domingo, 11 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 24 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 24 YA MWAKA-C
Somo: 1Kor 11:17-26, 33
Zab/Kit: 40:7-8a, 8b-9, 10, 17
Injili: Lk 7:1-10
Nukuu
Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara,” 1Kor 11:17 

 “Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo,” 1Kor 11:22

 “Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojaneni,” 1Kor 11:26, 33

 “Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya,” Lk 7:8

Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii,” Lk 7:9

TAFAKARI: “Ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu.”

Wapendwa wana wa Mungu, Maandiko Matakatifu yanatupa angalizo na kusema, “ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu,” Rum 14:17. Ni wazi jumuiya hii ya Korintho walianza kupoteza maana halisi la fumbo la ‘Ekaristi Takatifu,’ ingawa fumbo hili kwa nyakati zile lilijulkana kama ‘Kuumega Mkate Pamoja,’ Lk 24:35, Mdo 2:42. Mkusanyiko huo wa jumuiya ya kwanza ya Wakristo baada ya kusali na kujadili yaliyohusu jumuiya yao kimwili na kiroho, na swala zima la uinjilishaji, walishirikishana chakula cha pamoja ikiwa ni kukumbuka karamu ile ya mwisho ya Bwana wetu Yesu Kristo na Mitume wake.

Mkate na Divai ambavyo vilibeba fumbo hili Kisakramenti-ishara ya nje inayoonekana wazi kwa uwepo wa neema isiyoonekana, vielelezo hivi shikika na onekana, yaani, Mkate na Divai, kila mwanajumuiya aliyekuwa na uwezo alivileta kutoka nyumbani kwake. Kwa vile siyo kila mmoja kwenye jumuiya alikuwa na uwezo wa kuandaa hayo, masengenyo na kunyapaliana yalijitokeza. Na ndiyo maana kusanyiko lao katika mwono huo, Mtume Paulo analiita si kusanyiko lenye faida bali lenye hasara. Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara,” 1Kor 11:17. Maumbo haya ya Mkate na Divai licha ya kuwa ishara ya ndani lenye kutupa uzima wa mwili na roho, ilimaanisha pia upendo na umoja wa wabatizwa wote kama Mwili wa Kristo, nalo ndilo kusudi la kukusanyika kwao kama KANISA.

Badala yake, Mkusanyiko ule ulilenga upande mmoja tu, yaani, mwili, na kuelekeza nguvu zote kwa mfalme tumbo. Na hiki ndicho kisa cha sokomoko lote la kusengenyana, kutengana kwa masikini na matajiri, na hata kunyapaliana. Naye Mtume Paulo anasema, Kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu,” 1Kor 11:18-19. Mwelekeo huu wa kumwabudu mfalme tumbo, wengine kati yao walipitiliza na kutumia Divai ile kama kileo na kuishia kulewa na kupoteza maana halisi ya uwepo wa Mkate na Divai kama Mwili na Damu ya Kristo-Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kwa mshangao huu, Mtume Paulo anasema, Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana; kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa,” 1Kor 11:20-21. 

 Kwa maana halisi ya Maumbo hayo ya Mkate na Divai, na uhusiano wake na Kanisa kama nilivyokwisha kusema hapa mwanzo, tendo lile la kunyapaliana na kukufuru kulikotokana na ulevi, matendo hayo siyo kusudi la kukusanyika kwako kama Kanisa- Mwili wa Kristo. Kwa maana nyingine, hapo siyo sehemu ya mambo hayo. Naye Mtume Paulo anazihoji dhamiri zao na kusema, Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau Kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo,” 1Kor 11:22. Hakika hakuna cha kujivunia kwa kuyafanya hayo yenye kupotosha maana halisi ya Mwili na Damu ya Yesu, na uhusiano wake na Kanisa, wewe na mimi tukiwa ndiyo viungo vyake, 1Kor 12:27

Baada ya kukemea hili, Mtume Paulo anatoa mafundisho halisi ya Fumbo hili la Mkate na Divai. Naye Paulo analisema hilo kadiri ya Mapokeo, yaani, kutoka Yesu Mwenyewe na Mitume wake. Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu,” 1Kor 11:23-24.

Ni ukumbusho katika maana ya Agano la Pekee alilolifanya Mungu kupitia Mwanaye Yesu Kristo, na twafanya hivyo kila mara tukikumbuka sadaka ile ya pekee ya Yesu Kristo pale Msalabani ambayo ndiyo sababu ya wokovu wetu kutoka utumwa wa dhambi. Na ndiyo sababu pia ya mimi na wewe kuwa wana na warithi wa Ufalme wa Mungu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu,” 1Kor 11:25. Na kwa kufanya hivyo kwa moyo mkunyufu na hofu ya Mungu, twaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Kwa hiyo, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojaneni,” 1Kor 11:26, 33

Ndugu yangu tunaye safiri sote katika tafakri hii, kwa maumbo haya ya Mkate na Divai, Mwili na Damu ya Yesu, Yesu Kristo ni uzima halisi. Kristo ni uzima halisi tunaposhiriki Ekaristi Takatifu katika mastahili yake. Yesu anatuambia, “Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe” Yoh 6:35. Ni katika kula chakula hiki-mwili na damu yake,  Yesu anahaidi mambo mawili makuu: Moja, ni ufufuko siku ya mwisho. Naye anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:54. Na katika kula chakula hiki-mwili na damu yake, Kristo hukaa ndani yetu. Naye anasema, Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:56.

Hata hivyo Mtume Paulo anatupa angalizo la chakula hiki cha uzima. Naye anasema, Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Yatupasa kuijongea Meza ya Bwana tukiwa na mastahili ya kufanya hivyo-usafi wa mwili na roho, yaani, pasipo hatia yoyote. Zaidi ya hapo ni kuikufuru Meza ya Bwana. Je, tuna IMANI hiyo au tunafanya kama tunavyofanya kwa mazoea tu?

Wapendwa wana wa Mungu, IMANI ya kweli inayoacha ubinafasi wetu pembeni na kumtanguliza Mungu, ndiyo anayoisifu Yesu leo katika Injili tuliyoisikia. Imani hii ndiyo aliyoistahajabia Yesu juu ya akida yule aliyekuwa na mtumwa wake mgonjwa aliyehitaji uponyaji wa Yesu. Baada ya kupata ombi hili kutoka kwa akida yule, Yesu anachukua hatua mara moja na akiwa njiani imani ya kweli ya akida yule inajidhihirisha.  “Basi Yesu akaenda pamoja nao. Hata alipokuwa si mbali na nyumba yake, yule akida alituma rafiki kwake, akamwambia, Bwana, usijisumbue, maana mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; kwa hiyo nilijiona sistahili mwenyewe kuja kwako; lakini, sema neno tu, na mtumwa wangu atapona,” Lk 7:6-7.

Huu ndio uhai halisi wa Kristo kati yetu, ambao leo upo katika maumbo ya Mkate na Divai, yaani, Ekaristi Takatifu. Tuwapo mbele ya uwepo huu halisi wa Kristo, ni wakati wa kushikamana na Kristo, na kuachana na ubinadamu wetu, vionjo vyetu, na matamanio yake, ikiwa ni pamoja na mamlaka tuliyonayo katika jamii. Katika kweli hii Akida yule anasema, Kwa maana mimi nami ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, mwenye askari chini yangu; nikimwambia huyu, Nenda, huenda; na huyu, Njoo, huja; na mtumwa wangu, Fanya hivi, hufanya,” Lk 7:8. Pamoja na nguvu na mamlaka hizi za kibinadamu Mungu abaki kuwa Mungu, na Kristo abaki kuwa Kristo, Baba na Mwakozi wetu.

Hapa ndipo Yesu alipostaajabu; Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii,” Lk 7:9. Ndugu yangu, mshangaze Kristo kwa kusimama katika imani iliyo kweli. Iwapo imani ya kweli, Kristo yupo na hujidhihirisha pasipo mawaa kabisa. Kristo hutenda yote pale tunaposhikamana naye. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa yule Akida na mtumwa wake mgonjwa kwamba,  Na wale waliotumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa ni mzima,” Lk 7:10. Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lihimidiwa milele na milele. Amina.

Tumsifu Yesu Kristo!

Yesu aliposikia hayo alimstaajabia, akaugeukia mkutano uliokuwa ukimfuata, akasema, Nawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa namna hii,” Lk 7:9


Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie Imani ya kweli, na mara zote utuepushe na vionjo vyetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario