KIPINDI
CHA KUZALIWA BWANA
MISA
YA USIKU
25/12/2015
Somo
I: Isa 9:2-7
Zab:
96: 1-3, 11-13
Somo
II: Tit 2:11-14
Injili:
Lk 2:1-14
Nukuu:
“Watu wale waliokwenda
katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru
imewaangaza,” Isa 9:2
“Maana kwa ajili yetu
mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani
mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa
milele, Mfalme wa amani,” Isa 9:6
“Maongeo ya enzi yake
na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme
wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata
milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo,” Isa 9:7
“Maana neema ya Mungu
iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo
yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na
haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa,” Tit 2:11-12
“tukilitazamia tumaini
lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu,”
Tit 2:13
“ambaye alijitoa nafsi
yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe
milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema,” Tit 2:14
“Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti,
akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni
wa mbari na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye
ana mimba,” Lk 2:4-5
“Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia, 7 akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika
nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hawakupata
nafasi katika nyumba ya wageni,” Lk 2:6-7
“Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa
makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku, Lk 2:8
“Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea
habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi
amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana,” Lk 2:10-11
“Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa
nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe,” Lk 2:12
“Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu
aliowaridhia,” Lk 2:14
TAFAKARI:
“Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
Wapendwa wana wa Mungu,
usiku huu Mama Kanisa amejawa furaha sana kwa tukio hili la upendo na ukarimu
uliotukuka wa Mungu kuchukua hali yate ya kibinadamu na kuwa sawa na sisi
isipokuwa dhambi, ili kutukomboa na kututoa katika hali yetu ya dhambi na kufa.
Hili ndilo fumbo tunalosheherekea leo, yaani, kumwilishwa, “neno kufanywa mwili
na kukaa kwetu.” Kipindi hiki cha kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, yapo mambo
makuu matatu tunayo yatafakari kwa kina katika umoja wake. Mambo haya matatu
hatuwezi kuyatenganisha ingawa katika kuyaelezea ili kujua kilichojificha
katika fumbo hili hatuna budi kufanya hivyo.
Kwanza kabisa kipindi
hiki tuna tafakari kwa undani tendo zima la Mungu kuchukuwa hali yetu ya
ubinadamu, yaani, ‘neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, “Verbum caro factum
est.” Huu ni upendo mkubwa sana wa Mungu kwetu, na unyenyekevu wa hali ya juu
alioufanya. Mtume Paulo analinena tendo hili kama NEEMA ya ajabu sana kwetu,
ambayo Mungu anakubali kuwa masikini ili mimi na wewe tuwe matajiri. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi
alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi
mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake,” 2Kor 8:9. Hili ndilo kusudio kubwa la
Mungu kwetu la kuchukua hali yetu ya ubinadamu. Hakuna shaka yoyote kwamba kwa
tendo hili Mungu yupo tayari kuanza upya nasi. Na huyu ndiye Mtoto tuliyepewa
leo. “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume;
Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa
ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani,” Isa 9:6. Huu ni
ushindi mkubwa sana kwetu, tunapotolewa katika giza na kuwekwa kwenye mwanga. “Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale
waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza,” Isa 9:2. Hakika
ingawa tunajua siku moja tutakufa, ila kuanzia sasa kifo hakina nguvu na
mamlaka tena kwetu. Mtoto huyu atalikamilisha hilo pale msalabani. Jambo hili
ndilo litakalo kamilisha safari yake hapa duniani. Ubinadamu huu wa Yesu, ambao
ni tokea zima la fumbo hili la kumwilishwa ndio tunalolitafakari usiku huu.
Pili,
katika kipindi hiki cha kuzaliwa Bwana na mwokozi wetu, tuna tafakari kwa undani hali yetu ya ubinadamu ya
kuinuliwa na kufikia hali ya Umungu ndani na katika Kristo Yesu, “Et habitabit
in nobis.” Ni kwa kupitia Mtoto huyu aliyezaliwa leo kwamba, “Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika
kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu
na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio
utakaotenda hayo,” Isa 9:7. Hapa kila mmoja wetu anarudishiwa hali yake ile ya
kutokufa iliyosababishwa na anguko la wazazi wetu wa mwanzo, Adamu na Hawa.
Tatu,
katika kipindi hiki cha Noeli, tuna tafakari kwa undani tendo la kufanywa vyote
vipya katika uumbaji wa Mungu, “Ecce nova facio omnia.” Ni kwa kupitia Kristo
ambaye ni Adamu Mpya nasi twafanywa wapya na kuwa warithi wa ufalme wa Mungu.
Tendo hili la kufanywa vyote upya ndani na katika Kristo linaenda sambamba na
kufanya kwetu toba ya kweli. Hivyo katika hali hii ya furaha kwa kuzaliwa kwetu
mwokozi na mkombozi, ni mwito pia wa kufanya toba ili tufanywe upya ndani na
katika Kristo. “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja
nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa
tangu zamani; ambaye ilimpasa
kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na
Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu,” Mdo
3:19-21. Nyakati za kuburudishwa ndio sasa.
Hayo
mambo makuu matatu ni NEEMA kubwa sana kwetu katika kipindi hiki cha Noeli.
Neema hii kwa tendo la ‘neno kufanyika mwili na kukaa kwetu,’ imemiminwa na
Mungu kwa watu wote. “Maana neema ya Mungu
iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo
yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na
haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa,” Tit 2:11-12. Msingi wa haya
yote ni uwepo wa Kristo duniani kama Neema ya Baba. Kwa maisha ya Kristo na
neno lake, yanatupa mafundisha halisi, na njia ya kufuata. Yesu “ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na
maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi
katika matendo mema,” Tit 2:14. Hili ndilo tumaini la kweli na lenye uhakika
katika maisha haya mapya tunayosheherekea leo, na “tukilitazamia tumaini
lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu,”
Tit 2:13. Hivyo ndugu zangu leo kwa namna ya pekee tunautazama ubinadamu ya
Kristo, na Kesho kadiri ya liturjia tutatafakari Umungu wa Kristo.
Hivyo,
Injili yetu ya leo inatufikirisha zaidi katika ubinadamu wa Kristo. Hivyo
kuzaliwa kwake Mwokozi na Mkombozi wetu Yesu Kristo, kumechukua taratibu zote
za kila siku na mahangaiko ya kila siku ya mwanadamu. Nyakati hizo karibia na
kuzaliwa kwake Mtoto Yesu, linatoka tangazo la kujiandikisha kwa lengo la kujua
idadi ya watu. Huu ni utaratibu wa kawaida wadola yoyote ile yenye mpango wa
maendeleo kwa watu wake. Takweimu hizi za sensa husaidia kujua ni wapi kuna
uhitaji zaidi na ni nini cha kufanya. Kuitikia wito huu, “Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa
Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa
kuwa yeye ni wa mbari na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye
amemposa, naye ana mimba,” Lk 2:4-5. Kwa tendo hili, Mungu anashiriki
misukosuko na mahangaiko yetu licha ya Ukuu aliyo nao.
Ubinadamu huu wa Kristo tunaoutafakari
usiku huu unatukumbusha kwamba historia
ya mwanadamu ipo mikononi mwa Mungu. Ni kwa namna hiyo kwamba ukubwa wa himaya
ya dola ya Kirumi unaishia horini ambapo kuna katoto kachanga kalichofungwa
nguo za kitoto, naye ndiye Yesu. Yesu hapa ni alama halisi ya upendo na huruma
ya milele ya Mungu. Waliofika kushuhudia upendo na huruma hii ya milele ya
Mungu ni wale walio masikini na waliodharauliwa sana katika jamii. Hawa ndio
wale wachungaji ambao mchana na usiku waliishi na mifugo huko makondeni. “Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji
wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku, Lk 2:8. Pamoja na udogo wao na hofu waliyokuwa nayo
kwa kile kilichotokea kisicho cha kawaida, kikiambatana na ishara nyingi, wanapata
fursa ya kwanza kuyashuhudia mambo makuu ya Mungu. Wakiwa katika sintofahamu
hii, “Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi
ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; maana leo katika mji wa Daudi
amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana,” Lk 2:10-11. Huyu ndiye
Mungu anayemsema Bikira Maria katika utenzi wake ule wa
‘Magnificat,’-Wamtukuza, kwamba, “Amewaangusha wakuu katika
viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Hakika Mungu ni wa ajabu
sana!
Wapendwa
katika Kristo, ni katika Yesu Kristo tunaona muunganiko wa umasikini wa watu na
Mungu. “Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto
mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng'ombe,” Lk 2:12. Hivyo
alama za Mfalme wetu aliyezaliwa leo ni kama zifuatazo; vipande vya vitambaa,
nguo za kitoto, mtoto, na hori “umasikini.” Katika hali hii, Yesu ni sifa kwa
Mungu na wokovu kwa watu. “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na
duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
Pamoja na Ufalme aliokuwa nao Yesu kupita falme zote za dunia hii
alikoswa mambo muhimu sana kupita hata kwa maisha ya mtu wa kawaida. Kama
Mfalme basi ingetazamiwa azaliwe kama siyo kwenye hospitali nzuri na zenye
huduma bora, basi ingekuwa kwenye moja ya majumba mazuri ya kifalme. Lakini
badala yake kazaliwa kwenye hori la ng’ombe.
Kama Mfalme,
tulitegemea kungekuwa na nderemo kila kono na viungo vyote vya miji ya Israeli
na dunia nzma huku shangwe hizi zikisindikizwa na kwaya mashuhuri kuutubuiza
usiku huu wa ajabu kwa kuwa Mungu yule aliyekuwa mbali sasa yu nasi, naye ni
Emanueli, yaani Mungu pamoja nasi. Badala yake bila shaka kulikuwa na kwaya ya
nzi wengi wakisaidiana na mbu, kwani mahali pale alipozaliwa palikuwa holini
mwa ng’ombe. Huyu ndiye Mungu aliyekubali kuchukua na kushuka chini kabisa
katika hali na ubinadamu wetu.
Tukio hili na mazingira
ya kuzaliwa mwokozi wetu linanikumbusha tukio la kujifungua kwa Yosephina mke
wa Barnaba. Yosephina na Barnaba ni wakulima wa kawaida sana. Mapato yao
yalikuwa ni kutoka mkononi kwenye kinywani. Hivyo hawakuwa na akiba yoyote.
Waliishi kwa kudra ya mwenyezi Mungu. Kazi nzito kipato kidogo. Haya ni maisha
ya familia nyingi wanayoyaisha leo. Hata usiku huu kati yetu tupo katika ukweli
huu wa Yosephina na Barnaba. Maisha yao ya umasikini, yaani Yosephina na
Baranaba, uliweza kuyatabiri haraka kwa namna ya vaa yao. Mama huyu hupenda
kujivunga kanga nyingi sana kiunoni na wakati mwingine hufanana na mwanasesere.
Siyo ukweli kwamba
Yosephina alipenda kufanya hivyo ili kuwachekesha na kuwafurahisha watu, ila
ukweli ni kwamba kila kanga aliyojifunga ilikuwa na matobo. Hivyo kujifunga
zaidi ya kanga moja alikuwa na lengo la kuyafunika matobo. Ni kwa namna hiyo
kila kanga ilikuwa na kazi yake. Binafsi niliyapenda maisha yao na ushiriki wao
katika Jumuiya. Ndoa yao ni kati ya ndoa zile zinazofungwa kwa kundi la
wanandoa wengi. Hata hivyo ilikuwa ni familia yenye furaha sana.
Yosephina na Mumewe
Barnaba hupenda sana kuudhuria misa za asubuhi na baada ya tendo hilo la ibada
huelekea pamoja mashabani mwao. Hakika maisha yalikuwa “HAPA KAZI TU,” licha ya
kuwa na mazingira magumu ya kazi na kipata kidogo. Akiwa mjamzito na kukaribia
kujifungua, alifika Misa ya asubuhi kama kawaida na baada ya Misa walielekea
mashambani. Mara walipofika shambani hali ilibadilika na ilimlazimu Mumewe
amsaidie kujifungua. Mungu mwema, zoezi hili lilikwenda salama. Baada ya saa
moja tu ya mapumziko, walikiweka kichanga chao chini ya kivuli cha mti kikiwa
kimeviringishwa kanga mili zenye mipasuko juu ya dodoro zuri la nyasi kavu na
kuendelea na kazi. Jioni ilipowadia, walirudi nyumbani na kachanga chao. Maisha
yaliendelea kama kawaida.
Wapendwa hata katika
hali hizi za kutisha, Mungu hutulinda kwa namna ya ajabu sana. Huyu ndiye Mungu
aliyekuja kutafuta kile kilichopotea. Leo tunaposheherekea siku hii ya kuzaliwa
Mwokozi na Mkombozi wetu, ni mwito vile vile wa kuwafikiria wengine hasa
majirani zetu ambao hakika leo hawajui watakula nini. Noeli ni sikukuu pia ya
Familia. Tusipoutazama utajiri wa Mungu na utayari wake wa kuwa masikini ili
sote tuwe matajiri, tukio hili la kuzaliwa Mwokozi na Mkombozi katika maisha
yetu halina maana kabisa. Ni vyema kujiuliza maswali haya;
Je, tukio hili la
kuzaliwa Kristo lina tafsiri gani katika maisha yangu? Je, ni mfululizo tu wa
moja ya siku za kihistoria ninazozijua na kuzisheherekea kama nilivyozikuta
katika jamii ninayoishi, au kuna kitu kikubwa zaidi ya hicho?
Je, kuzaliwa Kristo
kwangu ni kipindi cha kuzama zaidi katika fumbo hili la kumwilishwa, na kuona
mahitaji ya wengine kama Mungu alivyoona hitaji letu na kutukomboa, au ndiyo
fursa mpya ya kula, kunywa, kuvaa, na kufurahia biashara yangu kama
mfanyabiasha kwa kuuza zaidi?
Wapendwa wana wa Mungu,
lazima tuelewe jambo hili; Kristo amemwilishwa ili kutufanya nasi kuzaliwa
wapya ndani na katika historia ya wanadamu. Hivyo mimi binafsi bila kutambua na
kutaabika kwa ajili ya wahitaji na hasa wanaonizunguka, ni kupungukiwa
utoshelevu katika Kristo na fumbo zima la kuzaliwa kwake kwangu na kwetu.
Kama binadamu halisi,
Kristo kazaliwa ili kutupeleka katika hali ya juu ya Umungu wa Mungu. Hii ni
heshima kubwa sana kwetu. Je, kwa nafasi niliyonayo na uwezo niliojaliwa
na Mungu, ni wangapi walioduni kabisa
nimeweza kuwafikisha katika hali ya maisha ninayoishi? Kuzaliwa kwa Kristo ndio
mwanzo wa safari ya sisi kuzaliwa wapya ndani na katika Yeye.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu
aliowaridhia,” Lk 2:14
No hay comentarios:
Publicar un comentario