JUMANNE WIKI YA 5 YA KWARESMA
Somo:
Hes 21:4-9
Zab:
102:1-2, 56-17, 18-20
Injili:
Yoh 8:21-30
Nukuu:
“Watu wakamnung’unikia
Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe
jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai
chakula hiki dhaifu,” Hes 21:5
“Musa akafanya nyoka ya
shaba, akaiweka juu ya mti; hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile
nyoka ya shaba, akaishi,” Hes 21:9
“Ninyi ni wa chini,
mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo
naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya
kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu,” Yoh 8:23-24
“Mtakapokuwa mmemwisha
kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa
sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo.
Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya
sikuzote yale yampendezayo,” Yoh 8:28-29
TAFAKARI:
“Uovu wa Mwanadamu na ghadabu ya Mungu, toba ya kweli na Msamaha wa dhambi
kupitia kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo Msalabani.”
Wapendwa wana wa Taifa
la Mungu, leo na tutafakari neno hili, “Uovu wa Mwanadamu na ghadabu ya Mungu,
toba ya kweli na Msamaha wa dhambi kupitia kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo
Msalabani.” Huu ndio ukweli tunaouona katika somo letu la leo na injili.
Kwa uovu na hasa dhambi
ya manung’uniko ya Wayahudi kule jangwani, Mungu anaghadabika, na hivyo anatuma
nyoka za moto na watu wanang’atwa na kufa kwa idadi kubwa. “Watu
wakamnung’unikia Mungu, na Musa, “ Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya
Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu
zinakinai chakula hiki dhaifu,” Hes 21:5
Ni jambo la kawaida na
la hulka ya mwanadamu kulaumu na kusahau yote ya nyuma mazuri anapopatwa na
shida, na wakati mwingine kukosa shukrani. Ni wazi pia katika maisha yetu huwa
rahisi kukumbuka siku za shida kuliko siku zile ambazo mambo yalituendea vyema.
Manung’uniko ya Wayahudi yanafuta mema yote Mungu aliyo watendea na hasa
kuwatoa utumwani Misri. Manung’uniko yao yanakuwa chukizo kwa Mungu. Wayahudi
wanakosa uvumilivu na moyo wa shukrani.
Ndugu yangu, “Moyo usio
na shukrani ukausha mema yote.” Tendo lako la shukrani kwa Mungu ni kutambua
mema aliyokutendea na anayokutendea bila mastahili yako. Tendo hili la shukrani
hubadilika na kuwa ombi tena kwa kile alichokukirimia Mungu kwa upendo wake.
Mungu kamwe hachelewi
kurudisha ukarimu wake kwetu mara tunapotambua ukengeufu wetu, na kumrudia kwa
toba. Wayahudi wanatambua kosa lao na wanaomba huruma ya Mungu kupitia Musa
Mtumishi wa Mungu. Mungu anampa Musa maelekezo ya kufanya toba hiyo. Maagizo
hayo ya Mungu kwa Musa ni kama ifuatavyo, “Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke
juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya
nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti; hata ikiwa nyoka amemwuma mtu,
alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi,” Hes 21:8-9. Mimi na wewe kila mmoja
akiitazama historia yake tunaweza kugundua ni maeneo gani tulikosa moyo wa
shukrani na kudondoka katika dhambi ya manung’uniko. Hivyo ni wakati muhafaka
wa kupokea huruma hii ya Mungu kwa kufanya toba ya kweli na majuto ya dhambi.
Injili ya leo imebeba
taswira hiyo hiyo kama tulivyoona katika somo letu la leo. Wayahudi hawasadiki
ayafundishayo Yesu Kristo. Kristo licha ya kuyasema yote wazi wazi na kuwapa
chimbuko la yale ayasemayo, bado wayahudi wanakuwa na shingo ngumu kuyasadiki.
Kwa kosa hili la kutokuamini kwao, Yesu anawaambia watakufa kwa dhambi zao.
“Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa
ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa
sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu,” Yoh
8:23-24.
Hali ya ubinadamu wetu
ni hali ya chini katika maana halisi ya anguko letu katika dhambi. Hali hii ya
ubinadamu wetu, inahitaji msaada na neema ya Mungu kufikia ukamilifu. Mwenye
uwezo wa kuyakamilisha haya ndani mwetu na kuujenga tena uhusiano wetu
uliobomoka kwa sababu ya dhambi ni Kristo ambaye ni mpatanishi kati yetu na
Mungu. Kwa mantiki hii, tusipoyasikia na kuyasadiki ayasemayo Kristo,
hatutaweza kuokolewa katika dhambi zetu. Ni kwa kupitia Yesu Kristo kwamba,
“mtu huyu Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape
Waisraeli toba na Msamaha wa dhambi,” Mate 5:31. Kwa tendo hili, Yesu Kristo ni
zaidi ya Musa kwa sababu, “Mungu alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha
na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna
ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana,
mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” Kol 1:13-15.
Ndugu yangu, hakuna
njia nyingine kwetu kama Wakristo na wenye kufuata mafundisho yake Kristo,
kupata wokovu na msamaha wa dhambi bila Yesu Kristo. Tendo hili Yesu
kalikamilisha pale Msalabani alipoinuliwa kwa sababu ya dhambi zetu. Na hivi
Yesu anasema, “Mtakapokuwa mmemwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo
mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila
kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami;
hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo,” Yoh
8:28-29. Kama iliyokuwa nyakati za Musa walivyopata uponyaji kwa kupitia nyoka
ya shaba kule jangwani, msamaha wa dhambi zetu, na wokovu unapatikana kwa
kupitia mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo.
Ndugu yangu tendo hili
linawezekana tu kwetu tunapokuwa tayari kufanya toba ya kweli na kumrudia
Mungu. Kristo muda wote yupo katika kiti chake cha hukumu, yaani msalabani
akiwa ameifungua mikono yake na kutuambia, “ona nimefanya haya yote kwa sababu
ya upendo wangu kwako, njoo nami nakupokea kama ulivyo.” Je, mpendwa katika
Kristo, washiriki mara kwa mara upendo wa Mungu katika Sakramenti yake ya
upatanisho?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mtakapokuwa mmemwisha kumwinua
Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno
kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo,” Yoh 8:28
Tusali:-Asante
Yesu kwa kunipenda na kunipokea kama nilivyo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario