JUMAPILI YA 3 YA PASAKA-A
Somo I: Mdo 2:14, 22-33
Zab: 16:1-2, 5, 7-8, 9-10, 11
Somo
II: 1Pet 1:17-21
Injili: Lk 24:13-35
Nukuu:
“Yesu
huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake,”
Mdo 2:32
“Kisha Yesu akawaambia,
Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko
watakakoniona,” Mt 28:10
“Na ikiwa mnamwita Baba, yeye ahukumuye kila mtu pasipo
upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa
kukaa hapa kama wageni,” 1Pet 1:17
“Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa
vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu
usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya
mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19
“Ikawa
katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana
nao,” Lk 24:15.
“Macho yao yakafumbwa
wasimtambue,” Lk 24:16.
“Wakamwambia, Mambo ya
Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena
mbele za Mungu na watu wote; tena
jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa,
wakamsulibisha. Nasi tulikuwa
tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli,” Lk 24:19-21.
“Akawaambia, Enyi
msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii! Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na
kuingia katika utukufu wake?” Lk 24:25-26.
“Wakamshawishi
wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha,” Lk 24:29.
TAFAKARI:
“Kaa pamoja nasi Bwana.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa
anaadhimisha Dominika ya tatu ya Pasaka ya Mwaka “A” wa Kanisa. Masomo yetu ya
leo yanatutafakarisha namna ya kukaa na Bwana wetu Yesu Kristo. Huu ni mkao wa
Kipasaka. Ni mkao wa ufufuko. Ni mkao wa kuyatafuta yale ya juu Kristo aliko,
Kol 3:1.
Wapendwa wana wa Mungu,
moja ya kweli kwamba Kristo amefufuka na yu hai, ni ujasiri wa jumuiya ya
kwanza ya Wakristo kuishi kwa matendo na kumuhubiri Kristo mfufuka bila shaka
na wasiwasi wowote. Jumuiya hii ya kwanza wapo tayari kwa lolote limuhusuyo
Kristo Mfufuka. “Yesu huyo Mungu alimfufua, na
sisi sote tu mashahidi wake,” Mdo 2:32. Ushupavu
huu ni kutokana na kuguswa na kuishi uhasilia wa Ufufuko wa Kristo. Hapana
shaka kwamba Kristo amefufuka na yu hai katika maisha yetu na hali zetu kila
siku.
Injili
yetu ya leo inatupa umuhimu wa kukaa muda wote na Kristo Mfufuka. Maisha yetu
yanapita kwa kasi sana kama moshi, na wakati mwingine tunaishi tukiwa wakavu
sana kiroho. Yesu Kristo kwa walio wengi ni Yesu wa Historia. Kwa walio wengi
Yesu huyu hana nguvu tena. Tatizo kubwa tunalokutana nalo katika maisha ni
kuyaweka matamanio yetu mbele zaidi ya mafundisho na kweli anayotufundisha
Kristo. Sintofahamu hii inawakuta wanafunzi wale ambao wanaona Kifo cha Kristo
kama tukio la kudanganywa hivi, na hakuna maana kabisa kwa yule ambaye
walimtegemea sana na leo anawaangusha. Kifo hiki cha aibu cha msalaba kwa
wanafunzi hawa kimewatoa matumaini yote.
Yesu
Kristo hata katika sintofahamu hizi, bado yupo tayari kutusikiliza na kuzidi
kutufundisha, licha ya kwamba hatumuoni kwa kuificha taswira yake, ili mradi tu
tumpe nafasi. “Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa
mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote; tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa
wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha. Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye
ndiye atakayewakomboa Israeli,” Lk 24:19-21.
Yesu hachoki
kutukumbusha yaliyompasa kufanya na yaliyotabiriwa juu yake. Haya yote yapo
katika Maandiko Matakatifu. Mt. Jerome anasema hivi kuhusu Yesu Kristo,
“tunapokuwa wajinga wa maandiko matakatifu, ni kwa namna hiyo hiyo tu wajinga
kuhusu Yesu Kristo.” Kuhusu jambo hili Yesu anatupa sababu ya yale yote
yaliyojiri kuhusu Kifo na Ufufuko wake. “Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya
kuamini yote waliyoyasema manabii! Je!
Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?” Lk 24:25-26. Ndugu yangu hapa tunakumbushwa pia,
kwamba hakuna Utukufu pasipo Msalaba. Penye Msalaba pana Utukufu, na sasa ni
rahisi kuupata Utukufu kwa sababa Kristo kesha ushinda Msalaba.
Wapendwa,
Kristo anajifunua kwetu leo katika kuumega mkate. “Ikawa
alipokuwa ameketi nao chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa.
Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao,” Lk 24:30-31. Kuumega mkate kunatanguliwa na kulishwa neno lake
na kulielewa. Tukio la wanafunzi wa Yesu kukutana naye njiani kuelekea Kijiji
cha Emau, ni mtiririko mzima wa adhimisho la Misa Takatifu. Adhimisho hili lina
sehemu kuu mbili; Liturjia ya neno na liturjia ya Ekaristi Takatifu. Kwa
mantiki hii, uwezekano wa Kristo kujifunua kwetu wakati wa Ekaristi Takatifu,
unabebwa kwanza na ufahamu wetu wa kulisikiliza neno lake, kulipokea,
kulitafakari, kulishirikisha, na kuliishi. Wanafunzi hawa wa Yesu wanakuwa na
hamu ya kukaa naye zaidi baada ya kulishwa neno na Kristo ingawa hawakumfahamu.
Ndugu
zangu, wale ambao wamezoea kuchelewa na mara nyingine kushiriki tu liturjia ya
Ekaristi Takatifu, ni wavamizi wa Mlo Mtakatifu wasioujua vizuri. Ni sawa na
kukishambulia chakula kitamu na kizuri wakati ukiwa na mikono michafu. Ni
vizuri kuhudhuria sehemu zote mbili za kiliturjia na ndivyo inavyotakiwa kwa
Mkristo na hasa kwetu, ambao Ekaristi Takatifu kicho kiini cha yote. Wapo kati
yetu ambao huingia Kanisani na moja kwa moja kujongea Meza ya Bwana. Huu ni
uhuni wa hali ya juu kufanywa na Mkristo. Mwisho na muhimu tusichoke kuudhuria
mara kwa mara maadhimisho ya Maabudu ya Yesu wa Ekaristi-Sakramenti Kuu. Hapa
anakaa kwetu na kujifunua kwetu.
Kukaa na Kristu kunatuwajibisha kubadili
mitazamo yetu ikiwa ni pamoja na kuyaacha mazoea yetu yasiyokuwa na mwelekeo.
Kukaa na Kristo ni kuishi maisha yanayoongozwa na malengo. Jambo hili si rahisi
sana kwa sababu linakufanya uishi maisha ya kisadaka. Na sadaka nzuri na yenye
kumpendeza Mungu ni ili inayouma. Ni sadaka ili inayasema zaidi kile ulicho, na
ukitoe chote bila kujibakiza. Hili ndilo fumbo zima la Msalaba.
Pamoja na ugumu huo, Yesu anatutaka
tutofautishe namna yetu ya kutenda na kuishi ili tulenge fumbo lile la kifo
chake cha Msalaba ambapo ndipo ulipotundikwa wokovu wetu na kumpatia Kristo
Utukufu wake, nasi kuhesabiwa haki ya kuwa wana wa Mungu bila ya mastahili yetu
binafsi. “Nanyi mfahamu kwamba
mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka
katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya
thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,”
1Pet 1:18-19.
Damu hii yenye thamani
kubwa iwe chachu na kielelezo cha imani yetu na kumwamini Mungu. Ni kwa Damu
hii ya Mwana-kondoo huyu aliye na hila, Yesu Kristo, “ambao kwa yeye mmekuwa
wenye kumwamini Mungu, aliyemfufua katika wafu akampa utukufu; hata imani yenu
na tumaini lenu liwe kwa Mungu,” 1Pet 1:21. Hivyo tenda na ishi yetu isukumwe
kwa kuthamini kukombolewa kwetu huku kuliko kwa thamani kubwa ajabu.
Kristo Yesu hali akijua
hulka yetu wanadamu anatukumbusha kuepuka kutawala wengine kwa mabavu kama
asemavyo, “Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala
kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha,” Mk 10:42. Kristo hataki hilo litokee
kwa Mitume na wafuasi wake. Kinyume chake tutangulize mbele ‘kutumika vyema’ na
siyo ‘kutumikiwa wala kuogopwa.’ “Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja
kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi,” Mk 10:45.
Maana yake nini?
Wapendwa wana wa Mungu,
Kristo anatutaka tuelewa kuwa utumishi ni kujitoa kwa watu kwa upendo na
kuwapenda. Huwezi kuwatumikia watu vizuri kama huwapendi. Na ukifanya hivyo
(kuwatumikia ukiwa huwapendi) basi nyuma yake kuna ubinafsi mkubwa na
kujitazama wewe tu, familia yako, ndugu zako, marafiki zako, na mwisho kupoteza
dhima nzima ya kutumika na umma. Hapa tunahitaji nidhamu ya hali ya juu na
yenye kusukumwa na utii wa kweli. Hivyo, “Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii
kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi jitahidini
kupendana kwa moyo,” 1Pet 1:22. Kupendana kwa moyo ni kumwona Kristo Yesu kwa
wote unaotumika kwao. Hapa ndipo kule kutoa nafsi yako iwe fidia ya wengi, Mk
10:45b.
Pili, kuwa tayari
kutumika kunatutaka kusahu uzamani wetu na mazoea yetu. Ni kuzaliwa mara ya
pili kwa kuliishi neno la Mungu lenye uzima. Kuliishi neno la Mungu lenye uzima
kwanza kabisa ni kuwa tayari kuhusu neno hilo. Pili, ni kuwa na uwezo wa
kusikia neno, kulipokea neno, kulitafakari neno, kulishirikisha neno, na kuwa
shahidi wa neno hilo likiakisi maisha yako. “Kwa kuwa mmezaliwa mara
ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la
Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele,” 1Pet 1:23. Ndugu yangu, neno hili
tunahubiriwa kila siku. Lifanye kuwa sehemu ya maisha yako kwa sababu, “Neno
la Bwana hudumu hata milele. Na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa
kwenu,” 1Pet 1:25.
Tatu, kuwa tayari
kutumika ni kuukubali utumishi kwanza ambao mwisho wa siku ndio utakao sadifu
ukubwa ule kama kweli ndio unaoutamani. Hivyo, “bali mtu anayetaka kuwa mkubwa
kwenu, atakuwa mtumishi wenu,” Mk 10:43b. Pili, kuikubali hali ya utumwa kwa
ajili ya wote. Hali hii ya utumwa ndiyo itakayotuweka kuwa wa kwanza au wa
mwisho. Hivyo, “na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote,”
Mk 10:44.
Ndugu yangu, huu ndio
utumishi na kutumika kwa yeyote yule mwenye hofu ya Mungu. Na kama upo tayari
kutumika na unamatamanio haya, omba hivyo
ukifahamu wajibu wa kile
ukiombacho. La sivyo hutotumika vyema na mwisho wa siku
ni kupoteza vyote: Utakatifu wako, na uzima ule wa milele.
Mama Vituka aliye na
Kilabu cha pombe ya kienyeji kwa jina la ‘Kilimani’ ni marufu sana kijijini
Mtakuja. Jumapili iliyopita kwa jambo la kushangaza hakupata na wateja wa pombe
yake ya kienje hadi ilipofika saa kumi na mbili jioni alipoinga mlevi mmoja
maarufu kijijini hapa ajulikanaye kwa jina la Matumaini.
Matumaini alipofika
kwenye Kilabu kile, Mama vituka alimpatia bohora la pombe la ulanzi. Matumaini
alilifyonza kwa hisia kali huku akiimba wimbo wa mwanamzika Bob Marley, “Afrika
Unity” akiwa akidesadesa.
Basi wapita njia
walipomwoma Bwana Matumaini akikwa na bohora la ulazi huku akiimba kwa hisia
wimbo ule, nao walijongea kwani ilipata kiashirio kwamba sehemu ile pombe ipo.
Baada ya nusu saa
Kilabu kile kilijaa watu na pombe iliuzika haswa. Kwa kelele za Bwana
Matumaini, Mama Vituka aliamua kumtimua nje ili wateja wake wapate utulivu. Kwa
kitendo kile watu wote walisimama na kusema kwa ukali, “asingekuwa Bwana huyu,
tusingelijua hapa kama kuna kinywaji hiki. Tunaomba usimbughuzi. Mpe pombe sisi
tutamlipia.”
Ndugu zangu, wakati
mwingine yawezekana mambo yakakuendea vizuri sana, ila usibweteke. Yawezekana
kuna akina Bwana Matumaini wengi sana wamekufanya uwe kama ulivyo.
Hivyo, leo Kanisa letu
lipo imara kwa sababu Yesu Kristo Mfufuka na aliye hai yupo nasi. Uwepo wa
Ekaristi Takatifu waupa uhai Kanisa letu Takatikafu. Wengi miongoni mwetu na
wasio jua fumbo hili wanaweza kubeza sana kwa sababu wanaona maumbo haya ya
Mkate na Divai kama yalivyo kwa mwono wake wa nje, ila hawajui kile kibebacho
fumbo hilo. Amina!
“Ikawa alipokuwa ameketi nao
chakulani, alitwaa mkate, akaubariki, akaumega, akawapa. Yakafumbuliwa macho
yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao,” Lk 24:30-31.
Tusali:-
Ee Yesu, kamwe usituache katika sintofahamu zetu. Kaa nasi daima. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario