IJUMAA WIKI YA 3 YA PASAKA
Somo: Mdo 9:1-20
Zab: 117:1ab, 2
Injili: Yoh 6:53-58
Nukuu:
“Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu
unayeniudhi wewe,” Mdo 9:5
“Lakini Anania
akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi
aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata
hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako,”
Mdo 9:13-14
“Lakini Bwana
akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina
langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli,” Mdo 9:15
“Mara akamhubiri Yesu
katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa Mungu,” Mdo 9:20
“Basi
Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na
kuinywa damu yake, hamna uzima ndani yenu,” Yoh 6:53
“Kama vile Baba aliye hai alivyonituma
mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi,” Yoh 6:57
TAFAKARI:
“Hakuna lisilowezekana kwa Mungu; Sauli afanywa chombo kiteule cha Kristo,”
Wapendwa wana wa Mungu,
tukiwa tunazidi kutafakari hujuma dhidi ya jumuiya ya kwanza ya Wakristo huko
Yerusalemu, na baada ya kuuwawa Shahidi Stefano, Sauli anaomba barua ili
awakamate watu wa njia hii na kuwafunga gerezani. Ni katika mateso haya Kristo
mwenyewe analisimamia jambo hili, na kumwongoa mtesaji mkuu wa kundi lake.
Tendo hili la Yesu Kristo Mfufuka kulisimamia Kanisa lake na hasa wongofu wa
Sauli, linathibitisha kweli ya sala la Yesu kabla ya mateso na kifo chake cha
Msalaba. Yesu anasali, “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako
ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa
upotevu, ili andiko litimie,” Yoh 17:12. Sauli anapigwa upofu na kuanguka chini.
Katika hali hii ya giza na ukimya, Sauli anasema, “U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe,”
Mdo 9:5.
Kwa
matendo haya ya Sauli, Kanisa la mwanzo halikuwa na amani hata kidogo. Pamoja
na hofu hii ya Kanisa la Mwanzo juu ya Sauli na genge lake katika hujuma,
anatukumbusha siku ile ya kukamatwa kwake alipowauliza wale Maaskari,
‘Mnamtafuta nani?’ Yoh 18:7. “Yesu akajibu, Nimekwisha
kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa
waende zao. Ili litimizwe lile neno
alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao,” Yoh 18:8-9. ‘Ili
litimizwe lile neno alilolisema-wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao,’
Mwinjili Yohane anatukumbusha ile sala ya Yesu kabla ya mateso yake, Yoh 17:12,
na Yesu Kristo ni nani katika safari hii ya ukombozi wa Mwanadamu, Yoh 1:1-3,
14, 17 (Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno
alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo;
wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Naye Neno alifanyika
mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee
atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa
Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo)
Kwa
nyakati zetu za leo na hasa Kanisa letu la Tanzania kuna kila aina za dalili
kuibuka taswira ya Sauli mwingine wa nyakati zetu. Sauli huyu amefanikiwa kwa
kiasi kikubwa kujenga hofu ndani ya waamini leo. Imani yetu leo inawindwa sana.
Tumeanza kusongwa na hofu na mashaka hasa tunapokusanyika kwa wingi kumsifu na
kumwabudu Mungu. Leo tunaye Sauli mwingine, ambaye huwalipua wakristo na
kuwachinja kama kuku. Je, ni mungu gani anayekubali, kubariki na kutetewa na
binadamu anayemtoa binadamu mwenzake sadaka tena kwa ukatili kama huu?
Sauli
wa nyakati za jumuiya ya kwanza ya Wakristo aliogopeka sana. Hata katika hatua
za kumrudishia kuona kwake, haikuwa rahisi wakristo kusadiki kama mtu huyu
amemjeukia Kristo. Anania anapoambiwa na Bwana katika maono kufanya kazi hii,
anaingiwa na hofu kubwa na mashaka. Anania anajibu, “Bwana, nimesikia habari za
mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa
makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako,” Mdo 9:13-14. Jambo hili si rahisi
kulifanya. Sauli wa leo, siyo tu anamilipuko, bali amejikoka risasi, visu,
mapanga, mashoka, na tindikali. Nani anaweza kumsogelea? Nani anaweza kupeleka
ujumbe kwa Sauli wa leo kama Anania? Wapendwa wana wa Mungu, leo tunaishi nyakati
tofauti kabisa. Mtume Paulo ambaye kabla ya wongofu wake alijulikana kama
Sauli, anatupa njia ya kupambana na Sauli wa nyakati hizi kwa kusema, “Usishindwe
na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema,” Rum 12:21.
Ndugu
yangu, pasipo njia Bwana hufanya njia, I Kor 10:13. Ninayo imani kubwa sana juu
ya vita hivi vya kidini. Ni Kristo mwenyewe atakayempiga upofu Sauli huyu wa
sana, na kati yetu Kristo atawainua akina Anania na kufanya kazi yake. Yesu
Kristo anaondoa hofu ya Anania kwa kumpa ujumbe huu, “Nenda tu; kwa maana huyu
ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na
wana wa Israeli,” Mdo 9:15. Ninaimani katika neno hili kwa Sauli wa leo. Kristo
yupo tayari kumtumia Sauli wa leo alichukue Jina lake mbele ya Mataifa, na
wakuu wote wa dunia hii. “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa
Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Sauli wa leo ameibuka na ndoto kubwa na yupo mbioni
kuunda dola ya Kisauli. Ni kwa neema na kweli ndani na katika Kristo, naamini
kwa kupitia njia hii ya kuushinda ubaya kwa wema Kristo atalisimamia Kanisa
lake pote duniani na kumshinda Sauli wa nyakati zetu leo. Kristo tunayemwamini
na kumfuata ni Kristo hai na siyo wa historia.
Ni
Kristo huyu ninayemwamini na kumhubiri atakaye mgeuza Sauli huyu wa sasa, na
kwa kinywa chake atasema kama alivyosema mara ile ya kwanza baada ya kupigwa
upofu, na “mara akamhubiri Yesu katika masinagogi, kwamba yeye ni Mwana wa
Mungu,” Mdo 9:20. Naweza nisieleweke katika hili, ila hakuna lisilowezekana kwa
Mungu. Siamini kabisa kwamba Kristo atavumilia mateso ya waja wake wanaochinjwa
kama kuku huko Somalia, Ethiopia, Misri, na Irak. Siamini jambo hili hata
kidogo. Ni swala la wakati tu.
Ndugu
yangu, ni katika kuushiriki mwili na damu yake Kristo, hasa katika hali hii ya
mateso tunapata uzima wa milele. Naye anasema, “Amin, amin,
nawaambieni, Msipoula mwili wake Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamna
uzima ndani yenu,” Yoh 6:53. Mwili huu na damu hii twaweza kuula na kunywa
katika hali ya mateso kama sasa, na ndipo tunapofunuliwa na kuupata uzima huo
wa milele ndani yetu. Uhai wetu u salama ukiwa ndani ya Kristo kama Yeye alivyo
ndani ya Baba daima. “Kama vile Baba aliye hai alivyonituma mimi, nami ni hai
kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi,” Yoh 6:57. Je, waliamini neno hili?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Akasema,
U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe,” Mdo 9:5
Tusali: -Ee Yesu nipe Neema ya kujua maana ya
Mateso yangu katika wewe na ndani yako. Nifanye Chombo cha Amani yako, ili
niushinde ubaya kwa wema kama ulivyo tupenda upeo na kujitoa sadaka pale
Msalabani. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario