JUMATANO YA OKTAVA YA PASAKA
Somo:
Mdo 3:1-10
Zab:
105:1-2, 3-4, 6-7, 8-9
Injili:
Lk 24:13-35
Nukuu:
“Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema,
Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji
kupata kitu kwao. Lakini
Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho
nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:4-6.
“Akamshika
mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa
nguvu,” Mdo 3:7.
“Ikawa
katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana
nao,” Lk 24:15.
“Macho yao yakafumbwa
wasimtambue,” Lk 24:16.
“Wakamwambia, Mambo ya
Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele
za Mungu na watu wote; tena jinsi
wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa,
wakamsulibisha. Nasi tulikuwa
tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli,” Lk 24:19-21.
“Akawaambia, Enyi
msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na
kuingia katika utukufu wake?” Lk 24:25-26.
“Wakamshawishi
wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha,” Lk 24:29.
TAFAKARI:
“Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha; Ndiyo mkao wa
Kipasaka, yaani, Ufufuo na Uzima.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ni wakati mwingine tena tunapa fursa ya kuyatafakari Makuu ya Mungu. Kwa namna
ya pekee na tulitafakari neno hili, “Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na
mchana unakwisha; ndiyo mkao wetu wa Kipasaka, yaani, Ufufuo na Uzima.” Mkao wa
Kipasaka-Ufufuo na Uzima tunauona katika somo letu la leo, ikiwa ndiyo shabaha
kubwa ya jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Hamu na uhitaji wa kukaa na Kristo
Mfufuka, unajitokeza katika Injili yetu ya leo, pale wanafunzi wa Yesu
waliokuwa wakielekea Kijiji cha Emau kumtaka akae nao kwani kumekwisha kuchwa,
na mchana unakwisha.
Mkao huu wa
Kipasaka-Ufufuo na Uzima ndiyo nguvu la Kanisa la Kristo. Mitume hawana cha
kutoa zaidi NEEMA na BARAKA za Kristo Mfufuka. Mkao huu unabadilisha tabia na
mazoea yetu katika maisha. Kristo anapokuwa kila kitu katika maisha yetu,
hubadili maisha yetu na kuwa maisha ya uhai na uzima. Ni katika hali hii
tunaopolewa kutoka kwenye kiza na kuingizwa katika mwanga. Tunatolewa katika
makaburi yetu na kupelekwa kwenye mwanga na uzima. Tunatolewa katika kufa kufa
kwetu kunakotokana na magonjwa na mahangaiko ya maisha na kupelekwa kwenye
uzima na faraja.
Ni kwa sababu hii Mtume
Petro na Yohana wanamtoa Bwana yule ombaomba katika mlangoni katika kuchoka
kwake, na kumwingiza katika uzima na furaha ya kweli. Jambo hili linafanyika
ndani na katika jina la Yesu. “Na Petro, akimkazia
macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu,
lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti,
simama uende,” Mdo 3:4-6
Yesu
anapokuwa maisha yako ya kila siku unatiwa nguvu na kuondolewa kupooza kwako.
Jambo hili hufanyika na uwezekana tu pale unapokubali kuongozwa na kushikwa
mkono na Yesu. “Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo
vya miguu yake vikatiwa nguvu,” Mdo 3:7. Hapa ndipo tunapoanza maisha mapya
tunapokubali kuongozwa na Kristo Mfufuka.
Injili
yetu ya leo inatupa umuhimu wa kukaa muda wote na Kristo Mfufuka. Maisha yetu
yanapita kwa kasi sana kama moshi, na wakati mwingine tunaishi tukiwa wakavu
sana kiroho. Yesu Kristo kwa walio wengi ni Yesu wa Historia. Kwa walio wengi
Yesu huyu hana nguvu tena. Tatizo kubwa tunalokutana nalo katika maisha ni
kuyaweka matamanio yetu mbele zaidi ya mafundisho na kweli anayotufundisha
Kristo. Sintofahamu hii inawakuta wanafunzi wale ambao wanaona Kifo cha Kristo
kama tukio la kudanganywa hivi, na hakuna maana kabisa kwa yule ambaye
walimtegemea sana na leo anawaangusha. Kifo hiki cha aibu cha msalaba kwa
wanafunzi hawa kimewatoa matumaini yote.
Yesu
Kristo hata katika sintofahamu hizi, bado yupo tayari kutusikiliza na kuzidi
kutufundisha, licha ya kwamba hatumuoni kwa kuificha taswira yake, ili mradi tu
tumpe nafasi. “Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa
mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa
wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye
ndiye atakayewakomboa Israeli,” Lk 24:19-21.
Yesu hachoki
kutukumbusha yaliyompasa kufanya na yaliyotabiriwa juu yake. Haya yote yapo
katika Maandiko Matakatifu. Mt. Jerome anasema hivi kuhusu Yesu Kristo,
“tunapokuwa wajinga wa maandiko matakatifu, ni kwa namna hiyo hiyo tu wajinga
kuhusu Yesu Kristo.” Kuhusu jambo hili Yesu anatupa sababu ya yale yote
yaliyojiri kuhusu Kifo na Ufufuko wake. “Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya
kuamini yote waliyoyasema manabii! Je!
Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?” Lk 24:25-26. Ndugu yangu hapa tunakumbushwa pia,
kwamba hakuna Utukufu pasipo Msalaba. Penye Msalaba pana Utukufu, na sasa ni
rahisi kuupata Utukufu kwa sababa Kristo kesha ushinda Msalaba.
Wapendwa,
Kristo anajifunua kwetu leo katika kuumega mkate. “Ikawa
alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao,” Lk 24:30-31. Kuumega mkate kunatanguliwa na kulishwa neno lake
na kulielewa. Tukio la wanafunzi wa Yesu kukutana naye njiani kuelekea Kijiji
cha Emau, ni mtiririko mzima wa adhimisho la Misa Takatifu. Adhimisho hili lina
sehemu kuu mbili; Liturjia ya neno na liturjia ya Ekaristi Takatifu. Kwa
mantiki hii, uwezekano wa Kristo kujifunua kwetu wakati wa Ekaristi Takatifu,
unabebwa kwanza na ufahamu wetu wa kulisikiliza neno lake, kulipokea,
kulitafakari, kulishirikisha, na kuliishi. Wanafunzi hawa wa Yesu wanakuwa na
hamu ya kukaa naye zaidi baada ya kulishwa neno na Kristo ingawa hawakumfahamu.
Ndugu
zangu, wale ambao wamezoea kuchelewa na mara nyingine kushiriki tu liturjia ya
Ekaristi Takatifu, ni wavamizi wa Mlo Mtakatifu wasioujua vizuri. Ni sawa na
kukishambulia chakula kitamu na kizuri wakati ukiwa na mikono michafu. Ni
vizuri kuhudhuria sehemu zote mbili za kiliturjia na ndivyo inavyotakiwa kwa
Mkristo na hasa kwetu, ambao Ekaristi Takatifu kicho kiini cha yote. Wapo kati
yetu ambao huingia Kanisani na moja kwa moja kujongea Meza ya Bwana. Huu ni
uhuni wa hali ya juu kufanywa na Mkristo. Mwisho na muhimu tusichoke kuudhuria
mara kwa mara maadhimisho ya Maabudu ya Yesu wa Ekaristo-Sakramenti Kuu. Hapa
anakaa kwetu na kujifunua kwetu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Lakini Petro
akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho.
Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende,” Mdo 3:6
Tusali:-Ee Yesu, Bwana wangu na Mungu wangu, kaa
nasi Bwana nyakati zote za maisha yetu hapa duniani ili tuweze pia kufika kwako
mbinguni. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario