IJUMAA WIKI YA 26 YA MWAKA-C
Somo:
Ayu 38:1, 12-21, 40:3-5
Zab/Kit: 139:1-3, 7-8, 9-10, 13-14ab
Injili: Lk 10:13-16
Nukuu:
“Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza?
Umeyajulisha mapambazuko mahali pake?” Ayu 38:12
“Ndipo
Ayubu akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini?
Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4
“Ole wako Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa
kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni,
wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi katika nguo za kigunia na majivu,” Lk
10:13
“Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa hata mbinguni?
Utashushwa hata kuzimu,” Lk 10:15
“Awasikilizaye ninyi
anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi
amkataa yeye aliyenituma,” Lk 10:16
TAFAKARI:
“Awasikilizaye ninyi anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi;
naye anikataaye mimi amkataa yeye aliyenituma.”
Wapendwa wana wa Mungu,
katika maisha yapo “mambo fulani” na hata wakati mwingine hutokea “mambo
fulani,” ambayo kwayo kwa ufahamu wa ubinadamu wetu hukoswa na majibu. Huu
“ufulani wa mambo” tusioujua katika maisha, huyafanya maisha hayo kuwa fumbo.
Fumbo siyo tatizo na lingekuwa tatizo basi lingekuwa na jibu au suluhu yake.
Fumbo halina suluhu zaidi ya kulizungumzia katika maana ya kulihusisha na kile
tukifahamucho ili tuzame katika undani wa fumbo hilo. Lengo ni kupata mwanga
katika fumbo hilo.
Ili kumfanya Ayubu
azame ndani ya yale yaliyompata, Mungu kupitia upepo ule wa kisulisuli
anamuuliza, “Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha
mapambazuko mahali pake?” Ayu 38:12. Msingi wa swali hili ni kumtaka Ayubu
afahamu kuwa yapo mambo mengine ambayo kwayo kwa mazoea yetu twayaona ya
kawaida, ila yamebeba fumbo zito kwa Yule anayeyaratibisha, yaani, Mungu
mwenyewe.
Katika mwendelezo huo
wa maswali ya kina, Ayu 38:13-20, yanamfanya Ayubu kufunguka na kuzama zaidi
katika fumbo lile la maisha yake na yote yaliyompata. Yote tuyapatayo katika
maisha yana kusudi la umilele kwa sababu tumeumbwa tuishi milele, na hili ndilo
kusudi la Mungu kwako na kwangu. “Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, Na
hesabu ya siku zako ni kubwa!” Ayu 38:21. ‘Ukubwa wa hesabu za siku zako’ ni
umilele wa maisha yako.
Baada ya kuzamishwa
katika tafakari hii, na kupata mwanga wa fumbo la maisha yake, “ndipo Ayubu
akamjibu Mungu, na kusema, Tazama, mimi si kitu kabisa, nikujibu nini? Naweka
mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4. ‘Mimi si kitu kabisa, naweka mkono
wangu kinywani pangu,’ ni hali ya kujisalimisha kabisa bila kujibakiza kwa
Mungu Mweza wa vyote. Kujisalimisha huku si kwa kijinga, bali ni kujisalimisha
katika ‘ufahamu na umaana’-“rationality and significativity.” Akimaanisha
ufahamu na umaana, Ayubu anasema, “nimenena mara moja, nami sitajibu; Naam,
nimenena mara mbili, lakini sitaendelea zaidi,” Ayu 40:5. Hii ni hatua kubwa na
ya ukomavu katika maisha ya kiroho.
Je, kuna uhusiano gani
kati ya Imani na miujiza? Imani siyo miujiza! Ila miujiza usaidia imani changa
kukua na kukomaa. Mkristo anayebaki katika hatua ya miujiza tu, huyo bado hajakomaa
katika imani. Wapenda miujiza bila kukua katika imani, na wenye kuhama kutoka
nyumba moja ya sala na kwenda nyumba nyingine ya sala, huku wakivutwa na ‘nani
zaidi’, ni sawa na watoto wa ‘shule ya awali imani’ katika miaka yao yote. Na
hili ndilo analolikemea Yesu katika Injili ya leo na kusema, “Ole wako
Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza hiyo iliyofanyika kwenu
ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu tangu hapo, huku wakiketi
katika nguo za kigunia na majivu,” Lk 10:13. Miujiza ni mwito wa mabadiliko
katika Imani kuelekea ukomavu, na siyo kigoto cha imani. “Imani ni kuwa na
hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana,” Ebr 11:1
Watu waishio katika
miji hiyo iliyotajwa na Yesu tungeweza kusema ni “watoto wazee,” katika imani.
Na linganisho la ‘utoto uzee’ kiimani ni wakazi wa Tiro na Sidoni. Hawa wana
hofu ya Mungu. Naye Yesu anasema, “Lakini, siku ya hukumu itakuwa rahisi Tiro
na Sidoni kustahimili adhabu zake kuliko ninyi,” Lk 10:14. Wakazi wa mji wa Kapernaumu ni sawa na mbegu zile
zilizoanguka kwenye mwamba. Hawa ni “wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno
kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa
hujitenga,” Lk 8:13. Katika hali hii kiimani, Yesu anasema, “Nawe Kapernaumu,
je! Utakuzwa hata mbinguni? Utashushwa hata kuzimu,” Lk 10:15. Kukuzwa hata
mbinguni ni furaha kulipokea neno, ila wakati wa majaribu hukosa nguvu na
kushuka hadi kuzimu.
Pamoja na hali na
mazingira haya kiunjilishaji, Yesu anakuasa wewe na mimi tusivunjike moyo
katika kuitangaza habari njema ya wokovu wetu. Hapa na pale tutahuzunishwa na
hata kukatishwa tamaa, ila tusife moyo kwa sababu, “awasikilizaye ninyi
anisikiliza mimi, naye awakataaye ninyi anikataa mimi; naye anikataaye mimi
amkataa yeye aliyenituma,” Lk 10:16. Utume si lelemama. Utume ni kuvumilia
ndani na katika Kristo Yesu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Tazama, mimi si kitu kabisa,
nikujibu nini? Naweka mkono wangu kinywani pangu,” Ayu 40:3-4
Tusali:-Ee
Yesu, tujalie Roho ya Kimisionari tukiazia pale tulipo. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario