viernes, 4 de diciembre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 1 YA MAJILIO-C

JUMAMOSI WIKI YA 1 YA MAJILIO
5/12/2015
Somo: Isa 30:19-21, 23-26
Zab: 147:1-6
Injili: Mt 9:35-10:1, 6-8
Nukuu:
Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako,” Isa 30:20 

Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao,” Isa 30:26

Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake,” Mt 9:37-38

Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina,” Mt 9:1

Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 9:7

Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 9:8 

TAFAKARI: “Ufalme wa mbinguni umekaribia.”

Wapendwa wana wa Mungu, kauli mbiu hii “Ufalme wa mbinguni umekaribia,” inatualika kujiandaa kimwili na kiroho. Maandalizi haya yatuguse na kuona umuhimu wa kufanya hivyo. Wakati mwingine tunajisahau sana na kuishi bila mwelekeo wowote hasa kiroho. Ufalme wa mbinguni kwanza ni mwito binafsi kwa sababu hatujui siku wala saa. Hivyo ni mwaliko kwa kila mmoja binafsi, na pili wote kwa ujumla. Hiki ndicho Yesu anachowataka wafuasi wake wakifanye. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia,” Mt 9:7. Ufalme huu wa mbinguni uliokaribu unajidhihirisha kwa matendo makuu ya Mungu ya upendo na huruma yake. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure,” Mt 9:8. Matendo haya ya huruma na upendo yaanze hapo ulipo kwa kila kadiri ya nafasi yako na wito wako.

Ufalme wa mbinguni ambao tunausubiria ni hali ile ya kuanza upya vyote na Mungu. Kuanza huku upya na Mungu tunatudai kujiandaa vyema mwili na roho. Huku ndiko kutakakotupelekea kuponywa majeraha yetu. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao,” Isa 30:26.

Wapendwa wana wa Mungu, tutumie vizuri muda huu kujiweka vyema mwili na roho ili ufalme huo utakapofika tuwe tayari kuupokea. Chambua mahusiano yako na Mungu, jirani, na mazingira yako ya kila siku. Je, katika mahusiano hayo ni wapi palipokosa afya? Nenda kwa tabibu ili upate tiba stahiki. Sakramenti ya upatanisho inatuwezesha kuyarejesha mahusiano yetu na Mungu, Jirani, na mazingira yetu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Basi zaeni matunda yapasayo toba,” Mt 3:8

No hay comentarios:

Publicar un comentario