martes, 15 de diciembre de 2015

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 3 YA MAJILIO-C

JUMATANO WIKI YA 3 YA MAJILIO-C
16/12/2015
Somo: Isa 45:6c-8, 18, 21c-26
Zab: 85:9ab-14
Injili: Lk 7: 19-23
Nukuu:
Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote,” Isa 45:7

Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki; Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, Bwana, nimeiumba,” Isa 45:8

“Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, Bwana? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi,” Isa 45:21c 

Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Lk 7:19 

Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona,” Lk 7:21

Ndipo alipojibu, akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema,” Lk 7:22 

Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami,” Lk 7:23 

TAFAKARI:Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”

Wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya masomo yetu ya leo, yaani somo la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Isaya, na Injili kutoka kwa Mwinjili Luka tunao shahuku ya watu ilivyokuwa kubwa wakisubiri ukombozi. Somo la kwanza tunaona Mungu akijifunua kwa watu wake kupitia asili ya vitu. Asili hii inamthibitishwa uwezo wake wa kuwakomboa. Asili hii inawajengea watu wake imani naye na kuwaondolea hofu. Asili hii inajenga tena ukaribu kati ya watu na Muumba wao. Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote,” Isa 45:7.

Mungu ndiye haki ya watu wake, na ndiye peke yake mwenye uwezo wa kuwakomboa. “Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi,” Isa 45:21c. Kazi yote ya uumbaji wa ulimwengu na yale yote yaliyomo ililenga kumkomboa mwanadamu. Vyote hivyo vinadhihirisha ukuu wake na uweza, na kwa upande mwingine vinaonyesha lengo la kila kimoja vikimwelekea yule aliyeumbwa kwa sura na mfano wake Mungu, yaani wewe na mimi.

Huyu ndiye Mungu mwenye kuvishurutisha vyote alivyoviumba na humtii. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki; Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, Bwana, nimeiumba,” Isa 45:8. Kazi hii ya ukombozi inakamilishwa na Yesu Kristo. Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu,” Ebr 1:1-3.

Hata hivyo licha ya kwamba Maandiko Matakatifu yalionyesha wazi kuwa Yesu ndiye atakayeukamilisha ukombozi huu, Yohane Mbatizaji akiwa gerezani anaingiwa na mashaka. Na hii inaonyesha kwamba umasiha wa Yesu haukulandana na matumaini ya kibinadamu. Ndipo Yohana alipowaita wawili katika wanafunzi wake, akawatuma kwa Yesu akiuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Lk 7:19. Yesu hakujibu swali hili moja kwa moja. Hakika hapakuwa na neno la kibinadamu yenye kusema kwa ujumla kile alicho Yesu.

Maandiko Matakatifi yanamfunua kama ifuatavyo; Yesu ni Mfalme, Nabii, Kuhani, Mwana wa Adamu, Mtumishi…; lakini Yesu ni zaidi ya Ibrahimu. Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko,” Yoh 8:58. Yesu ni zaidi ya Musa na Eliya. Tunaona tukio hili pale aliojeuka sura akiwa mlimani. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu,” Mk 9:4. Yesu ni zaidi ya Yohane Mbatizaji. Yohane anakiri jambo kili na kusema, Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto,” Mt 3:11. Kwa mtazamo huu na kile alicho Yesu, haikuwa rahisi kujibu moja kwa moja kile alicho. Badala yake Yesu anawataka wale wanafunzi wa  Yohane Mbatizaji washuhudie yale ayatendayo na iwe shuhuda kwao na jibu sahihi kwa Yohane Mbatizaji.
 
Yesu anaendelea na kazi aliyoijia kama shuhuda iliyo hai na yenye kumtambulisha kile alicho. Na hivi ndivyo iliyotokea mbele ya wale wanafunzi waliotumwa na Yohani Mbatizaji kwa Yesu; Na saa ile ile aliwaponya wengi magonjwa yao, na misiba, na pepo wabaya; na vipofu wengi aliwakirimia kuona,” Lk 7:21. Baada ya kazi hii ya uzima na yenye kumtambulisha, Yesu anawaambia wale wanafunzi wa Yohane, Nendeni mkamweleze Yohana hayo mliyoyaona na kuyasikia; vipofu wanapata kuona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakasika, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, maskini wanahubiriwa habari njema,” Lk 7:22. Tofauti na wale wote waliomtangulia Yesu katika safari hii ya ukombozi, Yeye, yaani, Yesu, aliufunua Umungu kwake na kuudhihirisha kwa watu na wote waliomridhia kupitia kazi zake. Basi na Naye heri mtu ye yote asiyechukizwa nami,” Lk 7:23. Ukikutana na Yesu hawezi kukuacha hivi hivi. Lazima tu atakubadilisha na kuyaacha yale yote ya zamani. Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii ungependa kukutana na Yesu? Kama jibu lako ni ndiyo; basi kukutana na Yesu itakupasa kulisoma neno lake, kulipokea neno lake, kulitafiti neno lake, kulitafakari neno lake, na kulikumbuka daima neno lake.

Tumsifu Yesu Kristo!

Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa,” Yoh 15:7

No hay comentarios:

Publicar un comentario