lunes, 30 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 1 YA MAJILIO MWAKA-C

JUMANNE WIKI YA 1 YA MAJILIO
1/12/2015
Somo: Isa 11:1-10
Zab: 72:1-2, 7-8, 12-13, 17
Injili: Lk 10:21-24
Nukuu:
Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda,” Isa 11:1 

Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana,” Isa 11:2

bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya,” Isa 11:4 

Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza,” Isa 11:6 
Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira,” Isa 11:8 

Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10
Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21 

Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia,” Lk 10:22

TAFAKARI: “Kwake itasimama kweli, haki, Amani, na Upendo.”

Wapendwa wana wa Mungu, kumkomboa mwanadamu kutoka hali yake ya mateso, mahangaiko na dhambi, Mungu aliye Kweli, Haki, Amani, na Upendo kwa makusudi makubwa anapenda kuanzisha uhusiano na yule aliyemuumba kwa sura na mfano wake. Tendo hili la kuujenga uhusiano wa karibu nasi linamshusha Mungu chini kabisa katika hali ya mwanadamu. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu. Kipindi hiki cha majilio ni kipindi cha kutafakari upendo huu wa ajabu Mungu anaokwenda kutufanyia. Ikiwa zawadi hii ni kubwa sana kwetu hatuna budi kujiandaa vizuri mwili na roho ili atakapokuja atukute tupo safi na wenye afya njema hasa roho zetu.

Kufanikisha mpango huu, Mungu huyu aliye alfa na omega atachukua hali yetu ya kibinadamu, na hivyo atazaliwa ikiwa ni moja ya kushiriki hali yetu ya kibinadamu. Jambo hili linatabiriwa na Nabii Isaya. Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda,” Isa 11:1. Je huyu atakayezaliwa ataongozwa na mamlaka gani? Hakika kwa vile anakuja kuusimika ufalme wa kweli, haki, amani, na upendo, roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana,” Isa 11:2. Hivi ndivyo vitendea kazi vyake. Ujio wake kwetu ni hukumu pia ambayo itasimama katika haki. Hivyo, kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya,” Isa 11:4 

Ujio wa mfalme huyu ni ujio wa neema na baraka. Anakuja na kusimika mfumo wema na kuufifisha mfumo wa uovu. Anakuja kuondoa sintofahumu zetu kati yetu wanadamu na viumbe vingine alivyoviumba. Huyu hakika ni mfalme wa Amani. Hakutakuwa tena na sintofahumu kati ya wanyama aliowaumba. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza,” Isa 11:6. Mwanadamu ataishi kwa amani na hofu haitakuwepo tena. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira,” Isa 11:8.

Uwepo wa Mfalme huyu wa kweli,  haki, amani na upendo utajidhihirisha kwa utukufu wake. Mataifa yote watamfuata alipo kwa sababu kuna utukufu. Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10. Haya ndiyo atakayoyafanya na kuujenga tena uhusiano wetu ulioharibiwa na dhambi zetu.

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na hayo mazuri yote yaliyotabiriwa na Nabii Isaya kuhusu Mfalme huyu tunayemsubiri kwa hamasa kubwa, yatawezekana tu kama tutakuwa tayari kutoa ushirikiana naye. Mungu atukokoti kama Jemedari katili na mwenye silaha za kutisha. Utawala wake ni utawala wa Upendo. Mungu hakupenda kutuondolea uhuru na utashi wetu wa kumfuata. Ametuachia haya yote akijua kabisa kwa kuyatumia vizuri ni njia rahisi ya kumfikia, hata pale tutakapoyatumia vibari itakuwa njia rahisi pia ya kumrudia tukifanya toba ya kweli na majuto. Kwa hiyo, ‘aliyekuumba wewe pasipo wewe hawezi kukukomboa wewe pasipo wewe,’ Mt. Agustino wa Hippo.

Siri ya ukweli huu wa kutoa ushirikia na  Mungu ili kuwa sehemu salama anausema Yesu katika Injili ya leo. Siri hii ni kuwa kama watoto wachanga. Mtoto mchanga huamini yote kuwa salama anapokuwa mikono mwa wazazi wake. Mtoto mchanga kamwe hawezi kuacha kutabasamu hata kama akiwa mikononi kwa mtu mwovu. Maana yake mtoto mchanga mara zote anamtazamo chanya. Hii ndiyo hekima ilifichwa ndani ya watoto wachanga. Yesu anatutaka kuwa na unyenyekevu huu katika kuamini yote kuwa salama mikononi mwa Mungu. Naye Yesu, “Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21. 

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, leo Yesu anatufunulia jambo la pekee sana. Kwanza kabisa ni Yeye tu aliyebabidhiwa yote na Mungu. Pili hatuwezi kumjua Mungu Baba pasipo Yeye mwana, yaani Yesu Kristo. Kwa maana hiyo, kuwa na Yesu ni kuwa kwenye mikono salama. Naye Yesu, Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia,” Lk 10:22. Je, ulipo na ulipojikabidhi kuna usalama?

Tumsifu Yesu Kristo!

Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama,” Mit 18:10


domingo, 29 de noviembre de 2015

TAFAKARI: SIKUKUU YA MTAKATIFU ANDREA MTUME

JUMATATU WIKI YA 1 YA MAJILIO
30/11/2015
Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume
Somo: Rum 10:9-18
Zab: 19: 8-11
Injili: Mt 4:18-22
Nukuu:
Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9

Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:10 

Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka,” Rum 10:12-13 

Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo,” Rum 10:17

Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu,” Rum 10:18 

Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi,” Mt 4:18

Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt 4:19

Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mt 4:20

TAFAKARI: “Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.”

Wapendwa wana wa Mungu, mtihani mkubwa kwa mtu yeyote yule siyo hii tunayoifanya mashuleni na hata vyuoni, bali ni mtihani huu wa “kuamua,” uwe nini katika maisha yako. Si rahisi kufanya maamuzi hayo na kuchukua njia nyingine mpya kabisa usiyojua kifuatacho huko mbeleni. Mtu huwa na uhakika kwa kile alichokiishi jana na anachokiishi leo na sasa. Huu ni mzunguko wa kawaida katika maisha ya kila mmoja wetu. Kuwekeza maisha yako yote kwa kile usichokijua humjengea mtu hofu. Leo Kanisa linapofanya sikukuu za watakatifu na kwa maana ya pekee leo sikukuu ya Mt. Andrea Mtume, ni kusadifu yale waliyoyaamua na kuyaishi na ndiyo ukuaji wa Kanisa na uhai wake. Walifanya uamuzi wa kuacha yale waliyoyazoea na yaliyokuwa yanawapa usalama na kufuata kile wasichokijua wakijisalimisha kabisa katika hicho. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mt 4:20.

Mtume Andrea akiwa na ndugu yake Simoni Petro walikuwa wavuvi. Kazi hii iliwapa usalama na mahitaji yao ya kila siku. Yesu anawaita wamfuate nao wanaacha pale pale waliyokuwa wanafanya na kumfuata. Uamuzi huu ni mzito sana.Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi,” Mt 4:18. Kazi hii ndiyo iliyowapa makate wao wa kila siku. Embu fikiri leo kwa kazi unayofanya hasa wale wanaopata kipato kilichonona, aje mtu tu na kukuambia nifuate. Nini kitakuwa kitu cha kwanza kufanya? Bila shaka utaanza kumpiga maswali mazito na mwisho kumchukulia kama mwendawazimu hivi. Mitume hawa wanayaacha yote na kumfuata. Yesu Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt 4:19. Kuwa wavuvi wa watu ni mabadiliko mazima ya mfumo na namna ya kutenda na kuishi. Hapa ndipo tunaposema Mitume hawa walikuwa majitu ya sifa. Mioyo yao ilikuwa na ushupavu wa hali ya juu. Ni vigumu sana mtu kuubadili mfumo wa maisha yake aliouzoea.

Yesu Kristo alikuwa kila kitu katika maisha yao. Walijua pia hakuna wokovu pasipo Kristo. Iliwezekanaje hivyo haraka? Bila shaka kwa nguvu na neema za Mungu iliwezekana pale walipoonyesha utayari wao wa kumsikia Yesu na kumfuata. Mtume Paulo anatuambia, kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9. Jambo hili la kujisalimisha kabisa mikono mwa Yesu halikuwa na mashaka ndani ya mioyo ya hawa Mitume ingawa halikuwa jambo rahisi kufanya. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:10 

Wapendwa wana wa Mungu, sababu nyingine ya uwepo wetu hapa duniani licha ya kwamba ni kwa muda mfupi, ni kuwaelezea watu wengine habari njema ya wokovu wetu. Wewe uliyebahatika kuifahamu siri hii usibaki nayo mwenyewe. Ni furaha kubwa sana mbele ya Mungu kama watakuwepo baadhi ya watu waliofika mbinguni kwa sababu ulitumia muda wako kuwaelezea habari njema ya wokovu wetu. Mitume waliona na kuupokea wajibu huu mkubwa. “Maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 4:20. Neno hili sasa si kwa Wayahudi tu, ila lapaswa kusikika duniani kote. Kwa kupitia Kristo sote tumeunganishwa na kuwa familia moja yenye mastahili sawa mbele ya Mungu, na warithi wa ufalme wake. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka,” Rum 10:12-13. Mitume kwa namna ya pekee waliuona wajibu huu mkubwa wa kulihubiri neno la Mungu pasipo woga.

Msingi wa haya yote ni Imani ile waliyokuwa nayo Mitume, na kwa namna ya pekee leo Mama Kanisa anapofanya sikukuu ya Mt Andrea Mtume. Hivyo chanzo cha imani hiyo ni kusikia neno la Kristo. “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo,” Rum 10:17. Je, watu watasikiaje bila kuambiwa? Kumbe leo pia tunakumbushwa mimi na wewe kwamba kwa sakramenti ya ubatizo wetu inatufanya kuwa wamisionari. Ni wajibu wa kila mbatizwa kulitangaza neno la uzima na wokovu kwa watu wote. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu,” Rum 10:18. Hivi ndivyo walivyofanya Mitume, na leo Kanisa limesimama likiwa Kristo ndiye msingi wake Imara, na Mitume. Mimi na wewe tunadaiwa kuyatoa maisha yetu kama walivyofanya mitume ili habari njema iwafikie wote ambao bado hawajasikia. Je, nifanye vipi? Anza hapo hapo ulipo! Kuwa chumvi na mwanga ili uso wa Kristo uonekana katika maisha yao na yako.

Tumsifu Yesu Kristo! 


Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 1 YA MAJILIO

JUMATATU WIKI YA 1 YA MAJILIO
30/11/2015
Somo: Isa 2:1-5
Zab: 121: 1-2, 3-4a (4b-5, 6-7), 8-9
Injili: Mt 8:5-11
Nukuu:
Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,” Isa 2:3 

Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe,” Isa 2:4 

Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7

Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10 

TAFAKARI: Ajaye ni Bwana wa Amani.”

Wapendwa wana wa Mungu, Mwokozi tunayemtazamia kwa hamu ni Bwana wa Amani atakayetufundisha njia zake na kueneka katika mapito yake. Sheria yake kuu ni UPENDO. Ni wakati wa kuyajenga upya mahusiano yetu na Bwana huyu wa Amani. Ni Bwana wa Amani wa wataifa yote, na ulimwengu mzima. Nabii Isaya anasema habari za Mkombozi huyu: Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,” Isa 2:3.

Amani ya Mkombozi huyu inaendana pia na haki. Hivyo ajapo lazima ipite hukumu ya haki, na ndipo atakapousimika utawala wake wa Amani, Haki, na Upendo. Ili mambo haya yatendeke katika utawala wake yatupasa kubadili namna yetu ya kufikiri na kutenda. Ulimwengi wa leo vita na hasa ugaidi vinashamiri kwa nguvu kubwa sana na uhai wa mwanadamu ikiwa ni pamoja na amani vipo reheni. Nabii Isaya anasema, Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe,” Isa 2:4. Tunahitaji sana kwa sasa utawala wa Mkombozi huyu. Lengo la Mungu kuumba ulimwengu pamoja na mambo mengine, aliuumba ili pawe sehemu salama kwa ajili ya uhai wa viumbe vyote alivyoviumba na kwa namna ya pekee Mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27.

Kujenga mahusiano mapya na Mungu ni pamoja na kuwa na imani dhabiti naye. Leo katika Injili Yesu anakutana na mtu mmoja, Akida, aliyekuwa anauguliwa na mtumishi wake ugonjwa wa kupooza. Akida huyu anamwomba Yesu aende kumponya mgonjwa wake. Yesu anamjibu, Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7. Akida huyu akitambua uwezo wake na nafasi aliyokuwa nayo, na ule uwezo wa Yesu, bado anatambua kuwa umbali na uwepo wa Yesu aviweza kumzuia kumponya mtumishi wake. Akida anamtaka Yesu aseme neno tu na mgonjwa wake atapona. Hii ndiyo imani thabiti na isiyokuwa na shaka. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10. Je, waamini kuwa Yesu aweza kutenda maajabu ndani yako? Jenga uhusiano mpya naya kuanzia sasa!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6


sábado, 28 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMAPILI YA 1 YA MAJILIO MWAKA-C

JUMAPILI YA 1 YA MAJILIO YA MWAKA C
29/11/2015
Somo I: Yer 33:14-16
Zab: 25:4-5, 8-9, 10, 14
Somo II: 1The 3:12-4:2
Injili: Lk 21:25-28, 34-36
Nukuu:
Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii,” Yer 33:15 

Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 33:16

Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima,” Lk 21:34-35 

Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36

Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu,” 1The 3:12
Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana,” 1The 4:1  

TAFAKARI: “Bwana ni haki yetu.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, karibuni katika tafakari ya leo ikiwa Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kwanza ya majilio ya mwaka C wa Kanisa. Leo pia kwa namna ya pekee tunaanza mwaka C wa Kanisa. Masomo na tafakari zetu zitalenga katika kipindi hiki cha Kanisa. Kipindi hiki cha Majilio Kanisa linajifananisha na Taifa la Mungu la Agano la Kale linapotarajia kwa hamu kubwa ujio wa Mkombozi. Hivyo kipindi hiki Mama Kanisa anawaandaa wana wake kuwa tayari kumpokea Mkombozi. Hata hivyo kipindi hiki cha Majilio kina sura nyingine, ambayo inaufunua ujio wa siku ya mwisho wa Bwana. Ni kwa namna hii Kanisa limegawa kipindi hiki cha Majilio katika sehemu kuu mbili nazo ni hizi zifuatazo: Sehemu ya kwanza inaanza leo hadi hapo tarehe 16 ya mwezi Desemba. Mambo makuu katika kipindi hiki ni kutafakari juu ya ujio wa pili wa Kristo katika utukufu wake. Sehemu ya Pili, Mama Kanisa atakuwa anatafakari juu ya  matayarisho ya sikukuu ya kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Msukumo na wazo kuu katika kipindi hiki ni “Kristo yu karibu,” Yeye ni Mkombozi na hakimu.

Hivyo basi katika kipindi hiki cha Majilio tunajitayarisha kwa furaha kumpokea Kristo tukisikia na kuifuata sauti ya mtu yule aliye nyikani: “Itengenezeni njia ya Bwana.” Matengenezo ya njia hii hubeba thana nzima ya mwili na roho. Kristo atakapokuja atukute taa zetu zinawaka nasi tupo macho. Masomo yetu yote matatu yanamwelezea Bwana wetu na Mungu wetu kama mtu kwenye haki. Haki hii haipindishwi kwa lolote lile, bali ni matokeo ya ule utayari wetu wakujifungamanisha naye kuliko kweli na haki. Kama Mungu na Bwana wetu anajua yote kuhusu sisi, basi hatuna chochote cha kumficha wala kujivunua tukijidanganya kuwa ni mali yetu wenyewe. Yeye hubadili majira na nyakati; huuzulu wafalme na kuwamilikisha wafalme; huwapa hekima wenye hekima; huwapa wenye ufahamu maarifa; yeye hufunua mambo ya fumbo na ya siri; huyajua yaliyo gizani, na nuru hukaa kwake,” Dan 2:21-22. Ndugu yangu, ni nani basi zaidi ya Mungu wetu? Bwana ni haki yetu!

Siku ya hukumu ya mwisho licha ya kwamba hatujui ni lini, hatuwezi kuipuuzia kwamba haitakuwepo. Kila kitu kitapita ila neno la Bwana litabaki milele licha ya utofauti wake kati ya kile kisemwacho na tendo lenyewe kutokea. Kuchelewa kwa tukio lenyewe kusitutie upofu na uziwi wa kutokuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu na atakavyo. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Lk 21:33. Nabii Yeremia anatuambia kwamba katika mpango huu wa wokovu na hukumu ya mwisho utafanywa na Mungu chini ya chipukizi la haki na katika haki hiyo kila mtu atapata mastahili yake. Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii,” Yer 33:15. Kuokolewa kwetu ni tokeo la kuishi katika kweli na haki. Ni rahisi kufanya ujanja ujanja katika ulimwengu huu lakini si kwa Mungu aliye hai na mwona yote katika yote na muda wote. Hivi ndivyo atakavyofanya; Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu,” Yer 33:16.

Wapendwa katika Kristo, kwa vile muda wetu hapa duniani ni mfupi sana, ni vyema tukawekeza kwa yale yampendezayo Mungu hakimu wetu wa haki. Lengo la maisha yako na yangu katika ulimwengu huu siyo kuyafurahia maisha kwa sababu ya kuyafurahia tu, bali kuyatazama maisha katika umilele wake. Katika Injili ya leo Yesu anatukumbusha maana halisi ya uwepo wetu katika ulimwengu huu ukiendana na yale yatupasayo kufanya. Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima,” Lk 21:34-35. Namna ufikirivyo kuhusu hali yako ndivyo kwa namna hiyo huyafinyanga maisha yako. Wapo kati yetu maisha kwao ni kufurahia kila kunapo nafasi ya kufanya hivyo. Ila Mtume Paulo anasema juu ya jambo hili; ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu,” Rum 14:17. Uzima wa mtu ni zaidi ya haya ya leo na kesho.

Wapo pia kati yetu wanafikiri maisha ni kuwa na vitu na utajiri. Muda wao wote ni kuhangaika kuhusu mali na vitu, na mwisho wa siku ni huzuni na kukata tamaa. Mzaburi anatupa angalizo na kusema, “Usiogope mtu atakapopata utajiri, Na fahari ya nyumba yake itakapozidi. Maana atakapokufa hatachukua cho chote; Utukufu wake hautashuka ukimfuata,” Zab 49:16-17. Maisha ya utakaso ndiyo salama yetu siku hiyo ya mwisho. Utakaso huu ndiko tunakoalikwa kila siku kufanana na Yesu. Si jambo rahisi ila yakupasa kwa moyo wote uamue, ujitahidi kuishi maisha hayo, na utumudu katika maisha hayo hadi mwisho wake. Kudumu katika maisha hayo ndiko Yesu anaposema kukesha. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36. Tunamsubiri Mwokozi wetu kwa kukesha tukiitakatifunza miili yetu na roho zetu.

Kukesha huku katika kweli na haki hujionyesha kwa kuwa na mahusiano mazuri na wale tunaoishi nao kila siku. Upendo ni tokeo la maisha ya kweli na haki, na upendo huo huo usukuma maisha ya kweli na haki. Mtume Paulo anawasihi watu wake waige kile alichokifanya kwao na wenzake. Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu,” 1The 3:12. Hili ni jambo jema la kuiga. Neno la Mungu, watu, na mazingira humfinyanga na kumkomaza mtu na kukuza tabia yake. Tabia njema ndiyo itakayotufikisha kwenye uzima wa milele, na siyo utajiri tunaouangaikia usiku na mchana. Mwisho wa haya yote twapaswa kufanana na Kristo kwa sababu ni kwa njia yake wokovu wetu uwezekana. Hivyo, Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana,” 1The 4:1. Kristo Yesu ndiye kielelezo cha maisha yetu, na ufunuo halisi wa Mungu Baba. Kukesha huku Yesu anakutafsiri kama “kukaa,” katika neno lake. Kukaa huku katika neno lake ndiko kunatufanya wanafunzi wake wa kweli ambayo kweli hiyo itatufanya huru. Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31.32

Mzee Damas akiwa amelazwa hospitalini katika uzee wake wa miaka 85, chini ya uangalizi wa mjuu wake Onesmo, alikuwa na mashaka sana na huduma za Kanisa (Masakramenti), ikiwemo Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Onesmo akijua Babu yake alikuwa Mkristo na katika hali hii ya ugonjwa wake na mabadiliko ya mara kwa mara ilimlazimu kumwona Paroko wake kwa kupitia jumuiya yake ili Babu yake apate huduma hii ya wagonjwa.

Hivyo baada ya mawasiliano kwenda vizuri kati ya Onesmo, Jumuiya yake, na Paroko, siku ya jumatatu alfajiri ambayo ni siku rasmi ya kuwatembelea wagonjwa, Paroko alikwenda hospitalini kumwona Mzee Dismas na kumpa huduma hiyo. Jambo la ajabu na la kushtusha ambalo halikutegemewa na Paroko na wala Onesmo mjukuu wa Mzee Dismas, ni pale Mzee huyu alipomwona Padre na kujeukia ukutani uku akilivuta shuka lake kujifunika gubigubi.

Tendo hili lilimfikirisha haraka Padre na hivyo alimwomba Onesmo atoke nje kidogo ili aweze kuongea na Mzee Onesmo. Ilichukua muda kidogo hadi Mzee Onesmo kukubali kuongea na Padre na kusema kwa nini hataki huduma hiyo.

Tatizo kubwa la Mzee Dismas lilikuwa hili (nitalisema kwa lugha ya picha), ambalo aliona fika kabisa hawezi kusamehewa na Mungu. “Padre, nilivyokuwa na umri wa miaka saba hivi nilikwenda njia panda na kubadilisha vibao vile elekezi. Kibao kilichoonyesha Dar  es Salaam kuelekea Dodoma, nilikigeuza na kilisomeka Dar es Salaam Iringa. Je, ni wangapi nimewapeleka pasipo tangu nikiwa na miaka 7 hadi leo? Mungu gani anayeweza kunisamehe dhambi hii? Sipendi kumdanganya Mungu katika hili. Nipo tayari kupata adhabu yake," Mzee Dismas aliyasema haya akiwa na hofu kubwa.

Padre kwa kutambua hofu aliyokuwa nayo Mzee Dismas juu ya tatizo lake, alianza na maneno haya, “ndugu yangu Dismas, huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Bwana anasema na anakuambia leo maneno haya mazito kwako, ‘Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,’ Isa 1:18. Je, maneno haya hayana uzima ndani yako? Sote tunahitaji huruma ya Mungu. Yatupasa sote kukubali udhaifu wetu na kutii maelekezo ya Mungu.” Baada ya maneno haya Mzee Dismas alivuta pumzi na kupumua kwa nguvu kama vile mtu aliyetua jiwe kubwa sana kifuani mwake.

Uso wa Mzee Dismas ulionekana wenye furaha na kukubali kuungana dhambi zake na kuwa tayari kupokea huduma ile ya Ekaristi Takatifu na Mpako wa Wagonjwa. Ndugu zangu, katika kipindi hiki cha majilio tunavyojiandaa kiroho yatupasa kuyatafakari maneno haya ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa undani wake. Yesu anatuambia, Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi,” Mt 11:28-30. Hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Tujiachie kwake bila kujibakiza. Wokovu ndiyo sasa.

Ndugu zangu, niwatakieni majilio mema na yenye kumtafuta Bwana wetu na haki yetu kwa nguvu zote. Tuyarudi maisha yetu kwa kuyatazama madhaifu yetu na kuyapatia tiba ya kweli tukimtazama tabibu wetu Yesu Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo!


Wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu,” Lk 5:31-32

viernes, 27 de noviembre de 2015

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 34 YA MWAKA-B

JUMAMOSI WIKI YA 34 YA MWAKA-B
28/11/2015
Somo: Dan 7:15-27
Zab: Dan 3:82-87
Injili: Lk 21:34-36
Nukuu:
Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande,” Dan 7:23

Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati,” Dan 7:25

Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii,” Dan 7:27 

Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo,” Lk 21:34 

Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36

TAFAKARI: “Tumeumbwa ili tunafanane na Kristo kila siku ya maisha yetu, na kwa kupitia Yeye tuurithi ufalme wa mbinguni.”

Wapendwa wana wa Mungu, licha ya kwamba Mungu alichagua kutuumba kwa sura na mfano wake kwa sifa na utukufu wake, na kutupatia heshima kubwa kuliko viumbe vyote, alipenda pia tuwe na mahusiano naye. Hivyo sababu ya tatu ya kuumbwa kwetu, Mungu anapenda tufanane na mwanaye Yesu Kristo ili kwa kupitia Yeye tuurithi uzima wa milele. Ni jukumu la kila mbatizwa kila siku ya maisha yake kufanana na Kristo kwa sababu, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo,” Mdo 4:10-12. Hivyo maisha yetu hapa duniani siyo maisha ya anasa na furaha tu kwa sababu hakuna mbingu hapa duniani.

Katika Injili ya leo Yesu anatupa angalizo kuhusa maisha yetu hapa duniani. Naye anasema, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo,” Lk 21:34. Kwa vile hatuijui siku ya kiama yetu, yatupasa kuwa macho huku taa zetu zikiwa zinawaka kama wale wanawali watano wenye busara, Mt 25:4. Katika kile kituo cha tisa katika simulizi la mateso ya Yesu, njia ya msalaba, tunaambiwa kwamba Yesu anaanguka mara ya tatu. Moja ya mateso tunayomzidishia Yesu ni dhambi hii kama sala isemavyo, “mara nyingi mno ninajibovusha kwa kupenda mno starehe, anasa na tafriji.” Maisha yetu hapa duniani ni mafupi sana ukilinganisha na maisha ya umilele. Kila mmoja wetu anapaswa kuyapa maisha haya kipaumbele akilenga maandalizi ya maisha ya umilele. Katika jambo hili Yesu anatuambia, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika haya yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu,” Lk 21:36. Kukesha huku ni kufanana na Kristo kila siku kwa kutenda mema na kuishi utakatifu ule aliouishi ukijipokea kama ulivyo binadamu. Kuishi kama Kristo ni kuishi katika maisha ya utakaso. Ni kurejesha ile sura na mfano wa Mungu ndani yetu ilipotezwa na kuchakazwa na dhambi. Huu ndio ufalme aliokuja kuusimika Yesu Kristo duniani, yaani, kurudisha taswira ile ya Mungu ndani ya mioyo ya wanadamu.

Kazi hiyo ya Yesu inafunuliwa katika ndoto ya Nabii Danieli miaka mingi kabla. Akanena hivi, Huyo mnyama wa nne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande,” Dan 7:23. Kazi yake ya kwanza ni kuushinda uovu kwa wema. Nasi kila moja kwa nafasi na wito wake kama mbatizwa analo jukumu hilo, kuushinda uovu kwa kutenda mema. Hivyo kwa kushirikishwa kazi hii ya ukombozi kila mmoja kwa nafasi yake, na kuitenda kwa uaminifu na uadilifu, ndipo  utakapokuwa utakatifu wa kila mmoja wetu. Ni kutoa ushuhuda wa kweli katka maisha ya kawaida ya kila siku kwa kila mmoja kadiri ya nafasi na wito wake. Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii,” Dan 7:27.

Ndugu yangu, kwa nguvu zetu na maarifa yetu hatuwezi kamwe kuwa kama Yesu pasipo msaada ya Roho Mtakatifu. Twamwitaji Roho Mtakatifu kutuongoza na kutufunulia yale yaliyojificha katika maisha yetu. Roho huyu atatuongoza na kufanya njia pale pasipo na njia. 

Tumsifu Yesu Kristo!


Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu,” Rum 14:17