JUMAMOSI WIKI YA 2 YA MAJILIO-C
11/12/2015
Somo: YbS 48:1-4, 9-11
Zab: 79, 2ac, 3b, 15-16, 18-19
Injili: Mt 17:10-13
Nukuu:
Bila shaka
wamebarikiwa wale waliokuona kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa,
kwa maana unaishi,” YbS 48:11
“Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya
yuaja kwanza, naye atatengeneza yote,” Mt
17:11
“ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha
kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa
Adamu naye yuaenda kuteswa kwao,” Mt 17:12
TAFAKARI: “Wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana
unaishi.”
Wapendwa wana wa
Mungu, kuuishi ushuhuda katika maisha si kitu cha ajabu. Kuishi ushuhuda ni kuguswa na habari fulani
katika maisha, na habari hiyo ikawa kielelezo na dira ya maisha ya mtu.
Ushuhuda huu waweza kuwa mvuto wa maisha ya mtu yaliyojaa maadili mazuri na
roho ya upendo wa ajabu. Mvuto huu ukawa kioo cha kujitazama na kuwa kielelezo
cha maisha. Ushuhuda waweza kuwa wosia anaotoa mtu uliojaa hekima na busara kwa
wale anaowaacha. Hivyo watu wakavutwa na kuishi wosia huo kama kielelezo cha
maisha.
Mungu katika safari ya wokovu wa mwanadamu alitumia watu
mbalimbali kujifunua kwake na kuacha jumbe mbalimbali kama kielelezo katika
maisha. Watu hawa walikuwa: Waamuzi, Manabii, Wafalme, na Mwishoni kabisa Neno
aliyemwilishwa na kukaa kwetu. Kumbe baraka na neema ziliwafikia waja wa Mungu
kwa kupitia watu mbalimbali. Lakini pamoja na neema na baraka hizo,
kinachokaziwa hapa ni mwendelezo wa ile roho iliyoachwa na wale wapeleka
ujumbe. Kuishi kwa ile roho katika mioyo ya watu ni kuzuri zaidi kwa sababu ni
kuishi katika uzima wa Mungu. Hivyo, “Bila shaka wamebarikiwa wale waliokuona
kwa macho, wakafa; lakini wewe umezidi kubarikiwa, kwa maana unaishi,” YbS
48:11
Wanafunzi wa Yesu wanamuuliza Yesu katika Injili ya leo, “kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?”
Msingi wa swali hili unajijenga katika mwono wa Yesu ulivyo kwa jamii ile
iliyomzunguka. Bila shaka kulikuwa na mfanano mkubwa sana kati ya Yesu na
Manabii waliomtangulia ikiwa ni pamoja na Nabii Isaya. Naye Yesu anawajibu
wanafunzi wake, “Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote,” Mt 17:11. Bila shaka hapa Yesu anamzungumzia
Yohane Mbatizaji kwani ndiye aliyeitoboa siri ya Masiha, yaani, Yesu Kristo
kadiri ya utabiri wa Nabii Isaya. “Kwa sababu huyo ndiye
aliyenenwa na nabii Isaya, akisema, Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni
njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake,” Mt 3:3. Watu waliishi roho hii na
matumaini haya ingawa hawakujua ni lini itakuwa kweli.
Kwa
kuufafanua ukweli huu, Yesu anaenda mbali zaidi na kusema, “ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue,
lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda
kuteswa kwao,” Mt 17:12. Huyu waliyemtenda kama walivyotaka ni Yohani Mbatizaji
ambaye alikatwa kichwa siku ya sherehe ya ukumbusho wa kuzaliwa Herode. Mauti
yanamfika Yohane Mbatizaji kwa kusimamia kweli na haki. Yohane Mbatizaji
alimkemea Mfalme Herode kwa tendo baya la kumchukua mke wa ndugu yake Filipo. “Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata
Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa
kuwa amemwoa; kwa sababu
Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo,” Mk
6:17-18.
Kifo cha
Yohane Mbatizaji kinaashiria pia kifo cha Yesu Kristo. Yesu analiona hilo
katika maisha yake. Kwetu ni ushuhuda wa maisha kwamba tunaposimama katika
kweli na haki, maisha hayo yatatugharimu. Hata kama tutakufa kwa kuishi
ushuhuda huu, tutaishi na Kristo milele kwa sababu Yeye ndiyo kielelezo halisi
cha maisha yetu. Huyu ndiye Masiha tunayemsubiri. Tunapomsubiri Masiha wetu kwa
hamasa hii kumbwa na matumaini, yatupasa pia kutambua mapaswa yetu katika
ufuasi wake.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Na kila mwenye
matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh 3:3
No hay comentarios:
Publicar un comentario