JUMAPILI YA 2 YA PASAKA-A
Somo I: Mdo 2:42-47
Zab: 118:2-4, 13-15, 22-24
Somo II: 1Pet 1:3-9
Injili: Yoh 20:19-31
Nukuu:
“Wakawa wakidumu katika
fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika
kusali,” Mdo 2:42
“Kila mtu akaingiwa na
hofu; ajabu nyingi na ishara zikafanywa na mitume,” Mdo 2:43
“Na wote walioamini
walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali zao, na
vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na
haja,” Mdo 2:44-45
“Na siku zote kwa moyo
mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa nyumba, na kushiriki
chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu Mungu, na kuwapendeza
watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa,”
Mdo 2:46-47.
“Akaja
Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu,” Yoh 20:19b
“akawaonyesha
mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana,” Yoh
20:20
“Akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho
Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote
mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:22-23
“Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za
misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu
katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo,” Yoh 20:25
“Lete hapa kidole chako; uitazame mikono
yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali
aaminiye,” Yoh 20:27.
“Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu
na Mungu wangu!” Yoh 20:28
“Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa
heri wale wasioona, wakasadiki,” Yoh 20:29
“Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba
Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake,”
Yoh 20:31
“Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo,
ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye
uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika,
usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,” 1 Pet 1:3:4.
“ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina
thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto,
kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu
Kristo,” 1Pet 1:7
TAFAKARI: “Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na
katika kuumega mkate, na katika kusali,” Mdo 2:42.
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya pili ya Pasaka ya mwaka “A” wa Kanisa.
Na leo kwa namna ya pekee tutafakari neno hili: “Wakawa wakidumu katika
fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika
kusali,” Mdo 2:42. Mafanikio ikiwa ni pamoja na maendeleo makubwa ya Imani katika
jumuiya ya kwanza ya Wakristo yalijengeka katika msingi wa UPENDO KWA KWELI,
WALIPOISHI NDANI NA KATIKA KRISTO. Tendo hili la upendo, Kristo akiwa kielelezo
cha yote, uliwafanya wanajumuiya hawa wa kwanza kujitoa bila kujibakiza. “Na
siku zote kwa moyo mmoja walidumu ndani ya hekalu, wakimega mkate nyumba kwa
nyumba, na kushiriki chakula chao kwa furaha na kwa moyo mweupe, wakimsifu
Mungu, na kuwapendeza watu wote. Bwana akalizidisha kanisa kila siku kwa wale
waliokuwa wakiokolewa,” Mdo 2:46-47.
Ndugu yangu, hutoweza kuwa shahidi
wa Kristo na neno lake kama haupo tayari kushirikisha wengine kweli ya Kristo
iliyopo ndani yako. Kuishirikisha kweli ya Kristo ndani yako kwa wengine ni
tokeo la kulitafakari neno la uzima kwa kina kila siku ya maisha yako. Hutoweza
kusimama katika neno la Mungu kama hujalielewa na kuwa sehemu ya maisha yako.
Kama neno hili ni uzima basi yanipasa kulisoma kila siku na kulitafakari ili
liwe uzima ndani yangu. Ni vigumu pia kulitafakari neno la Mungu na kuwa sehemu
ya uzima wako kama huwezi kulisikia.
Kulisikia neno la Mungu siyo tu kwa
kupitia masikio yetu kama njia moja ya mlango wa fahamu, bali kulisikia kwa
kila kiumbe alichokiumba Mungu, na zaidi kutoka mazingira yale unayoyaishi leo
na sasa. “Ndipo
akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba
Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na
kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la
dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi
ndinyi mashahidi wa mambo haya,” Lk 24:45-48. Neno “kuanza tangu Yerusalemu,”
linaweza kutafsiriwa kuwa ni mazingira uliyopo na namna ile ulivyo kila mmoja
kadiri ya wito wake. Kuwa shahidi wa neno hili la uzima
yanipasa kuanzia pale nilipo. Neno hili lilete uzima ndani ya ndoa yako, maisha
yako ya wakfu, na katika huduma unayoitoa kwa watu.
Ni vigumu vile vile
kusikia neno hili la uzima kama haupo tayari kulipokea. Kulipokea Neno la Uzima
kamwe lisiwe Neno kihistoria, yaani simulizi fulani kwangu na lenye kunipa
taarifa ya mambo yaliyopita, bali Neno hilo lanihusu mimi leo na sasa na siyo
mtu mwingine. Huku ndiko kulipokea Neno la Uzima kutakapo kupelekea kulisikia,
kulitafakari, kulishirikisha, na mwisho kuwa shahidi na kufa shahidi. “Mimi
Yohana, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na
subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo, kwa ajili ya
Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu,” Ufu 1:9.
Wapendwa
katika Kristo, ushuhuda wa Neno la Uzima ulipelekea kujali na kutaabikiana kwa
upendo wa kweli kwa jumuiya ya kwanza ya Wakristo, na kuliweza kutatua matatizo
mengi makubwa. Hakuna miongoni mwao aliyeitaji akakosa mahitaji yake. Mt.
Augustino ambaye alichukua kielelezo hiki cha maisha ya jumuiya ya kwanza ya
Wakristo, na kufanya ndicho msingi wa jumuiya ya Kiagustino, anasema “UKIPENDA
UTAFANYA YOTE.” Ni kwa msingi huu na upendo huu wa kweli kwamba, “…wote
walioamini walikuwa mahali pamoja, na kuwa na vitu vyote shirika, wakiuza mali
zao, na vitu vyao walivyokuwa navyo, na kuwagawia watu wote kama kila mtu
alivyokuwa na haja,” Mdo 2:44-45. Jambo la kushangaza leo katika familia zetu, licha
ya wanafamilia, yaani Baba na Mama kuunganishwa kwa Sakramenti ya ndoa,
wamekuwa wabinafsi kiasi kwamba kila mmoja wao hujifanyia mambo yake bila
kumshirikisha mwenzake.
Tatizo kubwa hapa
lipo kwa akina Baba. Utaona kila mmoja wao anasema hiki ni changu. Wakati
mwingine Baba huwa na viwanja na hata biashara kubwa ambazo mkewe hajui lolote.
Mwisho wa siku kinapotokea kifo kwa upande wa Baba, mali yote hupotea na familia
kubaki katika hali ya umasikini uliokithiri. Hivi nyie akina Baba,
inawezekanaje kumwamini rafiki wako wa kufikia, kuliko kumwamini mkeo na
wanafamilia yako? Marafiki hawa wa kufikia ndio wanaojua mikataba yote ya mali
na biashara za Baba huyu wa familia. Tujirekebishe! Mkeo ni zaidi ya ndugu na
marafiki. Huyu umeunganishwa naye na kuwa kitu kimoja. Unapoanza kumtenga
unajipasua mwenyewe na mwisho wake hutobaki salama.
Ndugu zangu,
tusipoishi kweli hii hasa katika ngazi ya familia, hakika bado hatujamjua
Kristo. Katika kitabu cha ufunuo
tunaona namna Yesu anavyojifunua kwa Mtume Yohane kwa njia ya maona na kusema,
“Mimi
ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na
tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za
kuzimu,” Ufu 1:17b-18. Mimi na wewe tusipo ijua kweli hii tu bado katika
giza, na tunaishi maisha ya kuigiza kwa miaka yote, kila mmoja kadiri ya wito
wake. “Kila mtu aaminiye kwamba Yesu
ni Kristo amezaliwa na Mungu. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata
yeye aliyezaliwa na yeye,” 1Yoh 5:1.
Upendo wa
kweli ndiyo amri kuu kwa kila aliyebatizwa na kumwamini Kristo. Kwa yeyote
anayejiita Mkristo na anayejitambua kuwa ni Mkristo, hakuna mbadala dhidi ya
kupenda kuliko kwa kweli. “Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba
tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito,” 1Yoh 5:3. Ukipenda kweli,
utafanya yote kama asemavyo Mt. Augustino. Wepesi wa amri yeyote ni upendo
katika agizo hilo na kwa kutimiza matakwa ya hiyo amri. Jumuiya ya kwanza ya
Wakristo inaishi pendo la kweli na kuwa kivutio cha kweli katika huduma na
huruma ya Mungu. Na ndivyo ilivyokuwa kwamba, “Nayo makutano ya
watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa,
nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa,” Mdo 5:16.
Kupenda kuliko kweli ndiko
kuzaliwa na Mungu, na kuushinda ulimwengu dhidi ya uovu. Silaha kubwa ya
kuushinda ulimwengu huu dhidi ya uovu, ni kupenda kuliko kwa kweli. Wengi wetu
ujikuta kufanya maovu kwa vile tu hawakuwahi kupendwa na mara zote hujisikia
kusalitiwa na kuhuzunishwa. “Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu
huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani
yetu,” 1Yoh 5:4.
Jambo hili
la kutokupenda kutokana na majeraha na kuumizwa kwetu, linaonekana wazi katika
Injili ya leo ambapo tunaona watu wawili (Yesu Kristo Mfufuka na Mtume Tomaso)
waliojeruhiwa, ambao mwisho wa siku mmoja wao (Yesu Kristo Mfufuka) anamponya
mjeruhiwa mwenzake (Tomaso).
Uponyaji
wa kwanza anaoutoa Yesu Kristo kwa wanafunzi wake ni kuiondoa hofu kwa salamu
yake ya upendo, “Akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu,”
Yoh 20:19b. Tendo hili la kuwa na Amani ya kweli ndiyo mwanzo wa kuanza kupenda
kuliko kwa kweli na furaha ya kweli. Wanafunzi wa Yesu wanaonyesha furaha hii,
na kuanza kupenda tena, ingawa Mtume Tomaso hakuwepo katika kundi. Naye Yesu
baada ya salamu ya upendo iliyojaa matumaini mapya, “akawaonyesha mikono yake
na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana,” Yoh 20:20.
Furaha
hii inaendana na maagizo ya kufanya anayoyatoa Kristo kwa wanafunzi wake. Naye
Kristo akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea
dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh
20:22-23. Kristo hapendi furaha ya kweli aliyotupatia tubaki nayo wenyewe.
Hivyo furaha hii twapasa kuisambaza kwa wengine kila mmoja kadiri ya wito wake,
vipaji vyake, dhamana na nafasi yake katika jamii anayoishi. Ndugu yangu ukiona
hapo unapoishi hata mbwa wanakukimbia bila sababu, ujue wewe ni shiiiiida!
Tomaso
aliporejea anakokujua mwenyewe kwa kupoteza imani yake juu ya Kristo,
anapoambiwa jambo hili la kuonekana kwa Kristo, hakuamini hata kidogo. Naye kwa
ufahamu wake anatoa vigezo vya kutambua ukweli aliousikia kutoka kwa wenzake.
Naye anatoa vigezo na masharti ambavyo lazima vizingatiwe: -“Mimi nisipoziona
mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa
misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo,”
Yoh 20:25. Kwa masharti haya na vigezo hivi tunaweza kuona ni kwa jinsi gani
Tomaso alivyo jeruhiwa na kusononeshwa kwa tukio la kifo cha Bwana wetu Yesu
Kristo.
Wapendwa,
baada ya siku nane, tunaona tukio la kukutana kwa wajeruhiwa hawa wawili, yaani
Yesu Kristo Mfufuka na Mtume Tomaso. Mjeruhiwa wa kwanza ni Yesu Kristo. Yesu
anamkuta Tomaso na kumwonyesha majeraha yake, na kusema, “Lete hapa kidole
chako; uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala
usiwe asiyeamini, bali aaminiye,” Yoh 20:27. Tendo hili la Yesu kumwonyesha
Tomaso majeraha yake na kuumizwa kwake kunatoa picha ya majivuno ya Yesu na
wakati mwingine kama kujigamba vile. Jambo hili lina ukweli wake kwa mtazamo
huu wa majeraha na makovu aliyokuwa nayo Yesu. Majereha ya Kristo na maumivu
yake hayakuwa majeraha ya kushindwa, bali majeraha ya UPENDO WA KWELI. Majeraha
ya Kristo yalikuwa majeraha ya USHINDI uliotukuka. Hayakuwa majeraha ya kuuma,
bali majeraha ya UTUKUFU. Ni majeraha ya UPENDO. Upendo ambao upo tayari
kujitoa sadaka bila kipimo na kutojibakiza. Kristo anaonyesha ubavu wake na
mikono yake ilivyotobolewa si kwa kujionyesha, kujigamba wala kumuhukumu
yeyote, bali kuonyesha uzito na undani wa upendo wake kwa Mitume na kwetu sote.
Japokuwa
Tomaso hakuwa na majereha kwenye ngozi yake, na hakuwa na kuvuja damu kutoka
mwilini mwake, majeraha yake yalikuwa ndani ya moyo wake. Haya ni maumivu ya
ndani. Moyo wake ulijeruhiwa kwa kusikitishwa na kifo cha Bwana wake. Alijisikia
kudanganywa na Bwana wake Yesu Kristo. Alijisikia kushindwa baada ya kuyaweka
matumaini yote kwa Kristo kwa sababu alifikiri Yesu Kristo ni Masiha, Mfalme,
na kuhoji kwa nini Yesu afe kifo katili kama kile cha msalaba? Alifikiri Yesu
Kristo angeikomboa Israeli kutoka kwenye dola ya Kirumi. Anajiuliza hivi, kwa
nini hata yeye mwenye-Yesu ameshindwa kujinasua kutoka watesi wake? Mtume
Tomaso alisikitishwa na kusijikia kusalitiwa na Yesu. Tomaso alishawishika
kabisa kwamba alifanya uchaguzi usio sahihi kumfuata mseremala huyu wa
Galilaya. Kwa kweli Tomaso alikuwa na maumivu makubwa sana!
Wapendwa
maumivu na majeraha ya Moyo huchukua muda mrefu kupona. Majeraha haya na
maumivu ya Moyo yanachukua kuda mrefu kupona kwa sababu twaweza kuyaficha na
kujifanya hayapo. Twaweza kuongea na kutenda mambo yetu kama vile hakuna jambo
lolote baya au upungufu wowote kwetu. Wengi wetu twaweza kukaa katika hali hii
kwa miaka mingi kwa kujivisha taswira nyingine na mwonekano mwingine ambao sio
uhalisia wa kile kilicho ndani mwetu ingawa tunaendelea na mateso na maumivu
hayo. Lakini ukweli ni kwamba hatuwezi kudumu katika hali hii kwa muda wote na
nyakati zote. Mara tutaanza kujisikia vibaya na kujisikitikia na kufikiri
marafiki zetu wametutenga na wapo mbali bila kutusikiliza maumivu yetu
yanayotusonga moyoni. Mara tunajisikia kwamba hawajali na wanaubaridi kuhusu
maumivu yetu, na hivyo kuwachukia pia.
Hivyo,
katika kukutana kwa wawili hawa hasa kipindi hiki cha pasaka, mmoja wao yaani
Yesu Kristo ana majeraha ya UTUKUFU, na mwingine yaani Tomaso ana majereha ya
maumivu ya ndani. Yesu Kristo alikuwa tayari kujiponya kwa nguvu ya majeraha
yake. Tomaso alihitaji kuponywa majeraha yake lakini hapakuwa na mtu wa
kumponya. Hapa ndipo wanapokutana wajeruhiwa hawa wawili. Mjeruhiwa wa kwanza
anamponya wa pili. Uponyaji huu unajionyesha kwa maneno ya Tomaso mwenyewe
anapomjibu Kristo baada ya Kristo kumtaka kuvitia vidole vyake kwenye makovu na
majeraha yake, akisema, “Bwana wangu na Mungu wangu!” Yoh 20:28. Mwisho wa kukutana huku, kila mmoja
anapata majeraha ya UTUKUFU, na kuwa tayari kuponya wengine wenye maumivu.
Wapo maelfu ya watu
wameumizwa na kujeruhiwa miongoni mwetu. Wengine wanabeba chuki kwa usiri
mkubwa ndani ya mioyo yao kwa kusalitiwa kulikotokana na kutokuwa na uaminifu kwa
mwenzi wake wa ndoa. Wengine wanabeba chuki dhidi ya wanaofisi wenzao kwa
kuwaenezea umbea na uongo mitaani. Wengine pia wanabeba ndani ya mioyo yao
chuki na manung’unika kwa milongo ya miaka iliyopita kwa kukosa sehemu ya
kuponyeshwa na kusikilizwa. Wengine maumivu haya wanayabeba tangu kuzaliwa kwao
hadi sasa kutokana na namna ya kutungwa mimba kwao kuliko kataliwa na kwa
bahati mbaya au nzuri akazaliwa. Wengine wamesalitiwa na wapenzi wao na
kuyabeba hayo hadi sasa hata kama wanaishi maisha yao ya ndoa. Wapo wengi sana
waliojeruhiwa na kuumizwa vibaya kwa namna tofauti tofauti. Jambo hili linaweza
kutokea kwa yeyote yule, iwe mlei, mtawa na hata mtawa na mkleri.
Ndugu yangu, hata kama tutayaficha
majereha na maumivu yetu, kwa binadamu itafika wakati lazima atayaonyesha tu
wazi kwa kutafuta uponyaji. Ni njia mojawapo ya kurudisha mizania ya ndani
katika uumbaji wetu. Ukweli ni kwamba walioumizwa kweli na kupata majeraha ya
ndani hawawezi kuficha na kuvaa kinyago hicho kwa muda mrefu. Wanaweza
kuwadanganya wanaowazunguka kwa wakati tu, ila hawawezi kujidanganya wenyewe na
kuficha ukweli huu. Maumivu ya ndani ni vigumu sana kuyavumilia.
Watu hawa wanahitaji
uponyaji. Wangepewa nafasi na uchaguzi, wote wangependa kugusa majeraha ya
Kristo. Wanapenda kujua kwa uhakika kama kuna mtu anayewapenda vya kutosha kwa
kujeruhiwa kwao na mtu huyo yupo tayari kufa kwa kuwapenda. Tatizo kubwa ni
kwamba hawawezi kumwona tena Kristo. Wanaweza tu kuwaona watu wanaojiita
Wakristo. Wakristo ambao wanajulikana kwa kujinadi kulibeba jina la Kristo na
siyo kumuishi Kristo. Swali ni hili: Je wakristo hawa wapo kweli kama Kristo?
Je, wakristo leo wameumizwa vya kutosha kwa UPENDO kiasi kwamba wanaweza
kuwaponya walioumizwa? Je, ni kweli wakristo leo wamefufuka kutoka kifo cha
kujijali wenyewe, na ubinafsi, kwamba wanaweza kuwa matumaini na kielelezo cha
kuwarudisha waliopotea kwenye kundi kwa kuumizwa kwao?
Ndugu yangu, kuurithi
ufalme wa Mungu, ni kuishi vyema wito wako na vipaji alivyo kupa Mungu. Vipaji
hivyo siyo mali yako bali viwafaidie wengine, na hasa katika kuyaponyesha
majeraha na maumivu waliyokuwa nayo. Hiki ndicho kielelezo cha maisha yetu kama
Wakristo na wafuasi wa Kristo Mfufuka. Jambo hili si katika kuangamizana, bali
katika ufaidiana na kuongozana katika umilele ambao ndiyo makusudi ya Ufalme wa
Mungu.
Wapendwa katika Kristo,
ulimwengu wa leo unamwitaji sana Kristo. Kama ulimwengu usipomwona Kristo kwa
Wakristo wa leo, waliojerehiwa watajitoa kwa Mungu, na kubeba mioyo yao
inayovuja damu na vidondo visivyoponyeka kwingine kusipo Mungu. Na wanavyojitoa
huku ufikia mahali na kuinamisha vichwa vyao na kufikiri katika akili zao:
“Mungu amekufa!”
Wapendwa wana wa Mungu,
ikiwa wewe ni Mkristo uliye hai ni vyema ukafahamu thamani ya Ukristo wako,
yaani umekombolewa kwa Damu ya thamani kubwa sana, yaani Mwana-kondoo, Yesu
Kristo. “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha
au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu;
bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa,
yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Hivyo maisha yako na yangu hapa duniani
tunapaswa kuyasalimisha yote na kwa asilimia zote kwa Yesu Kristo Mwana wa
Mungu aliye hai. Tendo hili la kujisalimisha ndiko kuabudu kwenyewe kuliko hai
na kwenye kumpendeza Mungu.
Kujiita Wakristo bili
Kristo ni kupotea muda kabisa kwa sababu kwa kufanya hivyo maisha hayo hayana
njia, kweli, uzima (tungali hapa duniani) na ufufuo (maisha ya uzima wa
milele), Yoh 14:6. Hivyo ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii,
tungali hapa duniani wakuhimidiwa ni Mungu, na kwa njia ya pekee na ufunuo
uliokamilika kwa Yeye aliyemwilishwa (Neno), Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa Kristo
Yesu kuna Njia, Kweli, Uzima, na Ufufuo wa wafu. Kwake Yesu na kupitia kwake
tunahesabiwa haki na Mungu kwa wana na warithi wa ufalme wake Mungu. Na kwa
namna hiyo, “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema
zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka
kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio
na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,” 1 Pet 1:3:4. Ndugu
yangu, tumaini yenye uzima lipo kwa Kristo Yesu, na siyo kwa kile tulicho au
yale tunayoyamiliki hapa duniani. Tungali hapa duniani tu waangalizi wa muda
mfupi kwa yale tunayoyamiliki. Kwayo (tunayoyamiliki) kama yalivyo hayana
umilele ingawa tuliyakuta na tutayaacha.
Hivyo wapendwa katika
Kristo, yatupasa mimi na wewe kuyashinda majaribu tukiwa na ufahamu kwamba
‘maisha ni jaribu,’ na kulishinda jaribu ndipo kunakotupatia Imani yenye
thamani kupita yote tuwezayo kuwa nayo. Vita vyetu vya kiimani kama
anavyotufundisha Mtume Petro ni kulishinda jaribu “ili kwamba
kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo,
ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na
heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo,” 1Pet 1:7. Tokeo la kubebwa na
ulimwengu wa vitu ni anguko kubwa la ‘uzuni.’ Furaha ya kweli ipo pale
tunapoyasalimisha yote kwa Kristo Yesu. Kristo awe tegemeo na msukumu wa yote
tuyafanyayo, na tumuone kwa wengine yale yote tuyafanyayo katika jamii
tunayoishi. Lengo hapa siyo tu kuzishika au kuzifahamu amri za Mungu kama ndege
yule ‘kasuku,’ bali amri hizo za Mungu zimulike uhai uliopo ndani yetu binafsi
na wale wote tuliowekwa dhamana kwao ikiwa ni pamoja na wale wenye uhitaji wa pekee.
Bwana na Bibi Bakari
Salum wenye asili ya Uarabuni walijijenga kwa muda mrefu kwenye biashara yao ya
kuuza juice ya embe. Iliwachukua miaka 12 hivi kwa shida na taabu, na leo wana
kiwanda kikubwa cha juice.
Miaka miwili iliyopita
baada ya biashara kupanuka walimwajira kijana mmoja kutoka China kama Meneja
masoko. Hata hivyo kwa muda wote huo wa kuishi pamoja familia hii haikubahatika
kupata mtoto ingawa ilikuwa hamu yao kubwa.
Mwaka mmoja uliopita
ikiwa ni pamoja na kupanuka kwa biashara yao ya juice, walibahatika kumpata
mtoto wao wa kwanza wa kiume. Mtoto huyu tangu siku za uchanga wake alionekana
akiwa na macho madogo sana. Hali hii haikumfurahisha Bwana Bakari Salum. Hivyo
aliona ni vyema kuonana na Daktari bingwa wa macho kujua kulikoni.
“Daktari, mtoto wangu
huyu tangu kuzaliwa kwake naona ana tatizo la macho, na kama ikiwezekana afanyiwe
upasuaji ili aone vizuri,” Bakari alimweleza Daktari. Hata hivyo baada ya
vipimo Daktari hakuona tatizo lolote kuhusu macho ya mtoto yule.
“Ndugu Bakari, mtoto
wako ana macho ya kawaida kabisa na hana tatizo lolote. Tofauti ni kwamba macho
yake ni madogo kuliko yenu wazazi. Nafikiri mtu wa kufanyiwa upasuaji ni wewe
ili uone vizuri,” Daktari alimweleza Babari huku akitabasamu.
“Daktari wataka niambia nini kwa jibu
hili?” Bakari alimuuliza Daktari kwa taharuki. “Nenda nyumbani kwako na kazini
mwako mtafute mwenye mfanano wa macho ya mtoto wako. Ila kuwa na kifua kama
mwanamme,” Daktari alisisitiza.
Mara Bakari ilimjia picha ya Meneja wake
wa masoko, na hasa ukaribu wake na mke wake. Ujumbe wa Daktari ulifika mahali
pake!
“Bwana
wangu na Mungu wangu!” Yoh 20:28.
Tusali:-Ee Yesu Mwema kwa
majeraha yako ya Utukufu, yaponye maumivu yetu ya ndani. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario