JUMAMOSI WIKI YA 5 YA KWARESMA
Somo:
Eze 37:21-28
Zab:
Yer 31:10, 11-12abcd, 13
Injili:
Yoh 11:45-56
Nukuu:
“Tena nitafanya agano
la amani pamoja nao, litakuwa agano la milele pamoja nao. Nami nitawaweka na kuwazidisha,
na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele,” Eze 37:26
“Ninyi hamjui neno
lolote; wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala
lisiangamie taifa zima,” Yoh 11:49-50
“Na neno hilo yeye
hakulisema kwa nafsi yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule,
alitabiri ya kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa hilo. Wala si kwa ajili ya
hilo tu; lakini pamoja na hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili
wawe wamoja.” Yoh 11:51-52
TAFAKARI:
“Mungu katika wema na upendo wake; Binadamu katika hila, chuki, na uasi wake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tufafakari neno hili, “Mungu katika wema na upendo wake; Binadamu katika
hila, chuki, na uasi wake.” Umoja na Upendo ni kati ya sifa kuu za Mungu na
zenye kuonyesha asili yake. Mara zote tunapotafakari historia ya wokovu wetu,
hatuachi kuona sifa na uhasili huu wa Mungu. Ni katika kujifunua kwake kwa
mwanadamu tunaona Upendo wake wetu, na nikatika kufanya nasi maagano tunaona
Umoja wake kwetu.
Mungu kwa hali na mamna
alivyo, haitaji chochote kutoka kwetu ili ajikamilishe. Ila ni furaha yake kuwa
nasi kwa sababu uwepo wetu unaufunua uzuri wake kwa sababa sisi ni viumbe vyake
na kuwa sehemu ya tafakari ya Utakatifu wake Mungu. Mt. Franscisco wa Assis
anatufundisha sana jambo hili. Zaidi ya kuwa viumbe vyake kwa upendeleo mkubwa
sisi binadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wake. Tendo hili linatufanya viumbe
shirikishwa katika kazi ya uumbaji ya Mungu. Upendo huu wa ajabu hakupewa
Malaika. Kapewa tu mwanadamu.
Ukaribu wa Mungu na
utayari wake kwetu nyakati zote, unafunua wema na upendo wake kwetu. Ni katika
hali hii Mungu haachi wala hachoki kutukusanya kama vifaranga vyake ili tuwe
wamoja kama yeye katika umoja wao-Utatu Mtakatifu. Ni kwa kupitia hali hii ya
Kimungu, Mungu huendelea kufanya maagano nasi. “Tena nitafanya agano la amani
pamoja nao, litakuwa agano la milele pamoja nao. Nami nitawaweka na
kuwazidisha, na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele,” Eze 37:26.
Ndugu yangu wautambua upendo huu na wema huu wa Mungu kwako?
Kwa upande mwingine,
licha ya wema na upendo wa Mungu kwetu, binadamu anachagua hila, chuki na uasi
kwa uhuru wake mwenyewe. Taswira na hali hii yajionyesha kwenye Injili yetu ya
leo, ambapo Wayahudi wanamwinda Yesu Kristo ili wamuue. Wema na Upendo wa Mungu
kwetu, twaulipa kwa hila, chuki na uasi. Vita hii dhidi ya Mungu binadamu
hawezi kufanikiwa kamwe. Tazama hila za binadamu: -“Ninyi hamjui neno lolote;
wala hamfikiri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, wala
lisiangamie taifa zima,” Yoh 11:49-50. Binadamu kutokana na hila, chuki, na
uasi, yupo tayari kutumia muda wake, mali zake, na hata akili zake ili mradi tu
kuharibu wema na upendo wa Mungu.
Ikiwa mwenzako na
jirani yako kaumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, unapomtendea hila, chuki, na
hata kumwangamiza, unapigana na Mungu mwenyewe. Vita hii huwezi shinda. Waweza
kuutoa uhai wa mtu huyo ili upata unachotaka, ila ni kwa muda tu. Na kamwe
huwezi kufupisha au kuondoa mpango wa Mungu wa umelele kwa yule uliyeutoa au
kuukatisha uhai wake. Yesu Kristo katika hili anasema, “msiwaogope wauuao
mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili
na roho pia katika jehanum,” Mt 10:28. Kwa hila, chuki, na uasi wa mwanadamu
hufanikiwa kwa muda mfupi tu, umelele na enzi una Mungu daima.
Licha ya hila, chuki,
na uasi wa binadamu, havimzuii binadamu huyu kufikiri au kufikirishwa njia
iliyo kweli ya Mungu. Katika ubaya wake na matendo yake binadamu, Mungu huweza
kutumia tendo hilo kufanikisha mpango wake wa umilele. Jambo hili linajionyesha
katika utabiri wa Kuhani Mkuu Kayafa. “Na neno hilo yeye hakulisema kwa nafsi
yake; bali kwa kuwa alikuwa Kuhani Mkuu mwaka ule, alitabiri ya kwamba Yesu
atakufa kwa ajili ya taifa hilo. Wala si kwa ajili ya hilo tu; lakini pamoja na
hayo awakusanye watoto wa Mungu waliotawanyika, ili wawe wamoja.” Yoh 11:51-52
Pamoja na naono hayo,
na ufunuo huu wa tendo hili la Kimungu, Binadamu aliyezama katika hila, chuki,
na uasi, na kutompa Mungu nafasi huendelea na utekelezaji wake wa uovu. Je, kwa
nini Mungu hazuii jambo hili kutokea? Ndugu yangu, Mungu akutuumba kama
“maroboti,” yenye kufanya kazi kwa kuongozwa kama mitambo. Mungu katuumba watu
wenye akili na utashi wa kupembua mema na mabaya. Uwezo huu ndani yetu ndiyo
hukumu yetu tusipotumia vyema, na ndiyo salama yetu tunapotumia vyema.
Ndugu yangu, usichoke
kutenda mema. Kutenda mema ni kuwa upande salama wa Mungu, na ndicho Kristo
anachotufundisha kufanya kila siku ya maisha yetu. “Basi wapendeni adui zenu,
tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi;
nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na
waovu,” Lk 6:35.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi wao wakamtafuta Yesu,
wakasemezana hali wamesimama hekaluni, Mwaonaje? Haji kabisa sikukuu hii?” Yoh
11:56
Tusali:-Ee
Yesu, niongoze mara zote kwa lile lililo jema na lenye kuufunua uzuri wa Mungu
wetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario