miércoles, 30 de noviembre de 2016

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 1 YA MAJILIO


IJUMAA WIKI YA 1 YA MAJILIO

Somo: Isa 29:17-24

Zab: 27:1, 4, 13-14

Injili: Mt 9:27-31

Nukuu:

Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza,” Isa 29:18

Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli,” Isa 29:19

 vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi,” Mt 9:27

Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana,” Mt 9:28

Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate,” Mt 9:29

TAFAKARI: “Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Kwa kadiri ya imani yenu mpate.”

Wapendwa wana wa Mungu, tukiachana na yote yale mazuri yaletwayo na Masiha wetu kama tuonavyo katika somo letu la kwanza, kutoka kitabu cha Nabii Isaya, ni vyema tukajikita leo kwa undani juu ya haya yafuatayo: kuviondoa vilema vyetu na mapungufu, kujifunza ustahimilivu kwa yale tusiyoyajua, kujifunza katika shida na mateso, na kutokuchukulia vitu kwa mzaa mzaa au mazoea ili tuufaidi ujio wa Masiha. Huu ndio wito wa kipindi hiki cha Majilio. Hivyo leo tuangalie kwa undani juu ya mahangaiko yetu na mateso ambayo kwa kiasi kikubwa yanatutoa katika mwelekeo mzima wa Imani ya kweli. Ni kwa kadiri ya Imani yako utapata yale uyaombayo.

Bila shaka wewe ni mmoja wa wale ambao kwa namna mmoja au nyingine umekuwa ukizunguka kila kona ukitafuta suluhu la tatizo lako bila mafanikio. Hakuna shaka pia kwa tatizo hilo au matatizo hayo umeshasali kila aina ya sala na novena bila mafanikio. Kwa mtiririko huu naona pia unavyoangaika kutafuta majibu ya matatizo yako kutoka nyumba moja ya sala (vijikanisa vya majina ya watu)  kwenda nyingine, toka mchungaji mmoja kwenda mwingine bila mafanikio yenye utulivu wa kutosha. Naona unavyoshawishika kufanya ibada za giza kwa maagizo ya waganga wa kienyeji kupitia marafiki zako unaowaamini.

Wapendwa katika Kristo, leo Yesu anakuambia wewe na mimi maneno haya ya uzima kama alivyowaambia wale vipofu waliotaka kuona tena; “Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Kwa kadiri ya imani yenu mpate.” Swali hili analotuuliza leo Yesu ni swali la msingi sana. Wengi wetu ni wakristo wa majina na zaidi sana ni wakrito wa jumapili. Dini na Imani ya wengi imekuwa kama kautaratibu fulani kitumikacho kama utambulisho wa kawaidi katika matukio fulani ya maisha, na kisicho sema chochote kuhusu undani wa maisha wa mtu husika.

Licha ya kwamba mtu akiwa amebanwa na tatizo kubwa huweza kutekeleza ushauri wowote apewao, ni vyema kusimama katika Imani thabiti bila kuterereka. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana,” Mt 9:28. Yote hutendwa ndani yetu kwa uzito  ule ule tulionao kuhusu kile tuaminicho. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate,” Mt 9:29.

Mungu ana lengo kwa kila tatizo. Yeye hutumia mazingira kukuza tabia yetu ya kweli. Yeye hutegemeza zaidi mazingira katika kutufanya tufanane na Kristo. Ukweli ni kwamba unakabiliwa na mazingira masaa ishirini na nne kila siku. Yesu alituonya kwamba tutakuwa na matatizo ulimwenguni. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:33.

Hakuna aliye sugu kwa matatizo au amefunikwa asipatwe na mateso, wala hakuna aliye huru mbali na matatizo katika maisha. Maisha ni mfululizo wa matatizo. Kila unapotatua moja, jingine linasubiri kutokea. Si yote makubwa, lakini yote yana maana kwa Mungu katika kukuza tabia yako. Petro anatuhakikishia kwamba mtatizo ni ya kawadia, Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho,” 1Pet 4:12.

Mungu anatumia matatizo kukusogeza karibu naye. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa,” Zab 34:18. Ndugu yangu, wakati wako mzuri wa kuwa na ibada ya karibu na Mungu unaweza kuwa siku zile za giza sana, moyo wako unapokuwa umepondeka, unapohisi kuachwa, unapokuwa huna uchaguzi, maumivu yanapokuwa makubwa, na unamgeukia Mungu peke yake.

Ni wakati wa taabu ndipo tunajifunza kusali sala za kweli na uaminifu kutoka moyoni. Tunapokuwa katika maumivu, hatuna nguvu za sala za juu juu. Maisha yakiwa ya raha, tunaweza kumfahamu Yesu juu juu tu, tukimwiga na kumnukuu na kusema juu yake. Lakini ni katika taabu ndipo tutamjua Yesu. Tunajifunza mambo katika mateso, mambo ambayo hatuwezi kujifunza kwa njia nyingine yoyote.

Mungu angeweza kuzuia Yusufu asitiwe gerezani, Mwa 39:20-22. Mungu angezuia Danieli asitupwe kwenye shimo la simba, Dan 6:16-23. Mungu angezuia Yeremia asitupwe katika shimo la matope, Yer 38:6. Mungu angezui Paulo asivunjikiwe na jahazi mara tatu, 2Kor 11:25. Na Mungu angewazuia vijana watatu Waebrania wasitupwe katika tanuru la moto, Dan 3:1-26. Pamoja na hali hiyo Mungu hakufanya hivyo. Aliruhusu matatizo hayo kutokea, na matokeo yake kila mmoja wao alimsogelea Mungu karibu zaidi.

Matatizo hutulazimisha kumtazama Mungu na kumtegemea badala ya nafsi zetu wenyewe. Mtume Paulo anashuhudia faida hii. “Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu,” 2Kor 1:9. Kamwe hutajua kwamba unachohitaji ni Mungu tu mpaka pale utakapojikuta umebaki na Mungu tu. Bila kujua chanzo, hakuna tatizo lolote linaloweza kukupata bila ruhusa ya Mungu. Kila kinachotokea kwa mtoto wa Mungu kinachujwa na Baba, na amekusudia kukitumia kuleta mema ingawa Shetani na watu wengine wanakusudia mabaya.

Kwa kuwa Mungu anatawala yote, ajali ni matukio tu katika mpango mzuri wa Mungu kwa ajili yako. Kwa sababu kila siku ya maisha yako iliandikwa kwenye kalenda ya Mungu kabla hujazaliwa. “Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado,” Zab 139:16. Hivyo kila kinachotoka kwako kina umuhimu wa kiroho. Kila kitu! “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi,” Rum 8:28-29 

Wengi wetu hiki kifungu (Rum 8:28-29) hukinukuu na kukieleza vibaya. Hakisema, “Mungu husababisha kila kitu kufanya kazi kama ninavyopenda mimi.” Wala hakisemi, “Mungu husababisha kila kitu kufanya kazi ili kuleta maisha ya furaha duniani.” Hii si kweli pia kuna miisho ya huzuni duniani. Tunaishi katika ulimwengu ulioanguka. Ni mbinguni tu ndiko mambo yanatendeka kikamilifu kama Mungu alivyokusudia. Ndiyo maana katika sala ya Baba Yetu tumeelezwa kusali, “Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni,” Mt 6:10. Ili kuelewa vyema kifungu hicho kutoka Barua ya Mtume Paulo kwa Warumi ni vyema tuangalie kwa makini kila fungu la maneno.

“Twajua:” Tumaini letu wakati wa magumu hutegemea kufikiri chanya, kufikiri kwa kutarajia, au kule kutegemea mazuri kwa kawaida. Huu ni uhakika uliojengwa kwenye kweli ya kwamba Mungu anatawala kikamilifu ulimwengu na kwamba anatupenda.

Katika mambo yote:” Mpango wa Mungu kwa maisha yako unahusisha yote yanayokutokea-pamoja na makosa yako, dhambi zako, na maumivu yako. Pia ni pamoja na magonjwa, madeni, majanga, talaka, kifo cha uwapendao. Mungu anaweza kuleta mema kutokana na jambo ovu sana. Alifanya hivyo pale Kalvari.

Mungu hufanya:” Kuna mbunifu nyuma ya kila kitu. Maisha yako siyo matokeo ya bahati mbaya, ajali, au bahati nzuri. Kuna msanifu nyuma. Historia ni hadithi yake. Mungu anavuta nyuzi. Tunafanya makosa, lakini Mungu hakosei kamwe. Mungu hawezi kufanya kosa-kwa sababu yeye ni Mungu.

“Hufanya kazi pamoja:” Siyo kwa kipekee au kwa kujitegemea. Matukio katika maisha yako hufanya kazi pamoja katika mpango wa Mungu. Siyo matukio yaliyojitenga, lakini matukio yanayotegemeana katika machakato mzima wa kukufanya ufanane na Kristo. Ili kutengeneza keki lazima utumie unga wa ngano, chumvi, yai bichi, sukari, na mafuta. Kama kila kimoja kikiliwa peke yake hakina ladha nzuri au hata ni kichungu. Lakini ukivioka pamoja vinakuwa chakula kitamu. Na hiyo ndiyo keki. Kama ukimpa Mungu maono yako yote mabaya, matukio yasiyopendeza, atayaunganisha pamoja kuwa kitu chema.

“Wale wampendao katika kuwapatia mema:” Hii si kwamba kila kitu maishani ni chema. Mengi yanayotokea katika ulimwengu ni maovu na mabaya, lakini Mungu ni mtaalam wa kutoa mema kutokana na hayo. Katika ukoo wa Yesu Kristo, Mt 1:1-6, wanawake wanne wameorodheshwa: Tamari, Ruthu, Rahabu, na Bethsheba. Tamari alimhadaa baba mkwe wake. Rahabu alikuwa kahaba. Ruthu hakuwa Myahudi na alivunja sheria kwa kuolewa na Myahudi. Bethsheba alitenda uzinzi na Daudi, jambo lililopelekea mauaji ya mume wake. Hizi hazikuwa ni sifa nzuri, lakini Mungu alileta mema kutokana na mabaya, na Yesu akaja kupitia ukoo wao. Kusudi la Mungu ni kubwa kuliko matatizo yetu, maumivu yetu na  hata dhambi yetu. Neema na huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu.

“Wale walioitwa:” Ahadi ya Mungu ni kwa watoto wa Mungu tu. Si kwa kila mmoja. Kila kitu hufanya kazi pamoja kwa ubaya kwa wale wanaoishi wakimpinga Mungu na kukazia kufuata njia zao.

“Kwa kusudi lake:” Kusudi hilo ni lipi? Ni kwamba sisi “tufananishwe na mfano wa Mwana wake,” Kila kitu Mungu anachokiruhusu kutokea katika maisha yako kinaruhusiwa kwa kusudi hilo.

Wapendwa wana wa Mungu, sisi ni kama lulu, tumechongwa kwa nyundo na tezo ya taabu nyingi. Kama nyundo ya sonara haina nguvu sana kuweza kuondoa mikwaruzo, Mungu atatumia nyundo nzito zaidi. Kama sisi ni jeuri zaidi, anatumia nyundo nzito ya kunyanyuliwa na chombo maalum. Atatumia chochote kile.

Hivyo, kila tatizo ni nafasi ya kujenga tabia, na kadiri linavyokuwa gumu zaidi, ndivyo kunakuwa na matokeo makubwa katika kujenga msuli wa kiroho na uadilifu. Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini,” Rum 5:3-4. Kila kinachotokea kwa maisha yako ya nje si cha muhimu sana kama kile kinachotokea ndani yako. Mazingira yako ni ya muda mfupi, lakini tabia yako itadumu milele.

Maandiko Matakatifu hufananisha majaribu na moto wa kusafisha madini ambao huchoma takataka zote. Mtume Petro anasema, “ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima,” 1Pet 1:7a-d. Mfua fedha aliulizwa, “Je, unafahamu vipi kwamba sasa fedha ni safi? Alijibu, “ninapoona sura yangu ndani yake.” Unapokuwa umesafishwa kwa majaribu, watu wanaweza kuiona sura ya Kristo ndani yako. Yakobo anasema, “mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi,” Yak 1:3.

Kwa kuwa Mungu anakusudia ufanane na Kristo, atakupitisha katika yale Yesu aliyopitia. Hii ni pamoja na upweke, majaribu, dhiki, kulaumiwa, kukataliwa, na matatizo mengine mengi. “Alijifunza kutii kwa njia ya mateso” na alikamilishwa kwa njia ya mateso,” Ebr 5:8-9. Kwa nini Mungu atuepushe kutoka yale aliyomruhusu Mwana wake kuyapata? Mtume Paulo anasema, na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye,” Rum 8:17.

Tumsifu Yesu Kristo!

 Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote,” Zab 34:19

Tusali:-Ee Yesu, tujalie ustahimilivu wako katika mahangaiko na mateso yetu. Amina

martes, 29 de noviembre de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 1 YA MAJILIO


ALHAMISI WIKI YA 1 YA MAJILIO

Somo: Isa 26:1-6

Zab: 118:1, 8-9, 19-21, 25-27a

Injili: Mt 7:21, 24-27

Nukuu:

 Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini,” Isa 26:3 

Mtumainini Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele,” Isa 26:4

 Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21 

Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25 

TAFAKARI: “Afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni ndiye atakayeingia katika ufalme wa mbinguni.”

Wapendwa wana wa Mungu, kila kitu chenye uhai kwacho chenyewe au kundi huongozwa na mamlaka fulani. Ni kweli pia hata kwa upande wa mwanadamu katika ishi yake ikiwa ni pamoja na fikiri yake, tenda yake, amini yake, husukumwa na kitu fulani. Ukweli huu ni pamoja na kundi la watu ambao pia kwa kukaa pamoja husukumwa na nguvu ya mfumo fulani. Nguvu hizi au misukumo hii tunapoitimiza kama ilivyo ndiyo kwa namna hiyo tunalandana nayo na kujishikamanisha nayo. Huku ndiko kuwa na utii wa kweli katika mamlaka hizo kwani kwa kupitia utii huu tumeshikamanishwa na kile kinachotusukuma (mamlaka) kufanya hivyo.

Ndugu zangu katika Kristo, Injili ya leo inatuweka wazi kwa kutufunulia ni kipi kipasacho kusukuma maisha yetu. Kitu hicho ndicho kinachotakiwa kuwa na mamlaka juu ya maisha yako. Yesu anatupa angalizo na kusema, “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21. Kwa maana nyingine unaweza kuwa Mbwekaji mzuri sana kwa kuwapendezesha watu wanaokuzunguka kwa kuwaaminisha pasipo kumaanisha, ukawa kama Mbwa anayebweka usiku kucha kumwaminisha tajiri yake kwamba ulinzi upo, kumbe ni woga wa miluzi ya upepo. Kumbe ukweli ni kwamba, ni yule tu “afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni (Mungu) ndiye atakayeingia katika ufalme wa mbinguni.” Je, kufanya mapenzi ya Mungu kunamaanisha nini?

Wapendwa wana wa Mungu, kufanya mapenzi ya Mungu ni “kukaa katika pendo” la Mungu. “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake,” 1Yoh 4:16. Ni kuwa tayari kuongozwa na mamlaka ya Mungu katika mfumo wa Upendo. Tunakaa katika upendo wa Mungu kwa kuyatimiza mapenzi yake pale tu tunapolipokea neno lake, tunapolisoma neno lake, tunapolifanyia tafiti neno lake, tunapolikumbuka neno lake, na tunapolitafakari neno lake.

Haya mambo matano ni muhimu sana kama tunataka kweli kukaa naye na kuyafanya mapenzi yake. “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba,” Mt 7:24-25. Hakuna awezaye kutung’oa kwenye mwamba huu wa imani hata kikija kimbunga cha tsunami. 

 Tusipo lishika neno la Mungu vizuri tutakuwa tayari kuongozwa na mamlaka hizi; mila zetu (kwa kufanya yale yanayotutia hofu bila kuhoji sababu yake), desturi zetu (kwa kufanya kadiri ya mapokea ya wazee wetu katika hali ya upofu), hisia zetu (kwa kufanya kadiri ya miyeuko yetu na siyo utashi wetu). “Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa,” Mt 7:26-27. Hakika kwa hali hii tunabaki kuwa kama bendera fuata upepo. Na kwa sababu hiyo, kila ajitokezaye na kutushawishi hatutakuwa na nguvu ya kuimili vishindo vya imani kwani tu wepesi kama pamba.

Hivyo ndugu zangu katika kipindi hiki cha majilio tunapomsubiri Masiha wetu tukae katika neno la uzima. Ni katika hali hii kwamba Mungu “atamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini,” Isa 26:3. Mungu wetu ndiye mwamba wetu wa milele. Tumia muda wako vizuri kulitafakari neno lake la uzima. Kama unaweza kutumia masaa mawili au matatu kwenye runinga, tenga basi hata robo saa kulisoma neno la Mungu na ubaki nalo kwani ndilo lenye uzima. “Mtumainini Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele, kwa kuwa amewashusha wakaao juu, Mji ule ulioinuka, aushusha, Aushusha hata nchi, auleta hata mavumbini,” Isa 26:4-5. Yote yanayotupa matumaini leo na sasa bila Mungu hufifia kama mkaa wa mabua ya mahindi.

Tumsifu Yesu Kristo!

Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua,” 1Yoh 3:6

Tusali:-Asante Ee Yesu na Mwokozi wangu, kwa sababu kwako kuna uzima wa milele. Amina

lunes, 28 de noviembre de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA MTAKATIFU ANDREA, MTUME


Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume

30 Novemba

Somo: Rum 10:9-18

Zab: 19: 8-11

Injili: Mt 4:18-22


Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9

Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:10 

 Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt 4:19

Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mt 4:20

TAFAKARI: “Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.”

Wapendwa wana wa Mungu, mtihani mkubwa kwa mtu yeyote yule siyo hii tuifanyayo mashuleni na hata vyuoni, bali ni mtihani huu wa “kuamua,” uwe nini katika maisha yako. Si rahisi kufanya maamuzi hayo na kuchukua njia nyingine mpya kabisa usiyojua kifuatacho huko mbeleni. Mtu huwa na uhakika kwa kile alichokiishi jana na anachokiishi leo na sasa. Huu ni mzunguko wa kawaida katika maisha ya kila mmoja wetu. Kuwekeza maisha yako yote kwa kile usichokijua humjengea mtu hofu.

Leo Kanisa linapofanya sikukuu za watakatifu na kwa maana ya pekee leo sikukuu ya Mt. Andrea Mtume, ni kusadifu yale waliyoyaamua na kuyaishi na ndiyo ukuaji wa Kanisa na uhai wake. Walifanya uamuzi wa kuacha yale waliyoyazoea na yaliyokuwa yanawapa usalama na kufuata kile wasichokijua wakijisalimisha kabisa katika hicho. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mt 4:20.

Mtume Andrea akiwa na ndugu yake Simoni Petro walikuwa wavuvi. Kazi hii iliwapa usalama na mahitaji yao ya kila siku. Yesu anawaita wamfuate nao wanaacha pale pale waliyokuwa wanafanya na kumfuata. Uamuzi huu ni mzito sana.Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi,” Mt 4:18. Kazi hii ndiyo iliyowapa mkate wao wa kila siku. Embu fikiri leo kwa kazi unayofanya hasa wale wanaopata kipato kilichonona, aje mtu tu na kukuambia nifuate. Nini kitakuwa kitu cha kwanza kufanya? Bila shaka utaanza kumpiga maswali mazito na mwisho kumchukulia kama mwendawazimu hivi.

Mitume hawa wanayaacha yote na kumfuata. Yesu Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mt 4:19. Kuwa wavuvi wa watu ni mabadiliko mazima ya mfumo na namna ya kutenda na kuishi. Hapa ndipo tunaposema Mitume hawa walikuwa majitu ya sifa. Mioyo yao ilikuwa na ushupavu wa hali ya juu. Ni vigumu sana mtu kuubadili mfumo wa maisha yake aliouzoea.

Yesu Kristo alikuwa kila kitu katika maisha yao. Walijua pia hakuna wokovu pasipo Kristo. Iliwezekanaje hivyo haraka? Bila shaka kwa Nguvu na Neema za Mungu iliwezekana pale walipoonyesha utayari wao wa kumsikia Yesu na kumfuata. Mtume Paulo anatuambia, kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka,” Rum 10:9. Jambo hili la kujisalimisha kabisa mikono mwa Yesu halikuwa na mashaka ndani ya mioyo ya hawa Mitume ingawa halikuwa jambo rahisi kufanya. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu,” Rum 10:10 

Wapendwa wana wa Mungu, sababu nyingine ya uwepo wetu hapa duniani licha ya kwamba ni kwa muda mfupi, ni kuwaelezea watu wengine habari njema ya wokovu wetu. Wewe uliyebahatika kuifahamu siri hii usibaki nayo mwenyewe. Ni furaha kubwa sana mbele ya Mungu kama watakuwepo baadhi ya watu waliofika mbinguni kwa sababu ulitumia muda wako kuwaelezea habari njema ya wokovu kwa maisha yao. Mitume waliona na kuupokea wajibu huu mkubwa. “Maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 4:20. Neno hili sasa si kwa Wayahudi tu, ila lapaswa kusikika duniani kote.

Kwa kupitia Kristo sote tumeunganishwa na kuwa familia moja yenye mastahili sawa mbele ya Mungu, na warithi wa ufalme wake. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka,” Rum 10:12-13. Mitume kwa namna ya pekee waliuona wajibu huu mkubwa wa kulihubiri neno la Mungu pasipo woga.

Msingi wa haya yote ni Imani ile waliyokuwa nayo Mitume, na kwa namna ya pekee leo Mama Kanisa anapofanya sikukuu ya Mt Andrea Mtume. Hivyo chanzo cha imani hiyo ni kusikia neno la Kristo. “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo,” Rum 10:17. Je, watu watasikiaje bila kuambiwa? Kumbe leo pia tunakumbushwa mimi na wewe kwamba kwa Sakramenti ya Ubatizo tunafanywa wamisionari. Ni wajibu wa kila Mbatizwa kulitangaza neno la uzima na wokovu kwa watu wote. Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia, Sauti yao imeenea duniani mwote, Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu,” Rum 10:18.

Hivi ndivyo walivyofanya Mitume, na leo Kanisa limesimama likiwa Kristo ndiye msingi wake Imara, na Mitume. Mimi na wewe tunadaiwa kuyatoa maisha yetu kama walivyofanya Mitume ili habari njema iwafikie wote ambao bado hawajasikia. Je, nifanye vipi? Anza hapo hapo ulipo! Kuwa chumvi na mwanga ili uso wa Kristo uonekana katika maisha yao na yako.

Tumsifu Yesu Kristo! 

Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16

Tusali: Ee Yesu, wajalie neema na nguvu wale wote wanaofanya kazi ya kimisionari, na hasa kwenye mazingira magumu. Amina

domingo, 27 de noviembre de 2016

JUMANNE WIKI YA 1 YA MAJILIO YA MWAKA-A


JUMANNE WIKI YA 1 YA MAJILIO MWAKA-A

Somo: Isa 11:1-10

Zab: 72:1-2, 7-8, 12-13, 17

Injili: Lk 10:21-24

Nukuu:

Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda,” Isa 11:1 

 Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10

Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21 

Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia,” Lk 10:22

TAFAKARI: “Kwake itasimama kweli, haki, Amani, na Upendo.”

Wapendwa wana wa Mungu, kumkomboa mwanadamu kutoka hali yake ya mateso, mahangaiko na dhambi, Mungu aliye Kweli, Haki, Amani, na Upendo kwa makusudi makubwa anapenda kuanzisha uhusiano na yule aliyemuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Tendo hili la kuujenga uhusiano wa karibu nasi linamshusha Mungu chini kabisa katika hali ya mwanadamu. Huu ni upendo mkubwa sana kwetu. Kipindi hiki cha majilio ni kipindi cha kutafakari upendo huu wa ajabu Mungu anaokwenda kutufanyia. Ikiwa zawadi hii ni kubwa sana kwetu hatuna budi kujiandaa vizuri mwili na roho ili atakapokuja atukute tupo safi na wenye afya njema hasa roho zetu.

Kufanikisha mpango huu, Mungu huyu aliye Alfa na 0mega atachukua hali yetu ya kibinadamu, na hivyo atazaliwa ikiwa ni moja ya kushiriki hali yetu ya kibinadamu. Jambo hili linatabiriwa na Nabii Isaya. Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda,” Isa 11:1. Je huyu atakayezaliwa ataongozwa na mamlaka gani? Hakika kwa vile anakuja kuusimika ufalme wa kweli, haki, amani, na upendo, roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana,” Isa 11:2. Hivi ndivyo vitendea kazi vyake. Ujio wake kwetu ni hukumu pia ambayo itasimama katika haki. Hivyo, kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya,” Isa 11:4 

Ujio wa mfalme huyu ni ujio wa neema na baraka. Anakuja na kusimika mfumo wema na kuufifisha mfumo wa uovu. Anakuja kuondoa sintofahumu zetu kati yetu wanadamu na viumbe vingine alivyoviumba. Huyu hakika ni mfalme wa Amani. Hakutakuwa tena na sintofahumu kati ya wanyama aliowaumba. Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza,” Isa 11:6. Mwanadamu ataishi kwa amani na hofu haitakuwepo tena. Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira,” Isa 11:8.

Uwepo wa Mfalme huyu wa kweli,  haki, amani na upendo utajidhihirisha kwa utukufu wake. Mataifa yote watamfuata alipo kwa sababu kuna Utukufu. “Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu,” Isa 11:10. Haya ndiyo atakayoyafanya na kuujenga tena uhusiano wetu ulioharibiwa na dhambi zetu.

Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na hayo mazuri yote yaliyotabiriwa na Nabii Isaya kuhusu Mfalme huyu tunayemsubiri kwa hamasa kubwa, yatawezekana tu kama tutakuwa tayari kutoa ushirikiana naye. Mungu atukokoti kama Jemedari katili na mwenye silaha za kutisha. Utawala wake ni utawala wa Upendo. Mungu hapendi kuondoa uhuru na utashi wetu wa kumfuata. Ametuachia haya yote akijua kabisa kwamba kwa kuyatumia vizuri ni njia rahisi ya kumfikia, hata pale tutakapoyatumia vibari itakuwa njia rahisi pia ya kumrudia tukifanya toba ya kweli na majuto. Kwa hiyo, ‘aliyekuumba wewe pasipo wewe hawezi kukukomboa wewe pasipo wewe,’ Mt. Agustino wa Hippo.

Siri ya ukweli huu wa kutoa ushirikia na  Mungu ili kuwa sehemu salama anausema Yesu katika Injili ya leo. Siri hii ni kuwa kama watoto wachanga. Mtoto mchanga huamini yote kuwa salama anapokuwa mikono mwa wazazi wake. Mtoto mchanga kamwe hawezi kuacha kutabasamu hata kama akiwa mikononi kwa mtu mwovu. Maana yake ni kwamba, mtoto mchanga mara zote anamtazamo chanya. Hii ndiyo hekima iliyofichwa ndani ya watoto wachanga. Yesu anatutaka kuwa na unyenyekevu huu katika kuamini yote kuwa salama mikononi mwa Mungu. Naye Yesu, “Saa ile ile alishangilia kwa Roho Mtakatifu, akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya umewaficha wenye hekima na akili; umewafunulia watoto wachanga; Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyokupendeza,” Lk 10:21. 

Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, leo Yesu anatufunulia jambo la pekee sana. Kwanza kabisa ni Yeye tu aliyekabidhiwa yote na Mungu. Pili hatuwezi kumjua Mungu Baba pasipo Yeye mwana, yaani,  Yesu Kristo. Kwa maana hiyo, kuwa na Yesu ni kuwa kwenye mikono salama. Naye Yesu, Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia,” Lk 10:22. Je, ulipo na ulipojikabidhi kuna usalama?

Tumsifu Yesu Kristo!

Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama,” Mit 18:10

Tusali: Ee Yesu Mwana wa Adam, nakuamini. Amina

sábado, 26 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 1 YA MAJILIO MWAKA-A


JUMATATU WIKI YA  1 YA MAJILIO YA MWAKA-A

Somo: Isa 4:2-6

Zab: 122: 1-2, 3-4b, 4cd-5, 6-7, 8-9

Injili: Mt 8:5-11

Nukuu:

“Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,” Isa 4:3

 “Enyi wa nyumba ya Israeli, njoni, twende katika nuru ya Bwana,” Isa 4:5

Yesu akamwambia, Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7

Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10 

TAFAKARI: “Twende katika nuru ya Bwana.”

Wapendwa wana wa Mungu, Mwokozi tunayemtazamia kwa hamu ni Bwana wa Amani atakayetufundisha njia zake na kuenenda katika NURU yake. Sheria yake kuu ni UPENDO. Ni wakati wa kuyajenga upya mahusiano yetu na Bwana huyu wa Amani. Ni Bwana wa Amani wa wataifa yote, na ulimwengu mzima. Ni Bwana aliye katika kilele cha vilele vyote ambacho uthibitisha ukuu wake. Nabii Isaya anasema habari za Mkombozi huyu: “Na itakuwa katika siku za mwisho, mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na mataifa yote watauendea makundi makundi,” Isa 4:2

Haki ndicho kipimo na uwepo wa Amani ya Mkombozi huyu tunayemtazamia. Hivyo ajapo lazima ipite hukumu ya haki, na ndipo atakapousimika utawala wake wa Amani, Haki, na Upendo. Ili mambo haya yatendeke katika utawala wake yatupasa kubadili namna yetu ya kufikiri na kutenda. Na ndipo “mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,” Isa 4:3

Ulimwengu wa leo vita na hasa ugaidi vinashamiri kwa nguvu kubwa sana na uhai wa mwanadamu ikiwa ni pamoja na amani vipo reheni. Nabii Isaya anasema, “Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe,” Isa 4:4

 Tunahitaji sana kwa sasa utawala wa Mkombozi huyu. Lengo la Mungu kuumba ulimwengu pamoja na mambo mengine, aliuumba ili pawe sehemu salama kwa ajili ya uhai wa viumbe vyote alivyoviumba na kwa namna ya pekee Mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27.

Kujenga mahusiano mapya na Mungu ni pamoja na kuwa na imani thabiti naye. Uthabiti wa imani ya kweli hujengwa kwa kuyaacha mambo yako ya giza na kuikumbatia nuru. Wana wa Israeli waliiacha nuru na kulikumbatia giza. Mungu aliwaacha. “Maana wewe umewaacha watu wako, nyumba ya Israeli, kwa sababu wamejaa kawaida za mashariki, nao ni wapiga ramli kama Wafilisti, na wanapana mikono na wana wa wageni,” Isa 4:6 

  Leo katika Injili Yesu anakutana na mtu mmoja, Akida, aliyekuwa anauguliwa na mtumishi wake ugonjwa wa kupooza. Akida huyu anamwomba Yesu aende kumponya mgonjwa wake. Yesu anamjibu, “Nitakuja, nimponye,” Mt 8:7. Akida huyu akitambua uwezo wake na nafasi aliyokuwa nayo, na ule uwezo wa Yesu, bado anatambua kuwa umbali na uwepo wa Yesu aviwezi kumzuia kumponya mtumishi wake. Akida anamtaka Yesu aseme neno tu na mgonjwa wake atapona.

Hii ndiyo imani thabiti na isiyokuwa na shaka. Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli,” Mt 8:10. Je, waamini kuwa Yesu aweza kutenda maajabu ndani yako? Jenga uhusiano mpya naye kuanzia sasa! Yesu ni Rafiki wa kweli.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii,” Lk 17:6

Tusali: Ee Yesu Mwema, jenga tena uhusiano wangu nawe. Nijalie neema na nguvu nisikusaliti. Amina

viernes, 25 de noviembre de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 1 YA MAJILI YA MWAKA-A


JUMAPILI YA 1 YA MAJILIO YA MWAKA-A

Somo I: Isa 2:1-5

Zab: 122:1-2, 3-4a, 8-9

Somo II: Rum 13:11-14

Injili: Mt 24:37-44

Nukuu:

Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,” Isa 2:3 

Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe,” Isa 2:4 

“Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu,” Mt 24:37

 “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu,” Mt 24:42

 “Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru,” Rum 13:12

 “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake,” Rum 13.14

TAFAKARI: “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu.”

Wapendwa wana wa Mungu, karibuni katika tafakari ya leo ikiwa Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya kwanza ya majilio ya mwaka “A” wa Kanisa. Leo pia kwa namna ya pekee tunaanza mwaka “A” wa Kanisa. Masomo na tafakari zetu zitalenga katika kipindi hiki cha Kanisa. Kipindi hiki cha Majilio Kanisa linajifananisha na Taifa la Mungu la Agano la Kale linapotarajia kwa hamu kubwa ujio wa Mkombozi. Hivyo kipindi hiki Mama Kanisa anawaandaa wana wake kuwa tayari kumpokea Mkombozi.

Hata hivyo kipindi hiki cha Majilio kina sura nyingine, ambayo inaufunua ujio wa siku ya mwisho wa Bwana. Ni kwa namna hii Kanisa limegawa kipindi hiki cha Majilio katika sehemu kuu mbili nazo ni hizi zifuatazo: Sehemu ya kwanza inaanza leo hadi hapo tarehe 16 ya mwezi wa kumi na mbili. Mambo makuu katika kipindi hiki ni kutafakari juu ya ujio wa pili wa Kristo katika Utukufu wake. Sehemu ya Pili, Mama Kanisa atakuwa anatafakari juu ya  matayarisho ya Sikukuu ya Kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Msukumo na wazo kuu katika kipindi hiki katika sehemu hii ya pili ni “Kristo yu karibu,” Yeye ni Mkombozi na Hakimu.

Wapendwa wana wa Mungu, Mwokozi tunayemtazamia kwa hamu kubwa ni Bwana wa Amani atakayetufundisha njia zake nasi kuenenda katika mapito yake. Sheria yake kuu ni UPENDO. Ni wakati wa kuyajenga upya mahusiano yetu na Bwana huyu wa Amani. Ni Bwana wa Amani wa wataifa yote, na ulimwengu mzima. Nabii Isaya anasema habari za Mkombozi huyu: Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, nyumbani kwa Mungu wa Yakobo, naye atatufundisha njia zake, nasi tutakwenda katika mapito yake maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana katika Yerusalemu,” Isa 2:3.

Amani ya Mkombozi huyu inaendana pia na haki. Hivyo ajapo lazima ipite hukumu ya haki, na ndipo atakapousimika utawala wake wa Amani, Haki, na Upendo. Ili mambo haya yatendeke katika utawala wake yatupasa kubadili namna yetu ya kufikiri na kutenda. Ulimwengu wa leo vita na hasa ugaidi vinashamiri kwa nguvu kubwa sana na uhai wa mwanadamu ikiwa ni pamoja na amani vipo reheni.

Nabii Isaya anasema, Naye atafanya hukumu katika mataifa mengi, atawakemea watu wa kabila nyingi; nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe,” Isa 2:4. Kwa mantiki hii, tunahitaji sana kwa sasa utawala wa Mkombozi huyu.

Lengo la Mungu kuumba ulimwengu pamoja na mambo mengine, aliuumba ili pawe sehemu salama kwa ajili ya uhai wa viumbe vyote alivyoviumba na kwa namna ya pekee Mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Kwa mantiki hii, hakuna mwanadamu yeyote yule mwenye haki ya kuutoa uhai wa mwingine na hata kuudhuru. Leo, baadhi yetu kwa ulevi wa madaraka tunasahau kuwa nasi pia ni wanadamu, ipo siku tutakufa, na hukumu ya haki inatusubiri.

Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakari hii, Kristo mwenye haki bado anaendele kuteseka na kusulubiwa pale ninapowatenda vibaya wale wasiokuwa na sauti katika jamii yetu leo. Ninazidi kumtesa na kumsulubu Kristo, ninaposhindwa kutenda haki na kutoa haki kwa wale ambao hawana fursa sawa katika jamii yangu leo.

Kwa kosa hili, wewe na mimi tunayo njia moja tu ya kurejesha ushusiano huu. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe,” Mdo 3:19a. Tusianze kumtafuta mchawi wakati mchawi mwenyewe ni wewe na mimi. Yesu anasema, “Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi. Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele,” Mt 25:45-46. Ndugu yangu, wadogo anaowazungumzia Yesu hapa ni hawa wafuatao; wenye njaa, wenye kiu, wageni, walio uchi, wagonjwa, na wafungwa.

Kumbe kipindi hiki cha majilio, ambacho tunamsubiri Mkombozi wetu aliye upendo, haki, kweli, na amani, ni wakati mahususi wa kuyatafakari maisha yetu binafsi na makundi haya ya wahitaji katika jamii yetu. “Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini,” Rum 13:11. Hivyo, sasa ni wakati wa kuyavua matendo ya giza na kuzivaa sila za nuru, Rum 13:12. Na sila hizo za nuru ndizo hizi, “upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria,” Gal 5:22-23.

Ndugu yangu, maisha ya hapa duniani ni jukumu la muda mfupi sana. Ndugu, ili kutimiza vizuri maisha yako hupaswi kusahau ukweli wa aina mbili: Kwanza, yakilinganishwa na umilele, maisha ni mafupi sana. Pili, dunia ni makazi ya muda tu. Hatuwezi kukaa hapa kwa muda mrefu, hivyo usijishikamanishe sana nayo.Fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa,” Mt 24:34. Tumwombe Mungu atusaidie kuyaona maisha ya duniani kama anavyoyaona yeye mwenyewe. Mfalme Daudi aliomba, "Bwana, nijulishe mwisho wangu, na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani; nijue jinsi nilivyo dhaifu," Zab 39:4

Kwa maana nyingine, “Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru,” Rum 13:12. Matendo ya giza yako na yangu tunayopaswa kuyavua na bila kupepesa macho ni matendo haya ya mwili, nayo ni; uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21; Rum 13:13. Pona yako na yangu ni kumrudia Mungu, tukimvaa Yesu Kristo, Bwana wetu, na kutokuuangalia mwili hata kuwashwa tamaa zake, Rum 13:14.

Wapendwa katika Kristo, tusipende kujitenga katika kweli hii ya kupatanishwa na Mungu tungali hai. Mungu ameshatuwezesha vyakutosha katika hatua hii ya kupatanishwa naye. Kwa kupitia mwanaye mpenzi Yesu Kristo, yote yamerahisishwa. Naye Yesu anasema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yoh 14:6. Hatuna namna nyingine ya kupatanishwa na Mungu kama hatutamwelekea Yesu Kristo. “Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote,” 1Yoh 2:1a-2. Ndugu yangu, kinachokukwamisha kupatanishwa naye ni nini? Je, washuke malaika wakuambie mambo haya ndio uamini?

Injili ya leo ni mrejesho wa yale yote aliyokuwa akiyafanya Yesu, na ambayo anayafanya nasi katika hali hii ya ufufuko. Ni kumuishi Kristo katika ufufuko. Ni maisha ya ufufuko. Na ndiyo dhima ya Injili ya leo kwa maneno haya ya Yesu, Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu,” Mt 24:42.

Ndugu yangu hapana shaka wa mfahamu vizuri "inzi!" Mdudu huyu kadiri ya utafiki wa kisayansi huishi siku saba tu. Ni wiki moja kati ya wiki 52 katika mwaka mmoja. Tazama fujo na papara za inzi. Hutua kila mahali kwa siku hizo saba; kwenye vyakula (vilivyo chacha na visivyo chacha), kwenye vinjwaji, kwenye vidonda, kwenye vinyesi, nk. Tazama anavyoongea kwa ishara akiwa amenyanyua miguu yake ya nyuma na kusema, "yaliyopita yeshapita." Na anapoinua miguu ya mbele husema hivi, "yajayo na yaje, ponda mali, furahia yote, haya ndiyo maisha."

Ndugu yangu, tulio wengi leo maisha yetu hayana tofauti na haya ya inzi. Hutaka kufanya yote na kujaribu yote katika maisha. Hakuna muda wa maandalizi wala tafakari kuhusu umilele wetu kama zawadi ya pekee tuliyopewa sisi wanadamu. Katika kweli hii Yesu anakuambia wewe na mimi kwamba, Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja,” Mt 24:44

 Hata hivyo tunapewa kazi ya kufanya kuhusu Ufalme huu wa Mbinguni. Naye Yesu anasema,  “Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu,” Mt 24:42. Wajibu huu muhimu ni wa kila Mbatizwa na Kanisa kwa namna ya pekee. Haya ni maisha ya Kristo baada ya mateso, kifo na ufufuko wake. Ukeshaji ni mwitikio wa maisha ya ufufuko, na utayari wa maisha ndani na katika Kristo Yesu.

Jambo la kushangaza ni kwamba, licha ya mazoea yetu, kwamba mambo kwende kwa kiasi fulani kadiri ya mpango kazi wetu, ujio wa Kristo bado ni fumbo. Naye Yesu analithibitisha hilo kwa kusema, “kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu,” Mt 24:37. Jibu ni kwamba hakuna anayejua siku hiyo.

Kiama siku ya mwisho itakukuta katika hali uliyonayo sasa, yaani, kama utakuwa unajiboofusha kwa starehe na anasa, hodi ya pekee itapigwa kwako, na mwitikio huo ambao lazima uitikie utakuwa ndio mwisho wa pumzi yako. “Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu,” Mt 24:38-39. Nini maana ya neno hili?

Ukweli ni kwamba, leo shetani hawezi kutudanganya kwamba hakuna dhambi. Pia leo shetani hawezi kutudanganya kwamba hakuna hukumu ya mwisho.Na zaidi leo shetani hawezi kutudanganya kwamba hakuna mbingu. Ila leo shetani amechukua ufahamu wetu kwa kutusadikisha kwamba bado muda upo. Katika pumbaziko hilo kwamba, ‘bado muda upo,’ ndipo tunapopigwa na mshangao kwamba hakuna muda tena, na Mwana wa Adamu yupo mlangoni akipisha hodi. Hakutakuwa na maandalilizi! Na taswira ya kweli hii ni kwamba, “watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa,” Mt 24:40-41.

Ndugu yangu, kuepukana na kadhia hii ni KUKESHA ingali taa zetu zikiwa zinawaka na mafuta ya kutosha. Na kitendawili ni hiki; “Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa,” Mt 24:43. Je, upo tayari?

Pamoja na hayo yote tuliyoyatafakari siku ya leo, tusipofanya toba ya kweli na kuchukuwa wajibu huu muhimu katika maisha yetu kama Wafuasi wake Kristo, hata kama tukipewa “promotion” kwenda mbinguni hatutaona upekee wake, wala kufurahia ukweli huo, kwa sababu tu si mastahili yetu.

Mastahili ya kuurithi ufalme wa Mungu ni kuujenga kuanzia sasa; Kufurahia kuteseka na Kristo kwa ajili ya haki, kufa kwa ajili ya Kristo kila siku kwa ajili ya haki na upendo, na kufufuka naye kwa mastahili ya mateso na kifo chetu kitokanacho na haki, na upendo wa kweli. Hili ndilo badiliko túnalo hitaji kulifanya kipindi hiki cha majilio.

Miaka 15 iliyopita, mwenye hofu ya Mungu atokapo nyumbani mwake na kusafiri, kitu cha kwanza kukumbuka kubeba ilikuwa rozali, fedha, vitambulisho, na mambo mengine. Leo, kitu cha kwanza kukumbuka ni simu ya mkononi. Je, kuna ubaya katika hili? La hasha! Huu ni ujumbe kwamba tupo kwenye ulimwengu wa mawasiliano na ukaribu zaidi. Ndiyo maana kitokeacho leo Marekani, Bibi yangu Mzaa Baba pale Uru Mrawi anakipata kama kilivyo, yaani, ‘live.’ Je, kwa mabadiliko haya Mungu amepunguza upendo, huruma, na subira yake kwetu katika badiliko la kuyaacha maovu na kumwelekea? La hasha! Mabadiliko haya ni ufunuo wa upendo wake Mungu ndani yetu.

Na siri ya upendo huu ni kutupeleka katika ukamilifu ambao ndiyo Mungu mwenyewe. “Evolution is geared with love as an energe to wholeness.” Hata pamoja na mabadiliko haya ya sayansi na technolojia, Mungu hajapoteza uhasili wake, bali anazidi kujifunua katika mabadiliko hayo kwa sababu Yeye ndiye msukumo wa mabadiliko hayo kuelekea ukamilifu wake.

Siku mmoja watawa fulani katika monastery (maisha ya ndani ya kitawa, kujitenda katika ulimwengu huu kwa ajili ya Kristo) fulani, Kanisa lao lilipigwa radi na kuharibika isipokuwa altare ilibaki salama. Wakiwa katika sintofahamu hiyo, Mtawa mmoja aliyekuwa na umri kuliko wote aliwaambia wenzake, “afadhali radi hiyo imeipiga Kikanisa chetu. Mungu asingekuwa na huruma angepiga chumba chetu cha runinga. Hakika ingekula kwetu, na leo wote tungekuwa wafu hadi sasa!”

Ndugu yangu, embu fikiri, pamoja na maendeleo haya yote ya sayansi na teknolojia, Mungu wako akupaye uzima, unampa nafasi gani katika maisha yako? Tafakari tukio la watawa hao! Mungu wetu ni Upendo, Huruma, Msamaha, Haki, na Kweli. Tuwe karibu naye. Na hii ndiyo maana ya Majilio.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake,” Rum 13.14

Tusali:-Ee Yesu, azisha yote upya ndani yangu, kwako na ndani yako. Amina