ALHAMISI WIKI YA 3 YA MAJILIO-C
17/12/2015
Somo: Mwa 49:2, 8-10
Zab: 72:1-4ab, 7-8, 17
Injili: Mt 1: 1-17
Nukuu:
“Kusanyikeni, msikie, enyi wana wa Yakobo, Msikilizeni
Israeli, baba yenu,” Mwa 49:2
“Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria
kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa
watamtii,” Mwa 49:10
“Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana
wa Ibrahimu,” Mt 1:1
“Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU
aitwaye Kristo,” Mt 1:16
“Basi vizazi vyote tangu Ibrahimu hata Daudi ni vizazi
kumi na vinne; na tangu Daudi hata ule uhamisho wa Babeli ni vizazi kumi na
vinne; na tangu ule uhamisho wa Babeli hata Kristo ni vizazi kumi na vinne,” Mt
1:17
TAFAKARI: “Hata
atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”
Wapendwa wana wa Mungu, tu karibu kupokea tunda la haki na
Bwana mwenye milki, Masiha wetu na Mkombozi wetu. Huu ni wakati wa kusikiliza
kwa makini habari zake, siyo zile tu zitokazo nje, bali zile zitokazo ndani ya
mioyo yetu. Swali ni hili: Je, ajapo Masiha huyu atapata nafasi ndani ya moyo
wangu? Kama nafasi ipo, Je, nimejiandaa vizuri? Tusisahau kwamba Masiha huyu
ndiye mwenye milki yote, na hakuna chochote kile katika uwepo wake ambacho
hakikufanyika kupitia yeye. Mwinjili Yohane anasema, “Vyote vilifanyika kwa
huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Je,
ninakilicho changu? Kama kipo ni nini zaidi ya dhambi zangu?
Bila
shaka ili Mwokozi wetu akija akute nafasi ndani ya moyo wangu, sina budi kutoa
kile kilicho changu, yaani, dhambi zangu ili Mwokozi apate nafasi ndani yangu.
Atakapo kuja hata ondoka ikiwa nitampa nafasi. Mwokozi huyu anachohitaji
kingine kutoka kwangu ni utii. Utii huu kielelezo sahihi cha kuyapokea mapenzi
yake kwa sababu yeye ni UTII. “Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria
kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa
watamtii,” Mwa 49:10. Utii huu ndiyo siri ya Kristo na mafanikio yake ya
kuupokea msalaba na kukubali kuwambwa juu yake kwa hiari yake. “Tena, alipoonekana
ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya
msalaba,” Flp 2:8
Wapendwa wana wa Mungu, ili Mwokozi wetu alipate umbo hili
la mwanadamu, atamwilishwa na kuzaliwa kama sisi tulivyo na kuwa na asili kama
sisi tulivyo, yaani kutoka kwenye familia, koo, kabila, na taifa. “Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo
alikuwako kwa Mungu. Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu
wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh
1:1-2, 14.
Ndiyo “Alifanyika mwili, akakaa kwetu:”-hapa ndipo alipochukua
hali yetu ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na mazingira yetu isipokuwa hakutenda dhambi.
“Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake,”
1Pet 2:22. Hata hivyo anakubali kuzaliwa katika hali na mifumo ya kwetu katika
asili zetu. Hivi ndivyo ilivyokuwa, “Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana
wa Ibrahimu. Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye
Kristo,” Mt 1:1, 16. Historia ya familia ya Yesu, Ukoo, Kabila na Taifa,
unaufunua mpango mzima wa Mungu katika historia hii ya wokovu wetu.
Wapendwa wana wa Mungu, hakuna hata mmoja wetu aliyechakugua kuzaliwa
katika familia hiyo aliyopo. Hii ni pamoja na ukoo wake, kabila lake na Taifa
lake. Yote ni mapenzi na mpango wa Mungu. Tusema vipi basi pale tunapowaona
baadhi yetu wakizisifia familia zao, koo zao, makabila yao na Mataifa yao? Hivi
kweli kuna sababu yoyote ile ya kujisifia? Jibu ni HAPANA! Basi kama ni
kujisifu, Yesu angekuwa wa kwanza
kufanya hivyo. Lakini Yesu, “ambaye yeye mwanzo
alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu
cha kushikamana nacho; bali
alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa
wanadamu,” Flp 2:6-7
Wapendwa katika Kristo, kwa tendo la Neno kufanyika mwili na
kukaa kwetu akichukua hali yetu ya kibinadamu na mazingira yetu, ni heshima
kubwa sana kwetu. Pili, Mwokozi huyu anatufundisha unyenyekevu uliotukuka. Nasi
tujifunze kwa mwalimu wetu Yesu Kristo kwani kwake kuna ufahamu wote.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Msitende neno lo lote
kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe
kuwa bora kuliko nafsi yake,” Flp 2:3
No hay comentarios:
Publicar un comentario