IJUMAA WIKI YA 2 YA MAJILIO-C
11/12/2015
Somo: Isa 48:17-19
Zab: 1:1-2, 3, 4, 6
Injili: Mt 11:16-19
Nukuu:
“Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida,
nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata,” Isa 48:17b
“Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa
kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya baharí,” Isa 48:18
“Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka
katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa
mbele zangu,” Isa 48:19
“Maana Yohana alikuja, hali wala hanywi, wakasema, Yuna
pepo,” Mt 11:18
“Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa, wakasema, Mlafi
huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana
kuwa ina haki kwa kazi zake,” Mt 11:19
TAFAKARI: “Nitakifananisha na nini kizazi hiki?”
Wapendwa wana wa Mungu, leo tupo kwenye ulimwengu ambao
siyo kwamba tu watu wengi hawaamini kuwa Mungu yupo, bali hawataki kusikia
kabisa habari za Mungu. Kumbe leo kwa namna ya pekee Yesu anatuambia “nikifananishe
na nini kizazi hiki cha leo?” Kwa namna nyingine twaweza kusema tu kizazi
kisichokuwa na hofu ya Mungu. Ikiwa hawakumwamini Yesu wakati huo, je leo
watamwamini? Historia yajieleza kwamba, “Yohana alikuja, hali wala hanywi,
wakasema, Yuna pepo,” Mt 11:18. Na “Mwana wa Adamu alikuja, akila na kunywa,
wakasema, Mlafi huyu, na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na
hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake,” Mt 11:19.
Ikiwa tunaamini maisha ni safari kuelekea umilele, bila
uwepo wa Mungu kuufikia umilele huo haitawezekana. Kuna faida kubwa kuamini na
kuishi tukiwa na hofu ya Mungu. Mungu anasema, “Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida,
nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata,” Isa 48:17b. Njia atufundishaye Mungu
ndiyo njia salama na yenye uhakika. Usalama
wetu ni kuzishika na kuziishi amri za Mungu. “Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa
kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya baharí,” Isa 48:18. Mahali
popote pale penye utaratibu pana akili. Hivyo tu wacha wake Mungu tunapoishi
yale anayotutaka kuishi. Mawazo yake Mungu kwetu ni mawazo ya uzima na mema. “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema
Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za
mwisho,” Yer 29:11
Faida tuipatayo kwa kumwamini Mungu na kuishi kadiri ya
mapenzi yake ni kubwa sana. Mungu anatuambia, “Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka
katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa
mbele zangu,” Isa 48:19. Huku ni kuhesabiwa haki mbele ya Mungu pale tunapoishi kwa uaminifu na hofu juu
yake.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Wewe, Bwana, ndiwe utakayetuhifadhi, Utatulinda na kizazi
hiki milele,” Zab 12:7
No hay comentarios:
Publicar un comentario