viernes, 23 de septiembre de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 25 YA MWAKA-C


JUMAMOSI WIKI YA 25 YA MWAKA-C

Somo: Mhu 11:9-12:8

Zab/Kit: 90:3-4, 5-6, 12-13, 14, 17

Injili: Lk 9:44b-45

Nukuu:

“Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni,” Mhu 11:9

“Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia,” Mhu 11:19

“Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo,” Mhu 12:1

“Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu,” Lk 9:44

“Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile,” Lk 9:45

TAFAKARI: “Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu.”

Mpendwa katika Kristo, Je! Mahangaiko na Mateso yako yana sema chochote juu ya maisha yako? Bila shaka kupitia mahangaiko na mateso yako unaandaliwa kwa lililo kubwa zaidi mbeleni na kuwa walimu wazuri zaidi kwa wenye shida kama uliyo nayo wewe leo. Je, hupendi kuwa mwalimu mzuri na kufundisha kile ukijuacho katika undani wake? Kila kitu kina makusudio yake katika maisha. Kama tuliumbwa kwa sababu na makusudi ya Mungu, basi kila jambo ndani yetu lina sababu yake na ujumbe wake hasa kuhusu imani yako.

Bwana wetu Yesu Kristo anatujengea ujasiri wa kustahimili mahangaiko na mateso kama anavyowaambia wanafunzi wake nyakati zile, kwamba, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu,” Lk 9:44. Ni kweli na haki kabisa kwamba ujumbe huu kibinadamu hausikiki vizuri masikioni mwa wanafunzi wake kwa mtazamo waliokuwa nao juu ya Yesu Kristo. Maneno haya yanasikika kama jambo la kufikirika vile. Bila shaka swali la msingi mioyoni mwa wanafunzi wake Yesu lilikuwa hivi: maneno haya yana ukweli gani ikiwa Yesu huyu tunayemjua anaonekana kuweza vyote na mkono wa Mungu ukifanya kazi juu yake atiwe nguvuni mikononi mwa watu? Maandiko Matakatifu yana tuambia kwamba, “hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile,” Lk 9:45. Kwa makusudi na nia njema kabisa ya Mungu anaweza kuuficha ukweli fulani kwa lengo na kama kipimo cha Imani yetu.

Katika maisha yetu ya kila siku yapo mazingira fulani na hata nyakati fulani kwayo ukweli juu ya Mungu hujificha au kufichwa. Mara nyingi na tulio wengi nyakati za furaha na amani huwa hatuoni uwepo wa Mungu. Hali hii ututia kiburi cha kujinyanyua na kumweka Mungu kama hitaji la pili au la tatu katika maisha. Ni wakati wa “ponda mali kifo chaja.”  Kumbe wakati kama huo wa furaha ndiyo wakati mzuri zaidi kumpa Mungu sifa na shukrani. Ni wakati nzuri zaidi wa kuzama katika mafumbo na makuu ya Mungu ukijua kwamba utulivu husadifu uwepo wa Mungu.

Maisha yampendezayo Mungu ni maisha yale yanayoongozwa na malengo, na Mungu akiwa muhimili wa kila kitu katika maisha hayo. Mungu anapokuwa kila kitu na muhimili wa maisha yako, utajua na kutimiza sababu ya kuumbwa kwako. Na sababu ya kuumbwa kwetu ni hii; ili tumjue Mungu (Pendo likiwa ndiyo taa ya miguu yetu), tumpende Mungu (kwa kuishi vyema na jirani zetu), tumtukikie Mungu (kuonyesha upendo wa kweli kwa jirani zetu), na mwisho turudi kwake Mbinguni (tukiwa na cheo chetu, yaani, Utakatifu).

Kumbe katika maisha yangu kila siku na hasa katika hali ya ujana wangu, ni vyema nikatambua kwamba nina wajibu wa maana sana kuutimiza pamoja na nafasi niliyokuwa nayo ya kuyafurahia maisha. Kwenye wajibu huo muhimi, yaani, kuijua na kuitimiza sababu ya kuumbwa kwangu, ndipo penye hukumu yangu pia. Hivyo “Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni,” Mhu 11:9. Fursa nilizonazo leo zinikumbushe daima wajibu huo wa kuumbwa kwangu. Kamwe sipo duniani hapa kwa bahati mbaya.

Ingawa wakati mwingine na hata sasa katika hali yako yawezekana maisha yamekupiga, umechoka na hata kupoteza ramani ya maisha yako. Hali na mazingira hayo yasiwe sababu ya kulipoteza tumaini lile la Mungu. Na tumaini hilo ni hili: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele,” Yoh 3:16. Je, nina shaka na Pendo hili kubwa la Mungu kwangu licha ya shida na mahangaiko niliyo nayo leo na sasa? “Kwa hiyo ondoa majonzi moyoni mwako, nawe uuondoe ubaya mwilini mwako; kwa maana ujana ni ubatili, na utu uzima pia,” Mhu 11:19.

Ujana ni ubatili, na utu uzima pia kama tutaenenda na mambo ya ujana tu na hayo ya utu uzima tu, bila hayo kwayo kuwa na uhusiano na Mungu. Maisha hayo na kwayo kama yalivyo siyo mwisho wa kila kitu. Maisha hayo yatuwezeshe kuifikia ile mede ya dhahabu kama asemavyo Mtume Paulo, “si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu, na nakaza mwendo, niifikie mede ya thahabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu,” Flp 3:12, 14.

Kumbe wajibu wangu mwingine wa kila siku ni kulenga katika ukamilifu ingawa udhaifu ninao kama mwanadamu. “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo,” Mhu 12:1. Na maisha huwa kama yalivyo kwa namna unavyo kabiliana nayo kila siku. Ila maisha hayo hutakatifuzwa na kuwa na maana zaidi hata kama yatasongwa na dhiki na taabu yanapo husishwa na uwepo wa Mungu.

Wapendwa, “jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya mwanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” IKor 10:13. Tumwamini Mungu na tushikamane naye daima. Hakuna linalomshinda Mungu wetu aliye hai.

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue,” Lk 9:45a

Tusali:-Ee Yesu, uliye yashinda mateso na kuniweka huru kutoka utumwa wa dhambi, yape maana mateso na mahangaiko yangu leo na sasa. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario