ALHAMISI WIKI YA 1 YA MAJILIO
3/12/2015
Somo: Isa 26:1-6
Zab: 118:1, 8-9, 19-21, 25-27a
Injili: Mt 7:21, 24-27
Nukuu:
“Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea
Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini,” Isa 26:3
“Mtumainini Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa
milele,” Isa 26:4
“Kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha,
Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini,” Isa 26:5
“Si kila mtu
aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye
afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21
“Basi kila asikiaye
hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga
nyumba yake juu ya mwamba; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa
maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25
“Na kila asikiaye hayo
maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake
juu ya mchanga; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka;
nalo anguko lake likawa kubwa,” Mt 7:26-27
TAFAKARI: “Afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni ndiye
atakayeingia katika ufalme wa mbinguni.”
Wapendwa wana wa Mungu, kila kitu chenye uhai kwacho
chenyewe au kundi huongozwa na mamlaka fulani. Ni kweli pia hata kwa upande wa
mwanadamu katika ishi yake ikiwa ni pamoja na fikiri yake, tenda yake, amini
yake, husukumwa na kitu fulani. Ukweli huu ni pamoja na kundi la watu ambao pia
kwa kukaa pamoja husukumwa na nguvu ya mfumo fulani. Nguvu hizi au misukumo hii
tunapoitimiza kama ilivyo ndiyo kwa namna hiyo tunalandana nayo na
kujishikamanisha nayo. Huku ndiko kuwa na utii wa kweli katika mamlaka hizo
kwani kwa kupitia utii huu tumeshikamanishwa na kile kinachotusukuma (mamlaka)
kufanya hivyo.
Ndugu zangu katika Kristo, Injili ya leo inatuweka wazi kwa
kutufunulia ni kipi kipasacho kusukuma maisha yetu. Kitu hicho ndicho
kinachotakiwa kuwa na mamlaka juu ya maisha yako. Yesu anatupa angalizo na
kusema, “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme
wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt
7:21. Kwa maana nyingine unaweza kuwa Mbwekaji mzuri sana kwa kuwapendezesha
watu wanaokuzunguka kwa kuwaaminisha pasipo kumaanisha, ukawa kama Mbwa anayebweka
usiku kucha kumwaminisha tajiri yake kwamba ulinzi upo kumbe ni woga wa miluzi
ya upepo. Kumbe ukweli ni kwamba, ni yule tu “afanyaye
mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni (Mungu) ndiye atakayeingia katika ufalme
wa mbinguni.” Je, kufanya mapenzi ya Mungu kunamaanisha nini?
Wapendwa wana wa Mungu, kufanya mapenzi ya Mungu ni “kukaa
katika pendo” la Mungu. “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na
kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na
Mungu hukaa ndani yake,” 1Yoh 4:16. Ni kuwa tayari kuongozwa na mamlaka ya
Mungu katika mfumo wa Upendo. Tunakaa katika upendo wa Mungu kwa kuyatimiza
mapenzi yake pale tu tunapolipokea neno lake, tunapolisoma neno lake,
tunapolifanyia tafiti neno lake, tunapolikumbuka neno lake, na tunapolitafakari
neno lake. Haya mambo matano ni muhimu sana kama tunataka kweli kukaa naye na
kuyafanya mapenzi yake. “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya,
atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha,
mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana
misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25. Hakuna awezaye kutung’oa
kwenye mwamba huu wa imani hata kikija kimbunga cha tsunami.
Tusipo lishika neno lake la Mungu vizuri
tutakuwa tayari kuongozwa na mamlaka hizi; mila zetu (kwa kufanya yale
yanayotutia hofu bila kuhoji sababu yake), desturi zetu (kwa kufanya kadiri ya
mapokea ya wazee wetu katika hali ya upofu), hisia zetu (kwa kufanya kadiri ya
miyeuko yetu na siyo utashi wetu). “Na kila asikiaye hayo
maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake
juu ya mchanga; mvua
ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka;
nalo anguko lake likawa kubwa,” Mt 7:26-27. Hakika kwa hali hii tunabaki kuwa
kama bendera fuata upepo. Na kwa sababu hiyo, kila ajitokezaye na kutushawishi
hatutakuwa na nguvu ya kuimili vishindo vya imani kwani tu wepesi kama pamba.
Hivyo
ndugu zangu katika kipindi hiki cha majilio tunapomsubiri Masiha wetu tukae
katika neno la uzima. Ni katika hali hii kwamba Mungu “atamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani
kamilifu, kwa kuwa anakutumaini,” Isa 26:3. Mungu
wetu ndiye mwamba wetu wa milele. Tumia muda wako vizuri kulitafakari neno lake
la uzima. Kama unaweza kutumia masaa mawili au matatu kwenye runinga, tenga
basi hata robo saa kulisoma neno la Mungu na ubaki nalo kwani ndilo lenye
uzima. “Mtumainini Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa
milele, kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule
ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini,” Isa 26:4-5.
Yote yanayotupa matumaini leo na sasa bila Mungu hufifia kama mkaa wa mabua ya
mahindi.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kila akaaye ndani
yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua,”
1Yoh 3:6
No hay comentarios:
Publicar un comentario