JUMAPILI YA 5 YA
KWARESMA-A
Somo I: Eze 37:12-14
Zab: 130:1-2, 3-4, 5-6, 7-8
Somo II: Rom 8:8-11
Injili: Yoh 11:1-45
Nukuu:
“Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama,
nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu
wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli,” Eze 37:12
“Naye
Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu
wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo,” Yoh 11:4
“Lakini
Yesu alikuwa amenena habari ya mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena
habari ya kulala usingizi. Basi hapo Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa,”
Yoh 11:13-14
“Yesu
akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa,
atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.
Je! Unayasadiki hayo?” Yoh 11:25-26
“Akamwambia,
Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule
ajaye ulimwenguni,” Yoh 11:27
“Basi
Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake,
akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa,” Yoh 11:32
“Yesu
akalia machozi,” Yoh 11:35
“Wale
waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu,” Rum 8:8
“Lakini
ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata
roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake,” Rum 8:9
“Na
Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho
yenu i hai, kwa sababu ya haki,” Rum 8:10
“Lakini,
ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye
aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali
ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu,” Rum 8:11
TAFAKARI:
“Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu. Nami
nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi.”
Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na maendeleo aliyoyafikia mwanadamu leo,
ikiwa ni pamoja na kuishi kwa kujiwekea vilinda uhai wake, “life securities,”
hata hivyo uhakika huo bila Mungu ni sawa na kutwanga maji katika kinu. “Kwa
sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa
nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi,
twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama
tukifa, tu mali ya Bwana,” Rum 14:7-8. Ndugu yangu, pamoja na mipango yako ya
muda mfupi na mrefu uliyojiwekea, kati yetu hakuna ajuaye ni kitu gani kitakachomtokea
sekunde chachetu tu zijazo. Je, tusifanye chochote kwa kuwa huu ndio ukweli?
Hapana! Tuyafanye na kuyapanga yote katika usahihi wake, na tufanye hivyo kwa
kumshirikisha Mungu kwa kila jambo.
Mara nyingi penye
mafanikio-‘kibinadamu,’ wengi wetu hitaji na uwepo wa Mungu huwa hitaji la
nyongeza. Tunaamini yote huenda sawa bila Yeye (Mungu) kuwepo. Hiki ndicho
kiburi kikubwa sana cha mwanadamu asiye na hofu ya Mungu ndani yake. Hali na
mazingira haya yanawakuta wana wa Israeli nyakati zile za Nabii Ezekieli. Mungu anawafananisha waasi hawa wa imani kama
mifupa isiyokuwa na nyama. Na hivi ndivyo wana hawa wa Israeli
walivyofananishwa na Mungu (mifupa isiyo na nyama wala uhai) katika swala zima
la imani. “Mifupa hii ni nyumba yote ya
Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea;
tumekatiliwa mbali kabisa,” Eze 37:11. Bila mkono wa Mungu tuyafanyayo hata kama yatavuma
sana hayatakuwa na mwisho mzuri. Na hivi ndivyo Nabii Ezekieli alivyozamishwa
na Mungu katika tafakari nzito na chukuliwa nje katika roho ya Bwana.
Hata
katika hali hii ya uasi na kukosa dira katika imani, Mungu hapendi hata mmoja
wetu apotee. Mungu ndiye uhai na uzima kwa kila kipumuacho, na Yeye huweza
kubadili tabia na mienendo ya vyote alivyoviumba. “Bwana
huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. Bwana hufukarisha mtu, naye hutajirisha;
Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7. Mungu akiwa ndiye yote na katika
yote, kwa upendo na huruma wake, “humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha
mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi
cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka ulimwengu juu
yake,” 1Sam 2:8. Tunapomrudia Mungu katika toba na majuto ya kweli, Mungu
huyabadili maisha yetu na kutufanya wapya mbele za macho yake. Na hivi ndivyo
alivyoitoa ahadi yake kwa wana wa Israeli na kusema, “Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi
yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli,” Eze 37:12. Naye
Mungu asema hivi juu ya mifupa ile ikiwa ni pamoja na hali nzima ya udhaifu
wako na wangu kwamba, “Tazama, nitatia pumzi
ndani yenu, nanyi mtaishi,” Eze 37:5. Hakuna jambo la kumshinda Mungu kwa
sababu namna tulivyo, na vyote tulivyonavyo vyaonyesha Furaha ya Mungu, na
kuufunua Utukufu wake.
Wapendwa
katika Kristo, ukweli huu kwamba hakuna jambo la kumshinda Mungu, na kweli
kwamba namna tulivyo na vyote ulivyonavyo vyaufunua utukufu na furaha ya Mungu,
vinajidhihirisha katika Injili ya leo kwa Lazaro kurudishiwa uhai wake. “Naye
Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu
wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo,” Yoh 11:4. Pamoja na kweli
kwamba Wayahudi walimwinda Yesu ili wa mwangamize, Yesu hakuwa na hofu ya
kurudi kwao na kuyafanya mapenzi ya Baba yake. Naye “…akawaambia wanafunzi
wake, Twendeni Uyahudi tena,” Yoh 11:7. Wanafunzi wa Yesu kwa hofu iliyomwisha
jengeka kwa kukoswa koswa Yesu kuuawa, wanapokea habari hii kwa mashaka. “Wale
wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga
kwa mawe, nawe unakwenda huko tena?” Yoh 11:8.
Ndugu
yangu, mpango ‘ovu wa mwanadamu’ kamwe hauwezi kufanikiwa kwa lile jema
alilokwisha likusudia Mungu kulifanya, ingawa Mungu aweza ruhusu ovu ili
kulipata jema katika ukamilifu wake. Yesu akiwa analijua hilo aliwaondolea hofu
wanafunzi wake na kuwajibu, “Je! Saa za mchana si kumi na mbili? Mtu akienda
mchana hajikwai; kwa sababu aiona nuru ya ulimwengu huu,” Yoh 11:9. Kwa maneno
mengine Yesu anataka kukuambia wewe na mimi hivi: -‘palipo dhamiri njema na
safi katika kulifanya jambo jema na lenye kumpendeza Mungu hapana sababu ya
kuwa na hofu licha ya kweli kwamba mazingira ya kulifanya jambo hilo
yameghubikwa na utata.’ Leo mambo mengi yanakwenda ndivyo sivyo kwa sababu tu
kati yetu na tulio wengi tumejawa hofu pasipo hofu, kuifunga midomo yetu
tunapotakiwa kusema, na mwisho wa siku kwa kujua twashirika moja kwa moja
katika ‘ovu hilo’ licha ya kwamba twajiweka mbali na kweli hiyo. Na hapa ndipo
penye anguko kubwa kwa sababu mmoja kati yetu “…“akienda usiku hujikwaa; kwa
sababu nuru haimo ndani yake,” Yoh 11:10.
Ndugu
yangu, kile alichokisema Yesu, yaani, “…mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli
itawaweka huru,” Yoh 8:32, ndicho anachotaka kukithibitisha mbele ya wanafunzi
wake. Na zaidi ya hayo Yesu anakutaka wewe na mimi leo kuamini pasipo shaka
yoyote kwamba Yeye ndiye njia, na kweli, na uzima; na mtu haji kwa Baba, ila
kwa njia yake, Yoh 14:6. Ni katika mantiki hii Yesu anawaambia wanafunzi wake
kwamba, “…Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha,”
Yoh 11:11. Hata hivyo wanafunzi wake hawakufahamu alichomaanisha Yesu kwa
maneno hayo. Tafsiri ya alichokisema Yesu ni hiki: “…alikuwa amenena habari ya
mauti yake; nao walidhania ya kuwa ananena habari ya kulala usingizi. Basi hapo
Yesu akawaambia waziwazi, Lazaro amekufa,” Yoh 11:13-14.
Ukweli
ni kwamba hata baada ya Yesu kuiweka habari ile ya Rafiki yake wazi, yaani,
Lazaro kuwa amekufa, Tomaso aitwaye Pacha-mwanafunzi wake Yesu, anabeba habari
ile kwa wepesi mkubwa bila kufikiri na kuzama ndani kwa kile alichokisema Yesu.
Na hivi ndivyo ilivyokuwa: “Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi
wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye,” Yoh 11:16. Hapa Tomaso anaonekana
mtu asiye na hofu wala shaka, ila wakati utathibitisha kile alicho Tomaso. Ni
Tomaso huyu huyu baada ya ufufuko wa Yesu aliyekuwa mtu mwenye mashaka mengi
juu ya ufufuko wa Kristo.
Swali
la kujiuliza ni hili:-ikiwa Yesu alijua fika habari ya kuumwa kwake Lazaro hadi
kupatwa na mauti, kwa nini basi alijichelewesha kufika na kumponya ugonjwa wake
kabla ya kufikwa na mauti hiyo? Ndugu yangu mpendwa, sehemu ya kwanza la swali
hili Yesu mwenyewe kesha ijibu. Na jibu ni hili: -“Ugonjwa huu si wa mauti,
bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu atukuzwe kwa huo,”
Yoh 11:4. Na sehemu ya pili ya jibu la swali hili inathibitisha kile alicho
Kristo Yesu, yaani, ndani na katika Yeye ipo njia, kweli na uzima, Yoh 14:6. Na
ndiyo maana kwa makusudi kabisa Yesu anafika siku ya nne baada ya kifo cha
rafiki yake Lazaro. Siku ya nne ikiwa mwili waanza kuoza hakuna tena uwezekano
wa kurudi katika ‘hali hai’ kadiri ya mila na desturi za kiyahudi. Hivyo “…Yesu
alipofika, alimkuta amekwisha kuwamo kaburini yapata siku nne,” Yoh 11:17
Kuchelewa
kwa Yesu kunaongeza uzuni na majonzi kwa dada zake Lazaro- Martha na Mariamu.
“Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu
hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yo yote utakayomwomba Mungu, Mungu
atakupa,” Yoh 11:21-22, 32. Lakini ukweli ni kwamba alipo Kristo halijaharibika
jambo kwa sababu, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika
cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Yesu anawandolea hofu, mashaka, na uzuni
Martha na Mariamu kwa kuthibitisha kile alicho, kwamba, “Mimi ndimi huo ufufuo,
na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye
na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?” Yoh 11:25-26.
Naye Martha pasipo shaka anamjibu Yesu, “Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba
wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni,” Yoh 11:27. Huzuni
na majonzi haya ya Martha na Mariamu, pamoja na majirani zao, ikiwa ni pamoja
na imani ile waliyokuwa nayo juu ya Kristo Yesu, inaunyong’onyeza moyo wa Yesu
sana. “Yesu akalia machozi,” Yoh 11:35. Tendo hili linathibitisha pasipo shaka
asili wa pili wa Yesu, yaani, ‘ubinadamu wake.’ Hakika Yesu anakupenda wewe na
mimi upeo, Yoh 13:1.
Kwenye
jambo hili la ‘ubinadamu wake Yesu,’ linakuwa kejeri kwa Wayahudi. “Basi
Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda. Bali wengine wao wakasema, Je!
Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?” Yoh
11:36-37. Ndugu yangu, alipo Kristo halijaharibika jambo! “Basi Yesu, hali
akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na
jiwe limewekwa juu yake,” Yoh 11:38. Kwa nini basi Kristo ashindwe ikiwa “Vyote
vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika?”
Yoh 1:3. Ni swala la wakati tu! Hapa tunakumbushwa kuwa na subira kwa kila
jambo hasa pale tunapogubikwa na sintofahamu. Wewe na mimi katika hali hii ya
sintofahamu twapaswa kumwachia Kristo Yesu usukani wa maisha yetu. Majigambo na
kujikweza hakutatupeleka kokote. Kama wakati fulani ulifanikiwa na ukajiona
mafanikio hayo ni kutokana na uwezo wa kiakili zako, utajiri wako, na misimamo
yako kijamii na kisiasa, basi jua kwamba safari bado. Dhababu ili iwe thahabu
kweli lazima iwe imepita katika moto mkali. Na utajua dhahabu hiyo imefika
kiwango cha kuitwa dhahabu pale tu utakapoona sura yako kwenye dhahabu hiyo.
Je, waujua udhaifu wako?
Wapendwa
wana wa Mungu, ni Kristo peke yake awezaye kutuondolea uzuni na majonzi yetu.
Mara “Yesu akasema, Liondoeni jiwe.
Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana
amekuwa maiti siku nne,” Yoh 11:39. Haijalishi ni kwa kiasi gani tumedhoofishwa
na magonjwa yetu, mateso yetu, na sintofahamu zetu. Yesu anakuambia wewe na
mimi kwamba pamoja na hayo yote, ‘ukiamini utaona utukufu wa Mungu, Yoh 11:40.
Na ndivyo ilivyo kuwa kwa familia ya Martha na Mariamu. “Basi wakaliondoa lile
jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa
umenisikia. Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia siku zote; lakini kwa ajili ya
mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe
uliyenituma,” Yoh 11:41-42. Yesu ndiye kimbilio na mteteze wetu mwaminifu. Ni
wewe na mimi kujiaminisha na kujisalimisha kwake.
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa imani Yesu hututoa katika vifungo vya udhaifu wetu. Kristo
kesha ikata minyororo ya kuzimu naye anazo fungu za mauti na za kuzimu, Ufu
1:17-18. Kwa Kristo Yesu uzima upo. Hivyo “Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa
sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje,” Yoh 11:43. Lazaro anarudishiwa uhai wake, na
kwa tendo hilo Mungu anaufunua utukufu, uzuri, na furaha yake kwa wale wote
wenye kumwamini. “Basi wengi katika Wayahudi waliokuja kwa Mariamu, na kuyaona
yale aliyoyafanya, wakamwamini,” Yoh 11:45. Amina!
Hivyo
wapendwa wana wa Mungu, ni vema ukafahamu jambo hili la msingi
kuhusiana na uumbaji wa Mungu na sababu ya kuishi kwetu. Napenda kuyachukua
maneno haya ya Mtume Paulo kwamba, “kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa
uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina,” Rum 11:36.
Jambo la msingi hapa ni kweli kwamba Mungu hakuhitaji kukuumba wewe, bali
alichagua kukuumba kama ulivyo kwa furaha na utukufu wake. Kwa maana hiyo,
maisha yetu hapa duniani yapaswa kuufunua, kuuonyesha Utukufu wa Mungu, na
furaha yake.
Ndugu
zangu katika Kristo, mwanadamu angali akiwa hapa duniani utoa Utukufu wa Mungu
na furaha yake kwa kufanya mambo yafuatayo: Mosi, kwa kumwabudu Mungu, yaani
maisha yako yote, kwa kuwapenda watu wengine bila kumbagua ye yote. Pili, kwa
kuishi na kuwa kama Kristo. Tatu, kwa kutumia vipaji vyako vyote kwa ajili ya
wengine, yaani kufaidiana. Na nne, kwa kueneza habari njema za Mungu kila pande
za dunia. Hata hivyo licha ya ukweli huu, mwanadamu huyu anaweza kuufunua
utukufu wa Mungu na furaha yake kwa kutenda matendo ya roho, Gal 5:22-23, na
siyo yale ya mwili yasiyo na uzima ndani yake, Gal 5:19-21. “Kwa kuwa nia ya
mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na amani,” Rum 8:6. Mtu hawezi kumpenda Mungu kama anafuata matendo
ya mwili wake tu.
Ni kweli kwamba kiini cha
dhambi ni pale mtu anapojipenda yeye zaidi kuliko Mungu. “Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu,” Rum 8:8. Hivyo basi kama tunataka kuishi na kuwa kama
Kristo lazima tufuata sheria ya roho, yaani, matendo ya roho, ambayo ni upendo,
furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo
hakuna sheria, Gal 5:22-23. Uzima huu tuupatao kwa matendo ya roho upo ndani ya
Kristo pale tunapotaka kuishi na kufanana naye. “Kwa sababu sheria ya Roho wa
uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na
mauti,” Rum 8:2. Hivyo kwa kuishi na kufanana
kama Kristo tunaufunua Utukufu wa Mungu na furaha yake ya kutuumba.
Wapendwa wana wa Taifa la
Mungu, kwa upande mwingine, sheria ya dhambi ni matendo yale yasiyo na uzima
ndani yake, na kwayo kamwe hatuwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Matendo haya ni
haya; uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi,
wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda,
ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo. Mtume Paulo anasisitiza kwamba,
“katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu
watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Je,
hutaki kuurithi ufalme wa Mungu na maisha ya umilele?
Kuishi na
kutenda kwetu ili kuwe kwa sifa na utukufu wake Mungu kwa tulazimu kufikiria
mambo ya roho. “Kwa maana wale
waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri
mambo ya roho,” Rum 8:5. Ndugu yangu, utawezaje basi kuishi na kufanana na
Kristo kama muda wote wa ufuata mwili na kufikiri mambo ya mwili? Hii ni
changamoto kwa kila mmoja wetu. Ni kweli kwamba hatuwezi kuyawaza ya roho kama
hatuna mwili. Jambo la msingi na la kufahamu hapa ni kwamba ‘vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena
vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele,’ Rum 11:36. Hivyo hakuna kilicho
chako katika maana ya umiliki halali zaidi ya dhambi zako. Sasa nifanye nini
katika hali hii?
Wapendwa katika Kristo, tunahitaji roho wa Kristo ndani
yetu ili tuyafuate matendo ya roho na mwisho tuwe mali ya Kristo. Roho huyu ni
zawadi kwetu kutoka kwa Mungu, na hufanya kazi ndani yetu kadiri apendavyo yeye
kututumia kadiri ya mpango mzima wa Mungu. Hivyo, “ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani
yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo
katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu,” Rum 8:11. Hapa ndipo
tunapoona Upendo na Huruma ya Mungu kwetu. Mungu hapendi hata mmoja wetu apotee
kwa sababu ya dhambi zake. Mimi na wewe tunapewa kila siku fursa ya kutubu na
kumrudia Mungu. Katika mantiki hii yanipasa kuzitazama dhambi zangu, kuzitubu,
na mwisho kuwa huru kutoka utumwa huu wa dhambi. Ni kwa namna hiyo hiyo sina haki
wala sababu ya msingi kuwanyooshea vidole wengine ilhali mimi mwenyewe nahitaji
upendo na huruma ya Mungu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Wale waufuatao
mwili hawawezi kumpendeza Mungu,” Rum 8:8
Tusali:-Ee
Yesu na Mkombozi wangu, bila Wewe mimi si lolote wala chochote. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario