JUMATATU YA WIKI KUU
Somo:
Isa 42:1-7
Zab:
27:1, 2, 3, 13-14
Injili:
Yoh 12:1-11
Nukuu:
“Mimi, Bwana, nimekuita
katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la
watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani
waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,” Isa
42:6-7
“Mwache aiweke kwa siku
ya maziko yangu. Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi, bali mimi
hamnami sikuzote.” Yoh 12:7-8
TAFAKARI:
“Utulivu, amani, na upendo wa Bwana Yesu Kristo katika kujitoa sadaka; na
unafiki wa Yuda Iskariote.”
Wapendwa wana wa Mungu,
tuone katika tafakari yetu ya leo “utulivu, amani, na upendo wa Bwana Yesu
Kristo katika kujitoa sadaka, na kwa upande wa pili tuone unafiki wa Yuda
Iskariote.” Muonekano huu wa utulivu, amani, na upendo wa Bwana wetu Yesu
Kristo kukijongea kifo unajionyesha kwenye masomo yetu, yaani somo la leo, na
injili.
Nabii Isaya anatupa
taswira na picha ya huyo ambaye anayejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wa wengi.
Sifa ya kwanza kabisa Roho wa Mungu yu juu yake. Kwa maana hii, yote ayafanyayo
yana baraka ya Mungu na ni kwa ajili ya ushirika wake na Mungu. Kwa kuwa na
sifa hii, Mtarajiwa huyu, atakuwa na mamlaka ya kutoa hukumu kwa mataifa. Na
kwa vile yote yana mkono wa Mungu, kujitoa kwake sadaka hakuna makeke, ila
ujasiri uliojijenga katika misingi wa unyenyekevu.
Licha ya kuwa na sifa
hizo hapo juu, mteule huyu, kutokana na upole na unyenyekevu wake, umempatia
utukufu na uzima. Atakuwa uzima kwa mwenye kuitaji uzima huo. Atawaponya watu
kadiri ya mahangaiko yao; vipofu wataona, wafungwa watafunguliwa na kuwa huru.
Uthibitisho huu watoka kwa Mungu mwenyewe. “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki,
nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya
mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale
walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,” Isa 42:6-7
Ndugu yangu, utabiri
huu umekuwa kweli ndani na katika Kristo. Na sasa mwanakondoo huyu asiye na doa
anajongea kifo chake kwa ujasiri kujichukulia taji la ushindi. Wakati ndiyo sasa,
na yampasa kujongea Yerusalemu kuyatimiza yale yote yaliyotabiriwa juu yake.
Huyu ndiye Yesu Kristo atuambiaye, “nami nawapa uzima wa milele; wala
hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu,” Yoh
10:28
Pamoja na kutuhakikishia
uzima huo usiopokonywa ndani na katika mikono yake, binadamu tumekuwa tukitenda
kinyume na mara nyingine kile tusemacho sicho tunacho amini na kumaanisha. Huku
ni kumsaliti Kristo kuliko wazi kama anavyofanya Yuda Iskariote anapoona Yesu
akinawishwa kwa Marhamu. Yuda Iskariote anawaonea huruma Maskini kwa kuona
tendo lile la upendo analofanyiwa Yesu. Huu ni unafiki mkubwa sana kwa yeyote
yule kufanya.
Kwa hiyo, tunashauriwa
kufanya lililo jema kila wakati tunapowajibika kufanya hivyo. Kwa maana hiyo,
Yesu anasisitiza, “Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu. Kwa maana maskini
mnao sikuzote pamoja nanyi, bali mimi hamnami sikuzote.” Yoh 12:7-8
Ndugu yangu, unafiki ni
saratani mbaya sana hasa katika ufuasi wetu ndani na katika Kristo Yesu. Mwisho
wa siku hutojua ulikuwa unamtumikia nani hapa duniani. Ni ukweli usiotia shaka
kwamba, kutokana na hali ya kutokukamilika kwetu kama wanadamu, huwezi
kuwaridhisha watu wote kwa nyakati zote. Yakupasa kuchagua njia moja na yenye
kufaa. Katika uchaguzi huu ni wazi utakugharimu kama unavyomgaribu Bwana wetu
Yesu Kristo. Kwa upande wake, Yesu anapokea changamoto hiyo kwa amani, upole,
utulivu na upendo kwa sababu amefanya uchaguzi mwenyewe na ulio bora. Na wewe
Je?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu.
Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi, bali mimi hamnami sikuzote.” Yoh
12:7-8
Tusali:-Ee
Yesu, nijalie neema ya kuishi kile nilicho na kujitoa sadaka kila siku bila
kujibakiza. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario