JUMATATU WIKI YA 2 YA PASAKA
Somo: Mdo 4:23-31
Zab: 2:1-3, 4-6, 7-9
Injili: Yoh 3:1-8
Nukuu:
“Wafalme
wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya
Kristo wake,” Mdo 4:26
“Basi
sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako
kwa ujasiri wote,” Mdo 4:29
“ukinyosha
mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako
mtakatifu Yesu,” Mdo 4:30
“Hata
walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote
wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri,” Mdo 4:31
“Yesu
akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi
kuuona ufalme wa Mungu,” Yoh 3:3
“Mtu asipozaliwa mara
ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu,” Yoh 3:5
“Kilichozaliwa
kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho,” Yoh 3:6
TAFAKARI: “Kuishi na kuongozwa na
Roho Mtakatifu ni kuzaliwa mara ya pili na huku ni kuuona ufalme wa Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu, tukiwa
bado tunaitafakari jumuiya ya kwanza ya Wakristo, pamoja na umoja na upendo wao
wa kindugu, jumuiya hii iliongozwa kwa Nguvu za Roho Mtakatatifu. Umoja wao na
upendo wao, ni tunda la Roho Mtakatifu. Kwa kupitia Roho Mtakatifu, waliweza
kufanya mambo makubwa sana dhidi ya ukweli waliousimamia na kuushuhudia. Kwa
nguvu ya Roho Mtakatifu, mateso yao na manyanyaso yao walijeuka kuwa tunu na
msingi wa Imani. Roho Mtakatifu aliwaongoza vyema na kuwawezesha kuyapokea
mateso kama sehemu ya kujipatia utakatifu.
Kilio cha Jumuiya ya
kwanza ya Wakristo kwa kadiri ya mateso yao, walikielekeza kwa Mungu aliye yote
katika yote. Na hapa tunapata umoja wao huo katika kuishi, kunena, na kutenda
kwao. Wanajua sababu ya chanzo cha mateso yao na mahangaiko yao kimetokana na
nini. Sababu ya mateso na manyanyaso yao kimetokana na kuishi kweli katika
Kristo. “Wafalme wa dunia
wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo
wake,” Mdo 4:26. Ndugu yangu, hatutaweza kushinda vita vya kiroho kama hatujui
tunapigana na nini, na kimbilio letu ni nina. Leo kuna mashambulio mengi ya
kiroho. Yapo mashambulio yanayotoka nje na ndani ya nafsi yetu. Mashambulio
yatokayo nje ya nafsi yetu ni moja ya mikataba tunayoweka kwa kujua au kwa
kutokujua. Mikatamba hii ambayo mwisho wake ni mateso bila Kristo, ni pamoja na
ibada na mitambiko ya mizimu.
Wapo
Wakristo wengi na tena wale wa jumapili ambao kwayo ibada hizi ndizo vielelezo
vya maisha na Imani yao. Ukristo kwao ni kama chuma kilichopakwa dhahabu kwa
nje tu. Ukikikwangua kidogo chuma hiki unakutana na uhalisia wa chuma chenyewe.
Kwa maana nyingine ni kwamba ukristo wao ni wa juu juu tu ya ngozi. Kabla ya
kuikuta damu, unakutana na upagani uliokithiri. Wakristo wa mtindo huu
waliobatizwa na kumpoteza Roho Mtakatifu, kamwe hawataweza kuyasema maneno haya
waliyoyasema jumuiya ya kwanza ya wakristo mbele ya watesi wao. “Basi sasa,
Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa
ujasiri wote,” Mdo 4:29.
Mkristo
wa mtindo wa Ibada za kuzimu na mvaa mahirizi, hataweza kunena, kushinda uovu
kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, wala kuwa na uwezo wa kufanya ishara na maajabu
kwa mkono wa Yesu. Mambo haya yawezekana tu kwa wale waliozaliwa mara ya pili,
yaani wa Roho Mtakakatifu. Hawa ndiyo wenye mamlaka ya kunyoosha “mikono yao
kuponya; ishara na maajabu na hufanyika kwa jina la Mtumishi wao Mtakatifu
Yesu,” Mdo 4:30.
Waliozaliwa
mara ya pili ni watu wale ambao mara baada ya sala na maombi hunena kwa ujasiri
bila woga, na mahali hapo hutikiswa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Roho
anapofanya kazi yake, mahali hapo hutakaswa. Huku ndiko maana halisi kwa
kutikiswa. Jambo hili linatokea kwa jumuiya ya kwanza ya Wakristo. “Hata
walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote
wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri,” Mdo 4:31. Roho
huyu katika kufanya kazi yake mara baada ya kumpokea huleta umoja na upendo
katika jamii husika.
Jambo
la kusikitisha leo kumetokea mifumuko ya nyumba za sala zenye mwelekeo wa
ubinafsishaji wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu hatuwezi kumzuia kwa ukuta.
Roho Mtakatifu hufanya kazi yake kadiri apendavyo na kwa yeyote ampendaye.
Ninayaita “makanisa” haya nyumba za sala kwa sababu utambulika kwa majina
binafsi ya wachungaji wao, mfano; Kanisa la Edgar, Kanisa la nabii Ngowi,
Kanisa la Mzee wa Mpako Kagesa, nk. Kanisa ni la Kristo, na Roho huyu ufanya
kazi katika Kristo na ndani ya Kristo.
Somo
letu la Injili, Bwana Yesu Kristo anakazia sana kuzaliwa kwa mara ya pili. Naye
anamjibu Nikodemo, na anasema, “Amin, amin, nakuambia, Mtu
asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu,” Yoh 3:3. Ndugu yangu,
kumbe kuuona ufalme wa Mungu ni kuzaliwa mara ya pili. Nikodemo ambaye alikuwa
Mfarisayo aliyebobea, alikuwa mfuasi wa Kristo wa usiku, yaani wa siri. Kristo
anapomshauri azaliwe mara ya pili anamtaka kuvunja mikataba yake ya siri, na
hasa mashambulio ya ndani ya nafsi. Kuzaliwa huku mara ya pili ni kujiachia
kabisa bila kujibakiza nafsi yako kwa chochote nje ya Mungu Baba, Kristo na
Roho Mtakatifu. Ni kumruhusu Roho Mtakatifu awe mtawala wa hekalu lako yaani
mwili wako.
Ndugu yangu kukubali
mikataba hii ya ndani na nje ya nafsi, ni kubaki tu ndani ya mwili na kwa ajili
ya mwili, ambao hushambuliwa sana kwa sababu uhasilia wake, yaani, mwili ni
kuchoka na kuzeeka. Naye Yesu anasema, “Kilichozaliwa
kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho,” Yoh 3:6. Umilele wetu
upo kwenye Roho ya kweli ya Mungu kwa sababu yeye ni Roho halisi. Roho huyu
ndiye atupaye uwezo wa kulitamka jina la Yesu lenye mamlaka. Mtume Paulo
anasema, “kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa
Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana,
isipokuwa katika Roho Mtakatifu,” 1Kor 12:3.
Wapendwa
ni vizuri ukafahamu ukweli wa jambo hili. Mtu kamili anakuwa katika sehemu kuu tatu:-NAFSI, ROHO, na
MWILI. “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi Nafsi zenu na Roho
zenu na Miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja
kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” I The 5:23. Katika mwono huo, Roho na Nafsi huwa
pamoja na ndizo wewe mwenyewe. Mwili ni nyumba ya Roho na Nafsi. Katika uumbaji
Mungu aliumba mwili kwa udongo halafu akapulizia pumzi puani ambayo ni roho
yake ndipo mtu huyo akawa nafsi iliyo hai. “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa
mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwa.
2:7. Miili tuliyonayo ni nyumba ya NAFSI na ROHO. Kwa hali hii sisi binadamu ni
wawili. Kuna mtu wa ndani na mtu wa nje. Mtu wa ndani ni Nafsi na Roho, na mtu
wa nje ni Mwili lakini watu hawa wapo pamoja hatuwezi kuwatenganisha wala
kumwona kwa macho ya nyama huyu mtu wa ndani, ila yupo.
Kwa
maana hiyo, kwenye Nafsi
ndipo penye magonjwa yenyewe kwani ni katikati ya Roho na Mwili. Je, maumivu ya
ndani hutoka wapi? Tuone haya yafuatayo:-Kudumu katika madhara ya dhambi na
kuendelea kuhifadhi moyoni, Matukio mabaya yanayokusononesha, Kutosamehe kwa
muda mrefu. Vile vile hupata maumivu kutoka ROHONI:- Dhambi na Laana. Maumivu
kutoka MWILINI:-Mazingira, Tabia za watu wanaokuzunguka, Mateso na matukio ya
kuhuzunisha. Tuelewe kwamba NAFSI hutawaliwa na Hisia, mfano:-Hofu, Chuki, Hasira, Kujihukumu, Kujikataa, Kukosa
furaha, Kukosa
upendo, Kukosa
amani, n.k
Wapendwa
katika hali hii tufanye nini? Ni
muhimu sana mtu atawale hisia zake. Nafsi ambayo ipo katikati ya Mwili na Roho,
ikiegemea rohoni huleta matunda mzuri. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha,
amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama
hayo hakuna sheria.” Gal. 5:22-23. Ila nafsi inapoingia katika Mwili
mambo huwa mabaya kwani ufanya matendo ya mwili kama tusomavyo katika maandiko
matakatifu, “basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu,
ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka,
uzushi husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo
nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo
ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Gal.5:19-21. Ni
vizuri kujua nafsi yako imeegemea wapi. Ikiegemea rohoni utaenda Mbinguni,
ikiegemea mwilini hutaiona mbingu. Ni kwa ukweli huu ambao Yesu leo anaoungelea
kwa Nikodemo na kusema, “Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi
kuuona ufalme wa Mungu,” Yoh 3:5
Roho huyu Mtakatifu
ndiye atupaye muhuri wa ukombozi. “Wala msimhunishe yule Roho Mtakatifu wa
Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi,” Efe 4:30. Roho
Mtakatifu ndiye hutupa mastahili mbele ya Mungu na si kwa matendo ya haki,
au, ujanja na werevu wetu hapa duniani.
“Si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa
kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu,” Tit 3:5. Je,
ndugu yangu umefanya mkataba na nani katika maisha yako? Je, nafsi yako
imeegemea wapi?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mtu asipozaliwa mara ya pili,
hawezi kuuona ufalme wa Mungu,” Yoh 3:5
Tusali:-Ee
Yesu Kristo, tuwezeshe sisi kama viungo na Kanisa lako Takatifu kuzaliwa mara
ya pili kila siku ya maisha yetu tunapo mruhusu Roho wako afanye kazi ndani
yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario