JUMATATU WIKI YA 2 YA MAJILIO-C
7/12/2015
Somo: Isa 35:1-10
Zab: 85:9ab, 10-14
Injili: Lk 5:17-26
Nukuu:
“Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia
na kuchanua maua kama waridi,” Isa 35:1
“Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni
wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko
na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia,” Isa 35:10
“Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki,
umesamehewa dhambi zako,” Lk 5:20
“Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri
duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia,
Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako,” Lk 5:24
TAFAKARI: “Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi.”
Wapendwa wana wa Mungu, jana Dominika ya pili ya Majilio
tulitafakari kwa undani maneno haya ya Yohani Mbatizaji, “Na wote wenye mwili watauona wokovu wa
Mungu.” Maneno haya ya Yesu yanathibitisha ubinadamu wetu na uhitaji wetu wa
kuutafuta ukamilifu kila siku kwa msaada wa Mungu. Kwa maana nyingine maneno
hayo yanasema kuhusu udhaifu wetu kama wanadamu. Ni Mungu tu aliye makamifu, na
wito wake kwetu ni kuwa mkamilifu kama yeye. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama
Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48
Basi tukijua si wakamilifu hatuwezi kukwepa huruma ya Mungu
ikiwa ni pamoja na msamaha wake pale tunapodondoka katika udhaifu wetu. Mungu
peke yake ndiye mwenye kusamehe dhambi na kutuweka huru. Mwana wa Adamu-Neno
aliyefanyika mwili, “Neno Mwilishwa,” anayo amri duniani ya kusamehe dhambi. “Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; Kwa
kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema,” Yoh
1:1, 14a, 16. Ukweli huu Wayahudi hawakuupokea kabisa kama ilivyo kwa baadhi
yetu leo.
Leo
katika Injili tunaona baadhi ya watu walivyokuwa na Imani juu ya Yesu na
wengine wakiwepo Mafarisayo na Waandishi wakimbeza kwa kile anachofundisha na
kutenda. Hata hivyo Yesu anastaajabia Imani ya watu hasa pale ilipobidi
kulitoboa dari ya nyumba na kumwingiza mgonjwa ili apate kuponywa kwani
hapakuwa na nafasi ya kumpitisha. “Naye alipoiona imani yao, alimwambia, Ee rafiki,
umesamehewa dhambi zako,” Lk 5:20. Maneno
haya na tendo hili yanazua zogo kubwa katika ya Yesu, Mafarisayo na Walimu wa
torati. Zogo hili linazuka kwa sababu ya mitazamo waliyokuwa nayo Wayahudi juu
ya Masiha waliokuwa wakimsubiri, ikiwa ni pamoja na namna ya kufanya na kutenda
Masiha huyo. Kwa ujumla walikuwa na mashaka na Yesu. Walimtazamia Masiha ambaye
angewatoa na kuwaweka huru kutoka kwenye dola ya Kirumi. Masiha huyo
walimtegemea labda angeshughulikia sana mambo ya kisiasa na kifalme katika
maana kiutawala. Kumbe yote yalikuwa kinyume.
Yesu
kabla ya kifo chake anauweka ukweli huu mbele ya Pilato alipomuuliza kama Yeye
ni Mfalme wa Wayahudi, Yoh 18:33. “Yesu
akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa
ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa
Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa,” Yoh 18:36. Yesu hakujihusisha na
mambo ya leo na kesho. Alikuja ili tuupate uzima wa Milele na hilo ndilo lengo
la kuumbwa kwetu. Duniani hapa tunajiandaa kwa ajili ya uzima huo wa milele.
Naye Yesu anasema, “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi,
ajapokufa, atakuwa anaishi,” Yoh 11:25. Nasi kama wafuasi wa Kristo, mambo ya
leo na kesho yasitupotezee muda wetu na kuukosa uzima wa milele.
Leo Yesu
anaudhihirisha Umungu wake bila kupepesa Macho. Ni mtu mwenye kiburi tu
itamgharibu kuelewa ukweli huu. Naye Yesu anasema, “Lakini, mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri
duniani ya kusamehe dhambi, (alimwambia yule mwenye kupooza). Nakuambia,
Ondoka, ujitwike kitanda chako, ukaende zako nyumbani kwako,” Lk 5:24. Mamlaka
haya Yesu aliyakabidhi kwa mitume wake kabla ya kupaa kwenda mbinguni. “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho
Mtakatifu. Wo
wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi,
wamefungiwa,” Yoh 20:22-23. Kanisa limeratibu ukweli huu Kiimani na
Kisakramenti-“Sakramenti ya upatanishi/kitubio” tangu nyakati hizo na kubaki hata leo katika Kanisa Katoliki.
Hivyo wapendwa wana wa Mungu, tusione haya kwenda
kuziungama dhambi zetu. Mama Kanisa yupo muda na wakati wowote kutupokea kwa
huruma na upendo kupitia Sakramenti hii ya upatanisho. Ni wakati wa
kupatanishwa na upendo wa Mungu Baba ambaye yupo tayari kutukomboa kutoka
utumwa wa dhambi. Ni huyu tumsubiriaje ambaye, “Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia
na kuchanua maua kama waridi,” Isa 35:1. Anakuja kuuleta uzima pale
palipodhoofu, na furaha palipo na ukiwa. “Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni
wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko
na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia,” Isa 35:10. Ndugu yangu uliyesafiri
nami katika tafakari hii usiziache neema zikupite bure. Nenda kapatanishwe na
Mungu aliye hai.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na uzima wa milele
ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma,”
Yoh 17:3
No hay comentarios:
Publicar un comentario