lunes, 3 de abril de 2017

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 5 YA KWARESMA


JUMATANO WIKI YA 5 YA KWARESMA

Somo: Dan 3:14-20, 91-92, 95

Dan 3: 52, 54, 55-56

Injili: Yoh 8:31-42

Nukuu:

“Ee Nebukadreza, hatuna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha,” Dan 3:16-18

“Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31

TAFAKARI: “Kuishi imani ya kweli, na kweli ndani ya Kristo”

Wapendwa wana wa Mungu, tutafakari neno hili “Kuishi imani ya kweli, na ukweli ndani ya Kristo,” kadiri ya masomo ya leo. Somo letu la leo, ikiwa ni pamoja na Injili yanatuelekeza kufanya tafakari juu ya neno hilo. Tunaona ndugu hawa watatu; Shadraka, Meshaki, na Abednego wanavyosimama imara katika imani ya kweli bila kutishika wala kuterereka licha ya vitisho vya mfalme Nebukadreza. Mfalme Nebukadreza anajitengenezea sanamu yake ya dhahabu na kujifanya kuwa Mungu wake. Mfalme huyu anathibitisha matumizi mabaya ya madaraka yake. Kiongozi ye yote yule asiye na hofu yangu huiumba taswira yake, na mwisho huifanya sehemu ya maabudu. Mfano: kiongozi mwenye kujenga hofu kwa watu na kuwafanya kuwa na nidhamu ya woga, tendo hili hujeuka na kuwa sanamu ya kuogopwa na kuabudiwa.

Mambo ya nyakati hizo za Nabii Danieli  kwa kwa namna ya pekee ufalme wa Nebukadreza hayapishani sana na viongozi tuliokuwa nao leo. Sanamu ya kwanza ya kuabudiwa kwa viongozi wa leo na hasa bara letu la Afrika ni “HOFU TENGENEZWA.” Hofu hii tengenezwa lengo lake kuu ni kuwabakiza madarakani kwa kile wanachoamini kitakuwa “Milele.” Ila historia na alama za nyakati zinapingana na ndoto yao hiyo. Sanamu ya pili ni pesa na mali. Viongozi wengi wanaabudiwa na watu kwa kujua au kutokujua kwa vile wanapesa. Mbaya zaidi hata wale wanaoonekana kuwa na hofu ya Mungu, wameingia katika mtego huu wa kuabudu matajari kutokana na pesa zao. Leo hata viongozi wa dini wameingia katika mtego huu wa kuwasujudia viongozi wenye pesa. Ndugu yangu, Mungu tu ndiye wakuambudiwa na kusujudiwa kwa sababu yeye ndiye ALFA na OMEGA, ‘mwanzo na mwisho,’Ufu 1:8, 21:6; 22:13.

Ndugu hawa watatu, Shadraka, Meshaki, na Abednego wanaonyesha imani yao ya kweli kwa matendo na kusema, “Ee Nebukadreza, hatuna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha,” Dan 3:16-18. Kwa ujasiri huu waliokuwa nao, Mungu anasimamia tendo hili ya Kiimani. Palipo na uwepo wa Mungu, hakuna kinachoshindikana. Mungu ni mweza wa yote. Huyu ndiye “Mungu aliye mkuu, aliye hodari, Bwana wa majeshi ndilo jina lake; mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake,” Yer 32:18b-19. Huyu ndiye Mungu wa kuabudiwa na kuogopwa.

Injili ya leo tunaona mwendelezo wa mapambano kati ya Yesu na Wayahudi juu ya mamlaka aliyokuwa nayo Yesu na mafundisho yake. Wayahudi hawapendi kupokea ukweli huu. Yesu anawaambia, “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31. Ndani na katika Kristo, kuna kweli. Ukweli wa Kristo ni ukweli wa Mungu mwenyewe kwani Yeye Kristo ni NENO aliyefanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Na tunazidi kufahamu ukweli huu kwa kusikiliza, kulipokea, kulitafakari, kulishirikisha, na kuliishi neno lake. Tunaposimama katika kweli ya Mungu tu huru. Tunapoujua ukweli wa kile kilicho malengo na hatma ya maisha yetu, njia ya kufika huko haitakuwa shida kuijua. Na kwa vile kule tunapotamani kufika ndiko kwenye umilele, basi kwa kufahamu ukweli tutaijua njia na uzima huo.

Yesu Kristo ndiye pekee mwenye uwezo wa mambo hayo yote matatu, ambayo kwayo ndiyo shahuku yetu hapa duniani. Yesu anasema, “mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Safari iliyosalama na ya huhakika ni ndani na katika Yesu Kristo. Safari ya kuelekea mbingu bila Yesu haiwezekani. Tunaenda kwa Baba mbinguni kwa njia ya Kristo. Kwa njia hii yatupasa kujikana wenyewe, kuchukua msalaba wetu na kumfuata Kristo, Mt 27:32; Lk 9:23. Bila kufanya hivyo ndugu yangu, hata kwa kuijua njia bado hatutakuwa kumepiga hatua.

Tumsifu Yesu Kristo!

 Mungu aliye mkuu, aliye hodari, Bwana wa majeshi ndilo jina lake; mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake,” Yer 32:18b-19.

Tusali:-Ee Yesu wewe ndiye Njia Kweli, na Uzima. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario