WAAMINI WOTE MAREHEMU
Somo I: Hek 3:1-9
Zab: 23:1-3a, 3b-4, 5, 6
Somo II: Rum 5:5-11
Injili: Yoh 6:37-42
Nukuu:
“Bali roho zao wenye haki wamo mkononi mwa Mungu, wala
maumivu hayatawagusa,” Hek 3:1
“Na kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafiri
kwao kutoka kwetu kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani,”
Hek 3:2b-3
“Kwa
maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili
ya waovu,” Rum 5:6
“Bali Mungu aonyesha
pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa
tungali wenye dhambi,” Rum 5:8
“Wote
anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe,”
Yoh 6:37
“Na mapenzi yake
aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja,
bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 5:39
“Kwa kuwa mapenzi yake
Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na
uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:40
TAFAKARI: “Roho zao wenye
haki wamo mkononi mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa pote duani
anaadhimisha Misa Takatifu kwa heshima ya Waamini Marehemu Wote waliotutangulia
katika haki. Kanisa la wana wa Mungu limegawanyika katika makundi makuu matatu.
Katika mgawanyiko huo lipo Kanisa la hija, yaani, Kanisa linalosafiri hapa
duniani ikiwa ndiyo mahali pa kujindaa kwa ajili ya uzima wa milele. Lipo
Kanisa la toharani, ambalo tunaamini ni Kanisa linaloteseka, na kwa kiasi
kikubwa linategemea maombezi ya Kanisa la hija na la Watakatifu Wote Mbinguni.
Mgawanyiko wa mwisho ni Kanisa la Watakatifu wa Mungu, ambalo ndilo mwombezi wa
Kanisa la hija na linaloteseka, yaani, Toharani. Kanisa hili ndilo
lililodhihirika la wateule wa Mungu, na wote waishio humo wanafana na Kristo na
kufurahia Utukufu wake na kumwona Mungu kama alivyo. Lakini “wapenzi,
sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya
kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo,”
1Yoh 3:2.
Wapendwa
wana wa Mungu, tungali hapa duniani yatupasa kuishi katika matumaini hayo
niliyoyasema pasipo shaka yoyote tukijua wazi kwamba maisha ya umelele
yakilinganishwa na haya ya duniani, tu hapa kwa muda mfupi sana. Hivyo, “kila
mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu,” 1Yoh
3:3. Kanisa hili la hija linatoa sadaka hii
ya Misa Takatifu kwa matumaini makubwa likijua kabisa kwa sadaka ile ya Bwana
wetu Yesu Kristo pale msalaba ni kielelezo cha utakaso wa Kanisa hili
linaloteseka huko toharani lipate Utakakatifu. “Wenye kumtumaini watafahamu yaliyo kweli, na waaminifu watakaa naye
katika upendo; mradi neema na rehema zina wateule wake,” Hek 3:9. Kanisa la hija linawajibu huu kama Sakaramenti ya
wokovu kwa watu wote. Mungu pekee ambaye ni Huruma, Upendo, na Msamaha na Haki
ndiye mwenye kuwahesabia haki wote waliotutangulia na hasa Kanisa hili la
toharani.
Haki hiyo ya Mungu tutahesabiwa kutokana
na sadaka ya damu ya Mwanaye Mpenzi Yesu
Kristo pale Msalabani. Hivyo, “Basi zaidi sana
tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye,”
Rum 5:9. Yapo maswali mawili ya msingi kwako na kwangu tutakayo ulizwa siku ya
Mwisho. La kwanza; Je, umefanya nini na upendo wa wangu [Mungu] kupitia
mwanangu Yesu Kristo kwa sadaka yake pale msalabani? La pili; Je, umefanya nini na vipaji
nilivyokupa? Ili uweze kujibu vizuri siku ya mwisho yakupasa kujiandaa vyema
kuyajibu maswali haya sasa kupitia ushuhuda wa maisha yako leo. Hatuwezi kuwa
na kesho yenye matumaini ya kweli kama hatuishi leo yenye matumaini ya kweli.
Wapendwa katika Kristo, maisha ya ushuhuda wa
kweli yanagharama zake. Kama yalivyo majira ya mwaka, yaani, kipindi cha
baridi, joto, vuli, na kipupwe, ndivyo yalivyo maisha ya binadamu. Yatupasa kuwa
wastahimilivu katika vipindi vyote vya shida, taabu, mateso na furaha, na hata
kufa kwa ajili ya haki na kweli. Pamoja na maumivu tutakayoyapata katika safari
hii ya kuelekea uzima wa milele, roho zetu zenye haki zitakuwa mikononi mwa
Mungu. “Bali roho zao wenye haki wamo mkononi
mwa Mungu, wala maumivu hayatawagusa,” Hek 3:1. Imani na matumaini ndiyo dira
ya kushinda na kufikia hatua hii muhimu.
Maisha ya ulimwengu wa leo ni maisha yenye kusukumwa na
falsafa ya umimi na ujimbilikiziaji wa mali. Katika hali hii ni vigumu sana
jamii inayokuzunguka kusadifu majitoleo yako kwa wahitaji. Tupo kwenye
ulimwengu wa kila mtu na yake na wakati wake. Hata katika hali na changamoto
hizi tusimuonee aibu Kristo Yesu hasa tunapojali na kuithaminisha damu yake
iliyomwagika pale msalabani. Kufa katika hali hii hakuna hasara yoyote. “Na
kufariki kwao kulidhaniwa kuwa ni hasara yao, na kusafiri kwao kutoka kwetu
kuwa ni uharibifu wao; bali wao wenyewe wamo katika amani,” Hek 3:2b-3. Tunayo
amani na matumaini kwa sababu Kristo alikufa kwa ajili ya waovu, na hasa pale
tulipokuwa hatuna nguvu za kuushinda uovu. “Kwa
maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili
ya waovu,” Rum 5:6.
Licha ya udhaifu wetu kama binadamu,
upendo wa Mungu unajidhihirisha kwetu kwa kumtoa mwanaye afe kwa ajili yetu
tungali tuna dhambi. Huu ni upendo Mkubwa sana kwetu. “Bali Mungu aonyesha
pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu,
tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8. Sadaka hii ya Yesu pale Msalabani ni
upatanisho wetu na Mungu, na kurudishiwa hadhi ya kuwa wana wake Mungu, waridhi
wa ufalme wake, na maisha ya uzima wa milele. Hivyo, “Kwa
maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake;
zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake,” Rum 5:10. Je,
tufanye nini sasa?
Wapendwa
wana wa Mungu, wenzetu wesha tutangulia katika haki ni jukumu langu mimi na
wewe tuishi kama tunayo siku hii ya leo na muda huu wa sasa. Hakuna kati yetu
anayejua litakalotokea kwake sekunde moja ijayo. Kristo Yesu yupo daima
kutusubiri na anayemwendea hawezi akampoteza. “Wote
anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe,”
Yoh 6:37. Kumwendea Kristo ni kuwa karibu
naye kila wakati. Ni kuishi maisha yasiyo na hatia. Ni kuupigania ukamilifu
ingawa udhaifu upo. Ni kuishi maisha ya kisakramenti na kuchota huko neema na
baraka za Mungu kila wakati na kwa kila nafasi tuipatayo kushiriki masakramenti
hayo. Ni kuwa waaminifu katika sheria na amri za Bwana kwa kuzishika na
kuziishi. Ni kuwa tayari kupokea neema na huruma ya Mungu, na kuwa vyombo vya
amani na upendo katika kusambaza neema na huruma hiyo ya Mungu kwa watu
wengine.
Kwa kuyashika na kuyaishi haya kamwe
Kristo Yesu awezi kutuacha leo, siku ya kufa kwetu, na mwisho siku ya ufufuo
wetu. Kwa kufanya hivyo tutakuwa kwenye mpango wa wokovu wa Bwana wetu Yesu
Kristo, naye atayatimiza mapenzi ya Mungu kwetu. “Na mapenzi yake
aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja,
bali nimfufue siku ya mwisho,” Yoh 5:39.
Kumtazama Mwana na kumwamini kuna maanisha kujazwa uzima wa milele.
Ndugu yangu unaye safiri nami katika
tafakari hii, tunamtazama Mwana na kumwamini tunapowajali wahitaji hasa
wagonjwa, wafungwa, wenye njaa, wenye kiu hasa ya haki, wageni, na walio uchi,
Mt 25:36-40. “Kwa
kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na
kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh
6:40. Je, hujakutana na Kristo Yesu bado kwa kumtazama na kumwamini? Usiende
mbali bali anza hapo hapo ulipo utakutana naye.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa
maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida,” Flp 1:21
Tusali:-Ee
Yesu, nijalie kifo chema. Amina