JUMANNE, SIKU 22 YA MAJILIO MWAKA-C
22/12/2015
Somo: 1Sam 1:24-28
Zab: 1Sam 2:1, 4-8
Injili: Lk 1: 46-56
Nukuu:
“Naliomba nipewe mtoto huyu; Bwana akanipa dua yangu
niliyomwomba;kwa sababu hiyo mimi nami nimempa Bwana mtoto huyu; wakati wote
atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu Bwana huko,” 1Sam 1:27-28
“Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,” Lk 1:46
“Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu,” Lk 1:47
“Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama,
tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa,” Lk 1:48
“Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge
amewakweza,” Lk 1:52
TAFAKARI: “Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama,
tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa.”
Wapendwa wana wa Mungu, masomo ya leo yanatualika
kuyatafakari Makuu ya Mungu kwa wanyenyekevu wake wa Moyo. Taswira hii na
fadhila hii ya unyenyekevu inajionyesha katika wimbo ule wa Ana na Bikira
Maria. Ana ana kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kumrudishia heshima yake
kama Mama kwa kumpatia Mtoto, Samweli. Kwa kutokuwa na mtoto alidharaulika sana
na kuonekana hafai. Hivyo inamlazimu kumrudishia Mungu sifa na shukrani kama
alivyokwisha kuhaidi mbele ya Eli, Kuhani huko Shilo. “Naliomba nipewe mtoto
huyu; Bwana akanipa dua yangu niliyomwomba; kwa sababu hiyo mimi nami nimempa
Bwana mtoto huyu; wakati wote atakaokuwa hai amepewa Bwana. Naye akamwabudu
Bwana huko,” 1Sam 1:27-28. Ndugu yangu, nawe hauna kitu cha kumshukuru Mungu
kama Mama huyu Ana? Ukweli ni kwamba, ‘moyo usio na shukrani ukausha mema
yote.’
Tenzi
hizi zote mbili, yaani wmbo wa Ana na Bikira Maria zinatuonyesha utendaji wa
Mungu katika historia ya wokovu. Kwa kuikamilisha safari hii ya wokovu, Mungu
aliwachagua baadhi ya watu, na wakati mwingine wale waliodharauliwa na hata
kutokujaliwa katika jamii. Watu hawa ni kama wale walizaliwa na wanawake
waliokuwa tasa mfano Samweli, Yohane Mbatizaji, Mama Bikira, na wengine wengi
tu katika historia hii ya wokovu.
Utenzi wa
Bikira Maria, “Magnificat,” wenye maana ya “Wamtukuza,” unaonyesha kutukuza na
kuinuliwa kwa hali ya juu roho na nafsi ya binti wa Sioni. “Moyo wangu
wamwadhimisha Bwana,” Lk 1:46. Utenzi huu unaonyesha matumaini mapya na furaha
mpya kwa kujibiwa kwa sala ambayo ilifanywa muda mrefu na wana wa Mungu
waliokuwa wakisubiri kujibiwa kwao. “Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili
kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata
milele,” Lk 54-55. Machozi, furaha na matumaini ya watu yamefungwa katika mioyo yao. Hivyo Mungu ndiye mwenye kutukuzwa
kwa sababu kamjibu mjakazi wake. Huruma ya Mungu imefanywa milele ndani ya
mjakazi wake. “Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama,
tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa,” Lk 1:48
Kwa maana
hiyo, Neno kufanyika mwili ni neno la kinabii ambalo huharibu na kutengeneza,
hung’oa na kupanda, Yer 1. Yesu Kristo ndiyo hitimisho la historia, nguvu
inayokamilisha ahadi za kale. “Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao
wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu
kwako na kwa uzao wako baada yako,” Mwa 17:7. Binti Sioni alitoa jina letu kwa
“Ndiyo” yake kwa Mungu, na Neno akafanyika mwili, 1Sam 2:1-10.
Wapendwa katika Kristo, unyenyekevu na kule kujishusha ni
silaha kubwa sana katika maisha, kuzijua njia za Mungu, na mwisho kutumika naye
kwa mambo makubwa na hata kutupita uwezo wetu kama wanadamu. Unyenyekevu ni
mama wa fadhila zote. Anza sasa kwa kutambua mipaka yako ikiwa ni pamoja na
madhaifu yako.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; Bali hekima hukaa na
wanyenyekevu,” Mit 11:2
No hay comentarios:
Publicar un comentario