JUMATATU WIKI YA 5 YA KWARESMA
Somo:
Dan 13:1-9, 15-17, 19-30, 33-62,
Somo
fupi: Dan 13:41c-62
Zab:
23:1-3a, 3b-4, 5, 6
Injili:
Yoh 8:1-11, Au Yoh 8:12-20
Nukuu:
“Ewe mzao wa Kaanani,
wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako. Hivyo
ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu
binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako,” Dan 13:56-57
“Mara hiyo makusanyiko
yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio,” Dan
13:60
“Yeye asiye na dhambi
miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.” Yoh 8:7
“Wala mimi sikukuhumu.
Enenda zako; wala usitende dhambi tena.” Yoh 8: 11b
“Basi Yesu akawaambia
tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani
kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima,” Yoh 8:12
“Ninyi mwahukumu kwa
kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu,” Yoh 8:15
“Nami nijapohukumu,
hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi na yeye
aliyenipeleka,” Yoh 8:16
TAFAKARI:
“Mungu mtetezi wa wanyonge, haki na hukumu vina Bwana Mungu wetu.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo tutafakari neno hili, “Mungu mtetezi wa wanyonge, haki na hukumu
vina Bwana Mungu wetu.” Wanyonge mara zote huishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu.
Kujisalimisha kwao katika unyonge wao ndiyo njia pekee iliyobaki. Haki na mastahili
ya mtu ni moja ya asili wake. Binadamu kwa hulka yake (hali ya kutokuwa na utoshelevu
na u mimi) na nafasi yake kijamii huvuka mipaka na kuvitwalia haki na mastahili
ya wengine (hasa wanyonge) kwa mabavu (ikiwa ni pamoja na kuzipindisha sheria).
Kunapokuwa na hali hii, mtetezi wa huyu mnyonge ni Mungu tu, ambaye kwa asili ndiye
aliyevifanya hivyo vyote ndani ya mwanadamu.
Somo letu la leo pamoja
na Injili, yanatufikirisha ni nini hasili ya haki na hukumu kwa lililo haki na
kweli. Binadamu kwa hulka yake ya kujipendelea yeye zaidi, hupora haki ya
binadamu mwenzake kwa tamaa zake. Mtume Yakobo anasema, “Lakini kila mmoja
hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile
tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa
mauti,” Yak 1:14-15. Wazee ambao kutokana na mang’amuzi yao kimaisha
walitegemewa sana kuwa watu wenye hekina, na hivyo kusimamia kweli na haki.
Lakini kwa bahati mbaya wanaheshimu tamaa zao za mwili na kudondoka katika
uovu.
Kutokana na tatizo hilo
katika jamii, Susana anakuwa mmoja ya wale ambao hukandamizwa na kuporwa haki
zao. Susana katika hali hii, kimbilio lake na usalama wake unabaki kuwa ni
Mungu anayeona yote kwa hali na nyakati zote. Susana anajisalimisha kwa Mungu
katika unyonge wake kwa kusema, “Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika,
wajua mambo yote yasijekuwako, Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na,
tazama, imenipasa kufa; walakini sikufanya kamwe mambo kama hayo, ambayo watu
hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi.” Dan 13:42-43. Ni katika kujiachia huku kwa
Mungu aliye hai, Mungu anasikia kilio cha Susana na kutoa utetezi wake na
kumsimamisha kijana Danieli ambaye anatenda kweli na haki ya Mungu.
Danieli anakuwa mfano
bora na wakuigwa katika jamii kwa kuona uovu ule na kusimama kutetea kweli.
Danieli anawaonya hata wale waliokuwa na kauli nzito katika jamii, yaani wazee
ambao kwa kuwashwa na tamaa zao wanashindwa kutenda haki na kusimamia kweli.
Danieli katika jamii yetu leo anasimama badala ya wasomi hasa waliobobea katika
fani ya sheria, ila kwa kuwaka tamaa zao na uroho wa mali wanashindwa kusimamia
haki na kweli kwa wote na hasa wanyonge. Danieli anasimama katika nuru ya
kweli, na ndani yake umo uzima. “Yesu
anasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,
bali atakuwa na nuru ya uzima,” Yoh 8:12
Ni katika nuru na uzima
huu Danieli anayasema maneno mazito kwa watesi wa Susana bila kupepesa macho,
“Ewe mzao wa Kaanani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa
imeupotosha moyo wako. Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa
hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako,”
Dan 13:56-57. Mmoja kati yetu anaposimama katika kweli, na kutenda haki, Mungu
huonekana katika tendo hilo kupitia mtu huyo. “Mara hiyo makusanyiko yote
wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awaokoaye wamtumainio,” Dan 13:60.
Ndugu yangu, usiache kutenda mema na kusimama katika kweli. Kutokufanya hivyo
ni kumsaliti Mungu aliye kweli, haki, huruma, upendo na hukumu zake zina Yeye
daima.
Tukio la Susana
linatuonyesha ni kwa namna gani watu wengi na hasa wafungwa wanavyoweza jikuta
katika hali ya ufungwa pasipo haki na ukweli, na wakati mwingine hata kupoteza
maisha na mali zao. Na si jambo la kushangaza, wezi wakubwa na wahujumu wa
kubwa wa uchumi wa nchi hii kuwaona mitaani wakifurahia maisha. Jambo hili si
kwamba Mungu haoni, ila lina muda na wakati wake. Mungu kwa kutumia watu wake
ipo siku atamsimamisha mmoja kati yetu kama Danieli na yote yatakuwa sawa.
Injili yetu ya leo
inasema jambo hilo hilo juu ya kutokuwa na haki sawa kwa wote, ambapo mizani ya
hukumu huegemea upande mmoja. Injili inatupa angalizo pia pale tunapotaka
kupingana na Mungu na hata kumjaribu. Yesu anapoletewa mbele yake Mwanamke
mzinifu, watu hawa, ambao wakiwemo na Wazee, wanataka kumtia hatiani. Yesu Kristo
anatambua uovu wao na kuzikumbusha dhamiri zako zilizokufa. Yesu anafufua ndani
ya waovu hawa neema na uelewa wa amri ya mapendo. Upendo ambao wameufifisha kwa
kutenda uovu, Yesu Kristo anaufufua dhamiri hiyo iliyokufa na kuwafanya watende
mema. Kipimo cha kutenda mema ni wao wenyewe kwa kujiweka katika hali ya
wanyonge na wale ambao haki zao zinafinyangwa. Zoezi hili la dhamiri Yesu
analifanya baada ya kutafakari na kujua uovu wao, na kusema “Yeye asiye na
dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.” Yoh 8:7. Kwa maneno
haya siyo kwamba Yesu anatutaka tusitoe haki kwa njia ya sheria na hukumu iliyo
kweli. La hasha! bali tunapolifanya jambo hili, tujipime kwanza kama na sisi
tunayo mastahili hayo mbele ya Mungu. Vile vile, Yesu anatukumbusha kwamba,
uhai ni zawadi ya Mungu kwetu, na ni mali yake Mungu. Hukumu yoyote ile kabla
na baada itanguliwe na huruma na upendo
wa kweli.
Ndugu yangu, huruma na
msamaha wa kweli, ni dawa na njia mwafaka wa kumrekebisha aliyetenda kosa. Mara
nyingi watu wengi hawabadiliki tabia zao kwa sababu hawajawahi samehewa wala kuonewa
huruma. Unapomsamehe mtu kwa kosa ambalo anajua wazi si rahisi kusamehewa,
msamaha huo huwa dawa ya ugonjwa wake wa muda mrefu. Yesu Kristo anatumia njia
hii kwa mwanamke huyu mzinifu, na kusema, “Wala mimi sikukuhumu. Enenda zako;
wala usitende dhambi tena.” Yoh 8: 11b. Furaha aliyoipata mwanamke huyu ni
kubwa sana. Inawezekana katika maisha yake, hakuwahi kupata msamaha kama huu.
Hapa pia tunajifunza kwamba, “Mungu mtetezi wa wanyonge, haki na hukumu vina Bwana
Mungu wetu.” Ndugu yangu, kwa nini unakosa huruma na msamaha wa kweli hasa
katika hali kama ya huyu mwanamke aliyokuwa nayo? Je, wasubiri kupigiwa chetezo
na matari?
Tumsifu Yesu Kristo.
“Nami nijapohukumu, hukumu yangu ni
kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi na yeye aliyenipeleka,” Yoh
8:16
Tusali:-Ee
Bwana, unifanye chombo cha amani yake. (Mt. Franscisco wa Assis).
No hay comentarios:
Publicar un comentario