JUMANNE YA OKTAVA YA PASAKA
Somo:
Mdo 2:36-41
Zab:
33:4-5, 18-19, 20, 22
Njili:
Yoh 20:11-18
Nukuu:
“Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa
jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha
Roho Mtakatifu,” Mdo 2:38.
“Kwa
kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio
mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie,” Mdo 2: 39.
“Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya,
akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi,” Mdo 2:40.
“Yesu
akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania ya kuwa
ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie
ulipomweka, nami nitamwondoa,” Yoh 20:15.
“Yesu akamwambia,
Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani, Mwalimu),”
Yoh 20:16.
“Yesu akamwambia.
Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu
ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu
naye ni Mungu wenu,” Yoh 20:17.
TAFAKARI:
“Kwa Ufufuko wa Yesu Kristo sote twahesabiwa haki kwa kufanya toba ya kweli;
Naam, sote kwa upendo wa Mungu twaitwa wana wake na yeye ni Mungu wetu.”
Wapendwa wana Mungu,
tendo la ufufufuko wa Bwana Wetu Yesut Kristo, linatuwezesha na linakuwa neema
na baraka kwetu, hasa ule uwezo wa kupokea vipawa vya Roho Mtakatifu pale tu
tunapofanya toba ya kweli. Ni kwa dhambi zetu imekua sababu ya kifo cha Bwana
wetu Yesu Kristo, na ni kwa kupitia toba ya kweli kwa dhambi zetu twapokea
neema na baraka, na kuhesabiwa tena haki kuwa warithi na wana wa Mungu. Ni kwa
sababu hii, leo kwa namna ya pekee tutafakari juu ya neno hili, “Kwa Ufufuko wa
Yesu Kristo sote twahesabiwa haki kwa kufanya toba ya kweli; Naam, sote kwa
upendo wa Mungu twaitwa wana wake na yeye ni Mungu wetu.”
Mtume Petro, kwa
kujaliwa ujasiri na nguvu ya Kristo Mfufuka, haoni haya kuwaambia Wayahudi
ukweli kuhusu wokovu wao baada ya kufanya kosa la kumwua mwenye haki-Yesu
Kristo. Hata sasa Mtume Petro ananiambia mimi na wewe ambao twahitaji huruma na
neema ya Mungu. “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu
Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho
Mtakatifu,” Mdo 2:38.
Ndugu
yangu, ni kwa jina la Yesu Kristo tu twaweza kupata msamaha wa dhambi, na
kupatanishwa tena na Mungu Baba. Na ni kwa njia ya ubatizo tunafia dhambi na
kuzaliwa wapya kama ishara halisi ya Ufufuko wa Yesu Kristo. “Naye alituokoa
katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa
pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni
mfano wa Mungu alisiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote,” Kol 1:13-15.
Ili tufaidi neema za Ufufuko wa Bwana Yesu Kristo, ikiwa ni pamoja na vipawa
vya Roho Mtakatifu, yatupasa kufanya toba ya kweli, ikiambatana na kuzaliwa upya
kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Toba
ya kweli ni kutambua kule kujikwaa kwetu, na kuyaacha maanguko hayo, huku
tukifuata njia iliyo sahihi. Yesu Kristo pasipo shaka yeyote, ndiye njia sahihi
ya kufuata, kwani kwa Ufufuko wake, yaliyo ya kale, na yasasa, na yajayo
yamekwisha eleweka. Tuendako sasa twakujua. “Yesu akamwambia.
Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu
ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu
naye ni Mungu wenu,” Yoh 20:17. Ili tupate
mastahili ya kumshika Kristo Mfufuka, yatupasa kufanya toba ya kweli kama
nilivyokwisha kusema. Yesu anamwambia Mariamu na kumbumbusha toba ya kweli. Huu
ni wito wa kujitakasa kwa yale mambo yanayotukwamisha kuiona sura ya Mungu.
Mastahili yetu baada ya kuhesabiwa haki kwa kufanya toba ya kweli, ni maisha ya
utakatifu.
Maisha mapya baada ya Ufufuko, ni maisha
ya Utakatifu kwa wote wanaoridhia njia ya Kristo. Kuridhia njia hii ni kufanya
toba ya kweli. Tendo hili la toba ya kweli ndani na katika Kristo, linatupa
mastahili sawa bila kujali historia zetu mbaya, makabila yetu, na hata utaifa
wetu. Tendo hili linatupa uhalali wa kuwa wana wa Mungu. “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu,
na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu
wamjie,” Mdo 2: 39. Tendo hili ni
upendeleo mkubwa sana kwetu, na upendo wa Mungu wa ajabu. Je, watambua jambo
hilo? Je, wayajua mapungufu yako? Na je! waona umuhimu wa kupatanishwa na Mungu
Baba kupitia ushindi wa Mwanae dhidi ya uovu na dhambi?
Njia
na namna yetu ya kuishi baada ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo inatusukuma
kuishi upya katika kutenda na kunena. Ni maisha ya ushuhuda wa kweli. Kwa maana
hii, Mtume Petro anasema, “Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi,” Mdo 2:40. Leo
tunaisha katika kizazi chenye ukaidi uliokithiri. Leo walio wengi siyo kwamba
tu hawaamini, ila pia hawaoni umaana wa maisha yenye uhusiano na Mungu. Wengi
wamefikia hatua ya kuona historia nzima ya wokovu wetu kama hadithi za
kufikirika tu. Tupo kwenye wakati wa “ponda mali kifo chaja.” Kwa mtu yeyote na
hasa kiongozi akikosa hofu ya Mungu ndani yake, maisha na utu wa binadamu hauna
tofauti na bidhaa rahisi na isiyodumu kuwahi kutokea. Leo tunashuhudia mauaji
ya wazi na kikatili kuwahi kutokea.
Jambo
muhumu la kujiuliza katika maisha yako, “unatafuta nini, na kwa sababu gani?”
Mariamu anamtafuta Yesu Kristo kaburini akiwa analia, ili hali Yesu Kristo
keshafufuka. “Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta
nani? Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa
umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa,” Yoh 20:15. Mariamu bado yupo kwenye fikra za
umauti wa Yesu.
Ndugu yangu, Mariamu mara baada ya
kumtambua Kristo, anaanza maisha mapya. Yesu anakuwa mwalimu wa maisha mapya.
Mariamu analisema jambo hili toka ndani ya moyo wake. Na hali ilikuwa hivi: “Yesu
akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (Yaani,
Mwalimu),” Yoh 20:16. Mwalimu ndiye ajuaye yale tunayotaka kujifunza. Mwalimu
ndiye ajuaye siri ya kile tunachotaka kukijua. Mwalimu hutuongoza, kutuelekeza,
na kutuonyesha kuona kile anachokiona yeye ambacho ndiyo kusudi la yale
tunayojifunza.
Ndugu yangu, hatuwezi
kuona na kujua siri ya maisha ya umilele, bila kuwa na Mwalimu wetu Yesu
Kristo. Tutaona yale ayaonayo Kristo endapo tu tanamwamini. Yesu anasema, “mimi
ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye
hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35. Kupata neema na baraka yatupasa kumwamini Kristo.
Naye anasema, “aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji
hai itatoka ndani yake,” Yoh 7:38. Kuishi maisha ya ufufuo na uzima yatupasa
kumwamini Kristo. Naye anatupa hakikisho hilo kwa kusema, “mimi ndimi huo
ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi,” Yoh 11:25.
Kumwamini Yesu Kristo
ni kumwamini Mungu Baba aliyempeleka na kumwamuru kuyafanya yote. “Naye Yesu
akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye
aliyenipeleka,” Yoh 12:44. Tunapomwamini Kristo, tunafunuliwa makusudi yake
hapa duniani na kufanywa kila mara kuishi katika nuru yake. “Mimi nimekuja ili
niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46.
Na mwisho tunaweza
kujua na kuzifanya kazi alizozifanya Kristo endapo tunamwamini. “Amin, amin,
nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya;
naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12.
Ndugu yangu, Yesu ni nani kwako? Je, unayo imani thabiti kwa hayo unayoishi
ndani na katika Kristo?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Petro
akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate
ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu,” Mdo 2:38
Tusali:-Ee
Yesu, tuwezeshe kufanya toba ya kweli. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario