sábado, 29 de abril de 2017

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 3 YA PASAKA


JUMANNE WIKI YA 3 YA PASAKA

Somo: Mdo 7:51-59

Zab: 31:3cd-4, 6, 7b, 8a, 17, 21ab

Injili: Yoh 6:30-35

Nukuu:

Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo,” Mdo 7:51

“Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:55

“Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:56

Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,” Mdo 7:57

Wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli,” Mdo 7:58

“Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu,” Mdo 7:59

Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani?” Yoh 6:30

Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni,” Yoh 6:32

“Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35

TAFAKARI: “Kifo Chema ni kuishi katika Kristo na ndani ya Kristo, yeye ndiye chakula cha uzima.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna shaka kabisa wote tuliozaliwa ipo siku wote tutakufa kila mmoja kwa wakati wake. Kifo kwa Mkristo ni daraja ya kuvuka kwenda upande mwingine wenye mazingira tofauti na haya tuliyonayo: wenye uzima na uhai. Kifo kwa anayemwamini Kristo ni mlango ambao watupitisha kwenye maisha mengine ya umilele. Kifo kina maana ndani na katika Kristo kwa sababu kupitia mateso yake, na kifo chake msalabani, laana ya kifo imefutwa. Kwa Mkristo kwenye imani, kifo si kitu cha kuogopa bali ni tukio la kujiandaa.

Maandalizi ya kifo Chema ni kuishi kweli ya Kristo kila siku. Ni kumshuhudia Kristo kwa yale yaliyomema na anayotuwasa kuyafanya kama watoto wa Mungu. Ni kutokumwonea aibu Kristo mbele za watu hata kama yatupasa kufa kwa ajili ya kweli. Ukweli huu ndiyo anaouishi Shahidi Stefano na kuhushuhudia. Stefano Shahidi anawaaambia Wayahudi, “Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo,” Mdo 7:51. Jambo la kuelewa hapa katika maisha yetu ya Kiroho, hatuwezi kupingana na mpango wa Roho Mtakatifu. Sifa na kazi mojawapo wa Roho Mtakatifu ni kuleta umoja wa kweli na wakimungu kwa wote walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:26.

Palipo na Roho Mtakatifu kuna umoja wa kweli na hapo Roho Mtakatifu utenda mambo yake kwa wale aliwaridhia. Shihidi Stefano, “akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:55. Stefano Shahidi anapewa hakikisho la kile anachokisimamia na kukishuhudia. Pamoja na ukweli huu, watesi wake “wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja,” Mdo 7:57.

Ndugu yangu, ni mara ngapi katika mazingira yetu tunakutana na hali kama hii na wala hatufanyi chochote? Yawezekana hali isiwe kama ya Shahidi Stefano ya kupondwa mawe. Ila wote ni mashahidi na labda tumeshaona jinsi watoto wadogo wanavyotendwa kwenye usafiri wetu wa daladala. Mzazi ambaye naye anamtoto kama huyo anayeteswa na kunyanyapaliwa na kondakta, asemi wala akemei chochote. Je, tunatofauti gani na waliomrarua Shahidi Stefano? “Wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli,” Mdo 7:58. Sauli, ambaye leo anajulikana sana kama Mtume Paulo, anashiriki katika kosa hili. Mtume Paulo analifanya kosa hili kwa kutetea mila na desturi za mababu zake, ambaye baada ya kuongoka kwake anakuwa mtetezi mashuhuri wa Kristo na mkosoaji wa mila na desturi hizo. Huku ndiko maana halisi ya kuongoka.

Katika kipigo hiki cha kikatili, Stefano anaikabidhi roho yake kwa Mungu, kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyofanya. “Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu,” Mdo 7:59. Hata katika hali hii ya kutisha, Stefano Shahidi habadili msimamo wake, wala hakatishwi tamaa kwa kujitoa kwake muhanga. Mungu anabakia kuwa tumaini lake hadi mwisho. Wengi wetu katika hali kama hii na mara nyingine tunapo ugua kwa muda mrefu bila kujua sawasawa sababu ya magonjwa yetu, hukata tamaa na kusaliti Imani yetu na Mungu wetu. Ni mara ngapi tunawaona Wakristo waliokuwa mstari wa mbele wanakwenda kupiga ramli na hata wengine wanakutwa na umauti kwa waganga wa kienyeji?

Mpendwa, haijalishi wewe ni nani ila kuwa Mkristo bila kuwa na imani thabiti ni hatari sana. Ni sawa na mkate usioiva vizuri kwani ni hatari kwa tumbo. Yesu Kristo katika Injili ya leo anawashangaa wale wasio mwamini pamoja na yote anayoyaishi na kuyatenda. Nao wanataka kuona ishara ili wamsadiki kwamba yeye ndiye kweli wanayemtumainia. “Wakamwambia, Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani?” Yoh 6:30. Kwa Wayahudi, Musa alikuwa na nafasi ya pekee sana hata kuweza kuvuka uelewa wa Mungu. Kwa mantiki hiyo, yeyote aliyekwenda kinyume na kile alichosema au fanya Musa alionekana kama mhaini hivi. Yesu kabla ya yote anawapa uelewa wa Mungu ni nani na Musa ni nani. “Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni,” Yoh 6:32. Musa aliweza kuyafanya hayo yote kwa mkono wa Mungu, ila Kristo ni zaidi ya Musa kwani kwake upo uzima. Kiu na mahangaiko yetu yote yanamajibu tunapoishi katika yeye na ndani yake. “Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35. Je, unamwamini Kristo? Hakuna sababu ya kutafuta ulizi kwa njia ya giza kama tunaye Kristo. Hakuna sababu ya kuzindika majumba yetu na kutembea na mahirizi kama tunaye Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35

Tusali:-Ee Yesu wangu, nami nasadiki wewe ndiye chakula na uzima wangu. Amina

 

No hay comentarios:

Publicar un comentario