jueves, 13 de abril de 2017

TAFAKARI: VIJILIA YA PASAKA-A


KUFUFUKA KWA BWANA

USIKU MTAKATIFU

VIJILIA YA PASAKA

Somo I: Mwa 1:1-2:2

Somo II: Mwa 22:1-18

Somo III: Kut 14:15-15:1

Somo IV: Rum 6:3-11

Zab: 118:1-2, 16-17, 22-23

Injili: Mt 28:1-10

Nukuu:

Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26

“Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba,” Mwa 1:27

Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi,” Mwa 1:28

“Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia,” Mwa 22:2

“Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,” Mwa 22:12

Katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu,” Mwa 22:17-18

“Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake,” Kut 14:17

“Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini,” Kut 15:1

“Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima,” Rum 6:4

“Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu,” Rum 6:10-11

“Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia,” Mt 28:1b-2 

Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu,” Mt 24:3-4

Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa,” Mt 28:5-6

“Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona,” Mt 28:9-10

“Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka,” Mk 16:6 

“Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia,” Mk 16:7

Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta; nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?” Lk 24:4-5

“Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya, akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya tatu,” Lk 24:6-7

“Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine waliokuwa pamoja nao; hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo. Maneno yao yakaonekana kuwa kama upuzi kwao, wala hawakuwasadiki,” Lk 24:10-12a

“Lakini Petro aliondoka akaenda mbio hata kaburini, akainama akachungulia ndani, akaviona vile vitambaa vya sanda tu; akaenda zake akiyastaajabia yaliyotukia,” Lk 24:12b

TAFAKARI: “Mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa, amefufuka; yupo nasi kila siku katika maisha yetu, na tunakutana naye Galilaya.”

Wapendwa wana wa Mungu, Usiku huu Mtakatifu, Mama Kanisa popote duniani anafanya Sikukuu kubwa sana, ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ni ushindi dhidi ya dhambi na Kifo. Ufufuko wa Yesu Kristo ni hitimisho la malengo ya Mungu kumkomboa mwanadamu, na ni hakikisho la umilele, na maisha mapya ndani ya Kristo, na katika Kristo kuelekea umilele. Hivyo Usiku huu Mtakatifu tunasoma habari hii Njema ya wokovu wetu kama ilivyoandikwa na Wainjili ‘fanana’ watatu, ikiwa kila mwaka kulingana na mwaka wa Kanisa tuliopo. Kwa namna hiyo, usiku huu tukiwa mwaka “A” wa Kanisa tunasikia simulizi hili kuu kama lilivyosimuliwa na Mwinjili Mathayo 28:1-10. Kwa mwaka “B” wa Kanisa tulisikia kutoka Mwinjili Marko 16:1-8, na kwa mwaka “C” wa Kanisa tulisikia simulizi hili kuu kutoka Mwinjili Luka 24:1-12.

Wapendwa wana wa Mungu, masomo yote ya agano la Kale tuliyoyasikia usiku huu Mtakatifu, yanatupatia historia nzima ya wokovu wetu. Kwa maana hiyo, uwepo wetu hapa duniani si wa bahati mbaya, wala wewe kuwa katika ulimwengu huu si kwa bahati mbaya. Ulimwengu umeumbwa kwa Upendo wa Mungu kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine ulimwengu huu kama ulivyo umemlenga mwanadamu na kwa lengo la kumweka huru.

Msingi wa haya yote, na sababu yake, tunauona kwenye kitabu cha mwanzo. Wakati ulipotimia na kufaa, Mungu aliumba ulimwengu kwa neno, na ukawa kama ulivyo. Ni siku ya sita alipoona inafaa na kumpendeza akamwumba mwanadamu kwa sura na mfano wake. Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi,” Mwa 1:26. Kwa vile ulimwengu ulimlenga mwanadamu, ni binadamu huyu tu, anayepewa mamlaka ya kuvitawala vile alivyoviumba Mungu. Utawala huu siyo wa kujifanyia tunavyotaka, ila kuvimiliki katika maana ya kuvitunza ili viongezeka na kudumu. Tunapewa wajibu huu mkubwa kabisa ambao hata malaika hawakupewa.

Binadamu huyu kwa upendo wa Mungu, ameumbwa katika usawa. Hakuna mtumwa wala mtwana, au bwana na mjakazi. Wote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu tukiwa na mastahili sawa kati ya mwanaume na mwanamke. “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba,” Mwa 1:27. Mastahili haya yanaendana na wajibu wetu, kila mmoja kadiri ya jinsia yake. Kwa upande mwingine, haikumaanisha kwamba jinsia moja kuitawala nyingine kwa vigezo vya utamaduni wetu, mila zetu, makabila yetu, wala utaifa wetu. Mbele za Muumba wetu sote tu sawa.

Na ni kwa sababu hii, kunakuwa na uwezekano wa kuzaa na kuongezeka kadiri ya mpango wa Mungu. Ni kwa sababu hii binadamu anabarikiwa, anawezeshwa na anashirikishwa uumbaji wa pamoja akishirikishwa na Mungu. Binadamu anakua “Co-creator of God.” Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi,” Mwa 1:28. Ndugu yangu, pamoja na uhuru tuliopewa, Mungu hakutupa mamlaka ya kubadili mpango wake ndani yetu.

Leo kutokana na ufahamu wa binadamu kuongezeka katika kuyafahamu yanayomzunguka, amefikia hatua ya kumkosoa Mungu, na kufanya kinyume cha kile alichokinuia. Leo wapo baadhi yetu wangependa na wanapigana kwa nguvu zao zote kujigeuza jinsia zao na kuwa vingine. Hili ni kosa ndugu yangu. Kuwa kile alichokufanya; yaani sura na mfano wake. Tuelewe kwamba ufahamu wa binadamu wote na wenye kustaajabiwa, ni ujinga wa Mungu. Yatupasa kufuata mapenzi na matakwa ya Mungu. Hivyo, “Kumcha Bwana ni mwanzo wa hekima; Na kumjua Mtakatifu ni ufahamu,” Mit 9:10.

Kuishi Imani hii na mwelekeo huu wa Mpango wa Mungu, utapimwa kila wakati. Mungu utupima imani yetu juu yake. Katika safari nzima ya mwokovu wetu, tumeona watu mbalimbali wakipimwa imani zao. Ibrahimu ni mfano nzuri ya Imani na Utii kwa Mungu. Mungu anamjaribu Ibrahimu,  “Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia,” Mwa 22:2. Kwa utii Ibrahimu anafuata maagizo ya Mungu, licha ya kuwa na mtoto huyo tu mpendwa, na tena mtoto wa uzee wake.

Baada ya kufanya maandalizi hayo na kuchukua kisu ili amtoa sadaka mtoto wake, Mungu ananena na Ibrahimu, “Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,” Mwa 22:12. Mwitikio huu ya Imani na Utii unampatia baraka Ibrahimu. Katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu,” Mwa 22:17-18. Mungu Muumba wetu ni Mungu mwenye wivu katika maana ya viumbe vyote twapaswa kumrudia na kufanya kadiri ya matakwa yake, ingawa twaweza kukataa. Ila tukitaka baraka na neema yatupasa kuyafanya yote kadiri ya matakwa yake.

Mipango ya Mungu ndani yetu ucheleweshwa na wakati mwingine kusubirishwa pale tunapoenda kinyume na mipango yake au kuandaliwa zaidi katika fumbo hilo tusilolijua bado. Jambo hili linajitokeza katika kitabu cha kutoka. Licha ya wana wa Israeli kukaa utumwani Misri kwa miaka mia nne na ushee, Mungu bado anampango na taifa lake teule. Ilipofikia wakati wake, Mungu anamtoa mmoja katikati yao, yaani Musa kuendeleza makusudi ya Mungu. Jambo hili halikuwa rahisi kwa Waisraeli kuendelea na mpango wa Mungu baada ya miaka yote hiyo. Ndugu yangu, wapo waliozaliwa Misri na kufia huko huko Misri. Wengine walikuwa na mababu waliozaliwa Misri na kufanya maneno ya Musa kwa maelekezo ya Mungu, kutosadikika na kueleweka. Ilikuwa vigumu kuyaacha maisha yale na kwende kule Mungu alipowaandalia.

Hivyo Mungu anaamua kuifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu ili Waisraeli watambue ujumbe wake na kuondoka. Misri hapakuwa hitimisho la Mungu. Mungu anamwambia Musa, “Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake,” Kut 14:17. Mungu hutumia mazingira na hali zetu za kila siku ili tuujue ujumbe wake. Je, unapopatwa na mazingira kama hayo unaweza kuzisoma alama za nyakati? Au, kila mara unapenda kupingana na Mungu?

Wana wa Israeli walipotambua mpango wa Mungu, na kutii, Mungu anatenda jambo kubwa juu yao. “Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia Bwana wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini,” Kut 15:1. Hakuna lisilowezekana kwa Mungu tunapoishi kadiri ya mpango na malengo yake kwetu.

Ni kwa upendo huo aliokuwa nao Mungu ndani mwetu wakati ulipotimia alimtuma mwanaye mpenzi kuikamilisha nia na makusudi yake. Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5. Kwa vile vyote viliumbwa kupitia Yesu Kristo, ni kwa namna hiyo Mungu alipenda kupitia kwake vyote vikombolewe. Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6. Kazi hiyo Kristo ameifanya na mwisho wa siku ilimgharimu maisha yake kwa ajili yako na yangu. Na kwa tendo hili leo dunia nzima inashuhudia wokovu huu.

Ndugu yangu, leo ni ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Je, unastaajabu? “Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka,” Mk 16:6. Wapendwa, kuna shuhuda mbali mbali za uthibitisho wa ufufuka wa Kristo. Zipo zile shuhuda ya mbali na karibu. Shududa za mbali ni pamoja na unabii uliotabiriwa juu ya Yesu Kristo, ikiwa ni pamoja na makusudi yake hapa duniani, na lengo lake mahususi. Pia Kristo mwenyewe amekuwa akilisimulia jambo hili la uteswa, kufa na kufufuka, (Mt 17:22, Mk 9:31, Lk 9:22, na Yoh 2:19)

Hatuna sababu yoyote ya kustaajabu mpango huu wa Mungu. Shuhuda za karibu, ni pamoja na Kaburi kuwa wazi. Huu ni ushuhuda kwamba Kristo hayupo na amefufuka. Uimara wa imani katika kumuhubiri Kristo, pamoja na ukuaji wa jumuiya ya kwanza ya Wakristo na hadi sasa Kanisa lake ulimwenguni pote, ni uthibitisho kwamba Kristo kafufuka na anaishi ndani mwetu hasa kwa wale waliomridhia. Je, sasa tunakutana na Kristo Mfufuka wapi?

Wapendwa katika Kristo, leo tunakutana na Kristo Mfufuka tunapoishi kwa uaminifu wito wetu, kila mmoja kadiri ya mpango wa Mungu. Hapo ndipo Galilaya yako. “Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia,” Mk 16:7. Mimi kama mtawa na padre, na wewe kama mlei, sote kwa nafasi ya upendeleo tunakutana naye kila siku ya maisha yetu tunapoishi kwa uaminifu wito wetu. Hii ndiyo Galilaya ambapo twaweza kumwona. “Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona,” Mt 28:10.

Wapo wengi miongoni kwetu, twaingiwa na kishawishi cha kutafuta maisha mbadala baada ya kukiri. Kubabaika huku ni kupoteza muda ilhali wakati na masaa hayatusubiri. Kengele itakapolia, hatutakuwa na sababu ya kujitetea. Tunapotazama masimulizi mbalimbali ya Maandiko Matakatifu na hasa Injili, utagundua kwamba yote yanalenga katika nia moja. Kufahamu makusudi ya Mungu, na mwisho wa safari kutokupata nafasi ya kujitetea kokote kule wakati wa kutoa hesabu ya maisha yako hapa duniani.

Leo usiku huu kupitia Injili hizi “fanana,” ufufuko wa Kristo umeturahisishia kujua sintofahamu yetu pale tunapojaribu kupoteza muda kwa kujiulizauliza kama nipo njia sahihi. Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya, akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya tatu,” Lk 24:6-7. Ujumbe huu wa malaika kwa bahati mbaya haupokelewi vizuri na Mitume wale wa Yesu. “Nao ni Mariamu Magdalene, na Yoana, na Mariamu mamaye Yakobo, na wale wanawake wengine waliokuwa pamoja nao; hao waliwaambia mitume habari ya mambo hayo. Maneno yao yakaonekana kuwa kama upuzi kwao, wala hawakuwasadiki,” Lk 24:10-12a. Ni wazi kutokupokeleka kwa habari hii njema na wanafunzi wa Yesu kunatufundisha uovu uliopo kwenye mila na desturi zetu juu ya mitazamo ya kijinsia.

Wapendwa wana wa Mungu, kadiri ya mila na desturi za kiyahudi, ushahidi kutoka kwa mwanamke haukuaminika kabisa. Lakini kadiri ya tendo hili la ufufuko tofauti zetu zilikwisha ondolewa kwa kifo chake Yesu pale msalabani, na hasa alipoitoa roho yake ikiendana na ishara ya kupasuka kwa pazia la hekeluni. “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi,” Mt 27:50-53. Ishara hii ni mwanzo mpya ndani na katika Kristo Yesu kwa kila mmoja wetu. Ni kwa mantiki hii, leo Kanisa linamtambua Maria Magdalene kama ‘Mtume wa Mitume,’Apostola Apostolorum. Leo Yesu anatuelekeza tutakapokutana naye. Na inanipasa kumwona Kristo Mfufuko kwa ye yote yule ninaye kutana naye. Hapo ulipo kadiri ya wito wako ndipo kwa kukutana naye. Ndugu yangu, jambo la msingi kupita yote ni kuboresha hali yako hapo ulipo.

Kuboresha hali hiyo ni pamoja na kujihoji nafsi kama unaishi kadiri ya huo wito ulioitiwa. Ukipata jibu la swali hili, hakika utakuwa njia moja na yule aliyekuita, Yesu Kristo akiwa dereva wa yote utakayofanya. Ni Kristo tu kwa kufufuka kwake na kuyashinda mauti anayejua usalama wa njia tusafiriyo kuelekea umilele. “Maana kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi mara moja tu; lakini kwa kule kuishi kwake, amwishia Mungu. Vivyo hivyo ninyi nanyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi na walio hai kwa Mungu katika Kristo Yesu,” Rum 6:10-11. Ndugu yangu ni nani kama Kristo katika maisha yako?

Wapendwa, tunapoifia dhambi pamoja na Kristo, kwa njia ya ubatizo, ni mwanzo wa maisha mapya pamoja naye. Hakuna utukufu pasipo msalaba. Na kufa kwetu huku kila siku na Kristo dhidi ya dhambi ndiko kunakotuweka salama kuelekea umilele. “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima,” Rum 6:4. Je, mateso na mahangaiko yangu ya kila siku nayachukulia kama sababu ya utakaso wangu?

Lucia, mmoja wa viongozi wa kikundi cha Wanalegio Maria, hakuwahi hata mara moja kuishi zaidi ya mwezi mmoja bila kuugua au kuuguza mara baada ya ndoa yake. Lucia akiwa na umri wa miaka 38, na miaka 15 ya ndoa yake, aligundulika kuwa na kansa ya kizazi. Jambo hili lilimtia majaribuni sana na wakati mwingine kukatishwa tamaa kwa kuona kwamba Mungu, na hasa kupita Mama Bikira Maria kutokuyasikia maombi yake.

Mara zote aliombea familia yake afya, ikiwa pamoja na yeye, lakini mambo hayakuwa hivyo. Wengi waliomwomba awaombee kwa nia mbalimbali, walirudi na kumshukuru kufanikiwa kwa maombi yao. Kwa upande wake hakuweza kuelewa nini sababu ya hali ile. Mara zote alijisemea moyoni hivi, “Nikifa na kubahatika kumwona Yesu, nitamwuliza swali hili, ‘kwa nini mara zote hukutaka kunisikia shida zangu na badala yake uliwasikia wengine kupitia mimi?’

Lucia akiwa na umri wa miaka 45, alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya kizazi. Mungu hakuacha kutimiza ile nia yake ya kumwona na kumwuliza Yesu swali lake. Mara alipomwona Yesu alijawa na huzuni na kumwuliza. ‘kwa nini mara zote hukutaka kunisikia shida zangu na badala yake uliwasikia wengine kupitia mimi?’ Yesu akamjibu, “Lucia, kuwa na furaha na amani moyoni mwako. Nimekuwa nawe muda wote wa maisha yako na sasa yale yote uliyokumbana nayo ndiyo hayo yaliyokufanya uhesabiwe haki na kuwa mahali hapa. Isitoshe napenda nikuonyeshe safari yako yote uliyoishi ukiwa duniani. Mimi ndiye Bwana.”

Mara wakatoka na kuanza kutembea na mara Yesu akasimama na kumwuliza Lucia. “Je, unaona nini mbele yako? Bwana naona nyayo za watu wawili wakielekea njia moja,” Lucia alijibu wa upole. “Basi upande wa kulia nilikuwa mimi, na upende wa kushoto ulikuwa wewe. Wakati ukiwa katika shida ndogondogo nilikuwa upande huo wa kulia nikikusaidia, na ilikuwa sehemu ya utakaso wako na utakatifu wako,” Yesu alimwelezea huku akimwonyesha kwa mkono.

“Mbona hapa naona nyayo za mtu mmoja?” Lucia alicharuka kwa kumwuliza Yesu. “Hizi ni nyayo zangu. Nyakati hizi ni zile ambazo ulikuwa mauti uti. Ilibidi nikubebe. Pia nyakati hizi ni zile watu walipokuomba uwaombee na hasa kupitia nia zao kwa mama yangu Bikira Maria. Kwa vile ulikuwa umechoka ilinipasa nikubebe ili uzitamke nia hizo. Na kwa sababu hiyo, jina langu limesikika sana juu yao, na mama yangu kuheshimiwa kwa uaminifu wake kwa kuyaleta maombi yote kwangu. Mimi ndiye Bwana wa wazima na wafu.” Yesu alimjibu Lucia akiwa ameshika bega lake la kulia.

Ndugu yangu, Kila teso tupatalo hasa tunapoishi na Kristo Mfufuka lina maana sana juu ya maisha yetu. Yote hayo tuyapatayo yanalenga katika umilele. Pili, hapo ulipo sasa kadiri ya wito wako ndipo Galilaya yako na kutakapo kupatia cheo chako, yaani UTAKATIFU WAKO. Hakuna sehemu nyingine utakayoweza kukutana na Yesu. Je, waamini hilo?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona,” Mt 28:10

Tusali:-Ee Yesu Mfufuka, kwa tendo hili kuu la wokovu wetu, asante sana kwa kuyafumbua yote ya umilele ndani ya wito na maisha yangu. Amina.

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario