SIKUKUU YA WATAKATIFU FILIPO NA
YAKOBO MITUME
MEI
3
Somo:
1Kor 15:1-8
Zab:
19:2-3, 4-5
Injili:
Yoh 14:6-14
Nukuu:
“na ya kuwa
alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko,” 1Kor
15:4
“baadaye
akamtokea Yakobo; tena na mitume wote,” 1Kor 15:7
“Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na
uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6
“Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha,” Yoh
14:8
“Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani
yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba
akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake,” Yoh 14:10
“Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani
yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe,” Yoh 14:11
“Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi
nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya,
kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12
“Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili
Baba atukuzwe ndani ya Mwana,” Yoh 14:13
“Mkiniomba
neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya,” Yoh 14:14
TAFAKARI:
Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu. Nanyi
mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya
Mwana. Naam ninaamini.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Watakatifu Pilipo na Yakobo Mitume.
Kadiri ya mapokeo ya Kanisa, Mtume Filipo alizaliwa Bethaida na alikuwa mwanafunzi
wa kwanza wa Yohana Mbatizaji na baadaye alimfuata Yesu Kristo. Yakobo mwana wa
Alfayo, mtumwa wa Mungu, na wa Bwana Yesu Kristo Yak 1:1, alichaguliwa na
kuliongoza Kanisa la Yerusalemu. Mtume Yakobo aliandika moja ya waraka wa
Kanisa kwa watu wote, “Barua ya Yakobo.” Kama kiongozi wa Kanisa la Yerusalemu,
Yakobo Mtume aliishi maisha kamili na ya mateso mengi kwa ajili ya Imani, na
kwa tendo hilo aliwaongoa Wayahudi wengi katika Imani na kumfuata Kristo.
Alikufa kifo shahidi mwaka 62 baada ya Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu,
kama ilivyokuwa kwa Paulo Mtume na wengine, msingi wa Imani kwa Wakristo upo
kwenye kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa kifo cha Kristo ambacho
ni tokeo la dhambi zetu, kimetufanya sote tuhesabiwe haki mbele ya Mungu na kupata
mastahili ya kuwa watoto wake Mungu na warithi Ufalme wake, 1Kor 14:13. Hapa
ndipo ulipo uhai wetu kwa sababu, “alijeruhiwa
kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu
yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona,” Isa 53:5. Ufufuko
wa Bwana wetu Yesu Kristo uliamsha hari mpya na maisha mapya katika ufuasi
wake. Huu ni wito wa kila mmoja wetu kuishi maisha mapya na Kristo, yaani,
maisha ya ufufuko. Maisha haya ya ufufuko yanatudai kila siku kulenga katika
ukamilifu licha ya kwamba udhaifu upo. Kwa maana nyingine, kama mfuasi wa
Kristo na kama ilivyokuwa kwa Filipo na Yakobo Mitume, tusijiridhishe hata mara
moja katika hali ya udhaifu wetu na kumsaliti Yesu kwa matendo yetu maovu na
dhambi.
Maisha haya ya ufufuko
na mapya kwa kila mfuasi wa Kristo ni maisha ya ushuhuda kwa yale
aliyotufundisha Kristo na kuyaona kila siku ya maisha yetu. Hata hivyo hatuwezi
kuwa mashahidi wa ushuhuda wa ufufuko wa Kristo kama hatupo tayari
kushirikishana habari njema ya wokovu wetu. Pili, hatutaweza kushirikishana
habari hii njema ya wokovu kama hatupo tayari kulitafakari neno lake. Tatu,
hatutaweza kulitafakari neno lake kama hatupo tayari kulipokea neno hilo na
habari njema hiyo ya wokovu. Na nne, hatutaweza kulipokea neno hili la wokovu kama
hatupo tayari kulisika. Hivyo, mwito wa kuwa mashahidi wa ushuhuda wa ufufuko
wa Bwana wetu Yesu Kristo na habari njema ya wokovu wetu, kwatutaka kufanya
haya yafuatayo: Kulisikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, na
kulishirikisha neno. Hivi ndivyo walivyofanya Mitume hawa Filipo na Yakobo, na
Mitume wote wa Kristo, na wale wote waliomfuata hasa tunapolitazama Kanisa hili
la Mwanzo. Kwa ushuhuda wao, na kifo dini chao kwa kumwaga damu zao kwa ajili
ya Mwana-Kondoo wa Mungu, Kanisa limekuwa na msingi Imara na Imani hadi leo.
Ndugu yangu unayesafiri
nami katika tafakari hii, maisha na ufuasi wako kama Mkristo lazima yaongozwe
na malengo hayo niliyoyasema kama kweli wataka kuwa ndani na katika Kristo
Yesu. Naye Yesu anakuambia wewe na mimi hivi; “Mnisadiki
ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo,
sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe,” Yoh 14:11. Ndugu yangu, hapa ni Imani ya
kweli katika Kristo Yesu! Na msingi Imara ni kumwona Kristo pasipo shaka yoyote
katika mambo haya matatu anayotuambia, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima;
mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Maana ya maneno haya ni nini? Ndugu yangu kama
nilivyokwisha kusema mahali pengine, si vibaya nikakukumbusha na leo pia. Yesu
Kristo ni njia kama ulivyo Mlango pekee wa kuufikia uzima wa milele. Na njia
aliyoichagua Yesu ni Msalaba. Kwa kuibeba misalaba yetu na kuchukuliana kindugu
katika misalaba ya wenzetu kwa uaminifu na hofu ya Mungu, tunakutana naye
Kristo katika hali na mazingira hayo. Yesu Kristo ni kweli halisi. Kweli hii
tunakutana nayo katika neno lake hasa pale tunapokuwa tayari kulisikia neno,
kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na mwisho kuwa shahidi
wa neno.
Na Yesu Kristo ni
uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika
mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi
ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye
hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu
yake, Yesu anahaidi mambo mawili makuu:
Moja, ni ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, “Aulaye
mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya
mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa
ndani yetu. Naye anasema, “Aulaye mwili
wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh
6:56. Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo
la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, “Basi
kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili,
atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa
kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na
roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana.
Kwa uelewa huo, Yesu Kristo
anamtoa mashaka Filipo pale alipomtaka Yesu awaonyeshe kwa Baba nayo inatosha,
Yoh 14:8. Kuthibitisha kwamba Yeye, yaani, Kristo ndiye Njia, Kweli, na Uzima,
na ndiyo mlango sahihi wa kumfika Baba, na Ufalme wa mbinguni, anasema, “Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi
nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya,
kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12. Ndugu yangu, kwa kumwishi Kristo na
kumwamini una kitu cha kupoteza? Maneno haya ya Yesu kwamba yeye ni njia,
kweli, na uzima si maneno ya kufikirika bali ndio kweli yenyewe na jibu sahihi
alilolitaka Mtume Filipo. Je, bado unamashaka? Kama bado upo kwenye mashaka,
Yesu anakuambia, “Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo
nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana,” Yoh 14:13. Hatupaswi kuwa na
mashaka kama kweli twataka kuishi maisha mapya, yaani, maisha ya ufufuko.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Mkiniomba neno
lo lote kwa jina langu, nitalifanya,” Yoh 14:14
Tusali:-Ee Yesu na
Mkombozi wetu, wewe kwetu watosha. Amina
Watakatifu
Filipo na Yakobo, Mtuombee.
No hay comentarios:
Publicar un comentario