martes, 25 de abril de 2017

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 2 YA PASAKA


JUMAMOSI WIKI YA 2 YA PASAKA

Somo: Mdo 6:1-7

Zab: 33:1-2, 4-5, 18-19

Injili: Yoh 6:16-21

Nukuu:

“Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2

Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno,” Mdo 6:3-4

“Ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao,”Mdo 6:6

Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu,” Yoh 6:18

Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope,” Yoh 6:20

TAFAKARI: “Msiogope”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa namna ya pekee tulitafakari neno hili, “Msiogope.” Hofu ni moja ya dalili za maumivu ya ndani. Hofu tunayotaka kuiongelea hapa si hofu ya nyoka au simba, na vingine kama hivyo. Ni hofu ya vitu vya kawaida kabisa kama asemavyo Mzaburi, “hapo waliingiwa na hofu pasipokuwapo hof” Zab. 53:5a.

Mfano:- Kuogopa giza sana kiasi cha kutothubutu kutoka chumba kimoja kwenda kingine wakati wa usiku, Kuogopa kutembea barabarani mpaka uwe na mtu; Kuogopa wadudu na viumbe kama mende, chura, panya, kinyonga, mjusi. Kuogopa watoto wachanga na wazee. Mtu akiona kikongwe anapita yupo tayari hata kubadili njia ili asipishane naye.

Hofu ya maisha yatakavyokuwa magumu; Hofu ya maisha ya kesho; Hofu ya kuolewa na kuoa: wakijiuliza itakuwaje watakapoanza maisha ya ndoa? Hofu ya matukio magumu ya maisha huleta mapepo “HALI KINZANI” inayotufanya tumchukie MUNGU na kutenda dhambi. Hofu huzaa kushtuka shtuka na kufanya mtu kuugua magonjwa ya mwili, na pia hofu ni  mbaya zaidi inapokutawala.

Jumuiya ya kwanza ya wakristo kadiri ya somo la leo, wanaingiwa hofu kutokana na jumuiya hiyo kuongezeka, na huduma kutokwenda sawa. “Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2. Hivyo wanaona ipo hatayari ya kuacha kulihubiri neno wakabaki kutatua matatizo yanayotokana na manung’uniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.

Jumuiya hii kwa kuongozwa na nguvu ya Kimaadili, Unyenyekevu, na Roho Mtakatifu, wanakabiliana na hofu hii kwa kufanya uteuzi wa watu saba “Mashemasi,” kutatua tatizo hilo. Mitume wanatoa agizo na vigezo vya kuwachagua wasaidizi hao na kusema, “basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno,” Mdo 6:3-4.

Baada ya vigenzo na masharti kuzingatiwa, wateuzi hawa wanawekwa wakfu kwa tendo “ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao,” Mdo 6:6. Tendo hili linamsisitizo wa umoja wa Mitume ambao leo tungesema umoja wa maaskofu, “Collegiality of Bishops.” Umoja huu ni muhimu sana leo katika Kanisa letu. Tunapoona mmoja katika kundi hili akitamka yake kama anavyojisikia, ni wazi taasisi hii muhimu na fundishi inaingiliwa. Tulio wengi tunajiuliza, hilo alinenalo kalitoa wapi, na kwa baraka ya nani? Na kama jambo hilo asemalo linaukweli, Je, ni kwa manufaa ya nani?

Leo katika Injili wanafunzi wa Yesu wakiwa wanasafiri wenyewe wanaingiwa na hofu kwa sababu ya mabadiliko ya hali ya hewa ndani ya baharí. “Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu,” Yoh 6:18. Katika mtafaruku huu, Yesu anajitokeza akitembea juu ya baharí na kuwaambia, “Ni mimi, msiogope,” Yoh 6:20. Hata leo Yesu anakuambia wewe na mimi “usiogope.” Yesu analiambia Kanisa pia kama Sakramenti ya wokovu, chombo kinachosafiri, na chombo ambacho kipo hija, kwamba, “Msiogope,” ni MIMI. Swali ni hili, Je, tunaweza kumwona Yesu katika hatari hii ya kuangamia na tukabaki na msimamo na imani yetu? Tunaitaji jicho la Imani na ufahamu wa kutosha kuzisoma alama za nyakati zetu. Yapo mambo mengi leo hayaendi sawa hasa kwenye jamii yetu. Tumeingiwa hofu hata pale pasipo na hofu kusema mzaburi, Zab 53:5a.

Mpendwa, neno “usiogope” lipo mara 366 katika Biblia. Hii ina maana Mungu anatuambia kila siku “usiogope”. Unapokuwa na hofu ya kitu chochote, basi kitu hicho ndicho chenye uwezo wa kuamua hatima yako. Kwa mwenye Imani ya kweli, na watu wa Mungu tunatakiwa tuelekeze hofu yetu kwa Mungu tu na si kwingineko kwani tutakapoielekeza kwa Mungu yeye ni mwaminifu na atatuelekeza kufanya ya Mbinguni.

Maandiko Matakatifu yanatuambia ni nani twapaswa kuwa na hofu naye; “Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu,” Isa 8:13. Yesu anasema hivi kuhusu hofu, “Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo,” Lk 12:4-5. Katika kitabu cha Ufunuo wa Yohani tunaona adhamu ya watu mwenye woga. “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili,” Ufu 21:8

Ndugu yangu, Hofu haileti madhara ya kiroho tu bali hata ya kimwili. Huleta mshtuko na penye hofu pana wasiwasi, palipo na haya huleta magonjwa ya “Organic” {sehemu za mwili zifanyazo kazi maalumu} na hitilafu katika shehemu hizi husababisha vidonda vya tumbo {ulcers} shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya ini, upungufu wa damu mwilini, n.k.Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha,” Isa 21:3-4.

Wapendwa wana wa Mungu, kuna mambo kwa binadamu ni ya wazi kabisa na lazima tutayapitia tupende tusipende. Kifo ni mojawapo ya jambo ambalo halipingiki katika uhasilia wake. Wote lazima tutakufa. Kitu cha kuogopa hapa si kifo, bali hofu. Yatupasa kuishinda hofu dhidi ya kifo. Uhakika wa maisha baada ya kifo tunayo. Kristo ndiye kielelezo chetu katika uzima huo baada ya Kifo. Acha hofu! Wote tupo safarini kuelekea tukio hili muhimu, kwenda upande wa pili wa ukweli kuhusu Maisha ya UMILELE. Katika jambo hili Yesu anasema, Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi,” Yoh 12:24. Kwa mantiki hii, yatupasa kufa ili kuishi maisha hayo ya UMILELE.

Tumsifu Yesu Kristo!

Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope,” Yoh 6:20

Tusali:-Ee Yesu uliye kielelezo chetu, tuondolee hofu, tujaze matumaini na ujasiri wa kukabiliana na sintofahamu zote katika maisha yetu ya kila siku. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario