IJUMAA WIKI YA 2 YA PASAKA
Somo:
Mdo 5:34-42
Zab:
27: 1, 4, 13-14
Injili:
Yoh 6:1-15
Nukuu:
“Lakini
mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa
na watu wote, akasimama katika baraza, akawaambia, Enyi waume wa Israeli,
jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa,” Mdo 5:34a-35.
“Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu
hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu,
itavunjwa, lakini ikiwa imetoka
kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu,” Mdo
5:38-39
“Nao walipowaita mitume, wakawapiga,
wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao,” Mdo
5:40b
“Nao wakatoka katika ile baraza,
wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya
Jina hilo,” Mdo 5:41
“Na
kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao, hawakuacha kufundisha na kuhubiri
habari njema za Yesu kwamba ni Kristo,” Mdo 5:42
“Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu
waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa,” Yoh 6:2
“Yesu akasema, Waketisheni watu. Basi
watu waume wakaketi, wapata elfu tano jumla yao,” Yoh 6: 10a-10c
“Basi Yesu akaitwaa ile mikate,
akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale samaki kwa kadiri
walivyotaka,” Yoh 6:11
“Kusanyeni vipande vilivyobaki,
kisipotee cho chote,” Yoh 6:12b
“Hakika huyu ni nabii yule ajaye
ulimwenguni,” Yoh 6:14b
“Akajitenga, akaenda tena mlimani yeye
peke yake,” Yoh 6:15b
TAFAKARI:
“Nguvu ya Maadili na Unyenyekevu hutuhesabia haki na kweli kama wafuasi wa
Kristo. Mwono huu wa maisha utuweka karibu na Kristo nyakati zote.”
Wapendwa wana Mungu,
kwa pamoja tutafakari masomo ya leo na hasa nini maana ya nguvu ya kimaadili na
unyenyekevu kwa kile tunachoishi kama wafuasi wa Kristo. Matokeo ya ukweli huu
ndiyo ushuhuda wa kweli kwa jamii inayotuzunguka. Hapana shaka yoyote kwamba,
jumuiya ya kwanza ya Wakristo walipata nguvu ya kulinena jina la Kristo, na
hivyo kugeuka kuwa mwiba mkali kwa watesi wao, kutokana na nguvu yao kimaadili
na unyenyekevu waliokuwa nao.
Mamlaka haya ya
kimaadili hujijenga kwanza kabisa kwa KUJITAMBUA. Kujitambua huku ni pamoja na
kujua nini shabaha ya kile unachokiishi, na malengo yake. Kwa upande mwingine
ni kujua malengo ya maisha yako. Maisha ya aina yoyote ile huongozwa na
malengo. Maisha yanapokuwa na malengo, maisha hayo huwa na mwono tofauti
kabisa, kwani rasilimali muda hutumika vizuri. Maisha yasipoongozwa na malengo
ni sawa na wingi wa miaka usio na maana.
Haina maana yoyote
kujitapa kwa kuwa na miaka 50 au 90-(yaani kuishi kwa ‘bonus’), bila kutafakari
umaana wa miaka hiyo na uhusiano wako na Mungu. Ni ukweli pia idadi ya miaka
kwa Mungu haina maana. Umaana wa idadi ya miaka huja pale tu, unapoanza
kujiuliza na kufanya tafiti moyo ya “ulichofanya na idadi hiyo ya miaka
uliyopewa kama zawadi.”
Ndugu yangu tunaye
safiri wote katika tafakari hii, ukishajitambua katika maana niliyokwisha isema
hapo juu, hatua ya pili itakuvuta KUJISHUSHA. Na hii ndiyo maana halisi ya
kujinyenyekesha kwa kile ulichodhani mwanzoni ulikuwa kumbe sivyo, ili uwe kile
ulicho katika uhalisia wako na yale unayotaka kuyafanya ili ufikie malengo
halisi ya maisha yako. Jambo hili kulifikia si hatua ya mara moja kama kulala
na kuamka. Kinachotukwamisha mara nyingi ni pale tunapovaa kinyago “mask” kwa
kuficha ukweli wetu halisi ambao mara nyingi hatupendi kuugusa wala
kuuzungumzia popote pale. Hakuna filamu nzuri ya maisha zaidi ya maisha yako mwenyewe.
Kuitazama filamu hii ni kujinyenyekesha kuliko kwa ndani kabisa. Ukiweza fanya
hivyo, ni mwanzo wa safari ya maisha yenye malengo.
Mambo haya mawili
muhimu; kujitambua na kujishusha ambayo matokeo yake ni kuwa na nguvu kimaadili
na unyenyekevu. Hii ndiyo silaha pekee ya kumjua Kristo na maagizo yake kadiri
ya mafundisho yake. Jambo hili ndiyo sababu ya kuogopwa kwa jumuiya ya kwanza
ya Wakristo na kuwafanya tofauti na waliowatangulia kama akina Theuda na Yuda
Mgalilaya ambao walipata umaarufu na mara wakatoweka, Mdo 5:37-37.
Jambo hili kwa Kanisa
la Mwanzo lilikuwa na faida kuu tatu; kwanza kabisa waliumega mkate-kwa
kutambua mahitaji yao ya kila siku “basic needs.” Pili waliumega Mkate kama
adhimisho la Ekaristi Takatifu-ikiwa ndicho kiungo pekee cha umoja wao
kijumuiya. Yesu Kristo hapa alikuwa kiunganishi cha umoja huo hadi leo. Jumuiya
yeyote ile ya Kikristo kwa mfumo wowote ule wa maisha bila Yesu wa Ekaristi
kuwa kiungo cha maisha hayo, jumuiya hiyo hubakia kuwa kama kikundi cha
waigizaji wasicho kijua wakiigizacho, Yoh 15:5. Na tatu waliumega mkate kwa
kulisikiliza, kulifundisha, na kulinena neno la uzima, yaani Maandiko
Matakatifu.
Wapendwa, ni katika
maana hii tunaona mtu maarufu kama Gamalieli akisimama na kutoa angalizo kwa
mafarisayo wenzake kuhusu dhuluma wanayoifanya dhidi ya wafuasi hawa wa Kristo.
“Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye
kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akawaambia, Enyi waume wa
Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa,” Mdo 5:34a-35. Mambo
wayafanyayo Wakristo hawa msingi wake ni Kristo, na utendaji wake ni nguvu ya
Kimaadili na Unyenyekevu.
Wakati mwingine tusipo
lijua jambo hili, hubaki kupingana na nguvu tusiyoijua. Gamalieli anawakumbusha
uwepo wa Mungu na uweza wake juu ya lililo haki. Kamwe hatuwezi kushinda dhidi
ya haki ya Mungu. Vita hii na msuguano huu dhidi ya Mungu ni angamizo kubwa
kwetu binafsi. Gamalieli anasema, “basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu
hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu,
itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa
Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu,” Mdo 5:38-39.
Leo mimi binafsi najiuliza ‘nini sababu ya mfululizo wa matukio ya kutisha
katika Taifa letu, ikiwa ni pamoja ajali barabarani, mauji ya kutisha, uvamizi,
utekaji, watu kutoweka kusikojulina, na majanga mengine ambayo kwa kiasi
kikubwa ni huzuni na majonzi katika jamii.’
Wapendwa, nina Imani
pasipo shaka kwamba, yawezekana wakati fulani mahali fulani, na watu fulani
hatukutenda iliyo haki. Ni ukweli pia katika jamii yetu, licha ya maovu mengi
tunayotenda mbele za Mungu, jambo hili ni wazi kabisa hatujachukua hatua za
utosha. Kumekuwepo na dhuluma za muda mrefu katika jamii yetu, na kubwa zaidi
ni dhulumu dhidi ya uhai. Ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi-Maalbino wamekuwa
wakiwindwa na kuuwa kama vile si binadamu na hawana haki ya kuishi. Vyombo vya
usalama ikiwa ndola yenyewe, haijafanya vya kutosha kunusuru maisha haya ambayo
ni zawadi ya Mungu kwa kila mwenye pumzi. Uhai ukiwa ndiyo uwepo wa Mungu
mwenyewe, kuukatiza au kuuchukua bila mamlaka yake Mungu ni kupingana na Mungu
mwenyewe. Je katika jambo hili tupo na
tutakuwa salama?
Jambo lingine ambalo ni laana pia kwa
taifa hili, ni kufumbia macho haki za wanyonge, na kuzipora haki hizo bila woga
wowote. Leo usipojulikana na mbaya zaidi kama huna fedha, huwezi patiwa haki
yako. Jambo hili limeshakuwa la kawaida kabisa hata pale unapotakiwa kupata
haki zako za kijamii kadiri ya katiba, kama vile matibabu, elimu na mengineyo.
Rushwa na Ufisadi ndiyo virusi hatari kabisa katika jamii yetu leo. Je, na hili
tupo na bado tutakuwa salama? Ni Mungu gani ambaye hatajitokeza na kusimama
katika uovu huu?
Wakristo wetu wa kwanza wanahesabiwa
haki kwa nguvu yao ya kimaadili na unyenyekevu pale wapoishi yale wayasemayo na
kuyashuhudia dhidi ya dhuluma ya watesi wao, na uovu wao juu ya mwenye haki
Yesu Kristo waliomwondosha katika ulimwengu huu kwa ukatili mkubwa kushuhudiwa
na binadamu. Wanapopigwa na kuteswa Wafuasi wa Yesu hawaachi kusimama katika
kweli na haki. Wanapokatazwa kulisema jina hili lenye nguvu ya ajabu-Yesu
Kristo hawaachi kuwa na furaha. Baada ya kipigo na mateso, “nao wakatoka katika ile
baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa
ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:41.
Ndugu yangu, ni mara
ngapi wafurahi kwa kuaibishwa kwa ajili ya Jina hili kuu ya Yesu Kristo
Mnazareti? Ni mara ngapi twataka kusafishwa majina yetu kwa vile tu
hayakutendewa haki? Ni mara ngapi tunapenda kutambulika tulivyo zaidi ya
kumtambulisha Kristo aliye mfalme wa amani, haki, upendo na unyenyekevu? Ni
ukweli usiotia shaka kwamba Kristo anapoinuliwa kwa yale tuyafanyayo ni kwa
namna hiyo hiyo nasi tunavyoinuliwa. Kinyume chake ni balaa kubwa, na maanguko
yake hayana mfano. Kristo asipokuwa kielelezo
cha maisha yetu, hatutaweza kumshuhudia hata majumbani mwetu, majirani zetu na
jamii inayotuzunguka. “Na kila siku, ndani ya hekalu na nyumbani mwao,
hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema za Yesu kwamba ni Kristo,” Mdo
5:42. Bila nguvu ya kimaadili na unyenyekevu bado hatutaweza kufikia hatua hii
ya Kanisa la mwanzo.
Bila shaka kila mmoja
wetu anayo sababu kubwa kabisa ya kuwa hapo alipo sasa. Jambo la kujiuliza ni
hili; Je, sababu hiyo imebeba ukweli wa kile ninachokichuchumilia kila siku ya
maisha yangu? Injili ya leo inatupa angalizo kuhusu changamoto hii muhimu ya
maisha. Ni kweli kila aliyemwona Yesu na kumfuata alikuwa na sababu yake.
Injili ya leo inatupa mbili ya sababu za kumfuata Kristo kadiri ya kundi lile
siku ile na wakati ule. “Na mkutano mkuu wakamfuata, kwa sababu waliziona
ishara alizowafanyia wagonjwa,” Yoh 6:2. Je, kutakuwa na sababu yeyote ya
kumfuata Yesu Kristo kama akiwaponya wangonjwa wote tulikuwa nao leo? Ndugu
yangu ishara tu ya kitu fulani katika ufuasi wa Kristo hauakisi Imani ya kwetu
juu ya Kristo licha kwamba ni moja ya kutupa uhakika wa nguvu na uwezo wa
Kristo.
Tunachopaswa kufanya
kama wafuasi wa kweli wa Kristo ni kufundisha ukweli juu ya Kristo na nafasi
yake katika maisha yetu ya kila siku. Huku ni kuwaketisha chini wanaotaka
kumjua. Yesu akasema, Waketisheni watu. Basi watu waume wakaketi, wapata elfu
tano jumla yao,” Yoh 6: 10a-10c. Kuwaketisha watu chini wenye shahuku ya kumjua
Kristo ni kutoa mafundisho ya kweli, ili kuziponya mwili, nafsi na roho zao
kutoka katika mahangaiko ya kila siku. Leo katika tukio hili, Kristo anawaponya
hangaiko hilo la mwili kwa kuwalisha mikate na samaki. Tendo hili ni moja ya
yale mambo makuu matatu waliyoyafanya mitume na wafuasi wengine wa Kristo baada
ya ufufuko wake.
Tendo hilo la kuwalisha
kimwili katika mahitaji yao, linatanguliwa na shukrani kwa yale
aliyowashirikisha, ambayo leo tunapata taswira halisi ya adhimisho la Ekaristi
Takatifu. Adhimisho hili ni karamu ya Kristo na shukrani kwa Mungu. “Basi Yesu
akaitwaa ile mikate, akashukuru, akawagawia walioketi; na kadhalika katika wale
samaki kwa kadiri walivyotaka,” Yoh 6:11. Ndugu yangu, moyo usio na shukrani
hukausha mema yote machoni mwa Mungu. Ni kwa moyo huu wa shukrani wanakula na
kusaza na kukusanya mabaki yaliyoyajaza makapu kumi na mbili. Makapu haya kumi
na mbili ni idadi ya makabila kumi na mbili ya Israeli. Kwa maana nyingine
kilichobaki kiliweza kuwalisha taifa zima. Kwa maana hii, muujiza huu wa Yesu
siyo tu kwa watu wale elfu tano waliokula na kusaza. Kristo katika jambo hili
la shukrani anatukumbusha wajibu muhimu sana. Kwa vile yote tulivyonavyo
tumepewa kwa upendo na huruma ya Mungu. Hivyo ili tuendelee kupata neema hizo,
yatupasa kuhifadhi yale yaliyobaki kwa sababu hatuna uhakika wa kesho. Yesu
anasema, “Kusanyeni vipande vilivyobaki, kisipotee cho chote,” Yoh 6:12b. Ni
mara ngapi unatumia hovyo aliyokukirimia Mungu kwa upendo ili hali jirani yako
analala na njaa kila siku? Je na baada ya kula na kushiba, bado unaona sababu
ya kumfuata Kristo kwa karibu?
Ndugu yangu, kula na
kunywa vikiongozwa na ishara mbalimbali, siyo sababu msingi wa imani yetu
kumfuata Kristo, na imani yetu haijajengwa katika mambo hayo. Tunaona baada ya
watu hawa kula na kushiba walitaka kumfanya Yesu kuwa mfalme wa Mikate. Kwa
maana nyingine tunamgeuza Kristo kama “Supermarket” ambayo tunauhakika wa
kupata kila kitu, na pale tu tunapokuwa na hitaji hilo. Tunapokuwa na mwono
huu, Kristo ujitenga nasi kwa sababu bado hatujamjua vizuri, na hatujui nafasi
na lengo lake katika maisha yetu ya kila siku. “Akajitenga, akaenda tena
mlimani yeye peke yake,” Yoh 6:15b. Kwa mantiki hii, inawezekana sala zetu
hazijibiwa kadiri tuombavyo kwa sababu tunamchukulia Kristo kama sehemu ya
kuyapata tu yale tuyamataniyo hata kama siyo ya muhimu katika maisha yetu. Na
ndiyo maana Mtume Yakobo anatupa angalizo kwa kutuwasa, “Hata mwomba, wala
hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” Yak 4:3
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nao wakatoka
katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili
kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo,” Mdo 5:41
Tusali:-Ee
Yesu na Mchungaji wetu Mwema, lisimamie Kanisa lako leo katika nguvu ya
kimaadili na Unyenyekevu kwa Viongozi wako na Wakristo wote kwa ujumla wao.
Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario