domingo, 9 de abril de 2017

TAFAKARI: JUMATANO YA WIKI KUU


JUMATANO YA WIKI KUU

Somo: Isa 50:4-9a

Zab: 69:7-9, 20-21, 30, 32-33

Injili: Mt 26:14-25

Nukuu:

“Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia, kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya,” Isa 50:6-7

“Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu?” Mt 26:15a

“Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti,” Mt 26:15b-16

“Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa,” Mt 26:24

TAFAKARI: “Ujasiri na utayari wa Yesu kubeba aibu yetu itokanayo na dhambi; hakika ni laana kubwa kumtenda kwenye haki.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo tutafakari ujasiri na utayari wa Yesu Kristo kubeba aibu yetu itokanayo na dhambi; hakika ni laana kubwa kwa kumtenda kwenye haki.” Kadiri tunavyoijongea ile saa ambayo Bwana wetu Yesu Kristo anayatoa maisha yake kwa faida yangu na yako, ndivyo tunavyouona ujasiri wake, na utayari wake katika kuyakabili mateso na kifo hiki cha msalaba.

Nabii Isaya anatoa wasifu wa mtu kwenye haki ambaye yupo tayari kuufia ulimwengu ili utakaswe na kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Unabii huu unamlenga Yesu Kristo. “Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia, kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya,” Isa 50:6-7. Tendo hili la ujasiri na utayari, msingi wake siyo kujionyesha kwa ulimwengu kwamba anaweza, bali ni tendo linaloonyesha unyenyekevu na kujishusha chini kabisa kusiko kwa kawaida.

Sifa na ukuu, si kielelezo cha kujitoa sadaka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, kwa sababu vyote vilivyopo vimeumbwa kupitia yeye. “Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:2-3. Yaliyopo katika ulimwengu huu kwa yenyewe hayawezi kusadifu majitoleo na sadaka ya kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Tendo hili la unyenyekevu msingi wake ni upendo. Mt. Augustino anasema ‘ukipenda kweli utafanya yote.’ Mungu kupitia mwanaye Mpenzi anatupenda upeo, na kwa maana hiyo yupo tayari kufanya yote.

Pamoja na upendo huu wa Mungu Baba kwetu, inatuwiya vigumu sisi wanadamu kutambua thamani yake, na hivyo tupo tayari kuusaliti na hata kuushusha chini kabisa na kuufanya kama bidhaa isiyo na mwenyewe. Hili linaonekana hasa tunapoona Yuda Iskariote akifanya mnada kwa kumwuza Mkombozi wetu. Yuda Iskariote anataka kujua atakachopata kwa kumsaliti Yesu kwa Wayahudi. Yuda Iskariote anawaauliza, “Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu?” Mt 26:15a. Wapendwa hakuna kitu chochote ambacho tunaweza kubadilisha chenye dhamani ya uhai na utu wa mtu. Hakuna popote hapa duniani ambapo unaweza kununua uhai na utu wa mtu.

Uhai na utu wako na wangu, ni zawadi kwetu, na ni mali ya Mungu. Itakuwaje kuuza uhai utu wa yule atoaye uhai? Yesu Kristo ni Uzima wetu. “Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima milele. Mimi ndimi chakula cha uzima.” Yoh 6:47-48. Uhai wa Yesu unathaminishwa kwa vipande thelathini vya fedha. “Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti,” Mt 26:15b-16.

Uhusiano wa Yesu Kristo na wanafunzi wake haukuwa ule wa mtumwa na mtwana, kiasi kwamba mtumwa angeshawishika kumpindua na hata kumfanyia hila mtwana wake. Yesu Kristo anasema wazi uhusiano wake na upendo wake kwa  wanafunzi wake; “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu,” Yoh 15:13-15. Kwa mantiki hii, Yuda Iskariote hakuwa na sababu yo yote ya kumsaliti Yesu Kristo. Hakuna jambo lolote baya au zuri Yesu Kristo alilolificha kwa wanafunzi wake.

Ndugu yangu, tunapoishi maisha ya kila siku katika kweli na haki aliyotufundisha Kristo, sisi tu rafiki zake Kristo. Tunapoishi maisha ya usaliti ndani na katika Kristo, hatuna mastahili hata kidogo kuwa rafaki yake Kristo. Dhambi hii katika usaliti ndani na katika Kristo ni nzito sana. Majuto yake ni sawa na kutokuwepo katika ulimwengu huu. Yesu anatoa angalizo hili kwako na mwangu pia, kwa kusema, “Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa,” Mt 26:24. Je, leo Kristo asalitiwi?

Ndugu yangu, Kristo mara nyingi amejifananisha kwa maskini, hasa maskini wa roho na anasema hivi, “heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao,” Mt 5:3. Maskini wa roho ni kwa yeyote yule mwenye uhitaji wa Mungu, mwenye nafasi ya Mungu ndani yake, na yeyote yule ambaye mwenye hofu ya Mungu ndani yake na kuyafanya yote ndani na katika Kristo. Maskini hawa tupo nao muda wote hadi mwisho wa nyakati. “Kwa maana maskini mnao sikuzote pamoja nanyi; bali mimi hamnami sikuzote,” Yoh 12:8. Leo maskini hawa ndio wahanga na wadhulumiwa wa haki zao. Ndiyo wanaotumika kama barabara na madaraja ya kuvukia matajiri, wafanya biasha, na wanasiasa. Mwisho wa siku, maskini  hawa hawana mtetezi wala mahali pa kutolea kilio chao hasa kwenye utawala ulio kithiri kwa rushwa na udhalimu kama Tanzania yetu leo.

Yesu Kristo katika Taifa letu hili kupitia maskini hawa, anateseka sana na tunamsulubisha sana. Hata wale ambao tuliowategemea kuwa sauti ya wasio na sauti-maskini, wamekuwa mstari wa mbele kuwahujumu maskini ili kulinda nafasi zao na familia zao. Kundi hili la uovu lielewe vizuri maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo kwamba ‘ingekuwa heri kwao kama wasingezaliwa.’ Kama wapo hai na wanafanya vitendo hivi vya  ukandamizani wajue fika hukumu ya Mungu haikwepeki hata kidogo.

Hawa ndiyo wale wanasiasa ambao wanamwuza Yesu kwa vipande thalamini vya pesa na kuusaliti umma wa walio wengi. Dhambi hii ndugu yangu, hata ukiama chama kimoja cha siasa na kuamia kingine kwa usaliti wako kamwe hutopata amani ndani mwako. Mwisho wa siku ni kuchukua maamuzi ya Yuda Iskariote ya kujinyonga. Hawa ndio wale ambao wanafupisha maisha ya mabinti wadogo kwa kuwauza kwa “sahani ya chips, nusu kuku, na soda ya Pepsi.” Hakika afadhali wasingelizaliwa! Laana hii haitawaacha. Hawa ni wale ambao kwa kudanganywa na ulafi wao wa madaraka na mali wapo tayari kuwauwa walemavu wa ngozi “Albinos” kufikia haja zao. Hakika afadhali wasingelizaliwa! Hawa ndio wale ambao wapo mstari wa mbele wa kuwateka wenye haki na kuwatesa kwa sababu tu hawataki kusikia kweli na wala kufichuliwa uovu wao. Hawa bado wanaendeleza soko la kumnadi na kumuuza Yesu Kristo.

Ndugu yangu, yawezekana umezoea kuzinyonga haki za wanyonge kwa njia mbalimbali, elewa leo usomapo tafakari hii, ni mwaliko wa kuacha kumtesa na kumdhalilisha Kristo. Tenda haki hata pale pasipo na msukumo wa kufanya hivyo. Kwa kufanya hivyo utakuwa mtetezi wake Yesu Kristo, naye atakutetea mbele za Baba yake aliye mbinguni. “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 10:32. Kuwatetea wanyonge na kuwatendea haki, ni kumkiri Mungu mbele za watu. Je, ni mara ngapi nimeshindwa kufanya hivyo kutokana na wito wangu, nafasi yangu, cheo changu, na uwezo wangu?

Tumsifu Yesu Kristo!

“Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa,” Mt 26:24

Tusali:-Ee Yesu, niongoze katika njia ya haki na kweli. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario