JUMAPILI YA
MATAWI-A
Somo I: Isa 50:4-7
Zab: 22:7-8, 16-17a, 18-19, 22-23
Somo II: Flp 2:6-11
Injili: Mt 26:14-27:66
Nukuu:
“Bwana Mungu amenizibua
sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatokea wapigao
mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate
fedheha na kutemewa mate,” Isa 50:5-6
“naye hakuona kule kuwa
sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana
utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, tena,
alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti,
naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:6-8
“Wakati
huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa
makuhani, akasema, Ni nini
mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta
nafasi apate kumsaliti,” Mt 26:14-16
“Yuda Iskariote, yule
mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate
kumsaliti kwao. Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta
njia ya kumsaliti wakati wa kufaa,” Mk 14:10-11.
“Walakini,
tazama, mkono wake yeye anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, Kwa kuwa Mwana wa Adamu aenda zake
kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule amsalitiye!” Lk 22:21-22
“Yesu
akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake,
wakipiga kura,” Lk 23:34
“Hapo
ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la
hekalu likapasuka katikati,” Lk 23:44-45
“Yesu
akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu,” Lk
23:46
TAFAKARI:
“Yesu Kristo Mfalme Mtaabika na Masikini
ili mimi na wewe tuwe warithi na matajiri, mwili na roho.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha jumapili ya Matawa ya mwaka “A” wa Kanisa, ingawa
tofauti ipo tu kwenye somo la Injili kwa mwaka “A”, “B” na “C”. Somo la Injili
ambalo hubeba simulizi la mateso, kufa, na kufufuka kwake Kristo, kwa Mwaka “A”
tunasoma Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo, mwaka “B” Mwinjili
Marko, na Mwaka “C” Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka.
Jumapili hii ya Matawi
kama tulivyoona, sehamu ya kwanza tunaona Bwana wetu Yesu Kristo anavyoingia
Mjini Yerusalemu kwa shangwe na vifijo, huku alaiki ya watu wakiimba Hosana
Mwana wa Daudi. Yesu anaingia Kifalme na kupokelewa kifalme. Mashangilio haya
na maandamano tuliyokwisha yafanya yana maana kuu tatu: Kwanza, tunamuungama
Kristo kwa tendo hili la umati wa watu. Pili, tunatambua njia yake ni njia yetu
katika maisha yetu yote. Njia hii ni njia ya mateso ambayo ndio mlango wa
Utukufu na Ufufuko. Hivyo nasi tutafufuka naye tukimwamini na kumfuata mpaka mwisho.
Yesu anatuhaidi katika hili kwamba, “mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye
atakayeokoka,” Mt 24:13, Mk 13.13. Na tatu, tunakubali njia hii na tunamwahidi
Kristo kumfuata. Hivyo katika juma hili Mama Kanisa anatuzamisha katika
tafakari kuhusu mateso, kufa na kufufuka kwake Kristo.
Sehemu ya pili tunaona
Mkombozi wetu Yesu Kristo anavyotaabika na kuhujumiwa na kusalitiwa na zile
nderemo na vifijo alivyopewa awali. Furaha na shangwe inageuka kuwa mateso, na
kifo.
Mpendwa katika Kristo,
leo tumtazame Bwana wetu “Yesu Kristo aliye Mtaabika na Maskini ili mimi na
wewe tuwe warithi na matarijiri, mwili na roho.” Mungu aliyeupenda ulimwengu na
viumbe vyake hasa mwanadamu, anamtoa mwanaye mpenzi kuteseka, na kuufia
ulimwengu ili mimi na wewe tuwe warithi wa kweli, matajiri wa kweli, mwili na
roho. “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini
kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa
umaskini wake,” 2Kor 8:9.
Kazi na njia ya kufika
hatma hii si rahisi kutokana na hali na uharibifu wa mwanandamu anayetakiwa
kukombolewa. Nabii Isaya anatabiri dhihaka hii ya huyu atakayebeba jukumu hili
na kusema, “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala
sikurudi nyuma. Naliwatokea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu
yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate,” Isa 50:5-6.
Yesu Kristo yupo tayari
kuteseka, na kufa kwa ajili yangu na wewe. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu.
Lakini binadamu haachi kuwa kigeugeu. Tunapenda utukufu pasipo mateso.
Tunapenda maisha mazuri pasipo kufanya kazi. Tunapenda kuwa wafalme bila
kutumikia. Tunapenda kuwa na mali bila kujishughulisha. Hakika tunapenda
Utukufu pasipo Msalaba. Hii tamaa ya kupenda kusiko kuwajibika ni mwinamio wa
dhambi na mwelekeo wa dhambi. Leo Bwana wetu Yesu Kristo anakubali kuteseka na
kufa ili tuwe hayo tunayotamani katika kweli, haki na ukamilifu.
Tunakuwa warithi na
matajiri wa kweli, tunapoachilia haya ya ulimwengu kwa kujisalimisha kila siku
mikononi mwa Mungu. Kristo anatufanya warithi na matajiri mwili na roho kwa
kujisalimisha mikononi mwa Mungu bila kusita na kuwa na mashaka kwa unyenyekevu
mkubwa. “Naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana
nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana
mfano wa wanadamu, tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza
akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:6-8. Ndugu yangu
kujisalimisha kwa kujinyenyekesha kwa kila mmoja wetu kupitia wito ulioitiwa na
Mungu, (Ndoa, maisha ya wakfu, na ukleri) ndiyo njia pekee ya kuurithi utajiri
anautoa leo Yesu Kristo kwa njia ya mateso na kifo chake.
Tokeo la
kujinyenyekesha ni kukuzwa na kuhesabiwa haki, siyo kwa mkono wa mwanadamu, bali
Mungu mwenyewe. Mtoza ushuru anahesabiwa haki kwa kujisalimisha kwa
kujinyenyekeza. “Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu
hata kuinua macho yake mbinguni; bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu,
uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake
amehesabiwa haki kuliko yule (Mfarisayo); kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa,
naye ajidhiliye atakwezwa,” Lk 18:13-14.
Ndugu yangu, yapo mambo
mengi sana tunayoweza kujifunza katika njili ya leo, ila napenda tujikite sana
katika usaliti wetu, unaotokana na dhambi. Tamaa kubwa ya mwanadamu ni ile ya
kupenda kuwa kitu kingine zaidi na kujikataa kuwa kile alicho. Yesu Kristo
anasalitiwa na wale wanaomjua vizuri na kuonja upendo wake. Leo tuseme hivi;
wanaomsaliti Bwana wetu Yesu Kristo, ni wafuasi wake, yaani mimi na wewe tulio
Wabatizwa. Yuda Iskariote, mfuasi wake wa karibu, na mshika kasma, ndiye
anayemsaliti Kristo. Huku ni kukosa shukrani, fadhila na moyo wa upendo kwa
yule anayekutegemeza kila siku na kwa kila kitu. Ni sawa na kukata tawi la mtu
ulilolikalia. Habari hiyo ilikuwa hivi, kadiri ya Mwinjili Mathayo; “Wakati huo
mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa
makuhani, akasema, Ni nini
mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi
apate kumsaliti,” Mt 26:14-16. Yesu anawindwa
na yule anayemfahamu vizuri.
Naye Mwinjili Marko
anaongelea usaliti huo hivi; “Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara,
akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. Nao waliposikia
walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa
kufaa,” Mk 14:10-11. Na habari hiyo pia ilikuwa hivi, kadiri ya Mwinjili Luka,
“Walakini, tazama, mkono wake yeye
anayenisaliti upo hapa pamoja nami mezani, Kwa
kuwa Mwana wa Adamu aenda zake kama ilivyokusudiwa; lakini, ole wake mtu yule
amsalitiye!” Lk 22:21-22. Ndugu
yangu, ni mara ngapi unamsaliti Kristo kadiri ya wito wako? Kumsaliti huku
Kristo ni pale tunaposhindwa kuishi ahadi za wito na ubatizo wetu. Kila mmoja
wetu ajitazame na kujipima uaminifu wake katika wito wake.
Mzee Amani katika ndoa
yake alifanikiwa kumpata mtoto mmoja tu wa kiume ambaye alijulikana kwa jina la
Upendo. Upendo alikuwa ndiye kila kitu kwa Mzee Amani. Upendo alikuwa karibu
sana na watu, alipendwa na kila mtu kwani pamoja na utajiri alikuwa nao Baba
yake kamwe hakujigamba nao. Tendo hili lilimpa sana faraja baba yake, na hivyo
hakuona shida kuwaandalia wageni wa Mtoto wake Upendo kila anapokuwa na
marafiki zake nyumbani.
Pamoja na Upendo kuwa
na marafiki wengi, Sikujua Mafikiri alikuwa rafiki yake wa karibu sana, kiasi
kwamba wengi walidhani ni ndugu yake. Ukaribu huu wa Upendo na Sikujua
Mafikiri, ulimfanya Mzee Amani amchukulie Sikujua kama mwanaye pia. Basi Mzee
Amani alimshauri mwanaye Upendo kama inawezekana Sikujua aishi pia nyumbani
kwake.
Upendo alifurahi sana
kusikia jambo hilo la faraja kutoka kwa Baba yake. Hivyo Sikujua aliamia
nyumbani kwa Mzee Amani na kushiriki kila kitu cha nyumba ile bila utofauti
wowote. Basi siku moja Mzee Amani alikuwa akiongelea mali alizokuwa nazo na
hata miradi aliyokuwa akiifanya. Na mwisho ya maongezi haya, Mzee Amani alisema
hayo yote ni kwa ajili ya familia yake kwa sasa, akimaanisha wote, Upendo na
Sikujua Msafiri.
Kusikia vile, Sikujua
aliingiwa na wivu na tamaa, na kuanza kufikiri ingekuwa vyema kama yeye
angeyapata hayo yote. Basi baada ya miezi kama sita hivi, Sikujua aliamua
kuchukuwa sumu na kumwekea Upendo kwenye chai. Upendo alifariki, na kilio kile
kilisikika kila kona ya kijiji, kwani Upendo alipendwa na kufahamika na kila
mtu wa kijiji kile.
Baada ya msiba na
matanga kumalizika, na ikiwa zishapita wiki kama tatu hivi, Sikujua aliugua
sana rohoni mwake kwa tendo alichokifanya. Hivyo aliomba kuongea na Mzee Amani.
Mzee Amani alimruhusu. “Baba sidhani kama utanielewa na kuelewa nitakayo
kuambia jioni ya leo. Ukweli ni kwamba, baada ya kuongelea kuhusu mali zako na
miradi yako niliingiliwa na tamaa na kuona ingekuwa vizuri kama mimi ningekuwa
mrithi wa mali zote. Hivyo tamaa hii ilinichukua na kuamua kumuua mwanao
Mpendwa na rafiki yangu Upendo. Nilifanya jambo hilo kwa kumwekea sumu kwenye
chai. Hivyo nakuomba sana msamaha kwa tendo hilo, na ninajuta sana,” Sikujua
alilisema neno lile kwa majuto makubwa. “Mwanangu kuwa na Amani moyoni mwako.
Ni jana tu, nimetoka mahakamani kubadili mrithi wa mirathi ya mali zangu zote.
Mwanzoni kabla la mwangu kufariki, nilizigawa nusu kwa nusu, yaani wewe na
yeye. Na sasa mali zote ni zako, na kwa sasa nawe ndiwe mwanangu Mpendwa.
Nimefarijika sana na kuwa na furaha tena
kwa majuto yako, na kukubali kuwa mwanangu. Hii hapa nakala ya mirathi yako,”
Mzee Amani aliyasema hayo kwa upole na upendo mkubwa huku akamkabidhi hati ile
ya mirathi.
Ndugu yangu, huu ndio
upendo wa Mungu Baba kwetu sisi wanadamu. Mwanaye Yesu Kristo na Mfalme, kwenye
milki zote, anakuwa masikini kwa mateso na kifo chake msalabani, ili wewe na
mimi wadhambi tuwe warithi na matajiri mwili na roho. Kibarua chetu ni kimoja
tu; kuupigania ukamilifu kwa kufanya toba na majuto ya kweli ya dhambi zetu, na
kuishi katika hali ya neema. Ukamilifu ndiyo cheo cha kila mbatizwa, na huu
ndiyo wito wa utakatifu tunaoitiwa kila siku. “Basi
ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt
5:48.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Wakati huo mmoja wa wale
Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami
nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi
apate kumsaliti,” Mt 26:14-16.
Tusali:-Ee
Yesu Kristo, kwa kifo chako cha aibu cha msalaba nijalie neema ya kuona
umasikini wako uliopeleka mimi leo kuwa mrithi na tajiri, mwili na roho. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario