JUMAPILI YA PASAKA
MISA
YA MCHANA
Somo I: Mdo 10:34;
37-43
Zab: 118:1-2, 16-17, 22-23
Somo II: Kol 3:1-4
SEKWENSIA
Injili: Yoh 20:1-9
Nukuu:
“Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu
hana upendeleo,” Mdo 10:34
“Nasi
tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika
Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini,” Mdo 10:39
“Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu
ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu. Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa
jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi,” Mdo 10:42-43
“Basi
mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi
mkono wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1
“Basi Petro akatoka, na
yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini,” Yoh 20:3
“Akainama na
kuchungulia, akaona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia,” Yoh 20:5
“Basi akaja na Simoni
Petro, akaingia ndani ya kaburi,” Yoh 20:6
“Basi ndipo alipoingia
naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na
kuamini,” Yoh 20:8
TAFAKARI:
“Tuyatafute yaliyo juu Kristo aliko; Yote yatafunuliwa katika Maisha yetu
kuelekea alikoketi mkono wa kuume wa Mungu,”
Wapendwa wana wa Mungu,
jumapili hii ya Pasaka yaani tukio hili la kufufuka kwake Bwana wetu Yesu
Kristo, ndiyo uliokuwa mwanzo wa Wakristo, yaani wafuasi wake Yesu Kristo,
kuanza kuadhimisha Matendo Makuu ya Mungu, ambayo kwa leo hii inajulikana kama
Misa Takatifu. Kanisa kama lilivyo leo kupitia historia nzima ya wokovu wetu,
na hasa jumuiya ya kwanza ya Wakristo, iliweka msisitizo wa kufanya mkukanyiko
wao siku ya kwanza ya Juma, yaani Jumapili ya tokeo ya Ufufuko wa Kristo,
tofauti na siku ya Jumamosi-kupumzika kwake Mungu katika swala la uumbaji
kadiri ya masimulizi ya kikasisi “Priestly Traditional.” Masimulizi haya ndiyo
yalikuwa kielelezo cha Wayahudi cha kufanya siku ya Jumamosi kuwa pekee na
kutojishughulisha na maswala ya kazi, bali kumsifu Mungu na kumwabudu. Ufufuko
wa Kristo unaanzisha mpango mpya na wenye kuitimiliza torati (sheria) kwa kumwabudu
Mungu na kumsifu. Hili ndilo tendo Kubwa la kipasaka. Na haya ndiyo makusudi na
fundisho la Yesu Kristo juu ya sheria yaani torati. “Msidhani ya kuwa nalikuja
kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17
Kwa maana hiyo, leo
basi kwa namna ya pekee, tuyatafakari maneno haya, “Tuyatafute yaliyo juu
Kristo aliko; Yote yatafunuliwa katika Maisha yetu kuelekea alikoketi mkono wa
kuume wa Mungu.” Tendo la Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo linatusukuma toka
ndani ya mioyo yetu na imani yetu kuyatafuta yaliyo juu kule Kristo aliko. Kwa
Mkristo yeyote hapa duniani asipolifanya jambo hili kuwa kielelezo cha maisha
yake, basi ajue kwake Ufufuko hauna maana ye yote. Mtume Paulo anasema hivi
kuhusu ufufuko, “tena kama Kristo hakufufuka, basi, kuhubiri kwetu ni bure na
imani yenu ni bure,” 1Kor 15:14. Ufufuko wa Kristo ndiyo kiini cha Imani yetu.
Ndugu yangu,
tunapotambua jambo hili ni rahisi kuona upendo na mapendeleo ya Mungu kwetu
katika maisha ya kila siku. Mtume Petro analiona hilo kwa wale anaowahudumia
ambao hapo mwanzoni hawakuwa katika Taifa lile Teule, yaani Israeli. Mpango
mpya wa Mungu kwa watu wote wenye kumcha ulianza pale siku ya ijumaa kuu
lilipopasuka Pazia. “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho
yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini;
nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi
ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka
kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi,” Mt 27:50-53. Kupasuka huku
kwa pazia la hekalu ni mwanzo mpya wa kumwabudu Mungu kuliko kuzuri na
ukamilifu zaidi. Kuabudu huku kumetoa matabaka yote, na kushirikisha kila
mwenye hofu ya Mungu kuupata utakatifu ambao sasa ndiyo cheo chetu. Haya Yesu
aliyasema hata kabla ya kupasuka kwa hekalu. “Lakini saa inakuja, nayo sasa
ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana
Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni roho, nao wamwabuduo yeye
imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” Yoh 4:23-24.
Ndugu yangu, saa
yenyewe ndiyo sasa baada ya kutukuzwa Mwana wa Adamu, nikimaanisha baada ya
kuyashinda mateso, na umauti. Kristo sasa yupo kwenye Utukufu wake. Hili ndilo
lengo kuu la kuyatafuta yale yaliyo juu kule ambako Kristo yupo yaani kwenye
Utukufu na Utakatifu. Ni katika msingi huu, Petro haoni haya kusema mambo haya,
“Nasi tu mashahidi wa mambo yote
aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua
wakamtundika mtini,” Mdo 10:39. Ndugu yangu, Petro alikuwa na elimu ya kawaida
sana. Alikuwa mvuvi wa kawaida, ila mzoefu kutokana na Umri wake. Ila alikuwa
shujaa na mwenye elimu kubwa kutokana na ufunuo wa Imani yake iliyotokana na
upya wa maisha ya ufufuko. Katika jambo hili anaona wazi maagizo ya Kristo
ndani ya imani hii ya kweli na kusema, “Akatuagiza tuwahubiri watu na
kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na
wafu. Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye
atapata ondoleo la dhambi,” Mdo 10:42-43.
Ndugu yangu, hii ndiyo imani ya kweli kwa Mkristo ye yote
baada ya ufufuko. “Basi mkiwa mmefufuliwa
pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa
Mungu,” Kol 3:1. Mara nyingi tumependa kuchukulia mambo kwa mazoea. Bila shaka
kwa umri uliokuwanao umekwisha sheherekea Pasaka nyingi. Kwa mantiki hii,
yawezekana pia nyakati zote hizo hukuwahi kufufuka na Kristo. Ndugu yangu
tafakari kwa makini ufufuko wa Kristo ndani ya maisha yako. Lifanye jambo hili
kuwa la pekee katika maisha yako sasa, na achana na mambo ya kale umvae Kristo.
Mtakatifu Augustino alikuwa ndani ya Kristo na Katika Kristo, baada ya kufahamu
jambo hili pale alipofungua Biblia Takatifu baada ya kusikia sauti ikisema,
‘chukua usome,’ “Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa
ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni
Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake,” Rum
13:13-14. Hii ndiyo “METANOIA” yaani kugeuka na kuanza upya ndani na katika
Kristo.
Ndugu
yangu, pamoja na Injili kuelezea tukio la ufufuko wa Bwana Yetu Yesu Kristu,
imekazia mambo makuu mawili. Kwanza, nafasi ya Kanisa, na pili, nafasi ya Mtume
Petro. Kwa namna ya pekee naomba tuyatafakari mambo haya. Tuelewe kwamba Yesu
Kristo alikwisha weka mfumo fulani wa uongozi kabla ya mateso, kifo na ufufuko
wake. Ni katika mfumo huyo wafuasi wake wapaswa kuufuata. “Nami nakuambia, Wewe
ndiwe Petro, na juu ya mwamba wako huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango
ya kuzimu haitalishinda,” Mt 16:18. Jambo hili na nafasi hii ya Petro
inajitokeza na kujionyesha wazi wakati wa Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. “Basi
akaja na Simoni Petro, akaingia ndani ya kaburi,” Yoh 20:6. Licha ya kwamba
Mtume Yohani ambaye Yesu alimpenda sana kuliko Mitume wote, ikiwa ni moja ya
sifa yake na uhusiano wake na Yesu Kristo, pia alikuwa ni kijani kuliko wote;
hakuwa wa kwanza kuingia katika kaburi licha ya kwamba alikimbia kuliko Mtume
Petro na kufika wa kwanza Kaburini baada ya kupata taarifa ya Kristo Mfufuka.
Yohane Mtume anatambua nafasi ya Petro kama kiongozi halali aliyepewa mamlaka
na Kristo mwenyewe. Hapa ndipo tunapoona nafasi ya Baba Mtakatifu kama HALIFA
wa Kristo. Huyu ndiye Petro, yaani mwamba ambapo Kanisa lake limeoteshwa na
kukua.
Kwa sababu hiyo, Mtume Petro
anakuwa wa kwanza kuingia Kaburini. Na baada ya Petro, Mtume Yohane anaingia na
kuona na kuamini. “Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine
aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini,” Yoh 20:8. Kuona na
kuamini kwa Mtume Yohane, kunachukuliwa kwa namna mbili. Moja, Mtume Yohane
mwenyewe kwa upendo aliokuwa nao Kristo juu yake, na upendo wa Mtume Yohane juu
ya Kristo. Pili, Yohane Mtume katika jambo hili la kuona na kuamini, anasimama
badala ya Mama Kanisa kama mshuhudia na mshuhuda wa kweli wa ufufuko wake Yesu
Kristo. Kanisa tuishilo leo na sasa linaishi katika ushuhuda huu wa Ufufuko.
Kanisa halipo kama hakuna Imani hii ya Ufufuko. Je, jambo hili linasema nini
kuhusu vipaumbele vyako katika Imani?
Ndugu yangu, yale
ambayo yanachukua muda wako mwingi katika maisha yako, ndiyo hayo yanayoakisi
maisha yako baada ya kifo. Yawezekana hadi sasa huna mpangilio wa maisha yako.
Mambo ya muhimu kufanya katika maisha yako mapya ya ufufuko ni haya:
Moja, Mshukuru Mungu
kwa kukutumia vyema, endapo unaishi vyema utume wako kadiri ya wito wako.
Katika jambo hili utafunuliwa siri ya umilele.
Pili, kila mmoja wetu
yampasa kufanya mkataba na Kristo kama ishara ya kuanza maisha mapya ya
ufufuko. Mkataba wako ulenge kufanya jambo jema kwa ajili ya Kristo kila siku.
Hapa haitegemei ukubwa wa jambo au udogo wake.
Tatu, lifanye jambo
hilo kuwa kiu yako kila siku na usichoke kulifanya. Nakuhakikishia utaanza
kuona mabadiliko makubwa katika maisha yako yakiambatana na Neema na Baraka za
ajabu.
Nne, Sala kuu yako iwe
kushukuru hata kwa yale ambayo bado kuyapata. Hapa ni kumwachia Kristo usukani
wa maisha yako. Yesu Kristo ndiye dereva maarufu kuliko wote waliokwisha
kutokea. Yeye ndiye “Njia, na Ukweli, na Uzima,” Yoh 14:6
Na mwisho, omba kifo
Chema kila siku na hasa mara uamkapo. Sala hii iambatane na Neema ya kutoa
msamaha bila kujibakiza.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi mkiwa
mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu Kristo aliko, ameketi mkono
wa kuume wa Mungu,” Kol 3:1
Tusali:-Ee
Yesu, nijalie neema ya kutafuta yale yakuelekeayo katika maisha yangu kila
siku. Amina.
No hay comentarios:
Publicar un comentario