martes, 25 de abril de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 2 YA PASAKA


ALHAMISI WIKI YA 2 YA PASAKA

Somo: Mdo 5:27-33

Zab: 34:2, 9, 17-18, 19-20

Injili: Yoh 3:31-36

Nukuu:

“Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu,” Mdo 5:28

“Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu,” Mdo 5:29

“Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31

“Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio,” Mdo 5:32

“Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote,” Yoh 3:31

Yeye aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba Mungu ni kweli,” Yoh 3:33

“Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia,” Yoh 3:36

TAFAKARI: “Maisha mapya ndani na katika Kristo ni kufanya naye agano la kudumu kwa kutenda jambo jema kama shukrani ya upendo wake kwako maisha yako yote.”

Wapendwa wana wa Mungu, maisha ya ufufuko ni maisha mapya yenye mwono wa kiagano na yule aliyetufia kwa sababu ya anguko letu la dhambi ili tuwe huru. Leo kwa namna ya pekee tutafakari neno hili pamoja, “maisha mapya ndani na katika Kristo ni kufanya naye agano la kudumu kwa kutenda jambo jema kama shukrani ya upendo wake kwako maisha yako yote.” Mpendwa tunaye safiri sote katika tafakari hii, jumuiya ya kwanza ya Wakristo, kama mwanzo wa maisha mapya ya ufufuko, waliweka agano la kudumu na la milele kwa Kristo kama shukrani na upendo wao kwake.

Jambo hili halikuwatia woga wala hofu kuusema ule ukweli walioushuhudia tangu wakati wa mafundisho yake, mateso, kusulubiwa na ufufuko wake. Pamoja na mateso wanayopata dhidi ya watesi wao, na makatazo juu ya jina hili yenye nguvu la Yesu Kristo, bado hawakomi wala kushtushwa katika kumuhubiri Kristo. “Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu,” Mdo 5:28. Vitusho hivi haviwababaisha kwa sababu jumuiya hii na kila mmoja ndani ya jumuiya hii ya ufufuko, wanajua wazi ni nani wanaye mtumikia. Naye Petro na Mitime wakawajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu,” Mdo 5:29. Imani isipokuwa na msingi mzuri na usio yumbishwa, haiwezi kudumu.

Yesu Kristo ndiyo msingi wa Imani hii na yote wanayoyafanya kama jumuiya. “Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu.” Mt 21:44. Hili ndilo agano la kudumu la Wakristo wa kwanza ndani na katika Kristo. Kristo ndiyo mwanzo na mwisho kwa kila kitu wakifanyacho. Ujumbe huu na ukweli huu juu ya Kristo Mfufuka, Wakristo hawa wa jumuiya ya kwanza hawaoni haya kuwaambia watesi wao. “Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi,” Mdo 5:31. Fundisho wanalotoa kwa watesi wao ni kwamba hata wao kama wanataka kupona na kutoka adhabu ya Mungu, yawapasa kufanya toba ya kweli ili wapate msamaha wa dhambi zao. Mungu ni Upendo na Huruma. Ni kwa sababu hiyo na ukweli huo juu ya Kristo, hawaachi kushuhudia na kuhubiri habari zake. “Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio,” Mdo 5:32.

Ndugu yangu, shahidi ni yule aliyeshuhudia jambo fulani kuwa kweli. Na ukweli huu anaujua vizuri na yupo tayari kuuweka wazi kwa wengine ili wajue kweli hiyo. Kwa imani yetu na kama tendo la shukrani kwa Kristo, kukubali kuwa shuhuda wa kweli ni kuingia agano na Kristo, yaani kuyasadifu yale yote aliyoyafanya juu ya maisha yako. Huku ni kuishi upya katika ufufuko.

Bila shaka hapo ulipo sasa na maisha unayoishi ni agano fulani ambalo umelifanya kutokana na utaratibu wa maisha fulani katika mapokeo fulani ya jamii kadiri ya mila na desturi zake. Maisha hayo hayajalishi unaishi maisha ya kisakramenti kama Sakrameti ya ndoa, Daraja Takatifu, au maisha ya Kiwakfu. Ingawa maisha hayo ni maisha ya kimaagano na ni utaratibu ambao lengo lake kubwa ni kuiishi imani iliyo ndani na katika Kristo, mtindo huo wa maisha ni sawa na chombo cha kusafiria ili kuvuka ng’ambo ya upande wa pili ambalo ndilo lengo msingi. Kufanya agano la kuwa katika chombo hiki; iwe ni maisha ya ndoa, daraja Takatifu na wakfu kama mtawa, haitoshi tu kama ilivyo. Kwa wewe kuwa mahali hapo tu kama tendo la muda na wakati siyo ufufuko na utakatifu wenyewe. Yakupasa kufanya zaidi ili kuleta umoja na utofauti hapo hapo ulipo, ikiwa ndicho kielelezo cha kuupata utakatifu wako ambao ndio cheo chako cha kudumu.

Tukifanya jambo lile lile kwa mtindo ule ule na mfanano ule ule mwisho wasiku tunapotesa hata ladha ya kile tulichokifanyia agano kama hatua ya kwanza. “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zetu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?” Mt 5:46-47. Yesu anakupa wewe na mimi changamoto ya kufanya zaidi ya yale tunayoyafanya kadiri ya mfumo wa maisha tuliyouchagua kuuishi. Agano hili ya pili ni kuzaliwa upya katika roho Mtakatifu. Ni kuwa pale ulipofanya agano lako la kwanza, ila kufanya tofauti zaidi na kwa kumpendaza zaidi Kristo kama shukrani ya upendo wake kwako.

Ni kufanya jambo jema karidi ya uwezo na upendo usiojibakiza wala kujigawa. Kama unaishi katika Sakramenti ya ndoa chagua kitu fulani kama tendo la upendo na lifanye tendo hilo kila siku bila kukoma. Jambo hilo mwisho wa siku huwa na sura mbili; kwanza ni sadaka ya hiari na ya kumpendeza Mungu, na pili ni shukrani kwa upendo huo wa Mungu juu ya maisha yako uliyo changua kuyaisha kama agano msingi. Kwa upande wa maisha ya daraja Tatatifu na maisha ya wakfu, jambo hili ni muhimu sana kufanya. Haitoshi mimi leo kuwa tu mtawa wa shirika la Waagustino kwa kufuata taratibu za kishirika na kuziishi bila kuzivunja. Hii haitoshi! Yanipasa kufanya kingine zaidi ndani ya maisha hayo hayo ya kitawa. Tendo hili linakuwa “fundamental Project of live,” bila kupoteza umoja katika shirika. Umoja katika utofauti ndio uzuri wa Mungu, na Mungu huonekana katika umoja na utofauti wetu kwani kila mmoja wetu amebeba sura na mfano wake, Mwa 1:27.

Kuishi katika kweli hii niliyoisema ni kutambua uhasili wa Yule tuliyejifungamanisha naye, yaani, Yesu Kristo. Maisha yako na yangu bila Yesu Kristo hatutaweza kufanya chochote. Naye Yesu anatuambia kweli hii waziwazi, “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,” Yoh 15:5. Kwani mwisho wa siku siyo kuishi hapa duniani kwa muda wote, bali maisha ya hapa duniani ni maandalizi tu ya maisha ya umilele. “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote,” Yoh 3:31. Kuishi ushuhuda huu katika umoja na utofauti wetu, ndiko kutiwa muhuri ikimaanisha maisha mapya ya kiagano na Kristo yenye mwelekeo wa Kimungu na umilele. Yeye aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba Mungu ni kweli,” Yoh 3:33

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, maisha yenye uzima wa kweli ni kumwamini Mwana wa Mungu, kwani yeye ndiye “njia, na kweli, na uzima; na mtu haji kwa Baba, ila kwa njia yake yaani Yesu Kristo.” Yoh 14:6. Kama hatuna imani na jambo hili, hapo ulipo na maisha unayoishi ni kama kukimbiza upepo tu. Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia,” Yoh 3:36. Haya ndiyo maisha mpya ndani na katika Kristo, ikiwa ni pamoja na kuingia agano naye kama shukrani kwa kile unachoikiishi na kukishuhudia kila siku ya maisha yako.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio,” Mdo 5:29, 32

Tusali:-Ee Yesu Mshindi, tuwezeshe kutambua kweli yako ndani ya maisha yetu ya kila siku. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario