JUMATANO WIKI YA 26 YA MWAKA-C
Somo:
Ayu 9:1-12, 14-16
Zab/Kit: 88:10bc-11, 12-13, 14-15
Injili: Lk 9:57-62
Nukuu:
“Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege
wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk
9:58
“Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima,
kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62
“Ndipo Ayubu akajibu,
na kusema, Kweli najua kuwa ndivyo hivyo; Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele
za Mungu?” Ayu 9:1-2
“Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo
katika nguvu; Ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?” Ayu
9:4
TAFAKARI:
“Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu; Ni nani
aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?”
Wapendwa wana wa Mungu,
kadiri ya Injili ya leo, Yesu
anampa angalizo mtu yule aliyekutana naye njiani na kusema yupo tayari
kufuatana naye ko kote atakapokwenda. “Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani
wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake,” Lk 9:58. Kwa
maneno mengine Yesu anatuambia hakuna maslahi yo yote kibinadamu zaidi ya
maisha ya umilele kutoka kwake. Kama ni swala la utajiri na kuwa na maisha
mazuri siyo kipaumbele cha kwanza katika ufuasi wetu kwake. “Bali utafuteni
kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Mt 6:9. Kazi yetu
ya kwanza ni kuutafuta ‘kwanza ufalme wa mbinguni’ na mengine yote tutapewa kwa
ziada na kadiri ya mahitaji yetu.
Jambo la
pili na la muhimu tunalofundishwa leo kuhusu Imani ya kweli na ufuasi usio na
mawaa ni ‘utambuzi wa kweli na kujua nafasi ya Mungu katika maisha yako.’ Bila
shaka wengi wetu tuna hofu ya kifo. Hata hivyo, kifo kipo pale pale upende au
usipende. Na kama umezaliwa basi ipo siku utakufa. Kuzaliwa si lazima, bali
kufa ni lazima kama umezaliwa. Kwa hiyo katika mantiki hii ya kifo na uhalisia
wake, hatupaswi kukiogopa. Yatupasa kuishinda hofu ya kifo ili uwe tayari
kukipokea kifo kama njia pekee ya maisha yale baada ya kifo hapa duniani,
kuishi umilele. Hakutakuwa na maisha ya umilele baadaye bila kupita katika fumbo
hili la kifo.
Hivyo
Yesu anamtoa hofu ndugu yule aliyetoa hoja ya kwenda kwanza kumzika Baba yake
ndipo amfuate. Naye Yesu anamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe
enenda ukautangaze ufalme wa Mungu,” Lk 9:60. Je, Yesu anatukataza kuwazika
wazazi wetu? La hasha! Kufanya hivyo angekuwa anaenda kinyumbe na ile amri ya
nne ya Mungu, “waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi
katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kut 20:12. Yesu anachotaka kukuambia
wewe na mimi leo ni kwamba, kifo ni ‘kweli isiyopingika na hivyo shughuli zake
na mazingira ya yake, isiwe sababu ya kutokupokea ujumbe wake wa uzima wa
milele.
Na jambo
la tatu na la mwisho tunalofundishwa leo kuhusu Imani na ufuasi thabiti ni
‘kule kuwa na msimamo thabiti wa wito ulio nao na kutunza kile ulichoitiwa.’
Hii ni pamoja na kutokuwa ndumilakuwili au kigeugeu cha kutaka‘kutazama au
kurudi nyuma ulikotoka kwa malengo ya kujaribu tena.’Bali lipaswalo ni kujenga uaminifu na utayari wa kutimiza kile ulichoitwa na
kukubali bila shuruti kwa sifa na utukufu wake Mungu. Na hicho ulichoitwa na
kukubali kwa hiari yako kiwe mwitikio chanya hasa pale linapojitokeza swala ya
huduma kwa watu au umma.
Wengi
wetu baada ya kubatizwa tumerudi kuishi maisha ya kipagani kabisa. Na wengi
katika kundi hili wamekuwa washirikina wa kupindukia na kuongozwa na nguvu za
giza ili hali wamejivika visakramenti mwili mzima. Ushirikina ‘ni kuamini nguvu
fulani kutoka kitu fulani kisicho na uhusiano kimantiki.’ Katika hili Yesu
anatupa angalizo, na kusema, “Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia
nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62. Kwa maneno mengine ni heri kuwa
baridi au joto, kuliko kuwa vuguvugu katika Imani.
Ayubu ni
mfano mzuri na dhahiri wa kusimama katika imani thabiti. Siri kubwa aliyokuwa
nayo Ayubu juu ya imani yake ni kutokushikamana na vitu na kujifananisha navyo.
Ayubu alijisalimisha kabisa mikono mwa Mungu. Baada ya kuyatafakari maisha yake
na uhusiano wake na Mungu, “ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
Kweli najua kuwa ndivyo hivyo; Lakini mtu huwaje mwenye haki mbele za Mungu?”
Ayu 9:1-2. Mungu ndiye haki, na Yeye tu ndiye mwenye kutuhesabia haki. Hivyo
mtu “kama akipenda kushindana naye, Hawezi kumjibu neno moja katika elfu,” Ayu
9:3. Katika hali na mazingira kama haya usalama wako upo pale tu utakapo
jisalimisha mikononi mwake bila kujibakiza.
Ayubu kwa namna ya
pekee pia anagundua kuwa Mungu ndiye kila kitu. Kwake hakuna linalomshinda, na
vyote vipo kama vilivyo kwa nguvu zake, Ayu 9:5-12. Mungu huyu aliye hai na
wapekee ndiye uiongoza mifumo yote hai (inayoonekana na isiyoonekana) kadiri
apendavyo Yeye. Ni kweli pasipo shaka kwamba
“Yeye ni mwenye hekima moyoni, na mwenye uwezo katika nguvu,” Ayu 9:4a.
Na vyote avifanyavyo Mungu vina lengo la umilele. Kushindana au kupingana na
Mungu kwa ufahamu wako ni kushindwa kabla hata ya kuanza kutekeleza jambo hilo.
Hivyo “ni nani aliyejifanya kuwa mgumu juu yake, naye akafanikiwa?” Ayu 9:4b.
HAKUNA!
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha
akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:62
Tusali:-Ee Yesu Mwema, tujalie
neema na nguvu na kupita katika majaribu ya Imani. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario