martes, 20 de septiembre de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA MTAKATIFU MATHAYO, MTUME NA MWINJILI

Sikukuu ya MTAKATIFU MATHAYO, Mtume NA Mwinjili
Somo: Efe 4:1-7, 11-13
Zab/Kit: 19:2-3, 4-5
Injili: Mt 9:9-13
Nukuu:
Kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani,” Efe 4:2-3

Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo,” Efe 4:7
Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe,” Efe 4:11-12

Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata,” Mt 9:9

Naye aliposikia, aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi,” Mt 9:12 

Lakini nendeni, mkajifunze maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” Mt 9:13

TAFAKARI: “Tumeitwa na kuwa kama tulivyo si kwa Mapenzi yetu, bali kwa Neema, Rehema, na Mastahili ya Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha sikukuu ya Mtume Mathayo Mwinjili. Mtume Mathayo ni kati ya wale wanafunzi wa Yesu kumi na mbili, yaani, Thenashara. Mtume Mathayo ndiye mwandishi wa Injili yenyewe ya Yesu Kristo ijulikanayo kama Injili ya Mathayo. Wasifu wa Mathayo kabla ya kuchaguliwa kuwa mmoja ya wale wanafunzi kumi na mbili wa Yesu, alikuwa akifanya kazi ya ukarani. Kwa upande mwingine alikuwa na elimu ya kutosha na kutokana na elimu hiyo alikuwa na maisha mazuri. Kwa hali hii twaweza kusema alijitosheleza kwa namna fulani katika mahitaji yake ya kawaida.

Wapendwa wana wa Mungu, ningependa leo tunaposheherekea sikukuu ya Mtume Mathayo Mwinjili, tuzame katika tafakuri yetu kwenye maneno haya, kwamba, ‘tumeitwa na kuwa kama tulivyo si kwa Mapenzi yetu, bali kwa Neema, Rehema, na Mastahili ya Mungu.’ “Kwa sababu hakuna miongoni kwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana.” Rum 14:7-8. Huu ndiyo uliokuwa msukumo wa wanafunzi wa Yesu katika kuyastahimili mateso yote, wakati wakiwa na Kristo mwenyewe na hata baada ya kifo na kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

Mwono huu chanya wa maisha ya Mitume katika utume na uinjilishaji wao, ulimjengea unyenyekevu Mtume Mathayo na hata kuyaacha yote na kumfuata Kristo. Hivyo, naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata,” Mt 9:9. Ndugu yangu, si jambo rahisi kuyaacha yale tuliyoyazoea na kuwa na uhakika nayo na mara kubadili njia na kuanza mfumo mpya wa maisha. Kwa hali ya kawaida jambo hili linahitaji tafakari kubwa na uamuzi wa kina na busara. Ni kweli kwamba sisi sote tuna mang’amuzi ya jana, uhakika wa leo, na sintofahamu ya kesho.

Kwa maana hiyo twaweza kuona ni kwa namna gani Mitume wa Yesu, na hasa Mathayo walivyokuwa tayari kuyahatarisha maisha yao kwa kile wasichokijua. Hapa ndipo tunapoona Neema, Rehemu na Mastahili ya Mungu katika miito yetu. Ni ukweli kwamba, “kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo,” Efe 4:7. Kuujua ukweli huu na kuuishi kwa hitaji unyenyekevu mkubwa sana tukijua sisi sote katika huduma hii ya pekee ni vyombo vya udongo. Hivyo Mtume Paulo anatukumbusha kuwa, “tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.” 2Kor 4:7.

Wapendwa wana wa Mungu, unyenyekevu wetu hujengwa katika hali ya kujijua na kujipokea kama tulivyo, yaani, uhodari wetu na udhaifu wetu katika hali ya unyonge wetu. Ndugu yangu, kila siku katika uhodari wako pambana kuuondoa udhaifu wako ukishirikiana na Kristo aliyekuwa tayari kuwa masikini kwa ajili ya udhaifu wako ili uwe tariji (fumbo zima la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo), 2Kor 8:9. Hivyo, Mtume Paulo anatuwasa sote ili tudumu katika huduma yetu kwa wenzetu akisema, kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani,” Efe 4:2-3. Hapa ndipo tunapojifunza falsafa ya Kondoo. Kondoo huficha mavi yake kwa mkia wake. Huku ndiko kuchukuliana na kuhifadhiana katika upendo na umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

Ndugu zangu, sote kwa pamoja tumeitwa kuishi ukweli huu ila kila mmoja kwa utofauti wake. Utofauti huu hujionyesha katika aina ya miito, na vile vile ndani ya wito ule ule. Hatukuitwa kuwa vivuli vya wengine, bali kwa utofauti wetu katika aina tofauti za miito yetu na ndani ya wito uleule, huo ndio uzuri wa Mungu wetu. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema, naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe,” Efe 4:11-12. Mwili wa Kristo, kwa tafsiri nyingine, yaani, Kanisa hai-wote waliobatizwa, upendeza na kujengwa katika umoja na utofauti wetu. Ni kwa nini basi hujisikii furaha kwa wito wako? Ni kwa nini basi hujipokei kama ulivyo? Na, ni kwa nini basi wapenda kuwa kivuli cha mwenzako?

Wapendwa wana wa Mungu, Yesu Kristo keshatupa majibu ya maswali hayo kwa kusema, “Nataka rehema, wala si sadaka; kwa maana sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” Mt 9:13. Yesu anatusihi tujifunze maana ya maneno haya kila siku ya maisha yetu. Yesu havutiwi hata mara moja kwa kiasi tukitoacho, bali ubora wa yale tuyatoayo. Hapa ndipo kwenye Neema na Rehema ya kweli mbele za Mungu na Msamaha wa dhambi. Ukweli huu ni kwamba, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi,” Mt 9:12. Basi tukiwa wote ni wahitaji, Kristo ndiye njia, kweli na uzima wetu, Yoh 14:6. Amina!

Tumsifu Yesu Kristo!

Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo,” Efe 4:7

Tusali:-Ee Yesu Mwema, tunasema asante kwa namna tulivyo. Amina

1 comentario: