SIKUKUU YA MWINJILI MARKO
25/4
Somo: 1Pet 5:5b-14
Zab: 89:2-3, 6-7, 16-17
Injili: Mk 16:15-20
Nukuu:
“Naam, ninyi nyote
jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye
kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5b
“Mwe na kiasi na
kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye,
huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,” 1Pet 5:8
“Na Mungu wa neema
yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha
kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na
kuwatia nguvu,” 1Pet 5:10
“Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri
Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na
kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16
“Na
ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema
kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata
wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya
wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18
TAFAKARI:
“Unyenyekevu wa kweli katika kuhudumiana; kumwona Kristo kwa wote tunaokutana
nao.”
Wapendwa wana wa Mungu,
fadhila ya unyenyekevu ni msingi wa fadhila zote. Neno hili unyenyekevu si geni
kwetu na hata masikioni mwetu. Vipo viashirio vingi vinavyothibitisha
unyenyekevu wa mtu. Leo kwa namna ya pekee na tunapoungana na Mama Kanisa tukisheherekea
Sikukuu ya Marko Mwinjili, tulitafakari neno hili kwa pamoja. “Unyenyekevu wa
kweli katika kuhudumiana; kumwona Kristo kwa wote tunaokutana nao.” Viashirio
vya mnyenyekevu wa kweli kabla ya yote, ni ile hali ya kujipokea na kujikubali
katika mapungufu uliyonayo. Ni kweli kabisa hakuna binadamu aliyekamilika
katika yote. Ila kutambua mapungufu yako na mazuri yako ni hatua ya msingi sana
ya kusonga mbele kwa kuanza kuyarekebisha yale mapungufu. Tusipokuwa tayari
kukiondoa kinyago hiki tunachojivika ambacho si chetu, maisha yote ya mtu
hubakia katika hali ya vita ya ndani dhidi ya uhalisia wake, na mwisho tunakuwa
washindwa wa kila kitu.
Jambo lingine la msingi
kuelekea maisha ya unyenyekevu ni kuwa tayari kusikiliza zaidi ya kuongea.
Binadamu licha ya kufanya tafakari ya kina ya maisha yake binafsi, kwa tendo
hilo tu la tafakari halitoshi kujijua katika maana ya mizania ya kweli. Mtu
mwingine nje yako na anayeona katika uhalisia wa vitu kama vilivyo, huwa msaada
mkubwa sana katika ukamilisho wako, hasa pale anapokuambia kile kilicho cha
kweli. Ukweli huu mara nyingi ni vigumu kuupokea kwa sababu utuanika kile
ambacho hatupendi kukiona na hata kukusikia kuhusu undani wa maisha yetu. Hiki
usichopenda kukiona na wala kukisikia ndicho kile ulicho. Utafaidika tu katika
jambo hili kama utakuwa tayari kusikiliza. Hii ni moja ya hatua kubwa sana ya
kukua kiroho ambayo itakufanya uwe kile ulicho na makusudi mazima ya uumbaji
wako.
Ni mtu mwenye kiburi tu
asiyekuwa tayari kupokea ukweli ulio ndani mwake. Ni hali ya kawaida mtu
kupenda uzuri ulionje yake, na hivyo kupoteza uhalisia wake kwa kuyatamani
yaliyo kwa wengine. Hali hii hutufanya kuwa vivuli vya wengine na kupoteza
uhalisia wetu na upekee wetu. Mungu hupenda tuwe kile alichokusudia tuwe kwa
sura na mfano wake, Mwa 1:27. Uzuri na utofauti huu tulio nao ndiyo furaha na
uzuri wa Mungu na ndiyo anavyotaka tuwe wawakilishi wake popote pale tulipo
katika maisha yetu yote. Tunapokuwa kile tulicho kadiri ya makusudi yake ya
uumbaji wetu tunamwakwakilisha vizuri Mungu. Mtume Petro anatuambia, “Naam,
ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu
huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema,” 1Pet 5:5b.
Tunapojifungamanisha na unyenyekevu, tunakuwa sababu na makusudi ya kweli
katika kutoa huduma isiyo na mawaa, na katika tendo hili la huduma kadiri ya
wito na vipaji vyetu, tunajazwa neema zaidi na zaidi. Hakuna aliyefilisika kwa
kumrudishia Mungu kilichochake, na kwa namna hiyo hakuna aliyekosa neema kwa
kufanya yaliyo ya Mungu.
Ndugu yangu, ukifanikiwa
katika hatua hii muhimu ya pili niliyokwisha isema, utaingia hatua ya tatu
ambayo ni muhimu sana katika utume wako. Hatua hii ya tatu itakufanya umwone
Kristo kwa kila utakaye kutana naye na kumuhudumia. Tunao kutana nao katika
huduma zetu hawana sura moja tu na yenye kupendeza. Wapo wenye furaha na wasio
na furaha, wapo wagonjwa na wenye afya, wapo walio huru na wasio huru, wapo
watana shati na walio uchi, wapo walioshiba na wasio na chakula, wapo walio na
makazi na wasio na pakuegemeza vichwa vyao. Sura hizi na mtazamo huu wa
mahangaiko ndiye Kristo utakayekutana naye kila siku katika utume wako.
Yeyote kati yetu
atakaye mrudishia Mungu kilichochake na kupata neema za kufanya zaidi na zaidi,
kwa tendo hili ni chukizo kwa yule mwovu na mtumikia mwovu. Hivyo yatupasa
daima kuwa tayari dhidi ya mashambulizi ya kiroho. Kunapokuwa na mwanga, giza
ujitenga, hivyo kivuli cha mwanga hakiondoki licha ya kwamba hatukioni.
Ninachomaanisha hapa ni kwamba, kinyume cha mwanga ni giza, na kinyume cha giza
ni mwanga. Hii ndiyo maana ya vita vya kiroho. Na hivyo Mtume Petro anasema, “Mwe
na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye,
huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze,” 1Pet 5:8. Hii ni changamoto kubwa
sana ya kukua katika maisha ya kiroho. Je, mbele ya vita hivi vya kiroho kuna
nini?
Wapendwa, ushindi wa
vita hivi vya kiroho ni kuingia katika utukufu wa milele uliokwisha wezeshwa na
Kristo Kristo mwenyewe kwa sadaka yake pale Msalabani. Kwa maana nyingine
hatutaweza kushinda vita hivi kama hatupo na Kristo na ndani ya Kristo. Na
kushinda huku si kwa nguvu zetu wenyewe au jeuri na ustadi wetu katika vita,
bali ni kwa neema za Mungu, ambazo tunajaliwa naye Kristo. Hivyo, “Mungu wa
neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha
kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na
kuwatia nguvu,” 1Pet 5:10. Tunathibitishwa au kwa maana nyingine tunahesabiwa
haki si kwa matendo yetu mema tu, bali kwa neema ya Kristo mwenyewe. Tunatiwa
nguvu si kwa mastahili yetu na mwono wetu, bali kwa kuyafanya yale yaliyo
makusudi ya Mungu kadiri ya wito na vipaji vyetu ambavyo ni mali yake mwenyewe.
Ndugu yangu,
unyenyekevu kwa upande wetu ikiwa ndiyo msingi wa mambo yote, na neema kutoka
kwa Mungu, vitatuwezesha kutenda maagizo haya muhumu ambayo ni agizo kwa kila
mbatizwa, yaani: “Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye
na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16. Kwa vile kile
tulicho ndicho tukiaminicho na kukiishi kadiri ya makusudi ya Mungu katika
uumbaji wetu, ni kwa namna hiyo kile tusemacha kwa watu na kukihubiri katika
kweli kitakavyokuwa hukumu ya kweli.
Mtazamo
huu wa kweli katika Imani, huambatana na ishaza za kimungu. Ishara hizi ni
uthibitisho wa yale tunayoyaamini na kuyatenda kwamba si kwa nguvu zetu na
akili zetu, bali ni Mungu mwenyewe
ayatendaye hayo kwa vyombo vyake vya udongo ili atambulike kupitia vyombo
hivyo. Na hivyo Yesu anawaambia mitume wake, “Na ishara hizi zitafuatana na hao
waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha
kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao
watapata afya,” Mk 16:17-18. Ujumbe huu na wosia huu wa mwisho wa Kristo, ndilo
agizo la kila Mbatizwa.
Wapendwa
wana wa Mungu, leo tunaposheherekea sikukuu hii ya Mwiinjili Marko tufanye
tafiti moyo juu ya unyenyekevu wetu, na matendo yetu tuyafanyayo kila mmoja
kadiri ya wito wake na vipaji vyake. Kama hakuna uhusiano wa ukweli huu, usione
aibu kurudi nyumbani na kuchukua tochi, kuliko kuendelea na safari yako ndefu
katika kiza kinene ambacho hujui kilichopo mbele ya safari hiyo. Nyumbani kwako
kuliko na tochi hiyo ni ile hali ya kujinyenyekeza, ili uhesabiwe haki kwa
kujazwa neema za kufanya zaidi na zaidi kama tunavyomsheherekea Mwiinjili Marko
leo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Akawaambia,
Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini,
atahukumiwa,” Mk 16:15-16.
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie unyenyekevu katika kweli yako, ili tuweze kuishi kile tulicho
kadiri ya wito na vipaji vyetu vilivyo mali yako. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario