitu kwetu, yaani
ndiye njia, kweli, na uzima, Yoh 14:6.
Tunapojitafiti
ni nini cha kufanya ili kuwa mikono salama ya Masiha wetu, yatupasa kuufahamu
ukweli huu kwamba huyu tunayemngoja ni hukumu katika utimilifu wake. Ni hukumu
katika maana ya kwamba ni “ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana
uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa
moto usiozimika,” Lk 3:17. Kwake hakuna rushwa wala ufisadi na wala haongeki.
Kila mtu atalipwa kadiri ya matendo yake. Hivyo ni vyema kuishi na tenda mema
ili kuepuka karaha zisizo na tija siku ya kuja kwake.
Pamoja na mapaswa hayo ikiwa ni pamoja na maandalizi ya
ujio wake, tendo la ujio wake ni furaha kubwa sana kwetu. Ni furaha kwa sababu
Mungu amekisikia kilio chetu na kuthibitisha kwamba, Yeye ndiye Mungu na wala
hakuna kama yeye. Nabii Sefania nauthibitisha ukuu huu wa Mungu kwa kusema, “Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui
yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu
tena,” Sef 3:15. Hii ndiyo furaha ambayo kila kwenye kuishi kwa hofu ya Mungu
na kutenda haki yampasa kuifurahia. Hivyo, “Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli;
Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu,” Sef 3:14.
Furaha hizi zitakuwa na maana kwetu kama tunatambua vyema wajibu wetu kwa
Mungu, jirani, na mazingira yanayotuzunguka. Mambo haya yakiwa sawa bila
ukinzani, hofu juu ya kuja kwake Masiha hutoweka na kubaki na furaha. Hatuna
sababu ya kuogopa ujio wake kwetu. “Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni;
mikono yako isilegee,” Sef 3:16. Je, ni nini
kinachokutia hofu kwa ujio wa Masiha? Kama kipo basi ni wakati wa kukitafutia
tiba. Wakati ndio sasa!
Tunaposimama
katika kweli na haki Mungu wetu husimama nasi hata pale panapoonekana
hapawezekani. Kanisa la mwanzo lilitesaka katika kweli na haki, na wakati huo
huo walionya furaha katika mateso. “Nao wakatoka katika
ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa
ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:41. Silaha kubwa ya kuushinda uovu ni kujenga tabia ya
kutenda mema. Mungu hutuinua kwa kuushinda uovu kwa wema na si vinginevyo.
Nabii Sefania anatuambia, “Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa;
Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa
kuimba,” Sef 3;17. Kumbe kutambulika kwetu kuwe kwa matendo mema na wema kwa
wote. Hii ndiyo nuru kwa kila mwenye hofu ya Mungu.
Nabii Isaya anaelezea nuru hii kwa kusema, “Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona
utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana,” Isa
62:2. Bwana uthibitisha ukaribu wake kwetu pale
tunapoishi kwa amani na wengine. Mungu ndiye atakayeigeuza uzuni yetu kuwa
furaha hata pale ulimwengu utakapo furahia mateso yetu yatokanayo na kutenda
mema. Naye Yesu anasema, “Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali
ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa
furaha,” Yoh 20:20. Bwana ndiye mfalme wa Amani,
Upendo, Haki, na Msamaha. Ni kwa maana hiyo kwamba, “Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu,” Flp 4:5. Huku ndiko kuishi ndani na katika Kristo. “Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya
kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya, 2Kor 5:17. Zaidi ya hayo ni kudumu katika sala na kuomba. Maombi yetu
yatakuwa na uzito kwa sababu tunajua ni nani tunayemtumikia na kumfuata. Hivyo,
“Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali
na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu,” Flp 4:6. Je, ndugu yangu katika maisha yako nini
kinachochukua muda wako mwingi?
Kudumu
katika kweli kadiri ya maelekezo ya Mungu kutatupasa uvumilivu na sadaka kubwa.
Mungu wetu hana haraka, ila anatutaka tudumu katika amani ya kweli na kukua
kila siku katika kweli na haki. Utulivu wa kweli ndani na katika Kristo, ndicho
kielelezo cha amani ya kweli katika utimilifu wa umilele wa Mungu. Maisha ya
Kristo ndiyo kielelezo sahihi kwetu. Ni mfano ulio hai kwetu na ndiyo jibu
sahihi kwa hiki ambacho bado hakijajifua kwetu katika ukamilifu wake. Pamoja na
sintofahamu nyingi katika maisha yetu, Kristo bado ndio mlango sahihi wa pitia.
Hivyo ndugu zangu katika Kristo, “amani ya Mungu,
ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu,”
Flp 4:7. Kristo ndiye mlango sahihi wa
kupita kwa sababu hata katika majaribu yetu hutupatia mlango wa kutokea. “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu;
ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini
pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,”
1Kor 10:13. Je, wataka kujua zaidi
kuhusu nini cha kufanya? Zama ndani ya nafsi yako na ongea juu ya yale ambayo
umekuwa ukiyaficha maisha yako yote. Hapo ndipo penye uhai wako, na ndicho
ulicho. Kupekua na kufika kwenye kilindi hiki cha nafsi kunahitaji ujarisi. Huu
ndio ujasiri na furaha anaouzungumzia Mtume Paulo kwa Wakorintho na kusema, “Ninao ujasiri mwingi kwenu; naona fahari kuu
juu yenu. Nimejaa faraja, katika dhiki yetu yote nimejaa furaha ya kupita
kiasi,” 2Kor 7:4. Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii,
usipopagusa pale usipotaka kupagusa kwa kuogopa, huwezi kuwa na furaha ya
kweli, kwa sababu bado hujajitambua kile ulicho. Bado umejivika kinyago na
kuukataa ukweli ambao ndio wewe mwenyewe.
Jumuiya ya Bikira Maria Mama wa Faraja ni moja ya Jumuiya
katika Parokia ya Huruma ya Mungu. Jumuiya hii imebarikiwa kwa kuwa na familiya
nyingi zenye uwezo, na mara kwa mara jumuiya hii huwa ya kwanza katika
majitoleo yao kiparokia. Familia ya Mzee Misalaba ni moja ya familia kumi na
mbili katika jumuiya hii ya Bikira Maria Mama wa Faraja.
Familia ya Mzee Misalaba ni familia yenye watoto nane. Ni
familia iliyo masikini kuliko familia zote za jumuiya hii ya Bikira Maria Mama
wa Faraja, na Parokia kwa ujumla wake. Watoto wawili wa mwisho wa Mzee Misalaba, yaani Mateso na Fikiri mara
kwa mara huonekana wakiwa nje ya nyumba yao mapema sana asubuhi kabla hata
majirani zao kuamka.
Ukweli ni kwamba sio hupenda kudamka mapema hivyo, bali usiku
kwao ni safari ndefu sana. Hulalia mikeka na kujifunika vipande vya kanga na
maboksi. Hivyo mara waonapo mwanga kupitia matundi ya kuta za nyumba yao
hujilazimu kutoka nje. Tatizo ni pale kunapokuwa na mbalamwezi nje. Huamka na
kurudi tena ndani na kuendea na safari yao ndefu. Jambo la pili linalowafanya
watoke nje mapema ni uwepo wa shimo la kutupia takataka na mabaki ya vyakula
kuto mmoja ya nyumba ya jirani yao ambaye ni tajiri wa kupindukia.
Hivyo Mateso na Fikiri huwa hawachezi mbali na shimo hili
kwani wakati mwingine mikate na vipande vya nyama na samaki hutupwa ndani mwa
shimo hili vingali bado havijaharibika. Siku mmoja mapema asubuhi, mfanyakazi
wa ndani wa nyumba ya huyu tajiri alimwaga vipande vya samaki kwenye shimo
hili. Mara alitokea Mbwa ambaye alianza kuvishambulia huku mfanyakazi huyu wa
ndani akiwa anamwangalia. Kitendo hiki kiliwahuzunisha sana Mateso na Fikiri
kwa sababu walijua hawana chao kwa siku ile.
Mbwa yule akiwa amebakiza vipande vitatu kumaliza, mfanyakazi
yule wa ndani aliondoka. Hapa ndipo hasira ya watoto wale ilipowaka juu ya mbwa
yule. Mateso akiwa na fimbo kubwa baada ya kuuvunja mti uliokua jirani yake, na
Fikiri akiwa na mawe, walimkimbiza mbwa yule na kumpiga bila huruma. Mbwa
alizidiwa nguvu na kuanguka chini huku akitapika vipande vile vya samaki
alivyokula. Na hapa ndipo ulipofika mwisho wa maisha ya yule Mbwa.
Wapendwa wana wa Mungu, kwa ujumla mbwa hakuwa na makosa hata
kidogo. Kungalikuwa na upendo wa kweli wa kuwajibika na kuwa tayari kujitoa kwa
ajili ya wengine, amani ingekuwa kwa wote, yaani familia ya Mzee Misalaba na
majirani zake matajiri, na kwa viumbe kama mbwa yule. Tunapokosa kuishi upendo
wa kweli hatuubomoi tu uhusiano kati yetu na jirani zena na Mungu, bali
tunaubomoa uhusiano huo na viumbe vingine visivyo na utashi kama mbwa.
Kama hiyo haitoshi, tunaharibu pia mazingira yanayotuzunguka.
Mfano, Mateso kuchukua fimbo kubwa ilimpasa kuuvunja mti ule ambao ulihitaji
kukua kadiri ya makusudi yake na asili yake. Fikiri kuchukua mawe na kumponda
Mbwa yule kulisababisha mtikisiko na mmomonyoko wa udongo pale jiwe lile
lilipochukuliwa na lilipotua baada ya kurushwa.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na
mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22
No hay comentarios:
Publicar un comentario