ALHAMISI
KUU
Somo
I: Kut 12:1-8, 11-14
Zab: 116:12-13,
15-16bc, 17-18
Somo
II: IKor 11:23-26
Injili:
Yoh 13:1-15
Nukuu:
“Maana nitapita kati ya
Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri,
wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri.
Mimi ndimi Bwana,” Kut 12:12
“Na ile damu itakuwa
ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo: nami nitakapoiona ile damu,
nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya
Misri,” Kut 12:13
“Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi
mtaifanya iwe sikukuu kwa Bwana: mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu
vyote, kwa amri ya miele,” Kut 12:14
“Yesu, hali akijua ya
kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye
aliamewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1
“Yesu, hali akijua ya
kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye
anakwenda kwa Mungu,” Yoh 13:3
“Aliondoka chakulani,
akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni,” Yoh 13:4
“Akaanza kuwatawadha
wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga,” Yoh 13:5
“Kama nisipokutawadha,
huna shirika nami,” Yoh 13:8b
“Basi ikiwa mimi,
niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu
ninyi kwa ninyi.” Yoh 13:14
“Kwa kuwa nimewapa
kielelezo,” Yoh 13:15a
“Kikombe hiki ni agano
jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu,” IKor
11:25
“Maana kila mwulapo
mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo,”
IKor 11:26
TAFAKARI:
“Karamu ya Mwisho ya Yesu Kristo na wanafunzi wake; Nguzo tatu za uhai na
umilele: Kielelezo cha upendo wa kweli, Chakula kwa uponyaji wa utapia roho
wetu, Daraja Takatifu-mwendelezo wa huduma uhai na upatanisho kati ya Mungu na
wanadamu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Kanisa linaingia katika siku tatu kuu muhimu; Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu, na
Jumamosi Kuu. Siku ya leo ni ile siku muhimu sana ambayo Bwana wetu Yesu Kristo
alifanya karamu ya mwisho na wanafunzi wake. Ni siku iliyobeba mafundisho
mazito na wosia muhumu wa Bwana yetu Yesu Kristo ambao hadi leo Kanisa
linaendelea kufanya na kutafakari kwa kina.
Ni siku ambayo Yesu
Kristo aliuvua UTUKUFU wake kama tutakavyoona baadaye, na kuuvaa UTUMWA kwa
kuonyesha maana halisi ya UPENDO kwa vitendo na nadharia. Leo pia ni siku
ambayo Bwana yetu Yesu Kristo anatuachia chakula kwa uponyaji wa utapia roho
wetu. Ili tuwe na afya ndani na katika Yeye, chakula hiki Kitakatifu-Ekaristi
Takatifu, ndicho KIINI cha uhai wetu, umoja wetu, mshikamano wetu, na undugu
wetu kama familia. Leo pia kwa namna ya pekee kabisa, Bwana wetu Yesu Kristo
analiweka Daraja Takatifu, kama mwendelezo wa HUDUMA hai na upatanishi kati ya
Mungu Baba yake na yetu, na sisi wanadamu.
Kesho tutatafakari
fumbo zima la mateso, na kifo cha msalaba cha Bwana wetu Yesu Kristo. Hapa
ndipo kwenye hitimisho zima la safari yetu ya Ukombozi. Hapa ndipo kwenye
ushindi wa umauti na mwelekeo wa umilele. Hapa ndipo sote kwa tofauti zetu
twafanywa upya na kuwa wana wapendwa wa Mungu. Hapa ndipo mimi na wewe kama
wafuasi wa Kristo twajivunia Ukristo wetu kwa sababu kuna maisha tena ya
umilele baada ya kifo kilichopigwa mwereka na ushindi wa Yesu Kristu dhidi ya
dhambi.
Na Jumamosi Kuu,
tunatafakari kwa shahuku kubwa maajabu ya Mungu ambayo kwetu bado ni fumbo
lililotandwa na kiza kinene. Hapa ndipo tunapoona ukimya mkuu ambao tangu
ulimwengu kuumbwa haukuwahi kutokea. Ni ukimya Mtakatifu. Ndugu yangu baada ya
kuona kwa ufupi nini na maana ya siku zetu hizi kuu tatu, nikurejeshe sasa
kwenye tafakari yetu ya leo.
Ndugu yangu unayesafiri
nami katika tafakuri hii, leo tuzame zaidi katika neno hili, “Karamu ya Mwisho
ya Yesu Kristo na wanafunzi wake; Nguzo tatu za uhai na umilele: Kielelezo cha
upendo wa kweli, Chakula kwa uponyaji wa utapia roho wetu, Daraja
Takatifu-mwendelezo wa huduma uhai na upatanisho kati ya Mungu na wanadamu.”
Karamu hii ya mwisho ya Bwana wetu Yesu Kristo, ilifanywa kipindi na wakati wa
maadhimisho ya kila mwaka ya Wayahudi kukumbuka siku Mungu “ALIYOPITA JUU
YAO,”-ikiwa ndiyo maana halisi ya PASAKA, kuwakomboa kutoka utumwani Misri.
Mungu aliyejaa HURUMA
na UPENDO, anasema basi na yatosha kwa mateso ya Taifa langu teule, na sasa
anawatangazia UHURU wa kweli. Kuonyesha kuwa Yeye ndiye Bwana, na amechukizwa
na vitendo viovu vya Wamisri, kupita kwake juu anatoa adhabu kama kielelezo cha
kukomesha uovu kwa wana wake, na Taifa lake Teule. “Maana nitapita kati ya
Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri,
wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri.
Mimi ndimi Bwana,” Kut 12:12
Adhabu hii
inafungamanishwa na mwanakondoo. Damu ya
Mwanakondoo huyu asiye na mawa, wala dosari ndicho kitambulisho thabiti cha
kuwafahamu wana wake wateule. Hivyo ishara hii inawekwa kama utambulisho na
utambuzi wao wakati Mungu akitandaza adhabu hii kwa Wamisri. “Na ile damu
itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo: nami nitakapoiona ile
damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu, nitakapoipiga
nchi ya Misri,” Kut 12:13
Nchi ya Misri, katika ‘operasheni’
hii ya Mungu, inasimama badala ya mfumo wowote ule wa uovu, na unaokwenda
kinyume na mpango mzima wa Mungu katika kumkomboa Mwanadamu aliye kielelezo na
taswira halisi ya Mungu, na utukufu wake. Kwa maana hii pia tunafundishwa
kwamba, uovu wowote ule na ukandamizaji dhidi ya ubinadamu hauwezi ukadumu
milele. Hakuna tawala yeyote ovu hapa duniani iliyodumu milele. Utawala
unaodumu milele ni UPENDO. “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya
matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.” IKor 13:13.
Tendo hili Mungu
analolifanya kwa Taifa lake lililoonewa, lengo lake ni kutufikirisha katika
umilele. Ni fundisho linalotupa taswira ya umilele. Haki na usawa kwa kila
binadamu, si jukumu la kupenda kutoa au kutokutoa haki hiyo, iwe kisheria au la
kibinadamu katika utu, ila ni haki la umilele, kwa uasili wa ubinadamu wetu. Ni
mpango wa Mungu tangu kuumbwa ulimwengu. Na hivi Mungu analiweka wazi jambo
hili. “Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa
Bwana: mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya miele,” Kut
12:14. Ndugu yangu, leo unaweza kuona haki zetu zinavyopindishwa na wakati
mwingine kunyang’anywa kwa ujanja ujanja na mawakili wadanganyifu wa kisukumwa
mfumo dhalimu. Hakika kwa yeyote yule mwenye kupindisha sheria ili kupokonya
haki ya mnyonge, Mungu hatafumba macho yake.
Ndugu yangu, ni katika
mtazamo huu ya Pasaka ya Kiyahudu, na katika mwendelezo wa historia ya mwokovu
wetu, twaweza zama ndani na kuona nafasi ya Yesu na umuhimu wake. Damu ya
mwanakondoo katika pasaka ya Kiyahudi siku ile ya kutolewa utumwani Misri
ilikuwa uthibitisho wa Mungu kulitambua Taifa lake Teule. Yesu Kristo
mwanakondo katika karamu hii ya mwisho anachukua nafasi mbili kwa wakati mmoja:
kwanza, kama sadaka itolewayo ambayo kilele chake ni kesho ijumaa kuu, na pili
kama mtoa sadaka, ambaye kwa kiasi kikubwa ndiyo mtazamo wa shughuli nzima
anayoifanya leo. Katika fumbo hili la sadaka na mtoa sadaka, linawachanganya
wanafunzi wake kwa sababu hawamwoni mwanakondoo.
Tendo hili la kujitoa
sadaka ni upendo uliotukuka wa Mungu kwetu sisi wanadamu. “Yesu, hali akijua ya
kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye
aliamewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo,” Yoh 13:1. Uhusiano
huu wa Mungu Baba na Mwana, unampa Yesu Kristo ujasiri wa kuijongea saa hii
bila shaka yoyote kwani anajua yote keshakabidhiwa na Mungu Baba, na anayafanya
kwa sifa na utukufu wake. “Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi
mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu,” Yoh 13:3.
Ndugu yangu, ni katika
hali hii Yesu Kristo anakubali kuuvua UMUNGU wake na kuuvaa UTUMWA ili wewe na
mimi tuwe tayari kujinyenyekesha kila mmoja kadiri ya wito wake. Tendo hili la
kuuvua Umungu wake analifanya kwa kuyavua mavazi yake na kujifanya mtumwa kwa
kuwatawadha wanafunzi wake miguu “Aliondoka chakulani, akaweka kando mavazi
yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni,” Yoh 13:4
Ndugu yangu, elewa hapo
kitambo kidogo huko nyuma, Yesu alijeuka sura na mavazi haya yalikuwa meupe
kupindukia. “Hata baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na
Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake
mbele yao; mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani
kuyafanya meupe,” Mk 9:2-3. Tendo hili lilionyesha utukufu wake kwa wanafunzi
hawa kabla ya kifo chake. Kwa upendo na mfano wa kutumikia, anajishusha chini
kabisa sawa na mtumwa, na kuacha utukufu na sifa sote kwa ajili yako na yangu.
Ni upendo wa Ajabu. Hivyo baada ya tendo hili, Yesu anatoa agizo, “Basi ikiwa
mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana
miguu ninyi kwa ninyi.” Yoh 13:14.
Tusipoyafanya haya kwa
wenzetu bila kujali undugu, ukoo, ukabila na utaifa wetu, basi hatuna ushirika
na Kristo. Na kama tupo kwenye maagano mbalimbali, iwe ndoa au maisha wa utawa
na ukleri na hatuyaishi haya basi tujue hatuna ushirika na Kristo hata kama
bado tupo kwenye maagano hayo. Mtume Petro anaonyesha hali ya kutokuwa tayari
kuoshwa miguu, na Yesu mara anamwambia kosa la kutokuwa tayari kwake. “Kama
nisipokutawadha, huna shirika nami,” Yoh 13:8b. Tendo hili Yesu halifanyi kama
kamtindo tu cha kupoteza muda, na wakati mwingine kadiri ya mazoea inakuwa
kamtindo cha kushangaa hasa siku ya leo ambayo wengi wetu hupigania kuoshwa
miguu bila kujua wajibu wake. Tendo hili Yesu analifanya kwetu ili liwe
kielelezo cha kutaabikiana na kutumikiana. “Kwa kuwa nimewapa kielelezo,” Yoh
13:15a
Ndugu yangu hiki ni
kielelezo cha utumishi usio na faida. Ni kufanya na kutenda kila mara lililo
jema bila kutarajia ujira wa pekee wala sifa na shukrani za kibinadamu. Ni
kujihesabia kuwa umefanya lile tu unalostahili kulifanya katika utimilifu wake.
Na Yesu anasema, “vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa,
semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya,” Lk
17:10.
Leo pia kwa namna ya
pekee, Yesu Kristo anatupa dawa na kuweka rasmi, chakula cha kutuponya kutoka
utapia roho wetu. Leo Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inawekwa rasmi. Hapa
ndipo penye kiini na chimbuko la uzima wetu tunaposhiriki mlo huu tukiwa safi
na mastahili yake. “Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye
kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35.
Tunapata uzima huu na neema zake tunaposhiriki mwili na damu yake Kristo tukiwa
safi. Mtume Paulo anasisitiza jambo hili kwa kusema, “Maana kila mwulapo mkate
huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo,” IKor
11:26. Twaitangaza Mauti ya Bwana mpaka ajapo kwa sababu hili ni Agano Jipya
kati yetu na Mungu, Kristo akiwa ndiye Mwimili Mkuu. “Kikombe hiki ni agano
jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu,” IKor
11:25
Ndugu yangu, leo pia
kwa namna ya pekee Yesu Kristo anaweka rasmi Sakramenti ya Daraja Tatatifu kama
mwendelezo wa huduma ‘uhai na upatanisho’ kati ya Mungu na wanadamu. Kwa
kusimikwa kwa daraja hili Takatatifu, mwendelezo na kazi yake Yesu Kristo haitafifia hadi mwisho
wa nyakati. Je, padre ni mtu wa namna gani?
Wapendwa, kwa namna ya
pekee, padre ni Kristo mwingine, "Alter Christus." Padre ufahamika
kwa kile afanyacho. Kwa kinywa chake anaweza kutamka maneno ya Bwana,
"mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya
mimi," Yoh 14:6. Padre ni mtumishi wa Mungu anayejitoa sadaka kwa ajili ya
wokovu wa watu wa Mungu.
Licha ya sadaka hiyo,
padre ni mwanadamu kama wanadamu wengine, aliyetwaliwa kati ya watu kwa mambo
ya muhusuyo Mungu, "maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu
amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo
na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na
wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu
hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake
mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya
dhambi, " Ebr 5:1-3.
Kama Kristo mwingine,
hakuna mtu anayependwa sana na kuchukiwa sana kama Padre. Lakini Padre hubakia
kuwa chumvi la dunia na nuru ya ulimwengu, Mt 5:13-14. Kuchukiwa kwa Padre ni
kutokana na kuyatenda mambo yamuhusuyo Mungu yanayopingana na mambo ya ulimwengu
huu. Yesu Kristo anasema,"mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu
umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa
ulimwengu," Yoh 17:14.
Wapendwa, tusisahau
kwamba Padre hata baada ya upadrisho wake anaendelea kuwa mwanadamu. Na hali ya
kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika pamoja na kukata tamaa.
Kumbe si halali: Moja, watu kukasirika wanapomwona Padre mnyonge kama wao.
Pili, kuwadai Mapadre kuwa na akili kama malaika. Na tatu, kutaka upendo wao
uyeyushe ugumu wa kila mkosefu au wawe na ufundi wa kutatua matatizo yote ya
maisha.
Wapendwa, Padre ni
upendo wa Mungu: Moja, palipo na huzuni Padre huleta furaha. Pili, pasipo na
haki Padre huleta haki. Tatu, kwa Vijana, Padre huwatia moyo na kuwafundisha
fadhila mbalimbali. Nne, Padre ni utii kwa watu wote. Na kufikika na wote.
Tano, Padre ni uaminifu. Sita, Padre ni moyo wa uwajibikaji na heshima kwa
watu.
Ndugu yangu,
wanaoteuliwa kuwa mapadre ni viumbe wanyonge wanaoshiriki unyonge wa ndugu zao.
Na hii inawawezesha kuwaombea ndugu zao bila unafiki. Padre ni zawadi kwa Mungu
ya watu kwa Mungu. Padre hutoa zaidi na hupokea kidogo, zaidi hulipwa chuki na
minong'ono. Kwa sadaka yake Padre inabidi apate heshima. Ni mtu anayemwakilisha
Kristo. Kama Mt. Francisco alivyosema, "kama ningekutana na malaika pamoja
na Padre, ningeweza kumsalimia kwanza Padre, kwani Malaika ni rafiki wa Mungu,
na Padre ni Mhudumu wa Mungu." Heshima ya Padre inatamkwa wazi na Bwana
wetu Yesu kristo, "awasikilizaye ninyi ananisikiliza mimi, naye awakataaye
ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma," Lk
10:16
Wapendwa, malaika
hufuata pale Mungu alipo, lakini Mungu ufuata pale Padre alipo. Mt. Yohane
Maria Viane alisema, "acha eneo na sehemu yoyote bila Padre kwa miaka
ishirini, matokeo yake watu wataanza kuabudu wanyama." Padre kwa Kanisa ni
zawadi kubwa kuliko zawadi zote zitolewazo.
Ndugu yangu, Mambo haya
matatu tuliyoyaona leo katika Karamu hii ya Mwisho ya Bwana wetu Yesu Kristo na
wanafunzi wake ni jumuisho la upendo uliotukuka, utumishi na unyenyekevu
ulitukuka, na uhai wa umilele tuupatao tunaposhiriki chakula hiki Kitakatifu.
Hivyo Basi ni vyema tukamtafakari sana Kondoo katika mahusiano yetu na wenzetu.
Kondoo anatabia moja ya pekee kupita wanyama wote. Licha ya upole wake, kondoo
hufunika mavi yake kwa mkia wake. Kwa maana hiyo, tunajifunza kubeba aibu za
wenzetu katika hali ya unyenyekevu kuelekea ukamilifu licha ya kwamba sisi si
wakamilifu. Kristo kama mwanakondoo wa Mungu anakubali kubeba aibu yetu hata
kufa kifo cha msalaba licha ya kwamba hakustahili kufanya hivyo. Ni upendo wa
ajabu kwetu wanadamu. Na tunafundishwa unyenyekevu wa hali ya juu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na
Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi.”
Yoh 13:14
Tusali:-Ee
Yesu, kwa karamu yako ya leo unikumbushe wajibu wangu wa kupenda na kutumika
bila kujibakiza. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario