sábado, 15 de abril de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI YA OKTAVA YA PASAKA


ALHAMISI YA OKTAVA YA PASAKA

Somo: Mdo 3:11-26

Zab: 8: 2ab, 5, 6-7, 8-9

Injili: Lk 24:35-48

Nukuu:

Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu,” Mdo 3:19-21.

“Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi,” Mdo 3:13-15.

Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu,” Lk 24:36.

Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo,” Lk 24:39.

“Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya,” Lk 24:46-48.

TAFAKARI: “Amani iwe kwenu; ni Salamu, Zawadi na Mtazamo mapya wa maisha ya Ufufuo na Uzima.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, maisha ya ufufuko ni maisha ya amani ya kweli ndani ya kila mmoja wetu anayeamini ufufuko wa Kristo. Ni kwa maana hii leo tunaalikwa kutafakari neno hili, “amani iwe kwenu; ni Salamu, Zawadi, na Mtazamo mpya wa maisha ya Ufufuo na Uzima. Amani kama maisha ya ufufuo na uzima yanajionyesha na kutendeka wazi katika jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Mtume Petro haogopi kulisema hili mbele ya Wayahudi wenye itikadi kali za kidini na hasa juu ya Yesu Kristo waliyeutoa uhai wake bila huruma. “Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu, ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule Mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi,” Mdo 3:13-15.

Wapendwa kwa kosa hili la kumwua aliye uzima, yaani, Bwana wetu Yesu Kristo, kurejesha huruma na msamaha wa Mungu, yatupasa kufanya toba ya kweli. Neema na baraka huja kwa kukiri pale tulipojikwaa kwa kujua na hata kwa kutokujua, kunakotokana hasa na kutotimiza wajibu wetu wa kila siku. Toba ya kweli ndicho kielelezo cha kujenga tena urafiki na uhusiano na Mungu ambao ulibomolewa kwa dhambi zetu, na tunazidi kuubomoa kwa dhambi zetu hata sasa. Daraja la kuelekea upatanisho huo na Mungu, limekwisha jengwa tayari kwa sadaka ya Kristo pale msalabani. Naye Petro anasema, “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu,” Mdo 3:19-21

Wapendwa wana wa Mungu, kwa sasa twaweza kuuona uso wa Mungu kwa kupitia kwanaye Yesu Kristo. Hivyo kupatanishwa na Mungu kunawezekana tu kwa kupitia mwanaye Yesu Kristo ambaye hata sasa Kanisa linamshuhudia. Kanisa kama chombo katika safari ya kuelekea uzima wa milele, na Sakramenti ya Wokovu, kinatuwezesha kwa kupitia maadhimisho ya Sakramenti zake kuuona uso wa Mungu baada ya kushiriki Sakramenti hizi kwa uaminifu wa kweli. Ndugu yangu, leo tunapatanishwa na Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo, kwa Sakramenti ya kitubio. Na hapa kwa namna ya pekee tunaonja upya huruma na neema ya Mungu. Je, lini ilikuwa mara yako ya mwisho kupokea sakramenti hii?

Injili ya leo inatuelekeza kuyaona maisha ya Uzima na Ufufuo kupitia Amani ya kweli ndani mwetu. Zawadi ya Yesu Mfufuka kwa wanafunzi wake na wale wote waliomridhia ni Amani. “Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu,” Lk 24:36. Baada ya tukio hili, amani inakuwa ndicho kielelezo cha maisha ya Uzima na Ufufuo. Hakika Mungu hapatikani katika fujo na machafuko yanayosababishwa na tamaa na ubinafsi wetu. Uhakikisho huu, yaani, Amani ndani ya mioyo ya Wakristo wa kwanza unaondoa woga na mashaka yote. Kristo yu hai kweli kweli na siyo hadithi za kufikirika. Yesu Kristo anawaambia wanafunzi wake waliokuwa wamejificha kwa hofu, “Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo,” Lk 24:39

Hili ni hakikisho la wazi kwamba Yesu Kristo hakuwa mzimu fulani katika hali yake ya kufufuka kwake. Hivyo kuthibitisha kwamba yeye si mzimu, alikula pia kipande cha samaki wa kuoka kuwahakikishia alikuwa mtu kweli baada ya ufufuko wake. Mtazamo huu, ndio mtazamo wa Kanisa leo, licha ya changamoto nyingi tunazozipata nje ya Imani yetu ya Kikristo ambao kwao wanataka kutulazimisha na kutufanya tuamini kwamba kilichotokea kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kilikuwa ni mchezo wa kuingiza. Kwa mantiki hiii, Kristo Mfufuka anasisitiza kwa kusema, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya,” Lk 24:46-48. Ndugu yangu uliyeimarishwa, wewe ni shahidi kweli wa Kristo?

Wapendwa katika Kristo, hapana shaka kabisa kwa sasa wengi wetu tunaishi kwa hofu kubwa sana tunapoona Wakristo wenzetu wanauwawa kwa ukatili uliokithiri kwa sababu tu wao ni Wakristo. Hata hivyo tusisahau ukweli kwamba hata Kanisa hili tunaloishi leo na kushuhudia imani, limekuwa Imara kama lilivyo kutokana na Damu za wafiadini waliotutangulia kwa nyakati tofauti katika historia ya Kanisa letu. Bila shaka ni wakati wetu pia kutoa ushuhuda huo kwa kufa kifo Dini na Imani ya kweli.

Tumsifu Yesu Kristo!

Yesu Akawaambia, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya,” Lk 24:46-48

Tusali:-Ee Yesu Kristo, katika hali hii ya sintofahamu juu ya Imani na Ukristo wetu leo, tujalie neema ya kufa kifo dini katika Imani ya kweli. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario