JUMATANO, SIKU YA SITA YA OKTAVA YA NOELI
30/12/2015
Somo: 1Yoh 2:12-17
Zab: 95:7-8a, 8b-9, 10
Injili: Lk 2:36-40
Nukuu:
“Nawaandikia ninyi,
watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu,” 1Yoh 2:12
“Msiipende dunia, wala
mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani
yake,” 1 Yoh 2:15
“Maana kila kilichomo
duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima,
havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia,” 1Yoh 2:16
“Na dunia inapita,
pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele,”
1Yoh 2:17
“Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa
kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume
miaka saba baada ya uanawali wake,” Lk 2:36
“Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika
hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba,” Lk 2:37
“Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote
waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake,” Lk
2:38
“Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na
neema ya Mungu ilikuwa juu yake,” Lk 2:40
TAFAKARI: “Msiipende dunia, wala
mambo yaliyomo katika dunia.”
Wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya masomo yetu ya leo, uhuru
wa kweli kutoka utumwa wa dhambi umewezekana kupitia Bwana wetu Yesu Kristo, na
kwa yeye Kristo tumemjua Baba Yetu wa Mbinguni, na hivyo kuushinda ulimwengu.
Barua hii ya Mtume Yohane kwa watu wote, anatambua wazi nafasi ya Yesu katika
maisha yetu, na kile alichokijia kukikomboa. Hivyo Mtume Yohane anasema, “Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi
zenu,” 1Yoh 2:12. Ni Yesu Kristo tu awezaye kutuoka kwa sababu upendo wake hauna
kipimo na alitupenda upeo. “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa
saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali
amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1. Hivyo niwapo
hapa duniani nina nyajibu kuu mbili; mosi, kuishi upendo huu kwa waamini
wenzangu, na pili, kuishi upendo huu kwa wale wasiomwamini Kristo. Kwa wale
wasiomwamini Kristo yanapasa kuishi ushuhuda wa ukimya kwa kuwapenda na kutenda
kama alivyofanya Kristo Yesu. Hivyo, “yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru,
ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu,” Yoh 3:21. Ni
“katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake
kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu,”
1Yoh 3:16. Upendo huu unatuwajibisha kumpenda Mungu na jirani.
Kadiri ya
mtazamo wa Yohane, ulimwengu ni ufalme wa dhambi. Kwa mantiki hiyo tuwapo hapa
duniani hatuwezi kuwatumikia mabwana wawili tukabaki salama. “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili;
kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na
kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24. Ndugu yangu, kwa
maana hii, huwezi kula keki na wakati huo huo wataka ibaki kama ilivyo. Ama
uile na isibaki au ibaki na usiile. Hivyo kumpenda Baba kweli ni kuichukia
dunia katika kuikoa nafsi yako. “Msiipende dunia, wala
mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani
yake,” 1 Yoh 2:15. Matendo ya mwili, Gal 5:19-21, yote hupatikana katika dunia
hii. Na katika hayo hakuna Mbingu. “Maana kila kilichomo
duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima,
havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia,” 1Yoh 2:16. Niwapo hapa duniani
yanipasa kuelewa kwamba ni mahali tu pa kujiandaa na kupita kuelekea umilele.
Yote
tuyaonayo hapa duniani hayana umilele kwa sababu ni vivuli vyo uhalisia ambao
unapatikana ulimwengu wa mafaa, yaani mbinguni alipo Mungu mwenyewe, kadiri ya
mtazamo wa falsafa ya Plato. Kwa maana nyingine ni kupoteza nguvu bure
tunapowekeza kiroho hapa duniani. Ukweli ni kwamba, “dunia inapita, pamoja
na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele,” 1Yoh
2:17. Kuyafanya mapenzi ya Baba ni kujitambua kwamba haupo ulimwenguni hapa kwa
bahati mbaya. Upo hapa duniani kwa shughuli maalum, yaani, kufanya kile
alichokijia Kristo katika kuukomboa ulimwengu. Yesu anasema, “Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote
alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 6:39. Wapo
wengi miongoni mwetu wanafikiri kwamba uwepo wao hapa duniani ni kuishi kwa
ujanja ujanja katika hila, fitina, ufisadi, ukatili na dhuluma. Haya siyo uliyoitiwa katika ulimwengu huu ndugu
yangu.
Kuyafanya mapenzi ya Mungu
wakati mwingine hakuhakisi kabisa miono na mitazamo ya
kibinadamu. Mitazamo yetu ni kwamba tuwapo karibu sana na Mungu na kufanya
mapenzi yake, ndiyo miminiko ya baraka na neema. Ndugu yangu uliyesafiri nami
katika tafakari hii, hatutendi mema wala kuwa waaminifu mbele ya Mungu ili tununue
baraka na neema zake, bali tunayafanya hayo yote kwa sababu ndiyo hali na uwepo
wa Mungu, na ndivyo impendezavyo sisi kufanya. Uwepo wetu hapa duniani ni moja
ya uzuri na utukufu wa Mungu. Mfano wa wale waliyafanya yote vyema ila
hayakuendana na miono na mitazamo ya kibinadamu ni Ana binti Fanueli. Tunambiwa
“Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti
Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa
na mume miaka saba baada ya uanawali wake,” Lk 2:36. Bila shaka Ana kama
Mwanamke na Mama, kuwa na familia kamili katika maana ya Yeye, Mumewe na mtoto
au watoto ilikuwa moja ya furaha yake
kubwa hapa duniani. Pamoja na kukosa hilo, hakuwa na nafasi ya kumlaumu Mungu
wala kuasi Imani yake. Aliishi kwa matumaini makubwa ingawa umri wake ulisogea.
“Naye ni mjane wa miaka themanini na minne;
haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba,” Lk
2:37. Wangapi kati yetu tunaujasiri huu tunapoona mbele yetu ni giza tupu?
Furaha ya Ana binti Fanueli inakamilika anapokutana na
Yesu. Ni kama asemavyo Mt. Agustino kwamba ‘mioyo yetu haitulii mpaka
itakapotulia kwako Ee Bwana.’ Ndivyo ilivyokuwa kwa Ana binti Fanueli
alipokutana na Yesu. “Huyu (Ana binti Fanueli) alitokea saa ile ile akamshukuru
Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea
habari zake,” Lk 2:38. Alichokua akikitazamia
amekiona kwa macho yake.
Na “Yule mtoto (Yesu) akakua, akaongezeka nguvu,
amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake,” Lk 2:40. Maana yake aliyaishi
maisha yetu, furaha zetu, mahangaiko yetu, na kuyashiriki yote bila kutenda
dhambi hadi kikomo chake pale Msalabani kwa kutuweka huru. Hivyo “Nanyi mfahamu kwamba
mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka
katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya
thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,”
1Pet 1:18-19. Je, una chochote chenye thamani
katika ulimwengu huu ambacho waweza kulinganisha na wokovu aliyokupatia
Kristo Yesu?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Lakini mimi, hasha,
nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14
No hay comentarios:
Publicar un comentario