sábado, 29 de abril de 2017

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 3 YA PASAKA


ALHAMISI WIKI YA 3 YA PASAKA

Somo: Mdo 8:26-40

Zab: 66:8-9, 16-17, 20

Injili: Yoh 6:44-52

Nukuu:

“Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?,” Mdo 8:36b

Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu,” Mdo 8:37 

Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi,” Mdo 8:39

Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44

Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu,” Yoh 6:51

TAFAKARI: “Kwa nini nashindwa kukata shauri kuhusu maisha yangu?”

Wapendwa wana wa Mungu, kuna msemo wa kiswahili usemao, ‘kuvuja kwa pakacha nafuu kwa mchukuzi.’ Msemo huu unaendana na somo letu la leo, na kile kilichotokea Jerusalemu baada ya kifo cha Shahidi Stefano. Jumuiya ya kwanza ilitawanjika sehemu mbalimbali, huku ikimbeba Kristo kwa kila walichokuwa wakikifanya. Hivyo tunaona Mtume Filipo akihubiri na mara hii akikutana na Towashi mmoja aliyekuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu. Bila shaka kwa namna alivyokuwa Towashi huyu alikuwa tayari ameandaliwa na Mungu mwenyewe kwa tukio ambalo Filipo atalifanya, kama Yesu anavyosema kwenye Injili ya leo, “Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44. Ukweli ni kwamba, Filipo anamkuta Towashi huyu akisoma chuo cha Nabii Isaya.

Baada ya mazungumzano na kuhubiriwa kuhusu Kristo, Towashi anafikia hatua ya kukata shauri na kuachana na maisha ya zamani na kuanza maisha mapya, na kusema, “Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?,” Mdo 8:36b. Mpendwa tunayesafiri wote katika tafakari hii, hakuna mtihani mgumu kwa binadamu kama “kufanya maamuzi” na hasa maamuzi ya maisha mapya na yenye mtazamo mpya. Wengi wetu mtihani huu umetushinda na tumebakia kudhani kwamba maisha yetu yamelaaniwa. Kukata shauri ni hatua ya kwanza ya kukua katika maisha ya kawaida na hasa ya kiroho.

Kukata shauri huku kunanikumbusha rafiki yangu mmoja aliyekuwa mtaratibu sana na mwenye kuipenda familia yake. Ila mambo hubadilika mara anapokunywa pombe. Jambo hili lilikuwa kero sana kwa mke wake, na kila lilipotokea basi nilikuwa msuluhishi. Mara zote jamaa huyu alikiri kuwa alifanya makosa na hivyo kuamua kuacha kunywa pombe.

Baada ya muda kama miezi miwili mitatu hivi, jambo hili lilijirudia tena. Na mara hii nilimwuliza; Rafiki, tatizo lipo wapi mbona unarudia kulekule ulipoamua kutokurudi? “Father, tatizo lipo hapo, ‘naomba unisaidie. Ingewezekana kuyatoa mabango yote huko barabarani yenye tangazo ya “KILI TIME,” ingenisaidia kuacha pombe. Ninapoliona tangazo hili, ujue bar ifuatayo lazima niingia na kusaka kinywaji hicho kwa uvumbi na uvumba,” Rafiki yangu alinijibu kwa upole wa hali ya juu.

Wapendwa wana wa Mungu, mtakubaliana na mimi kwamba mabango yalioko huko barabarani hayana tatizo. Tatizo kubwa lipo pale tunaposhindwa kufanya maamuzi ya kina na kuanza maisha mapya kama kweli tunataka mabadiliko. Towashi baada ya kuyaona maji aliamua kubatizwa. Filipo anamwambia, “ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu,” Mdo 8:37.

Ndugu yangu kwa nini unashindwa kukata shauri na kuanza maisha mapya kwa kuamini utaweza ndani na katika Kristo Yesu? Yapo mambo mengi ya kujikatalia ili ukue mwili na roho. Hapa hakuna jambo kubwa wala dogo kama kwa kiasi fulani linakwamisha kukua kwako kimwili na kiroho. Yawezekana, unaishi uchumba sugu, na hivyo kutoshiriki masakramenti. Uchumba siyo ndoa! Kata shauri na anza maisha mapya. Siku hizi ukipenda na kuamua kufunga ndoa unaweza hasa zile misa za alfajiri na baada ya tukio hilo ukaendelea na shughuli zako za kila siku. Achana na ndoa za matarumbeta na mbwembwe zisizo na maana. Ndoa nyingi zenye mbwembwe huishia mtindo huo huo wa mbwembwe.

Baada ya kazi hii muhimu aliyoifanya Filipo, Roho wa Bwana anamnyanyua na kumpeleka mahali pengine kwa kazi yake. “Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi,” Mdo 8:39. Nasi tunaotoa huduma za kiroho katika vituo tulivyopangiwa tunakumbushwa hapa kwamba, tukishafanya yale tuliyotakiwa kufanya kama watumishi, tusianze kujenga viota. Tuache viota hivyo na kwenda sehemu nyingine mara tunapoamuriwa kufanya hivyo. Wengi pia wameshindwa mtihani huu kwa kukosa utii kwa Roho Mtakatifu na wale waliotuweka kwenye tume hizo-Wahudumu wetu wakuu wa Mashirika.

Wapendwa katika Kristo, tunapomtumikia Kristo tunauhakika wa maisha yenye uzima wa kweli. Katika maisha hayo na Kristo, wote wahudumu na wahudumiwa hustawi na kufikia hatma yake. Ndani ya maisha haya tunapata furaha ya kweli, kwa sababu tunayemtumikia ndiye ALFA na OMEGA. Naye Yesu Kristo anasema, “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu,” Yoh 6:51

Ndugu yangu tuliyesafiri pamoja katika tafakari hii, nikuache na neno hili; uzima wako hasa wa hapa ulimwenguni bila Kristo hauna maana kabisa. Shughuli zako hapa duniani bila Kristo ni upepo tu usiojua uvumako na uendako. Usalama wetu kimwili na kiroho bila Kristo ni ndoto ya samaki kusihi jangwani. Hata kama ndoto hiyo itatimia, kifuatacho ni Kifo tu. Wapo watu wengi miongoni mwetu, walitamani ndoto kama hizo, na baada ya kufikia malengo ya ndoto zoa tulipigwa mshangao mkubwa na kusema hivi: “AMEKUFA MAPEMA KWELI BILA KUFURAHIA MATUNDA YAKE!

Tumsifu Yesu Kristo!

“Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?,” Mdo 8:36b

Tusali: Ee Yesu na Mwakozi wangu, niwezeshe kufanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi kuiokoa Roho, Mwili, na Nafsi yangu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario