JUMATATU WIKI YA 3 YA PASAKA
Somo: Mdo 6:8-15
Zab: 119:23-24, 26-27, 29-30
Injili: Yoh 6:22-29
Nukuu:
“Wakasimamisha
mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya
mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana
tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na
kuzibadili desturi tulizopewa na Musa,” Mdo 6:13-14
“Watu wote walioketi katika ile baraza
wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika,” Mdo 6:15
“Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin,
nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa sababu mliona ishara, bali kwa sababu
mlikula ile mikate mkashiba,” Yoh 6:26
“Msikitendee kazi chakula chenye
kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu
atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu,” Yoh
6:27
“Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo
kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye,” Yoh 6:29
TAFAKARI: “Mwenye haki ataishi Milele, kazi ya
Mungu, ni kumwamini Kristo mwana wa Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu, masomo yetu la
leo yanatualika kutafakari neno hili, “mwenye haki ataishi Milele, kazi ya
Mungu, ni kumwamini Kristo mwana wa Mungu.” Stefano anakuwa shahidi wa kwanza
anaposimama katika kweli na kuiishi. Akiwa mtu aliyenena na kuongozwa na Roho
Mtakatifu, Shahidi Stefano anajikuta katika mzozo mkubwa na Wayahudi ambao
hawakupenda, kusikia, wala kusadiki mambo yote aliyoyafanya Yesu Kristo.
Stefano anaundiwa genge na zogo na mwisho kutungiwa uongo ili kumwangamiza. “Wakasimamisha
mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya
mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana
tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na
kuzibadili desturi tulizopewa na Musa,” Mdo 6:13-14
Stefano shahidi anakuwa
mbegu ya kwanza ya Imani kuoteshwa katika jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Watu
wenye mtazamo wa Stefano katika jumuiya ya Wakristo hata sasa wapo. Unapojaribu
kusimama katika kweli, na kuishi kweli hiyo, jiandae kusongwa na mambo mengi.
Kwanza utatungiwa majina ya ajabu ili tu ukatishwe tamaa. Utatungiwa uongo
mwingi tu, ili uchafuliwe na Kristo achafuliwe. Unapomkiri Kristo katika kweli
na haki, unatangaza vita dhidi ya giza. Je, katika hali hii nini cha kufanya?
Kamwe usiache kusimama katika kweli na kunena lililo kweli hata ikikubidi kufa.
Stefano shahidi hakuacha kulisema lililo kweli na hata kulisimamia. Jibu katika
kweli hii linaonekana hata kabla hajakijongea kifo kile cha kupigwa mawe hadi
kufa. “Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona
uso wake kuwa kama uso wa malaika,” Mdo 6:15.
Ndugu yangu, Kristo
pekee ndiye mwenye kutuhesabia haki katika vita hivi vya mwanga dhidi ya giza.
Ni katika Kristo, na ndani ya Kristo tunaweza kushinda vita hivi kwa sababu
yeye kesha vishinda. Je, unamwamini Kristo? Wapo wengi waliokuwa wanamfuata
Kristo ila kwa malengo ya hapa na sasa tu, wala siyo imani ya kweli. Wengi
walipenda kumfuata Kristo kutokana na miujiza aliyokuwa akiifanya. Hivyo
walikuwa watu wa mshangao tu, na matukio. Wengi walimfuata wakijua kwa uwepo
wake utawahakikishia shibe. Mtazamo wa Kristo na watu hawa wa shibe, hauna
tofauti ma mahusiano ya fisi na Simba. Fisi anamatumaini makuwa kuwa akiwa na
Simba hawezi kukosa masalia ya mzoga.
Yesu Kristo analiona
hili mapema na kuwakemea wale waliokuwa wanamtafuta na kumwulizia kwa shahuku.
“Yesu akawajibu, akasema, Amin, amin, nawaambieni, Ninyi mnanitafuta, si kwa
sababu mliona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba,” Yoh 6:26.
Swali ni kwamba, je, ukipata mahitaji yako yote ya kila siku, Kristo bado ana
nafasi tena katika maisha yako? “Msikitendee kazi chakula chenye kuharibika,
bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu atawapa,
kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu,” Yoh 6:27
Wapendwa, tunaye Mtu
mmoja tu anayeweza kutufunulia siri za mbinguni na uzima wa milele. Mtu huyu ni
Kristo. Kujua siri za ufalme wa mbingini hatunabudi kumjua Kristo na kufuata
matafundisho yake. Kristo ndiye mwenye mamlaka yote ya ufalme wa mbinguni.
Ndiye aliyetiwa muhuri na Baba. Je, ni nini cha kufanya? Jambo la msingi kupita
yote ni kumwamini Kristo. “Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu,
mmwamini yeye aliyetumwa na yeye,” Yoh 6:29. Ulimengu tunaoishi sasa, baadhi
yetu siyo kwamba tu kwamba hawamwamini Kristo, bali hawapendi kusikua habari
zake.
Ni jukumu la kila
Mbatizwa na hasa wale waliopewa mamlaka hayo kutoa katekesi ya kina kuhusu
uhusiano nadharia kati ya maisha ya kila siku ya Mkristo na kile anachoamini.
Mara nyingi, wanachohubiriwa watu hakigusi maisha yao. Kristo anabaki kuwa ni
ukweli fulani unaoelea katika urefu fulani ambao hatuwezi kufika kwa urahisi.
Kristo anakuwa si tena yule Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi. Mfanye Kristo
kuwa Rafiki yako wa karibu, na anza kumuishi kuanzia hapo ulipo na hao
wakuzungukao. Kulifanya jambo hili kwa ukweli na kumwamini Kristo, ni kielelezo
tosha cha uinjilishaji wako mpya hapo ulipo. Leo tunaitaji sana ushuhuda huu wa
ukimya.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Msikitendee kazi chakula chenye
kuharibika, bali chakula kidumucho hata uzima wa milele; ambacho Mwana wa Adamu
atawapa, kwa sababu huyo ndiye aliyetiwa muhuri na Baba, yaani, Mungu,” Yoh
6:27
Tusali:-Ee
Yesu Kristo, tujalie neema ya kuijua kweli yako na kuishi kweli hiyo katika
maisha yetu ya kila siku. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario